Sunday, 11 December 2011


Ukiangalia picha hiyo juu kwa makini utabaini kuwa suruali ya Rais Kikwete ni kama inaashiria kwamba anaumwa.Of course,nusu ya juu iko kawaida (pengine kwa sababu ya bullet vest kama alikumbuka kuivaa) lakini nusu ya chini inaonyesha kama amekonda.

Inawezekana ni wembamba tu wa miguu ya Rais wetu lakini...well,nakuachia msomaji uhiimishe mwenyewe.


Mmoja ya mabloga ninaowaheshimu,Bwana Nkwazi Mhango (pichani juu) amenishushia tuhuma nzito akidai nimepokea hongo ya mafisadi kama inavyoonekana kwenye baruapepe ifuatayo (BONYEZA PICHA KUIKUZA)

Kama hukuweza kuisoma vizuri basi nainukuu hapa chini


Anonymous has left a new comment on your post "Nova Kambota: VIVA KAMANDA LOWASSA":

Chahali umenisononesha. Umeingiwa na nini hadi unampamba huyu fisadi wa kunuka? Sikuamini kuona naweka shairi langu la kumjibu huyu mtoto changudoa wa maadili wa Lowassa na ukalifuta. Kweli binadamu si viumbe wa kuamini. Hata hii futa kwa maslahi yako. Ila jua legacy uliyokwisha ijenga ina thamani kuliko hiyo hongo ya mabaki ya ufisadi.
Nkwazi Mhango


Publish
Delete
Mark as spam

Moderate comments for this blog.

Posted by Anonymous to Kulikoni Ughaibuni at 11/12/2011 01:16


Lakini cha kusikitisha ni ukweli kwamba baruapepe yenye shairi la Mhango analodai nililifuta (kutokana na hongo ya mafisadi) lilinifikia masaa mawili na dakika 31 baada ya barua pepe ya lawama.Kama ulivyoona katika picha ya hapo juu,Mhango alinitumia braua pepe ya kwanza (ya lawama) saa 7 na dakika 11 usiku kwa muda wa hapa Uingereza (angalia kulia juu kwenye email utaona imeandikwa Sent: Sun 11/12/2011 01.17).

Sasa angalia picha ya email ya shairi la Mhango hapa chini (cha muhimuni ametuma muda gani)

Kama picha inavyoonyesha,shairi la Mhango lilitumwa saa 9 na dakika 48 usiku kwa saa za hapa kama inavvoonekana katika picha hapo juu (kulia juu kuna maandishi kuhusu muda ambapo inasomekana bayana Sent on 11/12/2011 03.48

Anyway,nimekuwa nikimheshimu sana Bwana Mhango (na mmoja wa ushuhuda wa heshima yangu kwake ni makala hii ya Januari MWAKA 2008 isemayo MPAYUKAJI MSEMAOVYO...AU MSEMAKWELI? (bonyeza link kuisoma)

Tangu nianze uandishi wa blogu na makala sijawahi kupata tuhuma nzito kama hizi.Kinachosikitisha zaidi ni ukweli kwamba Mhango anafahamu fika nimetoka wapi katika vita yangu ya jeshi la mtu mmoja (one-man army) dhidi ya ufisadi.Anafahamu pia masahibu yaliyonikumba kutokana na mapambano hayo.Kwa hakika ngepaswa kuwa mtu wa mwisho kabisa kusema hayo aliyosema.Lakini kama alivyoandika mwenyewe,KWELI BINADAMU SI VIUMBE WA KUWAAMINI.

Natumaini baada ya kubaini kuwa alikurupuka kunilaumu kabla ya kuangalia vema kama shairi lake limeshanifikia,atafanya uungwana wa kuniomba samahani.

Saturday, 10 December 2011




Kikwete, Lowassa hapatoshi

Saed Kubenea's picture
Na Saed Kubenea - Imechapwa 30 November 2011
Printer-friendly versionSend to friend
HATIMAYE Edward Lowassa ametoka hadharani na kuonyesha kuwa anataka kupimana ubavu na Rais Jakaya Kikwete.
Ameeleza hadharani kuwa Rais Kikwete anahusika kwenye mkataba tata wa Richmond/Dowans; lakini pia, kuwa hafuati taratibu katika kuongoza chama chake.
Lowassa ambaye alikuwa nguzo muhimu katika mbio za urais wa Kikwete mwaka 2005, ameonekana kumgeuka waziwazi swahiba wake huyo kwa kuanika kile wachunguzi wanaita “udhaifu katika uongozi.”
Ndani ya kipindi cha siku nne, Lowassa ametoa kauli tatu nzito zinazoonyesha dhahiri ameamua kufanya mapambano na Kikwete.
Akiwa ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lowassa alinukuliwa akieleza hatua kwa hatua namna kampuni ya kitapeli ya Richmond Development Company (RDC), ilivyopewa zabuni ya kufua umeme wa dharura nchini.
Lowassa alijiuzulu wadhifa wa waziri mkuu mwaka 2008 kufuatia kashfa ya mkataba wa Richmond, kampuni iliyopewa kwa upendeleo zabuni ya kuzalisha umeme wakati haina fedha, haina uzoefu wala fedha za kufanyia kazi hiyo.
Alikiambia kikao cha NEC mjini Dodoma, “Hakuna jambo nililolifanya ambalo wewe Rais Kikwete hukulifahamu au hukunituma” kuhusu Richmond/Dowans.
Alisema, “…Mwenyekiti, natukanwa kwa ufisadi wa Richmond wakati wewe unafahamu yalichosababisha kashfa ya Richmond ni makosa ya watendaji walio chini yangu? Sasa kosa langu ni lipi? Ni kule kukubali kuwajibika kwa ajili ya serikali yangu na chama chetu? Kwa nini nihukumiwe kwa kosa hilo?”
Huku akimtolea macho Kikwete alisema, “Unakumbuka vema jinsi nilivyotaka kuvunja mkataba ule. Nilikupigia simu ukiwa nje ya nchi, lakini ukasema umepata ushauri wa kamati ya makatibu wakuu, ushauri ambao ulisababisha mkataba usivunjwe?”
Lowassa alisema Kikwete anafahamu kila kitu kwa kuwa ni yeye aliyeridhia Rostam Aziz kutafuta mbia baada ya Richmond kushindwa kuleta umeme.
“Uliponitaka ushauri wa mtu wa kutusaidia ili kuondokana na aibu ya Richmond kushindwa kutimiza mkataba wake, nilipokutajia jina la Rostam, haraka ulikubali na kusema, naona hilo ni sawa,” alieleza Lowassa kwa njia ya kumsuta Kikwete.
Hatua ya Lowassa kumuingiza Kikwete kwenye tope la Richmond/Dowans imezima moja kwa moja kauli yake iliyodai, “Siwajui wala siwafahamu wamiliki wa makampuni ya Dowans Tanzania Ltd na Dowans Holdings SA.”
Akihutubia kwenye maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, tarehe 5 Februari 2011, mjini Dodoma, Kikwete alikana kufahamu wamiliki wa kampuni hiyo na kwamba hajawahi kuwaona wamiliki wake.
Alisema, “Nataka kuuhakikishia umma kwamba, sihusiki na kampuni hii. Siifahamu na wala sijawahi kuwaona wamiliki wake…Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi.”
Kauli ya Kikwete ya kutoitambua Dowans wala wamiliki wake, ilikuwa ni mwendelezo wa kauli kama hizo zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya wasaidizi wake, zikilenga kumuondoa kwenye kashfa hiyo iliyomlazimu kuvunja baraza lake la mawaziri.
Akizungumzia kwa undani jinsi Richmond ilivyoingia na jinsi yeye na Kikwete walivyokuwa kitu kimoja kuhakikisha mkataba unasainiwa na kutekelezwa, Lowassa alisema, “Hakuna jambo nililolifanya ambalo Rais Kikwete hukulifahamu.”
Akizungumzia kwa undani suala hilo kwa mara ya kwanza tangu ajiuzulu wadhifa wa waziri mkuu, Februari 2008, Lowassa alisema, “Mwenyekiti kwanza napongeza uamuzi huu wa kurejesha jambo hili katika taratibu za kawaida, lakini napenda kufahamu kwa miezi saba nimetukanwa nikiitwa fisadi, watu wamezunguka nchi nzima kwa fedha za chama, hivi hatukujua kama kuna kamati hizo za maadili?”
Lowassa alikuwa akichangia pendekezo la Kamati Kuu (CC) ya CCM lililotaka kurejeshwa kwa suala la “kujivua gamba” kwenye vikao vya chini vya chama hicho baada ya watuhumiwa, isipokuwa Rostam Aziz, kukataa kuachia uongozi katika chama.
Kikwete alikiambia kikao cha NEC kuwa, uamuzi wa kutaka jambo hilo lirejeshwe kwenye vikao vya chini, umetokana na “taratibu kukosewa.”
Hata hivyo, kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya chama hicho aliliambia gazeti hili juzi Jumatatu, uamuzi wa Kikwete kulirejesha suala la kujivua gamba kwenye vikao vya chini ulitokana na hofu ya NEC kujaa wajumbe wengi kutoka kwa kundi la Lowassa.
“Unajua mle NEC, Kikwete hana chake. Mle ndani kuna kundi kubwa la Lowassa, ndiyo maana jamaa ameogopa suala hilo la kuvuana magamba lijadiliwe,” ameeleza kiongozi huyo ambaye ni waziri katika serikali ya Rais Kikwete.
Kanuni za CCM zinaeleza kabla ya tuhuma kufikishwa NEC, sharti wale wanaotuhumiwa wapewe haki na fursa ya kujitetea mbele ya vikao vya kamati ya usalama na maadili.
Akifunga mjadala huo kwa angalizo mwanana, Kikwete aliagiza suala hilo lipelekwe kamati ya maadili ambako alitaka kuwasilishwa ushahidi wa vielelezo na siyo hujuma dhidi ya watuhumiwa.
Wakati Lowassa akishusha tuhuma kwa Kikwete, kiongozi huyo wa nchi alionekana kama amepigwa ngazi. Hakukana hata tuhuma moja miongoni mwa yaliyoelezwa na swahiba wake huyo wa zamani.
Kikwete na Lowassa, wamejitambulisha mara kadhaa kuwa ni marafiki, huku mmoja akisisitiza, “Hatukutana barabarani.”
Haijafahamika mahusiano yao yamefikia wapi kwa sasa baada ya Lowassa kumhusisha mwenzake katika kashfa ya Richmond katika kile wachunguzi wanasema amechukua tabia ya “tufe sote au tukose wote.”
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kauli ya Lowassa ambayo ilitolewa mbele ya viongozi wake wakuu, akiwamo rais mstaafu, Benjamin Mkapa, ililenga kuonyesha udhaifu wa Kikwete ndani ya CCM kwa kuasisi falsafa ya kujivua gamba na kuikimbiza moja kwa moja kwenye CC na NEC, kinyume cha taratibu na kanuni za chama chake.
Kama hiyo haitoshi, juzi Jumapili akiwa mkoani Singida alikokwenda kusimamia harambaee ya kuchangia fedha za ujenzi wa kanisa, Lowassa alinukuliwa akisema, “Kwa vyovyote vile, nitaibuka mshindi dhidi ya vita vya kuvuana magamba.”
Akitiwa moyo na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Kati, Ushirika wa Amani, mjini Singida, Eliufoo Sima aliyesema, “suluhu ya mapambano ni kukabiliana nayo,” mwanasiasa huyo alisema, amekuwa akihusishwa na tuhuma ambazo hazina ukweli.
Askofu Sima alisema mapambano katika maisha hayatakwisha na “suluhisho siyo kuyaogopa, isipokuwa kuyatafutia majawabu kwa upole, hekima na utulivu.”
Vita vya magamba viliasisiwa na Kikwete 5 Februari 2011, kabla ya kudakwa na baadhi ya watendaji wa Sekretarieti ya CC ambao kwa miezi saba sasa, wamekuwa wakituhumu Lowassa na wenzake wawili - Rostam Aziz na Andrew Chenge – kuwa mafisadi wanaokidhalilisha chama mbele ya jamii.
Wakati hayo yakiendelea, taarifa kutoka ndani ya CC zinasema kushindwa kwa Rais Kikwete kutekeleza mkakati wake wa kumfukuza Lowassa ndani ya chama chake, kulitokana na upinzani mkali uliotokea kwenye mkutano wa CC.
“Ni kweli kabisa, ndani ya CC, Lowassa alipata uungwaji mkono mkubwa, kiasi ambacho mwenyekiti alilazimika kulipeleka suala hilo NEC. Alipofika NEC na kuona moto umekuwa mkubwa, ndipo alipoamua kuliondoa na kutaka lifanyiwe kazi kwenye vyombo vya chini,” kimeeleza chanzo kimoja cha gazeti hili.
Amesema wajumnbe wa Zanzibar, wakiongozwa na makamu mwenyekiti wa chama hicho visiwani, Amani Abeid Karume, muda wote wa mkutano walisimama imara kuhakikisha Lowassa hafukuzwi kwenye chama.
“Kuna wakati watu kutoka Bara walikuwa wanakaribia kushinda. Lakini baadaye Zanzibar wakapata nguvu pale Karume aliposimama na kusema, shutuma zote hizo hazijafuata taratibu,” ameeleza.



CHANZO: Mwanahalisi

Thursday, 8 December 2011



LEO NI SIKU MUHIMU KWANGU KWANI NINATIMIZA MIAKA KADHAA TANGU NIZALIWE.LAKINI SIKU HII NI MUHIMU PIA KWA TANGANYIKA KWANI NAYO INATIMIZA MIAKA 50 TANGU IZALIWE.


NAMSHUKURU MUNGU KWA MEMA YOTE ALIYONIJALIA,ANAYONIJALIA NA NINAYOAMINI ATAZIDI KUNIJALIA.NAWASHUKURU PIA WAZAZI WANGU-BABA MZEE PHILEMON CHAHALI NA MAREHEMU MAMA ADELINA MAPANGO KWA KUNILETA DUNIANI.LICHA YA KUNIZAA,MALEZI BORA NA MWONGOZO WALIONIPATIA TANGU NIZALIWE UMESAIDIA SANA KUNIFIKISHA HAPA NILIPO LEO.

NAWASHURU PIA NDUGU,JAMAA NA MARAFIKI KWA SAPOTI NA SALAMU ZA HERI KWA SIKU HII MUHIMU.SHUKRANI ZA PEKEE KWA MTU MAALUM ALIYENIPIGIA SIMU LEO SAA 6 KAMILI USIKU (KWA SAA ZA TANZANIA) KUNIPA SALAMU ZA BIRTHDAY.MUDA HUO,MIAKA KADHAA ILIYOPITA NDIO MUDA MAMA ALIKUWA ANAJIFUNGUA MIE (NILIZALIWA SAA 6 USIKU),NA KWA KUKUMBUKA KUNIPIGIA SIMU MUDA HUO KUNIPA HEPI BESDEI NI KAMA UMEMWAKILISHA MAMA AMBAYE KIMWILI HATUPO NAYE JAPO KIROHO YUPO NASI.

NIMALIZIE KWA KUSEMA 
HAPPY BIRTHDAY ME...
HAPPY BIRTHDAY TANGANYIKA




Wednesday, 7 December 2011


Miaka 50 ya Uhuru: Kwa nini bado tu masikini, swali gumu

Evarist Chahali Uskochi

IJUMAA, Desemba 9, mwaka 2011, ni maadhinimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Siku hiyo pia ina umuhimu wa kipekee kwangu kwani nami ninatimiza miaka kadhaa tangu nizaliwe.

Kama ilivyokuwa mwaka jana na miaka mingine iliyopita, huwa ninadhimisha siku yangu ya kazaliwa kwa sala, sambamba na kufanya tafakuri ya kina ya wapi nimetoka, nilipo na ninakoelekea. Si kwamba kwa kutofanya sherehe ninapuuza umuhimu wa siku ya kazaliwa bali ninaamini sala na tafakuri ni namna mwafaka zaidi.

Kwa upande wa nchi yetu, miaka 50 ya uhuru inatimizwa huku wengi wa wananchi wakihoji kama tupo huru kweli. Baadhi wanakwenda mbali na kuona haja ya kuwepo uhuru wa pili kwa maana uhuru wa kwanza ulikuwa kuachana na mkoloni ilhali sasa tunasumbuliwa na ‘mkoloni mwingine’ katika taswira ya ufisadi.

Wakati mkoloni anaweza kujitetea leo kuwa alifanya dhuluma, manyanyaso na wizi wa rasilimali zetu kwa vile hakuwa na uchungu na nchi hii, ni vigumu kwa mafisadi kuwa na sababu yoyote ile zaidi ya ulafi wao na kutokuwa na uchungu kwa nchi yetu na watu wake.

Katika wiki ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wetu, ripoti iliyopatikana mwishoni mwa wiki inaonyesha kuwa Tanzania ni nchi ya tatu duniani kwa kuombaomba misaada na inashika nafasi ya kwanza barani Afrika. Nchi pekee zinazoitangulia Tanzania ni Iraq na Afghanistan ambazo zimegubikwa na vita kwa miaka mingi.

Lakini kinachosikitisha ni kiwango cha misaada ambacho tumekuwa tukipatiwa - dola za Marekani bilioni 2.811 (zaidi ya shilingi trilioni tatu). Unaweza kujiuliza je, fedha hizo zote zinakwenda wapi na kutuacha tukizidi kuwa masikini?

Huhitaji kufanya hesabu kupata jawabu la swali hilo kwani kwa maisha ya anasa wanayoishi viongozi wetu ni wazi kuwa hata tukipewa mara 10 zaidi ya kiwango hicho itakuwa kazi bure.

Taarifa zinaonyesha kuwa takriban asilimia 20 ya fedha hizo za misaada zinatafunwa na mafisadi. Cha kuvunja moyo zaidi, hakuna dalili kwamba wanaguswa na umasikini wetu au kuona umuhimu wa kutumia rasilimali zetu ipasavyo ili tujikwamue.

Na katika kuthibitisha hilo majuzi tumesikia taarifa kwamba posho za wabunge zimeongezwa hadi kufikia shilingi laki tatu kwa siku, japo kwa sasa kuna utata kuhusu taarifa hizo. Nchi ombaomba mkubwa kuliko zote Afrika na wa tatu duniani lakini yenye matumizi ya anasa kuzidi hata hao wanaotumwagia misaada.

Bado napata shida kuelewa kwa nini mataifa tajiri yanayotupatia fedha hizo za misaada hayaonekani kushtushwa na namna sehemu ya fedha hizo inavyoishia mifukoni mwa mafisadi huku walengwa wakiendelea kuwa masikini.

Au ni kwa vile wengi wa mafisadi wanaweka fedha walizotuibia kwenye benki zilizopo katika nchi hizo zinazotusadia na hivyo, kwa namna moja au nyingine zinakuwa kama zimerejeshwa kwao?

Nimetanabaisha hapo juu kuwa hakuna dalili zozote kwamba viongozi wetu wanaguswa na hali mbaya ya nchi yetu kiuchumi. Lakini jambo ambalo linapaswa kutunyima raha ni ukweli kwamba hali ya uchumi wa dunia ni mbaya. Kwa hiyo, iwapo nchi zinazoendelea kutusaidia licha ya fedha zao kutotumiwa ipasavyo zinaweza kulazimika kupunguza misaada yao kwetu ili kukabiliana na matatizo yao binafsi.

Na si kama viongozi wetu hawafahamu kuhusu hilo hasa ikizingatiwa kuwa wamekuwa wakizurura huko na kule kwa kisingizio cha kusaka misaada (kana kwamba balozi zetu zimefungwa). Wanafahamu vema lakini hawajali kwa vile labda hawapo madarakani kwa maslahi ya nchi na wananchi.

Kwa upande mwingine, yayumkinika kuamini kuwa viongozi hao wanaweza kuombea hali ya uchumi wa dunia izidi kuwa mbaya kwani watakuwa na kisingizio. Wasichotaka kuelewa ni ukweli kwamba mtu mwenye njaa hana cha kupoteza. Kwa hiyo, hali ikizidi kuwa mbaya masikini wa Kitanzania wanaweza kudai haki yao kwa nguvu.

Maana haiingii akilini kusikia Serikali ikidai haina uwezo wa kuboresha maslahi ya watumishi wake lakini inamudu kusikiliza vilio vya wabunge wanaopata mamilioni kila mwezi kwenye mishahara na posho zao. Wengi tunakumbuka vizuri hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa kuhusu tishio la mgomo wa wafanyakazi. Moja ya sababu alizotoa ni kwamba Serikali yake haina uwezo wa kulipa kiwango kinachodaiwa na wafanyakazi hao.

Kama sijakosea, wafanyakazi walikuwa wanaiomba Serikali iwapatie shilingi 315,000 kwa mwezi. Lakini kiwango hicho walichoambiwa ni kikubwa mno, ni zaidi kidogo tu ya kiwango kipya ya posho ya mbunge inayoelezwa kufikia shilingi 300,000 kwa siku.

Ni vigumu kubaishiri mambo yatakuwaje huko mbele lakini miongoni mwa yanayoweza kutabirika ni uwezekano wa Serikali kuishiwa uwezo wa kumudu gharama za anasa za viongozi wetu. Sasa sijui wabunge nao watatishia kugoma pindi posho zao nono zikichelewa kutoka au ikalazimika kuzipunguza.

Pengine hali hiyo ikatokea inaweza kusaidia kwa namna fulani kwani Waswahili wanasema msiba wa wengi ni harusi. Pindi wabunge watakapoonja shubiri inayotawala maisha ya kila siku ya walalahoi labda watafunguka macho na kuanza kuhoji kwa makini kwa nini tuwe masikini licha ya utajiri lukuki wa rasilimali tulionao.

Miaka 50 ya uhuru uliogubikwa na umasikini inakabiliwa na tishio jingine la kiusalama. Majuzi, akaunti ya mke wa Rais, Salma Kikwete, kwenye mtandao wa kijamii wa twitter ilikuwa hacked (yaani ‘iliingiliwa na kutumiwa na mtu asiye na mamlaka ya kufanya hivyo). Yaliyoandikwa kwenye ukurasa wa Mama Salma hayaandikiki hapa lakini kwa hakika ilikuwa ni fedheha hasa pale ilipoonekana kana kwamba mke wa Rais anamkejeli mumewe.

Hivi Kurugenzi ya Teknolojia, Habari na Mawasiliamo (Teknohama) huko Idara ya Usalama wa Taifa ilikuwa wapi kwa takriban saa 24 ambazo akaunti ya mke wa Rais iligeuzwa kituko? Na tukio hili la kukera lilijiri wiki chache tu baada ya akaunti mtandao wa kompyuta ya Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu kuhujumiwa (hacked).

Ni kweli kwamba ni vugumu kuzuwia hacking kwa asilimia 100 lakini kinachoweza kufanyika kwa watu makini ni kupunguza madhara ya hujuma hiyo kama sio kuzuwia kabisa.

Hivi kama wahuni wa mtandaoni wanaweza kuihujumu akaunti ya twitter ya mke wa Rais kuna usalama kweli kwenye nyaraka nyingine muhimu kwa usalama wa taifa letu? Hivi upungufu kama huu si ishara kuwa watu tuliowakabidhi majukumu muhimu wanazembea?

Tukio hilo linaweza kuonekana dogo na lisilo na madhara makubwa hasa kwa vile idadi ya Watanzania wanaotumia mtandao si kubwa, lakini kama wasemavyo Waingereza, jambo dogo huwa kubwa pindi likiachiwa uhuru wa kukua.

Wakati baadhi yetu tukiadhimisha miaka 50 ya uhuru wetu kuna wenzetu watakuwa wanapiga hesabu ya fedha walizofanikiwa kuchuma katika kile kinachoitwa “maadhimisho kwenye taasisi mbalimbali za umma.” Mamilioni ya shilingi yametumika kwa sherehe zilizosheheni hotuba zilizoelemea kueleza mafanikio badala ya kuwekea mkazo tathmini ya wapi tumetoka, tulipo na tunapoelekea.

Sawa, siku ya kazaliwa ni muhimu kwa anayeadhimisha lakini umuhimu huo unaweza usiwe na maana kama hautolenga kuhakikisha siku kama hiyo inajiri tena na tena huko mbele ya safari. Kama taifa, tulipaswa kufanya mjadala wa kitaifa kuhusu hatima yetu inayotishiwa kwa kiasi kikubwa na kushamiri kwa ufisadi.

Ingependeza sana kama hotuba ya Rais Kikwete katika maadhimisho ya nusu karne tangu tupate uhuru wetu angalau ijumuishe habari njema kwamba sasa anafahamu kwa nini sie ni masikini (swali ambalo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwahi kujiuliza na hakuwa na jibu).

Hatuwezi kupata tiba ya umasiki wetu kama viongozi wetu hawajui (na hawajihangaishi kujua) kwanini sisi ni masikini licha ya kujaliwa raslimali nyingi.

Ningetamani sana kuona kuwa wakati ninasherehekea siku yangu ya kuzaliwa na nchi yangu inasherehekea miaka 50 ya kuzaliwa kwake, sote tuwe na mengi ya kujivunia tulikotoka na tulipo na pia kuona nuru ya huko mbele tunakoelekea. Kwa bahati mbaya (au kwa makusudi ya baadhi ya watu tuliowakabidhi udereva wa kutufikisha tuendako), safari ya “mwenzangu” Tanzania Bara imetawaliwa na majahili wasiojali kama atafika aendako au ataishia njiani.

Hata hivyo, nimalizie makala yangu kwa kusema HERI YA MIAKA 50 YA KUZALIWA KWA NCHI YANGU (huku nami pia nikijipa heri ya siku ya kuzaliw

Friday, 2 December 2011


Thursday, 1 December 2011


Tatizo kuu CCM si mafisadi pekee, bali hata wanaowalea

Evarist Chahali Uskochi

HATIMAYE mchezo wa kuigiza wa “kujivua gamba” umefikia kikomo. Baadhi yetu tulihisi tangu mwanzo kuwa usanii huo haukuwa tofauti na ahadi tamu zinazosheheni kwenye kila ilani ya uchaguzi inayotumiwa na CCM kuombea kura lakini mwisho wa siku ahadi hizo huishia kuwa porojo tu.

Kuna sababu lukuki kwa baadhi yetu kubashiri kwamba kama CCM itafanikiwa kuvua magamba basi chama hicho kitakuwa katika hatari kubwa ya kupoteza uhai wake. Japo magamba yaliyopaswa kuvuliwa na CCM hayakuwa mithili ya yale ya viumbe hai lakini kimsingi kiuhalisia kung’oa gamba la kiumbe kama kobe kunaweza kabisa kupelekea kifo cha kiumbe huyo. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa chama tawala.

Kwa muda mrefu sasa Chama Cha Mapinduzi kimekuwa tegemezi sana kwa watu wenye fedha pasipo kujali watu hao wamepataje fedha hizo. Yayumkinika kabisa kuhitimisha kuwa hata utaratibu usio rasmi kwamba ili kupata nafasi ya uongozi wa kisiasa nchini-hasa kwenye nafasi za udiwani na ubunge-mgombea anapaswa kuwa na mamilioni ya fedha za kununuliwa kura ni matokeo ya CCM kukumbatia wenye fedha, na hatimaye kupelekea uwezo wa kifedha kuwa kigezo muhimu cha ushindi kwa mgombea kuliko uwezo wake kiuongozi.

Lakini sababu kubwa kabisa iliyotengeneza kifo cha ajenda ya magamba tangu siku ya kwanza ni mwasisi wa wazo hilo, yaani Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete. Japo Watanzania tunasifika kwa usahaulifu lakini naamini wengi wetu tunakumbuka jinsi Rais Kikwete alivyopigana kufa au kupona kuwapigia kampenia na kuwatetea kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita, wanasiasa ambao baadaye waliitwa magamba.

Kikwete alisisitiza kwamba wanasiasa hao ni watuhumiwa tu na hawajafikishwa mbele ya vyombo vya sheria na hivyo hakuona ubaya kusimama majukwaani kuwaombea kura. Alikwenda mbali zaidi na kunadi uadilifu na uongozi wao bora, jambo lililoibua hisia kuwa hakuwa anawasaidia tu kupata kura, bali pia alikuwa anawatengenezea kinga pindi zikitokea jitihada za kuwachukulia hatua.

Ni hivi, laiti watuhumiwa hao wa ufisadi (au magamba) wangefikishwa mahakamani wangeweza kabisa kutumia hotuba za Kikwete kwenye kampeni zao kama utetezi wa tuhuma dhidi yao kwani sote tunajua kuwa kama Rais anaamini watu hao ni safi, basi hakuna hakimu au jaji ambaye angediriki kuwa na mtizamo tofauti.

Kwa lugha nyingine, Kikwete alikuwa akiwapatia watuhumiwa hao wa ufisadi kinga dhidi ya mashtaka ndani na nje ya Mahakama. Na kama wasemavyo Waingereza, hukumu ya umma ina nguvu kubwa zaidi ya hukumu halisi inayotolewa mahakamani. Hapa ninamaanisha kwamba “hukumu ya hawana hatia hadi watiwe hatiani” iliyotolewa hadharani na Kikwete kwa watuhumiwa wa ufisadi ilikuwa na nguvu kubwa kwa umma, hasa katika mazingira ya siasa za umungu-mtu wa Rais.

Kama ambavyo mara kadhaa nimeonyesha kutoelewa anayepaswa kubebeshwa lawama katika baadhi ya maamuzi ya Kikwete ni yeye mwenyewe au washauri wake nilipata tabu kumwelewa alipojipa jukumu la “kuwabeba” watuhumiwa wa ufisadi kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita. Haikuhitaji busara kwa Rais Kikwete kutambua kuwa wanasiasa hao waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi hawakuamka tu ghafla na kujikuta wanatuhumiwa bali kulikuwa na mlolongo wa matukio uliowaingia katika tuhuma hizo.

Angeweza kabisa kuepuka hali ya kuonekana anawatetea na laiti busara zingetumika basi angewaachia jukumu la kuomba kura na kujisafisha kwa umma mikononi mwao. Ndiyo maana miezi michache baadaye alipokurupuka na ajenda ya kuwashughulikia watu hao hao aliowasafisha majukwaani ilikuwa ni dhahiri kuwa usanii huo usingezaa lolote la maana.

Lakini kuna kubwa zaidi lililojiri katika vikao vya CCM vilivyomalizika wiki iliyopita mjini Dodoma. Kwa mujibu wa vyombo vya habari, mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi aliweka bayana jinsi Kikwete alivyofanya maamuzi ambayo hatimaye yalisababisha mwanasiasa huyo kuishia kuwa mtuhumiwa wa ufisadi. Kwa lugha nyingine, mwanasiasa huyo alikubali kubebeshwa mzigo wa lawama ambao kimsingi ulipaswa kubebwa na Kikwete.

Wakati usanii wa kujivua magamba unashika kasi kwenye vyombo vya habari kulizuka msamiati mpya wa “mapacha watatu” ambao ulimaanisha wanasiasa watatu waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi na ambao kimsingi ndio walikuwa walengwa wakuu wa ajenda ya kujivua gamba. Wanasiasa hao ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Mbunge wa zamani wa Igunga, Rostam Aziz na Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge.

Kwa wanaofuatilia kwa karibu harakati za Rais Kikwete tangu aliposhindwa kwenye mchujo wa kupata mgombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka 1985 hadi alipofanikiwa kuingia Ikulu mwaka 1995 ni wazi kuwa “mapacha watatu halisi” ni Kikwete, Lowassa na Rostam ambao kwa pamoja, waliweza kutengeneza mtandao wenye nguvu kubwa uliompa ushindi Kikwete.

Sasa katika mazingira ya kawaida tu, ingewezekanaje Kikwete ambaye kimsingi ndiye mwenye maamuzi ya mwisho ndani ya CCM awasaliti “mapacha wenzie” Lowassa na Rostam? Naomba ieleweke simaanishi kuwa angetaka kwa dhati kufanya hivyo asingeweza.

Nimesema “mazingira ya kawaida” kwa maana ya Kikwete tunayemfahamu sote: mwanasiasa anayeonekana kukumbuka sana fadhila alizofanyiwa na watu waliomsaidia kuingia Ikulu na kiongozi ambaye anachelea sana kuwaadhibu watendaji wake hata pale ambapo kuchelea huko kunaishia kumfanya aonekane kiongozi dhaifu na mwoga wa kuchukua maamuzi magumu.

Laiti Kikwete angetaka “liwalo na liwe” dhidi ya maswahiba zake ambao baadaye alionelea wanapaswa kuchukuliwa hatua ili kuinusuru CCM basi angeweza kabisa kuitumia Idara ya Usalama wa Taifa “kuwaandama” wanasiasa hao kwa minajili ya kuwadhibiti “wasimgeuke au kumdhuru.” Kama ambavyo taarifa za kiintelijensia zinavyosukuma haki za kikatiba za wananchi kuandamana kufinyangwa, basi ingewezekana kabisa kutumia mbinu hiyo kuhakikisha kuwa “magamba yakishang’olewa hayachipui tena.”

Na wala usidhani kwamba kungekuwa na haja ya matumizi ya “mbinu chafu” kuyadhibiti “magamba” bali wahusika wangeweza kukumbushwa “Rais ni nani” kwa njia nyepesi tu ya kile kinachofahamika kama ufuatiliaji wa waziwazi (overt surveillance).

Hii ni mbinu inayotumika kumfikishia ujumbe mlengwa kuwa anafuatiliwa, wafuatiliaji hawajihangaishi kujificha bali wanataka anayefuatiliwa afahamu kuwa anafuatiliwa na hivyo kumdhibiti kufanya jambo lolote lile “baya.”

Kwa hiyo laiti mwasisi wa wazo la kujivua magamba-Rais Kikwete angekuwa na dhamira ya kweli ya kutaka mkakati huo ufanikiwe basi wala kusingekuwa na haja ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kupita huku na kule akiwahadaa Watanzania kuhusu umakini wa suala hilo.

Sina hakika kama Nape alikuwa anafahamu “ngoma aliyokuwa anaicheza” lakini kilicho dhahiri ni kwamba muda huu anatambua kuwa “hakuna mwenye uwezo au uthubutu wa kumtenganisha Kikwete na watu ambao hakufahamiana nao mtaani (bali wametoka mbali pamoja).”

Lakini kifo cha usanii wa “kujivua magamba” kinaweza kutoa fundisho kwa CCM kuacha mtindo wa kudandia hoja za vyama vya upinzani hususan CHADEMA. Wenye kumbukumbu nzuri watakuwa wanafahamu jinsi CCM ilivyopinga kwa nguvu zote madai ya CHADEMA kuwa chama hicho tawala si tu kinakumbatia mafisadi bali pia kimegeuka kuwa kichaka cha kuwahifadhi mafisadi.

Sasa baada ya kuona kuwa CHADEMA inapata umaarufu mkubwa kutokana na msimamo wake thabiti dhidi ya ufisadi, CCM nayo ikakurupuka na ajenda ya kusaka umaarufu ikisingizia inataka kujisafisha. Lakini hata kama chama hicho tawala kungekuwa na dhamira ya dhati kutekeleza mpango huo ingewawia vigumu kufanikiwa kwa sababu ufisadi na CCM ni kama samaki na maji; ukimtoa samaki majini umemuuwa na ukiwaondoa mafisadi CCM basi umeua chama.

Nimalizie makala hii kwa ushauri wa bure kwa chama tawala. Tatizo la msingi si magamba bali aliyeyawezesha magamba hayo kukomaa. Kama ambavyo ni vigumu kudhibiti malaria kwa kugawa vyandarua na dawa za kukinga au kutibu ugonjwa huo pasipo kuangamiza mazalia ya mbu, ndivyo ambavyo ni vigumu kwa CCM kupambana na mafisadi pasipo kuwabana viongozi ambao si tu wapo madarakani kwa msaada wa mafisadi bali pia uhai wao wa kisiasa umewekwa rehani kwa mafisadi hao.

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget