Thursday, 5 December 2013

WIKI iliyopita nilizungumza na rafiki yangu mmoja, Mtanzania mkazi wa hapa Uingereza, ambaye alikuja likizo huko nyumbani hivi karibuni. Katika maongezi yetu, rafiki yangu huyo alionekana kuguswa na mambo kadhaa aliyoyashuhudia huko. Pengine kushangazwa kwake huko kulichangiwa na ukweli kwamba amekuwa mkazi wa hapa Uingereza kwa takriban miaka 20, na hutembelea huko nyumbani kwa nadra.
Katika hali ya kusikitisha, alikaribishwa nyumbani na 'wahalifu wa kola nyeupe' (white collar criminals), ambao katika mazingira ya kushangaza walifanikiwa kumwibia simu tatu. Kwa maelezo yake, wizi huo unaelekea kufanywa na wahusika katika uwanja wa ndege, lakini kilichomkera ni suala hilo kuonekana la kawaida kabisa kwa aliowaeleza.
Baada ya tukio hilo la wizi alipata fursa kadhaa za 'kuyaona maisha halisi ya Tanzania zaidi ya simulizi za mtandaoni au kwingineko. Anasema wakati kwa kuangalia haraka haraka, Jiji la Dar es Salaam limepiga hatua kubwa kwa majengo na idadi ya magari, hali huko vijijini ya kusikitisha mno. Alibainisha kuwa wakati wengi wa ndugu, jamaa na marafiki jijini Dar walionekana kuridhika na maisha (angalau kimaongezi), hali ya vijijini imetawaliwa na kukata tamaa ya maisha, huku dalili za umasikini zikiwa zimetawala kila kona.
Lakini moja ya mambo yaliyomgusa zaidi ni uwajibikaji ofisini. Alinieleza kuwa alipokuwa Dar alikaribishwa katika baadhi ya ofisini na rafiki zake kadhaa wenye nyadhifa muhimu katika sehemu wanapofanya kazi. Kwa kiwango kikubwa, wengi wa mabosi hao hawakuonekana kuchukulia majukumu yao ya kiofisi kwa umakini na baadhi hawakusita kumwambia "hii ndiyo Bongo bwana," kwa maana ya 'Who cares?' (Nani anajali?) hata wakiboronga kazi.
Alichobaini ni kwamba wengi wa mabosi hao 'wanakula vizuri' na mabosi walio juu yao, aidha makao makuu au wizarani. Kadhalika, katika nyingi ya ofisi alizotembelea aligundua kuwa wengi wa mabosi ni kama 'miungu-watu' kiasi kwamba uwezekano wa watumishi wa chini kuwakosoa mabosi wao, hata kama ni kwa manufaa ya ofisi husika, haupo.
Kingine alichoshuhudia ni jinsi ofisi za mabosi hao zilivyosheheni samani za gharama kubwa. Japo rafiki yangu huyo ni mmoja wa mameneja wachache Watanzania hapa Uingereza, alibaki mdomo wazi kuona sofa, televisheni na vikorombwezo vingine vya thamani ya juu katika takriban kila ofisi ya bosi aliyemtembelea. Alieleza kuwa inaonekana kama ni fasheni fulani kwa kila kiongozi katika taasisi kuhakikisha ofisi yake ni kama Ikulu ndogo kutokana na kusheheni samani za gharama na vitu vingine vya gharama kubwa.
Kadhalika, licha ya wengi wa marafiki zake hao wenye nyadhifa kumjulisha kuwa wanalipwa mishahara minono, walionekana kutumia muda mfupi ofisini, huku katika muda huo mfupi wakiwa ‘bize’ na masuala binafsi kuliko ya kiofisi. Anasema baada ya maongezi ya takriban nusu saa katika ofisi ya kigogo fulani, alijisikia kama anachukua muda muhimu wa kigogo huyo na hivyo kuamua kuaga. Kwa mshangao, kigogo huyo alimlazimisha waendelee na maongezi huku akidai hana jambo muhimu la kufanya ilhali taasisi anayoiongoza inalalamikiwa na wananchi kwa utendaji kazi kwa 'kasi ya konokono.'
Kuhusu ufisadi, alinihakikishia kuwa umekuwa ni kama utamaduni muhimu katika taasisi nyingi (angalau alizozitembelea huko nyumbani). Alinipa mfano wa ofisa mmoja mwandamizi katika taasisi moja ya umma ambaye amepangishiwa nyumba na taasisi hiyo na analipiwa dola 1,500 za Marekani (sina hakika ni kwa mwezi au kwa mwaka). Kichekesho ni kwamba yeye ndio mmiliki wa nyumba hiyo. Kwa hiyo licha ya kukaa bure katika nyumba anayoimiliki bado analipwa kodi ambayo ni mamilioni ya shilingi za Kitanzania.
Lakini wakati alishuhudia baadhi ya Watanzania wenzetu wanaoishi maisha ambayo hata kwa sie huku Uingereza ni ya kufikirika tu, kuna hali tofauti kabisa aliyoshuhudia hapo hapo jijini Dar es Salaam. Alinieleza kuwa katika baadhi ya maeneo aliyoyaita ya 'uswahilini' alishuhudia kilo ya sukari ikiuzwa kwa vijiko ili wananchi wasio na uwezo wamudu kununua ‘vijiko’ kadhaa kwa ajili ya chai. Binafsi, nilishawahi kusikia taarifa kama hiyo kabla kuja huku lakini sikupata fursa ya kushuhudia bayana.
Kwa mujibu wa maelezo ya rafiki yangu huyo, kuna baadhi ya familia 'uswahilini' jijini Dar es Salaam zinaishi katika chumba kimoja, ambapo baba, mama na watoto hawana faragha yoyote. Kadhalika, alieleza kuwa katika maeneo hayo ni jambo la kawaida kwa binti kuondoka 'kwenda kutafuta hela' na wazazi hawana kizuizi kwani bila hivyo siku inaweza kupita bila 'mkono kwenda kinywani.'
Kufikia hapa, ninapenda kukuomba samahani msomaji mpendwa kwa 'simulizi' hii ndefu. Lakini nimekusudia kuifanya mada ya makala hii ili angalau iibue tafakuri kuhusu mwelekeo wa jamii yetu na hatma ya taifa letu. Katika maelezo ya rafiki yangu, kitu kimoja kilicho bayana ni pengo kubwa kati ya walio nacho na wasio nacho (nafasi hairuhusu kuelezea uzoefu wa rafiki yangu kuhusu 'vijana wenye utajiri wa ajabu' ilhali shughuli wanazofanya hazieleweki).
Pengo hilo linachangia sana hali ya 'who cares' kwani kimsingi kwa wenye uwezo, mtizamo ni 'nani anajali ilimradi mie nile kama mbuzi ninayekula kwa urefu wa kamba yangu?' Na kwa walalahoi nao, mtizamo ni huo huo wa 'nani anajali kama wanafilisi nchi yetu ilhali nimemudu kupeleka mkono kinywani?'
Kuna tatizo jingine ambalo niliwahi kulizungumzia katika moja ya makala zangu huko nyuma; upungufu wa tabaka la kati unaochangia kukwamisha jitihada za kulisaidia au kulikomboa tabaka la walalahoi au kupambana (angalau kwa njia za amani) na tabaka la vigogo ili angalau kujenga jamii yenye usawa. Kwa tabaka la kati (ninatambua kuna wanaohoji kama kweli Tanzania yetu ina tabaka hilo), wengi wa waliomo humo wanatamani kuwamo ndani ya tabaka la vigogo na pale matamanio hayo yanapokuwa magumu basi wanajifariji kwa kuishi kama vigogo. Mfano mwepesi ni wababaishaji tunaowashuhudia wakituza maelfu ya shilingi kwenye dansi au sherehe ilhali hali zao binafsi kiuchumi ni taabani.
Na kama kuna kasumba ‘kongwe’ kwa tabaka hili, au pengine 'ugonjwa' unaosumbua Watanzania wengi ni kupenda sifa zisizo na msingi. Si jambo la ajabu kushuhudia mtu mwenye kipato cha wastani tu akijihangaisha kuishi 'maisha ya maonyesho' kwa minajili tu ya kupata sifa mtaani. Na baadhi ya 'mabishoo' hawa ni watu wasio na msaada wa familia na jamii hususan katika maeneo yao ya asili. Sasa ni wazi kuwa ni vigumu kwa ‘kizazi hiki cha wapenda sifa' kuwa na mchango wowote kuunganisha nguvu na tabaka la walalahoi kulibana tabaka la vigogo kujenga jamii iliyo sawa.
Nimalizie makala hii kwa kukuhamasisha wewe msomaji wa makala hii kufikiria zaidi ya maslahi yako binafsi. Msingi wa maendeleo ya nchi kama hapa Uingereza ulijengwa na vizazi vilivyoishi miongo, kama si karne, kadhaa zilizopita. Je, tunapata fursa ya kutafakari Tanzania yetu itakuwaje angalau miaka 50 ijayo? Tukumbuke kuwa pasipo jitihada za makusudi kubadili mwenendo wa mambo huko nyumbani, basi hatutokuwa na jinsi ya kuzuia wajukuu zetu kuyashambulia makaburi yetu kwa hasira huku wakishangaa jinsi tulivyowaachia nchi iliyo tupu kwa raslimali na jamii iliyo tupu kimaadili.
INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WAKO

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget