NI dhahiri sasa kuwa mjadala wa Katiba mpya, hususan kipengele cha muundo wa Muungano, unaelekea kulipeleka taifa mahali pabaya. Japokuwa dalili za Bunge Maalumu la Katiba linaweza kuishia kuwa jukumu ghali kwa walipakodi masikini, hasa baada ya kusikika madai ya baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kuwa posho ya shilingi 300,000 kwa siku haitoshi, lakini Watanzania wengi walikuwa na imani kwamba ‘upepo huo mbaya’ ungepita na hali ingekuwa shwari.
Hata hivyo, kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo hali inavyozidi kuwa mbaya. Kinacholeta wasiwasi zaidi kwa sasa ni kuibuka kwa dalili za ubaguzi wa waziwazi, sambamba na jitihada hatari za kumwaga petroli kwenye moto kwa kuingiza udini kwa nguvu kwenye siasa.
Lakini pasi ‘kuuma maneno’ naomba nielekeze lawama zangu kwa Rais Jakaya Kikwete na chama chake - CCM. Pamoja na wasiwasi uliokuwepo awali, kwamba huenda Rais Kikwete angeendeleza desturi iliyoota mizizi ndani ya CCM kwamba kila wazo lililoanzia vyama vya upinzani (kama hilo la umuhimu wa kuwa na Katiba mpya) ni baya, na hivyo angekwamisha uwezekano wa kupata Katiba mpya, alitushtua wengi alipoonyesha dalili za kuwa amepania kwa dhati kuweka historia kwa kufanikisha suala hilo muhimu.
Mambo yalionekana kwenda vizuri licha ya jitihada za hapa na pale ndani ya CCM kulifanya suala la Katiba mpya kuwa la kiitikadi zaidi kuliko la kitaifa. Wengi mtakumbuka vijembe walivyopigwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani walipotaka kukutana na Rais Kikwete. Badala ya kupongeza kile kilichoonekana kama mwanzo mpya wa siasa za maridhiano, baadhi ya wanasiasa huko CCM waliwakebehi wapinzani kuwa wanataka kwenda Ikulu kunywa chai tu!
Dalili za mwanzo kuwa hatma ya suala la Katiba mpya ipo shakani zilianza kujichomoza zaidi baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Jaji Joseph Warioba kuweka hadharani Rasimu ya Kwanza ya Katiba mpya, ambapo pendekezo la muundo wa Muungano wa Serikali tatu liliwekwa bayana. Taratibu, CCM, chini ya uongozi wa Kikwete, ilianza harakati za chini chini kujaribu kuingilia mchakato wa Katiba mpya, ikiwa ni pamoja na jitihada za kubinafsisha mchakato huo.
Lakini Mungu si Athumani au John, pamoja na vizingiti vya hapa na pale, hatimaye Rais Kikwete alitangaza majina ya wajumbe 201 kutoka makundi mbalimbali ya jamii, kuingia katika Bunge la Katiba. Lakini kabla ya hapo, tayari Rais Kikwete alishatangaza mkoani Mbeya wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM kwamba msimamo wa chama hicho ni Serikali mbili. Japo alitangaza msimamo huo kama Mwenyekiti wa taifa wa CCM, katika mazingira ya kawaida tu, isingewezekana kuwapo kwa mitizamo tofauti kati ya Kikwete wa CCM na Kikwete Rais.
Kuanzia hapo ikawa kama ‘jini lililopo kwenye chupa’ (a genie in the bottle) limefunguliwa. Zikaanza harakati za waziwazi ‘kulazimisha’ matakwa ya chama tawala kwamba muundo wa Muungano lazima ubaki kuwa wa Serikali mbili. Mara zikapatikana taarifa kuwa CCM imetengeneza rasimu yake ya siri.
Mara tu baada ya kikao cha Bunge Maalum la Katiba kuanza, ishara kuwa hali huko mbele inaweza kuwa si shwari zikawa zinajitokeza kila kukicha. Baada ya mshikemshike wa madai ya posho, likaibuka suala la utaratibu wa kupiga kura (yaani kura zipigwe kwa usiri au uwazi.)
Lakini kwa vile tangu awali CCM walionyesha kuwekeza nguvu zao kubwa katika suala la muundo wa Muungano wakitaka Serikali mbili, suala hilo limeteka takriban kila kipengele cha Katiba mpya, na kwa bahati mbaya au makusudi, mjadala wa muundo wa Muungano unazidi kutishia umoja na mshikamano wa taifa letu.
Japo lugha za matusi na kashfa si jambo geni kwenye vikao vya Bunge la Jamhuri, hali imezidi kuwa mbaya kwenye kikao cha Bunge Maalumu la Katiba, tunasikia baadhi ya wajumbe wakiwatuhumu wenzao kuwa mashoga, huko wengine wakienda mbali na kuhoji Uafrika wa wenzao. Lakini kama nilivyobainisha hapo juu kuwa tumeshazoea matusi na lugha chafu bungeni, kuna waliokuwa na imani kuwa “wakimaliza kutukanana, watarejea kwenye suala lililowakutanisha huko Dodoma.”
Mara vikaanza kuibuka vitisho kuwa iwapo Katiba mpya itaridhia Serikali mbili, jeshi litatwaa madaraka. Na aliyeanzisha vitisho hivi si mwingine bali Rais Kikwete katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge hilo la Katiba, wiki chache zilizopita.
Lakini wakati Rais Kikwete aliliongelea suala hilo katika jukwaa la kisiasa (bungeni), mmoja wa wasaidizi wake akaamua kulitoa suala hilo katika anga za siasa na kulipeleka kwenye nyumba za ibada. Hapa ninamzungumzia William Lukuvi.
Inaniwia vigumu kupata maneno stahili ya kumwelezea mwanasiasa huyo ambaye ghafla ametokea kuwa mtu mwenye kauli chafu, hatari na za kiharamia.
Huyu mtu bila aibu wala uoga amediriki kwenda kanisani na kutangaza waziwazi kuwa jeshi litaasi pindi uamuzi wa kuwa na Serikali tatu utakapopitishwa. Naomba nitamke bayana kwamba nahisi Lukuvi ana matatizo kutokana na hatua yake ya kwenda kanisani kufanya mahubiri ya kushawishi jeshi kuasi.
Lakini anayempa jeuri Lukuvi ni Rais Kikwete, kwani naye aligusia suala hilo kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la Katiba. Kwa hiyo anachofanya Lukuvi ni kusambaza tu ujumbe ulioanzishwa na Rais Kikwete.
Na wakati Rais Kikwete akiwakemea “wanasiasa wanaomtukana Nyerere na Karume” amekalia kimya matusi ya Lukuvi kwa Mwenyezi Mungu (naam, kutumia nyumba ya ibada kujenga chuki na kuhamasisha uasi wa jeshi ni matusi kwa Mungu.)
Ni watu wenye upeo mdogo tu watakaochukia kusikia kwamba Nyerere na Karume wana mchango katika matatizo tuliyonayo kuhusu Muungano, hasa kwa uamuzi wao wa kulifanya suala hilo kama lao binafsi bila kuangalia madhara yake miaka kadhaa ijayo.
Mara kadhaa Rais Kikwete amekuwa akiasa kuhusu athari za kuchanganya siasa na dini. Amewahi kudai kuwa kuna maadui wa nje wanaotumia suala la dini kwa minajili ya kututenganisha.
Lakini kipi cha kushangaza ilhali kwenye chaguzi kadhaa wamekuwa wakitumia nyumba za ibada kupandikiza chuki dhidi ya wapinzani wao?
Japo hainisumbui sana iwapo Katiba mpya haitopatikana, napata wasiwasi kuona uhuni wa kisiasa (political thuggery) ukihalalishwa kwa kisingizio cha ‘kuhubiri athari za Serikali tatu.’
Lakini nani wa ‘kuokoa jahazi’? Rais Kikwete anakemea wanaowatukana Nyerere na Karume, lakini anapuuza matusi ya wasaidizi wake kwa Jaji Warioba.
Nimalizie makala hii kwa kumkumbusha Rais Kikwete kwamba mwakani ataondoka madarakani na kurejea uraiani. Asipotengeneza mazingira mazuri kwake na kwa Watanzania, janga hili linalopikwa na akina Lukuvi litamwathiri naye pia.
Ni muhimu kwa Rais kuweka kando ushabiki wa kisiasa na kuchukua hatua za makusudi kuepusha nchi kutumbukia kwenye machafuko yanayochochewa na mahubiri ya ubaguzi na kuitumia dini kwa minajili ya kisiasa.
0 comments:
Post a Comment