“KATIKA taifa la ‘nani-anajali?’ (a who-cares nation) ajali zimeanza kuzoeleka kama mgao wa umeme,” ni ujumbe nilioandika juzi katika mtandao fulani wa kijamii baada ya kusoma habari kwamba matukio mawili ya ajali yamegharimu maisha ya Watanzania wenzetu 33.
Ujumbe huo ulibeba mambo mawili ya msingi. Kwanza, ni kasumba inayozidi kushamiri miongoni mwa Watanzania ya kupuuzia masuala ya muhimu kwao binafsi na kwa taifa lao. Mifano ni mingi lakini hapa nitabainisha michache.
Kama kuna vitu viwili vinavyonikera mno katika mitandao ya kijamii ni malalamiko yasiyoisha ya watumia huduma mbalimbali huko nyumbani. Maeneo mawili yanayozalisha walalamikaji wengi ni mgao wa umeme na huduma duni za baadhi ya kampuni za simu za mkononi.
Katika tatizo la mgao wa umeme, wengi wa walalamikaji hutumia lugha kali na hata matusi dhidi ya Tanesco, kana kwamba kwa kufanya hivyo shirika hilo la umeme litaona aibu na kuacha tabia inayoelekea kuwa ya kudumu sasa ya kukata umeme mara kwa mara, wakati mwingine mara kadhaa ndani ya siku moja.
Huwa najiuliza, hivi kitu pekee wananchi hawa wanachoweza kufanya ni kuitukana tu Tanesco? Lakini pengine kundi linaloweza pia kubebeshwa lawama licha ya wananchi hao ‘walalamishi’ ni wanasheria na wanaharakati wa haki za watumia huduma (consumer rights).
Kundi hili linajumuisha watu wanaojua sheria zinazomlinda mlaji (consumer), na laiti wangeguswa na tabia hii ya Tanesco basi ni dhahiri wangeweza kufungua kesi zinazofahamika kisheria kama class action. Kesi za aina hii ambazo ni maarufu zaidi nchini Marekani hufunguliwa na kundi kubwa la watu wanaowakilishwa na mwanasheria mmoja au kundi la wanasheria, dhidi ya mtu au taasisi.
Kwa mfano, mwaka 2008 wateja kadhaa wa kampuni moja ya huduma za mawasiliano nchini Marekani, AT&T, walifungua kesi dhidi ya Shirika la Ushushushu la nchi hiyo (NSA) wakilituhumu kwa vitendo vya kunasa mawasiliano na kufuatiliaji nyendo zao (surveillance).
Japo walalamikaji katika kesi hiyo walishindwa mahakamani, lakini mfano huo umelenga kuonyesha jinsi watumia huduma huko kwa wenzetu wanavyosaka haki zao. Japo mimi si mtaalamu wa sheria, je hakuna uwezekano wa kufungua kesi kama ya aina hiyo (class action) dhidi ya wahusika wote wa mgao wa umeme?
Kwa wanaolalamika kuhusu huduma zisizoridhisha za baadhi ya makampuni ya simu (hivi kuna hata moja isiyolalamikiwa?), wala haihitaji class action bali uamuzi tu kwamba “ninaachana nanyi kwa sababu mnaniona kama mteja nisiye na thamani kwenu.”
Hiyo ikizua kitu kinachojulikana kama domino effect (yaani kama goroli zikiwa kwenye mstari, ukiipiga moja inaisukuma nyingine, na nyingine, na kadhalika) hatimaye kampuni husika itabaini kwamba uhai wake upo hatarini laiti isipojirekebisha.
Kichekesho ni kwamba ‘domino effect’ iliyopo huko nyumbani miongoni mwa wateja wasioridhishwa na huduma za baadhi ya makampuni ya simu ni mtu mmoja kuitukana kampuni husika, na mwingine kufanya hivyo, na kadhalika. Na wasichotaka kujifunza kwa watangulizi wao ni ukweli kwamba hasira hayajawahi kuleta ufumbuzi wa tatizo lolote mahali popote pale.
Lakini kama nilivyoeleza mwanzoni mwa makala hii, mada ya wiki hii ni kuhusu kukithiri kwa ajali na mwamko mdogo miongoni mwa Watanzania kukabiliana na janga hilo ambalo kwa kiasi kikubwa linazuilika. Ndiyo, wanasema ‘ajali haina kinga’ lakini pindi ukiruhusu basi la abiria ambalo si tu linatumia injini ya ‘kibajaji’ lakini injini hiyo pia imechakachuliwa, ni wazi pindi basi hilo likipata ajali hatuwezi kudai kwamba ‘ajali haina kinga.’
Huo ni mfano wa kufikirika tu lakini ukweli unaochukiza ni kwamba asilimia kubwa ya vyombo vya usafiri wa abiria havipaswi japo kubeba majani ya kulisha mifugo au hata takataka. Sasa kwanini vyombo hivyo vya usafiri vinaruhusiwa kuwa barabarani?
Majibu mawili makuu ni aidha vinamilikiwa na vigogo ambao askari wa usalama barabarani hawawezi kuomba rushwa au kama mmiliki ni ‘mtu wa kawaida’ basi ni halali kwa askari kudai rushwa na kisha kuviruhusu viendelee na safari.
Wanasema ‘rushwa ni adui wa haki’ lakini kisichosemwa sana ni kwamba rushwa ni janga hatari kama ukimwi au ugaidi, vyote vyaweza kugharimu maisha ya watu wasio na hatia.
Na hata pale chombo cha usafiri kinapokuwa imara (kwa maana kinaweza kumudu kusafirisha abiria bila matatizo), tatizo jingine ni madereva. Katika mazingira ya kawaida tu, mtu akikesha baa kisha akaamka na mabaki ya pombe ya jana kichwani, anaweza kuwa na wakati mgumu kutembea kwa miguu achilia mbali kumudu kuendesha usafiri mwepesi kama pikipiki au hata baiskeli. Sasa dereva wa basi la abiria anaporuhusiwa kuendelea na safari huku ana ‘faida kichwani’ ni wazi kwamba hatma ya safari hiyo ni kama bahati nasibu.
Kwa nini madereva wasiostahili kuwao barabarani (maana hata mwendesha guta au bajaji akiwa na uwezo wa kuhonga trafiki ataruhusiwa kuendesha basi la abiria, hata kama hana leseni wala ujuzi stahili) wanaruhusiwa? Jibu ni lilelile: aidha chombo cha usafiri anachoendesha ni cha kigogo hivyo trafiki hawawezi kumdai rushwa au dereva anamudu kuwapatia trafiki haki yao ya rushwa.
Lakini kwa upande mwingine ni abiria wenyewe kutolipatia kipaumbele suala la usalama barabarani. Ni jambo la kawaida kusikia abiria wakipiga mayowe kwenye basi pindi dereva wa basi, kwa mfano, anapolikosakosa gari jingine barabarani, lakini hakuna ‘nguvu ya umma’ (kwa maana ya abiria kwa umoja wao ndani ya basi hilo) itakayotumika kumdhibiti dereva huyu. Na si kwamba abiria hao wanasafirishwa bure kiasi cha kuhofia kuwa “tukimbana dereva aendeshe kwa umakini atatushusha njiani.”
Kilichoniuma zaidi baada ya kusoma habari hiyo kuhusu wenzetu 33 waliopoteza maisha kutokana na ajali ni jinsi habari yenyewe ilivyoonekana ya kawaida miongoni mwa Watanzania wengi. Hata kwenye vyombo vya habari, magazeti mengi yalitawaliwa na habari kuhusu vituko vinavyoendelea kwenye Bunge Maalumu la Katiba huko Dodoma badala ya kulipa uzito janga hilo la kitaifa.
Katika salamu zake za rambirambi kwa wahanga wa moja ya ajali hiyo, Rais Jakaya Kikwete alieleza kwamba “vifo hivyo si vya lazima” na “ameshtushwa na kusikitishwa.” Lakini je inatosha tu kushtushwa na kusikitishwa ilhali, Mungu aepushie mbali, tuendelee kutarajia ajali zaidi hadi hapo hatua madhubuti zitakapochukuliwa ikiwa pamoja na kulifanya tatizo la ajali ‘zinazoepukika’ kuwa janga la kitaifa?
Lakini wakati Rais Kikwete anastahili pongezi kwa angalau kutoa salamu hizo za rambirambi, Watanzania wengine ukiachilia mbali wahanga wa ajali hizo, walifanya nini? Pitia pitia yangu kwenye mitandao ya jamii ilionyesha kuwa janga hilo lilikamata hisia za watu wachache sana ukilinganisha na, kwa mfano, klabu ya Liverpool ya hapa Uingereza kufanikiwa kushikilia usukani wa Ligi Kuu, au kimuhemuhe cha mpambano wa Ligi ya Mabingwa wa soka wa Ulaya kati ya Manchester United ya hapa na Bayern Munich ya Ujerumani jana.
Inasikitisha kuona Tanzania yetu inazidi kuwa taifa la ‘who cares?’ (nani ajali?). Na kwa kiasi kikubwa tatizo hili linaanzia kulekule kwenye kutokujali haki au stahili zetu binafsi. Ni wazi kuwa familia isiyojali inaweza ‘kuzaa’ ukoo usiojali, na hatimaye uwezekano wa kabila lisilojali, na hadi kufikia hapa tulipo: taifa lisilojali.
INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WAKO
0 comments:
Post a Comment