Ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijali mwaka mwingine katika uhai wangu. Tarehe kama ya leo, miaka kadhaa iliyopita, familia ya Mzee Philemon Chahali na mkewe marehemu mama Adelina Mapango (Mungu ailaze roho yake mahali mema peponi) ilipata mtoto wa tano, wa kiume, na kumpa jina la Jamhuri kwani alizaliwa siku ya Uhuru na Jamhuri. Baadaye mtoto huyo alibatizwa na kupewa jina la Mtakatifu Evarist.
Mwaka uliopita ulikuwa na majaribu kadhaa, kubwa zaidi ni tukio ambalo kamwe sintolisahau maishani mwangu, tarehe 2 ya mwezi Februari mwaka huu ambapo vyombo vya usalama hapa Uingereza vilinifahamisha kuwa kulikuwa na tishio la kuaminika (credible threat) dhidi ya maisha yangu. Wakati hadi leo sifahamu kwa undani kuhusu waliohusika na mkakati huo wa kidhalimu, wala kufahamu wanausalama wa hapa walifanikiwaje kujua kuhusu mpango huo, habari isiyopendeza ni ukweli kuwa hadi leo bado naishi kwa tahadhari. Wanausalama wa hapa wamekuwa wakini-update mara kwa mara, lakini wanasisitiza kuwa kwa vile hawajapata taarifa yoyote kuwa tishio hilo dhidi ya uhai wangu limekwisha, sina budi kuendelea kuzingatia ushauri wao kuhusu hatua za tahadhari kwa usalama wangu. Kwa hakika ni jambo gumu na la kuogofya lakini kwa sasa imekuwa ni sehemu ya maisha yangu ya kila siku. Hata hivyo, kwa ulinzi wa Mungu na jitihada zangu mwenyewe, ninatumaini kuwa nitaendelea kubaki salama.
Kwa bahati nzuri (au mbaya?) siku yangu ya kuzaliwa inagongana na siku ya kuzaliwa kwa Tanganyika (Tanzania Bara). Nasema kwa bahati nzuri kwa vile inapendeza kushea birthday na nchi yangu. Hata hivyo, kwa bahati mbaya (makusudi?) mwenendo wa birthday buddy wangu Tanzania Bara si wa kuridhisha hata kidogo. Kwa upande mmoja taifa letu linabakwa na mafisadi huku umasikini ukizidi kukua. Kwa hakika ni vigumu kubashiri hatma ya taifa letu angalau miaka 10 ijayo.
Hata hivyo, kwa vile leo ni sikukuu yetu ya kuzaliwa, basi sina budi kuitakia Tanzania Bara heri na baraka ya kuzaliwa na kujitakia happy birthday mie mwenyewe pia. Ndio maana kichwa cha habari kinasema HAPPY BIRTHDAY TANZANIA BARA, HAPPY BIRTHDAY ME!
0 comments:
Post a Comment