Miaka 50 ya Uhuru: Kwa nini bado tu masikini, swali gumu
Evarist Chahali Uskochi
IJUMAA, Desemba 9, mwaka 2011, ni maadhinimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Siku hiyo pia ina umuhimu wa kipekee kwangu kwani nami ninatimiza miaka kadhaa tangu nizaliwe.
Kama ilivyokuwa mwaka jana na miaka mingine iliyopita, huwa ninadhimisha siku yangu ya kazaliwa kwa sala, sambamba na kufanya tafakuri ya kina ya wapi nimetoka, nilipo na ninakoelekea. Si kwamba kwa kutofanya sherehe ninapuuza umuhimu wa siku ya kazaliwa bali ninaamini sala na tafakuri ni namna mwafaka zaidi.
Kwa upande wa nchi yetu, miaka 50 ya uhuru inatimizwa huku wengi wa wananchi wakihoji kama tupo huru kweli. Baadhi wanakwenda mbali na kuona haja ya kuwepo uhuru wa pili kwa maana uhuru wa kwanza ulikuwa kuachana na mkoloni ilhali sasa tunasumbuliwa na ‘mkoloni mwingine’ katika taswira ya ufisadi.
Wakati mkoloni anaweza kujitetea leo kuwa alifanya dhuluma, manyanyaso na wizi wa rasilimali zetu kwa vile hakuwa na uchungu na nchi hii, ni vigumu kwa mafisadi kuwa na sababu yoyote ile zaidi ya ulafi wao na kutokuwa na uchungu kwa nchi yetu na watu wake.
Katika wiki ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wetu, ripoti iliyopatikana mwishoni mwa wiki inaonyesha kuwa Tanzania ni nchi ya tatu duniani kwa kuombaomba misaada na inashika nafasi ya kwanza barani Afrika. Nchi pekee zinazoitangulia Tanzania ni Iraq na Afghanistan ambazo zimegubikwa na vita kwa miaka mingi.
Lakini kinachosikitisha ni kiwango cha misaada ambacho tumekuwa tukipatiwa - dola za Marekani bilioni 2.811 (zaidi ya shilingi trilioni tatu). Unaweza kujiuliza je, fedha hizo zote zinakwenda wapi na kutuacha tukizidi kuwa masikini?
Huhitaji kufanya hesabu kupata jawabu la swali hilo kwani kwa maisha ya anasa wanayoishi viongozi wetu ni wazi kuwa hata tukipewa mara 10 zaidi ya kiwango hicho itakuwa kazi bure.
Taarifa zinaonyesha kuwa takriban asilimia 20 ya fedha hizo za misaada zinatafunwa na mafisadi. Cha kuvunja moyo zaidi, hakuna dalili kwamba wanaguswa na umasikini wetu au kuona umuhimu wa kutumia rasilimali zetu ipasavyo ili tujikwamue.
Na katika kuthibitisha hilo majuzi tumesikia taarifa kwamba posho za wabunge zimeongezwa hadi kufikia shilingi laki tatu kwa siku, japo kwa sasa kuna utata kuhusu taarifa hizo. Nchi ombaomba mkubwa kuliko zote Afrika na wa tatu duniani lakini yenye matumizi ya anasa kuzidi hata hao wanaotumwagia misaada.
Bado napata shida kuelewa kwa nini mataifa tajiri yanayotupatia fedha hizo za misaada hayaonekani kushtushwa na namna sehemu ya fedha hizo inavyoishia mifukoni mwa mafisadi huku walengwa wakiendelea kuwa masikini.
Au ni kwa vile wengi wa mafisadi wanaweka fedha walizotuibia kwenye benki zilizopo katika nchi hizo zinazotusadia na hivyo, kwa namna moja au nyingine zinakuwa kama zimerejeshwa kwao?
Nimetanabaisha hapo juu kuwa hakuna dalili zozote kwamba viongozi wetu wanaguswa na hali mbaya ya nchi yetu kiuchumi. Lakini jambo ambalo linapaswa kutunyima raha ni ukweli kwamba hali ya uchumi wa dunia ni mbaya. Kwa hiyo, iwapo nchi zinazoendelea kutusaidia licha ya fedha zao kutotumiwa ipasavyo zinaweza kulazimika kupunguza misaada yao kwetu ili kukabiliana na matatizo yao binafsi.
Na si kama viongozi wetu hawafahamu kuhusu hilo hasa ikizingatiwa kuwa wamekuwa wakizurura huko na kule kwa kisingizio cha kusaka misaada (kana kwamba balozi zetu zimefungwa). Wanafahamu vema lakini hawajali kwa vile labda hawapo madarakani kwa maslahi ya nchi na wananchi.
Kwa upande mwingine, yayumkinika kuamini kuwa viongozi hao wanaweza kuombea hali ya uchumi wa dunia izidi kuwa mbaya kwani watakuwa na kisingizio. Wasichotaka kuelewa ni ukweli kwamba mtu mwenye njaa hana cha kupoteza. Kwa hiyo, hali ikizidi kuwa mbaya masikini wa Kitanzania wanaweza kudai haki yao kwa nguvu.
Maana haiingii akilini kusikia Serikali ikidai haina uwezo wa kuboresha maslahi ya watumishi wake lakini inamudu kusikiliza vilio vya wabunge wanaopata mamilioni kila mwezi kwenye mishahara na posho zao. Wengi tunakumbuka vizuri hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa kuhusu tishio la mgomo wa wafanyakazi. Moja ya sababu alizotoa ni kwamba Serikali yake haina uwezo wa kulipa kiwango kinachodaiwa na wafanyakazi hao.
Kama sijakosea, wafanyakazi walikuwa wanaiomba Serikali iwapatie shilingi 315,000 kwa mwezi. Lakini kiwango hicho walichoambiwa ni kikubwa mno, ni zaidi kidogo tu ya kiwango kipya ya posho ya mbunge inayoelezwa kufikia shilingi 300,000 kwa siku.
Ni vigumu kubaishiri mambo yatakuwaje huko mbele lakini miongoni mwa yanayoweza kutabirika ni uwezekano wa Serikali kuishiwa uwezo wa kumudu gharama za anasa za viongozi wetu. Sasa sijui wabunge nao watatishia kugoma pindi posho zao nono zikichelewa kutoka au ikalazimika kuzipunguza.
Pengine hali hiyo ikatokea inaweza kusaidia kwa namna fulani kwani Waswahili wanasema msiba wa wengi ni harusi. Pindi wabunge watakapoonja shubiri inayotawala maisha ya kila siku ya walalahoi labda watafunguka macho na kuanza kuhoji kwa makini kwa nini tuwe masikini licha ya utajiri lukuki wa rasilimali tulionao.
Miaka 50 ya uhuru uliogubikwa na umasikini inakabiliwa na tishio jingine la kiusalama. Majuzi, akaunti ya mke wa Rais, Salma Kikwete, kwenye mtandao wa kijamii wa twitter ilikuwa hacked (yaani ‘iliingiliwa na kutumiwa na mtu asiye na mamlaka ya kufanya hivyo). Yaliyoandikwa kwenye ukurasa wa Mama Salma hayaandikiki hapa lakini kwa hakika ilikuwa ni fedheha hasa pale ilipoonekana kana kwamba mke wa Rais anamkejeli mumewe.
Hivi Kurugenzi ya Teknolojia, Habari na Mawasiliamo (Teknohama) huko Idara ya Usalama wa Taifa ilikuwa wapi kwa takriban saa 24 ambazo akaunti ya mke wa Rais iligeuzwa kituko? Na tukio hili la kukera lilijiri wiki chache tu baada ya akaunti mtandao wa kompyuta ya Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu kuhujumiwa (hacked).
Ni kweli kwamba ni vugumu kuzuwia hacking kwa asilimia 100 lakini kinachoweza kufanyika kwa watu makini ni kupunguza madhara ya hujuma hiyo kama sio kuzuwia kabisa.
Hivi kama wahuni wa mtandaoni wanaweza kuihujumu akaunti ya twitter ya mke wa Rais kuna usalama kweli kwenye nyaraka nyingine muhimu kwa usalama wa taifa letu? Hivi upungufu kama huu si ishara kuwa watu tuliowakabidhi majukumu muhimu wanazembea?
Tukio hilo linaweza kuonekana dogo na lisilo na madhara makubwa hasa kwa vile idadi ya Watanzania wanaotumia mtandao si kubwa, lakini kama wasemavyo Waingereza, jambo dogo huwa kubwa pindi likiachiwa uhuru wa kukua.
Wakati baadhi yetu tukiadhimisha miaka 50 ya uhuru wetu kuna wenzetu watakuwa wanapiga hesabu ya fedha walizofanikiwa kuchuma katika kile kinachoitwa “maadhimisho kwenye taasisi mbalimbali za umma.” Mamilioni ya shilingi yametumika kwa sherehe zilizosheheni hotuba zilizoelemea kueleza mafanikio badala ya kuwekea mkazo tathmini ya wapi tumetoka, tulipo na tunapoelekea.
Sawa, siku ya kazaliwa ni muhimu kwa anayeadhimisha lakini umuhimu huo unaweza usiwe na maana kama hautolenga kuhakikisha siku kama hiyo inajiri tena na tena huko mbele ya safari. Kama taifa, tulipaswa kufanya mjadala wa kitaifa kuhusu hatima yetu inayotishiwa kwa kiasi kikubwa na kushamiri kwa ufisadi.
Ingependeza sana kama hotuba ya Rais Kikwete katika maadhimisho ya nusu karne tangu tupate uhuru wetu angalau ijumuishe habari njema kwamba sasa anafahamu kwa nini sie ni masikini (swali ambalo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwahi kujiuliza na hakuwa na jibu).
Hatuwezi kupata tiba ya umasiki wetu kama viongozi wetu hawajui (na hawajihangaishi kujua) kwanini sisi ni masikini licha ya kujaliwa raslimali nyingi.
Ningetamani sana kuona kuwa wakati ninasherehekea siku yangu ya kuzaliwa na nchi yangu inasherehekea miaka 50 ya kuzaliwa kwake, sote tuwe na mengi ya kujivunia tulikotoka na tulipo na pia kuona nuru ya huko mbele tunakoelekea. Kwa bahati mbaya (au kwa makusudi ya baadhi ya watu tuliowakabidhi udereva wa kutufikisha tuendako), safari ya “mwenzangu” Tanzania Bara imetawaliwa na majahili wasiojali kama atafika aendako au ataishia njiani.
Hata hivyo, nimalizie makala yangu kwa kusema HERI YA MIAKA 50 YA KUZALIWA KWA NCHI YANGU (huku nami pia nikijipa heri ya siku ya kuzaliw
0 comments:
Post a Comment