Thursday, 16 November 2006

KULIKONI UGHAIBUNI-37

Asalam aleykum,

Miongoni mwa mambo ambayo taasisi nyingi za huku ughaibuni zinajitahidi sana kuwa nayo ni hadhi na imani za wananchi kwa taasisi hizo.Na sehemu nzuri ya kuangalia hilo nalozungumzia ni kwenye taasisi za fedha.Kwa hapa Uingereza na nchi nyingine za Magharibi,wateja wa taasisi flani huwa ni kama wameweka “mikataba” na taasisi hizo. Usishangae ukisikia kuwa katika familia flani,tangu enzi za mababu wao wamekuwa wateja wa benki flani,kwa mfano.Na kinachowafanya waing’ang’anie benki hiyo ni jinsi inavyowathamini wao kama wateja na pengine hadhi ambayo benki hiyo imejijengea kwa jamii.Na ili kujenga hadhi hiyo na kuilinda taasisi husika inapaswa kufanya bidii kweli kwa vile kwa kiasi kikubwa hapa watu hawataki usumbufu usio wa lazima.Pia ushindani uliopo kati ya taasisi za kibiashara ni mkali sana,uzembe kidogo tu basi wateja “wanaingia mitini.”

Kwa huko nyumbani hali ni tofauti kwa kiasi kikubwa.Utasikia taasisi flani inatangaza kwamba mteja kwao ni mfalme lakini unaweza kujuta ukitia mguu kwenye majengo ya taasisi hiyo.Na si ajabu ukaishia kudhani kuwa tangazo uliloliona au kulisikia kuhusu taasisi hiyo ikidai kuwa mteja kwao ni mfalme (na pengine malkia) halikuwa tangazo lao.Kuna watumishi wanakuwa wamejisahau kabisa kwamba wanaweza kukosa mishahara pindi hao wateja wanaowadharau wakiwasusa.Pengine wanachoringia ni ukweli kwamba bado kuna ushindani dhaifu kwenye sekta mbalimbali huko nyumbani.Na siku wenye kujua namna ya kuendesha ushindani watakapoamua “kufanya kweli” basi haitoshangaza pale walio wababaishaji wakajiengua wenyewe.Mwaka juzi wakati narinyuu (hivi neno la Kiswahili ni nini hapo…) mkataba wa kiselula changu nilishangaa nilipokabidhiwa DVD Player na DVDs tatu (vyote vya bure) pamoja na simu mpya ya chaguo langu.Japokuwa kampuni iliyotoa zawadi hizo ilikuwa na uhakika wa kurejesha faida yake kadri ntakavyokuwa kwenye mkataba nao,sio siri kwamba nafsi yangu “ilisuuzika” sana.Wanafanya hivyo kwa vile wanafahamu kuwa kuna ushindani sana kwenye biashara ya viselula,na pindi ukimpoteza mteja basi ni vigumu sana kumrejesha.

Moja ya taasisi za huko nyumbani ambazo kwa hakika inaweza kuwa kielelezo kizuri cha mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa taasisi za umma ni benki ya CRDB.Zamani ilikuwa inaitwa Benki ya Maendeleo Vijijini lakini baadae ikajitengeneza vema,ikakaribisha watu kununua hisa na sasa benki hiyo inafanya kile ambacho Watanzania wengi wangependa kukiona kwenye taasisi nyingine zilizotolewa kutoka kwenye milki ya serikali pekee.Na miongoni mwa mafanikio makubwa ya huduma za benki hiyo ni ile ya akaunti iitwayo “Tanzanite.”Akaunti hiyo imewalenga zaidi Watanzania walio nje ya nchi ambao wangependa kujiwekea fedha zao kwenye benki ya huko nyumbani.Naomba kukiri kuwa mwanzoni nilihisi kuwa huduma hiyo isingekuwa na mafanikio sana,hasa kwa vile huduma zinazovuka mipaka ya nchi zinahitaji uangalifu na umakini mkubwa.Lakini CRDB wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuishi kulingana na matarajio ya wateja wao.

Binafsi nimekuwa nikiitumia huduma hii kwa takribani mwaka mzima sasa.Lakini mabadiliko yaliyofanya hivi karibuni yamezidi kunifanya nijiskie “mteja ni mfalme” kwa benki hiyo.Na hapa nadhani nimtaje Meneja mpya wa Uhusiano wa huduma ya Tanzanite aitwaye Jenipher Tondi.Kwa hakika anajituma sana kwa namna ambavyo anashughulikia masuala yanayohusu wateja wa Tanzanite Accounts.Unajua mawasiliano kati ya huduma ya Tanzanite na mteja aliye nje ya nchi yanategemea zaidi barua pepe.Na kama ilivyo kwenye huduma ambazo mawasiliano yanategemea simu,kauli na lugha za mtoa huduma kwa mteja ni kitu chenye umuhimu mkubwa sana.Ukisoma barua pepe kutoka kwa Meneja Tondi kuja kwa mteja unagundua kwa hakika kuwa yeye na benki yake wanakuthamini wewe mteja kwa hali ya juu kabisa.Na pia kasi ya kushughulikia matatizo ya wateja ni kubwa na haikuachi mteja unaomba dua lini utajibiwa au kutatuliwa matatizo yako.Majuzi kadi yangu mpya ya TemboVisa ilinasa kwenye ATM wakati nataka kuangalia balansi ya akaunti yangu.Nikaandika barua pepe kwa CRDB na baada ya muda mfupi tu nikapata majibu kutoka kwa Meneja huyo wa Tanzanite,majibu ambayo licha ya kunipatia ufumbuzi yaliniacha nikiwa nimeridhishwa na jinsi suala langu lilivyoshughulikiwa.Msomaji mpendwa usije ukadhani “nimepewa kidogodogo” (bakshish) kuipigia debe CRDB au Meneja Jenipher,bali ukweli ni kwamba kwa jinsi tunavyoona huduma zinavyotolewa na taasisi nyingi za huku ughaibuni (ukilinganisha na nyingi za huko nyumbani) nitakuwa mchoyo wa shukrani kama sintatoa pongezi kwa benki hiyo.Pongezi hizo zinapaswa kuwa changamoto kwa taasisi nyingine,za umma na za binafsi,kwamba porojo za mteja ni mfalme au malkia hazina maana iwapo mteja huyo anapofika mahala husika ili apatiwe huduma anabaini kuwa badala ya ufalme/umalkia alioahidiwa anaishia kuwa mtumwa (na inauma zaidi unapokuwa mtumwa sehemu ulohifadhi fedha yako mwenyewe).

Kwa mtazamo wangu,wasiwasi wa walio wengi kuhusu ubinafsishaji wa taasisi za umma unatokana zaidi na utendaji wa taasisi hizo baada ya kubinafsishwa na sio kwa vile tu zimebinafsishwa.Hakuna mtu anayejali kama kampuni inaendeshwa na Mpakistani au Mchina badala ya Mtanzania alimradi huduma inayotolewa ni bora kuliko ile ya awali.TBL imekuwa ikitolewa mfano mara kadhaa kuwa ni “success story” ya zoezi la ubinafsishaji.Hilo halina mjadala hata kama TBL iko chini ya Wasauzi Afrika.CRDB iko chini ya uongozi wa Mtanzania,Dr Kimei,na naamini mafaniko yake yamechangiwa na taasisi hiyo kutambua wajibu wake kwa wateja na Taifa kwa ujumla.Tunaweza kabisa kuwa na akina Dr Kimei au Jenipher Tondi wengine kwenye taasisi zetu nyingine iwapo taasisi hizo zitapotekeleza kwa dhati kauli mbiu zao za mteja ni mfalme/malkia.Kwa nyie mnaosuasua kutoa huduma kwa umma mtambue kuwa kuna siku mtajutia nafasi mlizonazo sasa ambapo bado wateja wenu wanaendelea kuwaamini licha ya usumbufu mnaowapatia.Siku watakapowakimbia hamtawaona tena kwenye majengo yenu.Kaulimbiu ya Kikwete na serikali yake ya Awamu ya Nne kuhusu “Maisha Bora kwa kila Mtanzania yanawezekana” inawahusu nanyi pia hasa kwa vile wateja wenu ndio wanawezesha maisha ya taasisi zenu kuwa bora.Kwa mantiki hiyo ni lazima nanyi myafanye yao kuwa bora kwa kuwahudumia kwa nguvu zenu zote.

Alamsiki

Kwa makala zilizopita,tembelea http://chahali.blogspot.com na http://chahali.livejournal.com

Monday, 13 November 2006

KULIKONI UGHAIBUNI:

Asalam aleykum,

Kwanza nitoe salamu zangu za rambirambi kwa familia ya dereva wa daladala aliyeuawa kwa kupigwa risasi na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Braza Dito.Ni matarajio yetu wengi kuwa sheria itachukua mkondo wake na haki itatendeka,na kwa wakati huu inatupasa tuiachie mahakama ifanye kazi yake bila kuingiliwa.

Wakati naandaa makala hii wananchi wa Marekani wanapiga kura katika uchaguzi wa kati ya muhula (mid-term) ambao unaotazamiwa kutoa hukumu kwa Rais George W Bush kuhusu sera zake za Irak.Pamoja na kwamba kuna mambo mengine ambayo wapiga kura wanayaangalia kwa makini lakini sio siri kwamba vita ya Irak ndio imekuwa ajenda kubwa zaidi.Uchaguzi huu unanikumbusha jambo moja lililowahi kujitokeza katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2004 ambapo Rais Bush alirejea tena madarakani.Wakati wa kampeni za uchaguzi huo ilijitokeza ishu ya binti ya Makamu wa Rais Dick Cheney aitwaye Mary ambaye (ashakum si matusi) ni msagaji (lesbian).Ilikuwa inafahamika bayana kuwa Cheney kama mhafidhina haafiki mapenzi au ndoa ya watu wa jinsia moja,lakini mwanae ndio hivyo tena.Pengine ni kwa vile tu chama cha makamu huyo wa Rais (Republicans) ni wajanja wa kuzima ishu zenye utata ndio maana suala hilo liliweza kudhibitiwa “kiaina” ili lisiathiri kampeni za Bush na Cheney na chama chao.Nimetoa mfano huo kuonyesha jinsi gani familia ya kiongozi ilivyo muhimu katika suala zima la uongozi na taswira anayotoa kwa anaowaongoza.

Mwaka 2002 nilibahatika kukutana na mtoto mmoja wa marehemu Baba wa Taifa.Huyu bwana anaitwa Makongoro Nyerere.Ndiye aliyenipokea mie na wenzangu tulipofika hapa kwa mara ya kwanza.Kwa vile kabla ya hapo nilikuwa sijawahi kukutana na mtoto wa Rais aliyestaafu au aliye madarakani basi nilikuwa na hisia kwamba huyu jamaa atakuwa kile watoto wa mjini wanaita “pozi” (pengine kwa Kiswahili kizuri tuite dharau,kujiskia au maringo).Lakini Makongoro alikuwa mtu tofauti kabisa.Yaani kwa “lugha ya mama” (Kiingereza) tungeweza kumwita “a down-to-earth person”,hakuwa na maringo,kujiskia au dharau bali alinichukulia mimi na jamaa zangu kama watu tunaotoka katika familia moja.Sintamsahau huyu bwana.Lakini nikapata bahati nyingine ya kuishi na mtu aliyetokea kuwa rafiki yangu wa karibu hadi kesho anaitwa Eustace,mtoto wa jaji flani mwandamizi huko nyumbani,na ambaye kabla hatujakutana hapa Uingereza alishawahi kukaa sana huku ughaibuni.Sasa kwa mazowea yetu,mara nyingi watu wa aina hiyo huwa ni wa kujiskia na wasioelewa namna ya kuishi na sie tuliokulia katika maisha ya kawaida.Lakini huyu rafiki yangu (mwenyewe atakuwa anacheka akisoma haya nayoandika,maana ni “muumini” wa safu hii na gazeti hili) alinithibitishia tena kuwa kutoka katika familia ya kigogo hakumzuii mtu kuwa wa kawaida.Niseme hivi,huyu jamaa kama sio ule mwonekano wake kuwa anatoka familia yenye neema huwezi kabisa kumdhania kuwa ni mtoto wa kigogo kwa vile ni “mtu wa kujichanganya” sana na hajitofautishi na mtu yoyote yule ukilinganisha na wengine ambao pengine hawako hata “levo” moja na familia anayotoka yeye.

Wikiendi iliyopita nilialikwa kwenye “bethdei pati” ya rafiki yangu mmoja anayeishi huko Salford,Greater Manchester.Kabla ya kuamua niende au la,nilidadisi kuhusu waalikwa wengine kwenye pati hiyo.Nikaambiwa miongoni mwao ni mtoto wa Jakaya aitwaye Ridhwani.Nikajikuta nimerudi kulekule kwenye mawazo nilokuwa nayo kabla sijamfahamu Makongoro au rafiki yangu mtoto wa Jaji mwandamizi.Unajua tena,sherehe ikiwa na baadhi ya wahudhuriaji ambao ni watu wenye majina au wale wenye kujiskia au wenye maringo basi inakuwa kama karaha vile kwa sie tuliozowea “maisha ya chinichini” au kwa kimombo “low profile”.Niite mwoga lakini naamini wengi wetu tuliotoka familia za kawaida huwa hatujiamini sana tukiskia kuwa kuna mjumuiko na watu kama viongozi wa juu serikalini au watoto wao.

Nikapiga moyo konde na kuamua liwalo na liwe,naenda kwenye pati.Mimi niliwasili sehemu ya sherehe kabla ya Ridhwani kwa hiyo nilikuwa na fursa nzuri ya kumwelewa ni mtu wa namna gani pindi atakapowasili.Kwani kama isingekuwa kufanana kwake na JK ningeweza kumdhania kuwa huyu ndio mtoto wa Rais wetu?Alipoingia hapo kwenye sherehe alitusalimia wote kwa namna ileile ambavyo marafiki mtaani wanasalimiana,kwa heshima,taadhima na furaha tele bila hata chembe ya kuonyesha yeye ni mtoto wa mtawala na sie ni watu wa kawaida tu.Baadae nilipata fursa ya kuongea nae kwa kirefu kiasi na sikumficha jinsi “nilivyozimia” anavyoweza kutojionyesha kuwa yeye ni mtoto wa Rais (kwa taarifa yako,watoto wengi wa vigogo wanasumbua sana huku na hawapendi “kujichanganya” na watu wa kawaida,na hiyo sio kwa watoto wa vigogo wa Tanzania pekee bali hata wa sehemu nyingine duniani ikiwa ni pamoja na wale wa Ughaibuni).Yeye akaniambia kuwa amelelewa katika maisha ya kawaida,ya Kitanzania na ya Kiafrika halisi kwamba kutoka katika familia iliyo juu kabisa hakumfanyi ajione kuwa yuko tofauti na watu wengine.Na nisiseme kuwa labda ni mie pekee niliyepewa upendeleo huo wa kuwa karibu na “JK Junior” bali kila mtu aliyekuwepo pale.Na pia sio mimi pekee niliyependezwa na tabia ya mtoto wa Rais wetu bali kila niliyeongea nae alionekana kukunwa na hilo.Jamaa mmoja ambaye yuko chuo kimoja na Ridhwani alinambia kuwa inawezekana kabisa huyu bwana akawa (kwa kimombo) “the most down-to-earth son of a president in the entire world.” (yaani mtoto wa Rais aliye “wa kawaida” zaidi kulinganisha na watoto wa marais wengine duniani)..

Wengi wetu tunafahamu jinsi watu wanavyopenda wawe “wenye majina” ndio maana niliwahi kuambiwa kuwa kwenye baadhi ya kumbi za starehe huko nyumbani kuna baadhi ya watu wanatoa fedha kwa DJ au “rapa” wa bendi atangaze kwamba “flani tuko naye hapa” (lugha wanayotumia wenyewe ni kama “papaa nanihii yuko ndani ya nyumba”…kwa lafudhi ya Kikongo).Na pia niliwahi kudokezwa kwamba baadhi ya wanamuziki huzawadiwa ili wataje majina ya watu flani kwenye tungo zao.Na imewasaidia,kwa vile baadhi ya watu “wenye majina” tumewafahamu kupitia kwenye rapu za kina Ally Choki,Muumini au Banza Stone.Sasa ukikutana na mtu ambaye hahitaji hata kutajwa kwenye nyimbo ili jina lake lijulikane kwa vile tayari jina lake liko juu,halafu yeye anajiweka kuwa mtu wa kawaida kabisa,nadhani itakuwa ni dhambi kutomsifia.Na ndio maana makala yangu ya leo imemlenga Bwana Ridhwani Kikwete.Si tu kwamba tabia yake inamfanya apendeke bali pia inatusaidia wengine kuijua familia ya JK.Na kama nilivyosema hapo awali,familia ya kiongozi ni sehemu muhimu ya uongozi wake na inatoa taswira flani kwa wananchi wake.

Alamsiki

Tembelea http://chahali.blogspot.com na http://chahali.livejournal.com kwa makala za zilizopita.

KULIKONI UGHAIBUNI-35:


Asalam aleykum,

Waziri Mkuu Tony Blair anatarajiwa kung’atuka mwakani.Ataondoka huku Waingereza wengi wakimwona kama kiongozi ambaye anapaswa kuingia katika vitabu vya historia kwa mambo mbalimbali,mazuri na mabaya.Pengine baya zaidi ni jinsi ambavyo wengi wanamwona kama kibaraka wa George W. Bush.Hata hivyo,wapinzani wa Blair wanakubali bila ubishi kwamba huyu Bwana akipewa fursa ya kujieleza huwa hafanyi makosa.Ukubaliane nae au upingane nae bado atasimamia hoja yake na kuielezea kwa umakini sana kiasi kwamba hata asieafikiana nae anaweza kukubali yaishe kwa kukubaliana kistaarabu kutokubaliana nae.Na kwa kiasi kikubwa ndio siasa za hawa wenzetu zilivyo.Hoja inawekwa mezani,inajadiliwa kiutu-uzima,mwafaka ukipatikana inakuwa poa.Mwafaka usipopatikana watu wanakubaliana kwamba hawajaafikiana na kutafuta namna nyingine ya kutatua linalojadiliwa.Mambo ya kuzibana mdomo ni adimu sana katika siasa za hapa.

Nimesoma gazeti moja la huko nyumbani lililobeba habari kwamba Waziri Mkuu Edward Lowassa anajaribu kuwaziba midomo wabunge wa CCM wasilishupalie suala la mgao wa umeme kwenye kikao cha bunge.Naomba kwanza nimjadili Mheshimiwa Lowassa kwa marefu na mapana.Moja ya mambo ambayo yanawafanya baadhi yetu tusimwelewe Waziri Mkuu wetu ni tabia yake ya kuwaumbua watendaji wake hadharani.Wapo wanaoona vitendo hivyo kama namna ya kutafuta umaarufu kuliko kurekebisha matatizo.Kuna ugumu gani kwa Lowassa kuwaita ofisini kwake au kuwapigia simu au hata kuwaandikia barua kuwaonya watendaji anaowaona wanakwenda ndivyo sivyo badala ya kutumia mikutano ya hadhara kuwaumbua?Sidhani kama yeye atafurahi iwapo atateleza na bosi wake JK akaamua kumshambulia kwenye hotuba zake za kila mwisho wa mwezi.Ukweli ni kwamba wataongea faragha kiutu-uzima na kupeana maelekezo ambayo mwisho wa yote ni kwa manufaa ya Taifa zima.Ndio maana (kama lilivyoripoti gazeti la Mwananchi) JK aliwahi kumpigia simu Lowassa saa saba usiku kumweleza masononeko yake kuhusu suala la umeme,badala ya kufanya hivyo kwenye mkutano wa hadhara.Pengine Lowassa anapaswa kuelewa kwamba wanachohitaji wananchi sio kuwalambisha peremende kwa kuwaumbua viongozi hao (ambao ni sehemu ya serikali anayoongoza yeye kama Waziri Mkuu) bali kuwapatia tiba ya matatizo yao lukuki ambayo yanaelekea kutokuwa na mwisho.Nakumbuka wakati flani aliomba aletewe orodha ya wadaiwa sugu wa maji ili awashughulikie.Sasa kwanini hakutumia njia hiyo alipokuwa waziri kwenye wizara hiyo?Au haoni kuwa kwa kufanya hivyo alikuwa akiuambia umma kuwa wenye mamlaka ya kukusanya madeni ya maji wameshindwa kutekeleza majukumu yao hadi inambidi yeye kama Waziri Mkuu kuingilia kati?Na pengine awaambie Watanzania kuwa hizo amri zake anazotoa kwa namna ya zimamoto zimebadilisha vipi maisha ya Watanzania,kwa mfano agizo lake kwamba kila mwanafunzi aliefaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana awe ameingia kidato cha kwanza.Wapo walioanza kumfananisha Lowassa na marehemu Sokoine,lakini nadhani Sokoine alikuwa mwingi wa vitendo kuliko maneno.

Ila kinachonifanya nisimwelewe huyu bwana ni hii tabia yake ya kuwaziba mdomo wabunge wa CCM ambayo ni namna ya kistaarabu ya kulea uzembe na maovu yanayowaumiza Watanzania.Kwenye kikao cha Bunge la bajeti alijitokeza kuwa mwokozi wa mawaziri waliokaliwa kooni na wabunge,na sio mwokozi kwa kutoa ufumbuzi wa yaliyokuwa yakiwakera wabunge bali kuwalinda wasiumbuke.Sasa iweje yeye awe anapenda kuwaumbua baadhi ya watendaji wa ngazi za chini lakini anakuwa mwepesi kuwatetea mawaziri wanaochemsha kwenye utendaji wao?Hivi vikao vya kuwekana sawa kati ya Lowassa na wabunge wa CCM ni kwa manufaa ya nani?Wabunge wanaingia bungeni kuwakilisha mamilioni ya Watanzania ambao haiwezekani kwao kuingia kwenye jengo hilo kwa mkupuo kuihoji serikali waliyoiweka madarakani.Kuwaziba midomo wabunge ni sawa kabisa na kuwaziba midomo wananchi,na hilo linapaswa kukemewa kwa nguvu zote.

Niliandika hivi karibuni kuwa Waziri Karamagi ana wakati mwepesi katika kujibu maswali magumu yanayohusiana na tatizo la umeme sambamba na sakata la kampuni ya Richmond.Jibu jepesi nililotabiri na ambalo inaelekea ndio atakalokuwa akilitumia kila atapohojiwa ni kwamba yeye ndiyo kwanza ameingia wizarani hapo na hakuwapo wakati mikataba ya kampuni hiyo ikisainiwa.Hilo ni jibu la kisiasa na linalengwa kukwepa kuwajibika kwa wananchi.Ningeweza kumwelewa Karamagi kama Waziri Msabaha angekuwa amehamishiwa wizara ambayo iko nchi kama Irak ambako mawasiliano ya simu ni ya kubahatisha na ambako sidhani kama mawaziri wa “serikali” ya nchi hiyo wanapata muda wa kubadilishana mawazo nyakati za jioni au wikiendi.Msabaha yuko Dar es Salaam,simu yake inafanya kazi,na ni suala dogo tu kwa Karamagi kumdadisi mwenzie kwamba hivi haya ambo yakoje?Na kama kweli anataka Watanzania wamuelewe vizuri ni lazima awe na majibu ya wakati uliopo na sio kutupiana mpira na mtu ambaye kwa sasa sio mhusika katika wizara hiyo.Kwa kifupi,yeye ndiye mwenye dhamana ya kutujulisha ni lini tatizo la mgao wa umeme litaisha (au pengine awasiliane na viongozi wa dini kufahamu ni lini “mitihani ya Mungu” itamalizika).

Turudi kwa Lowassa.Ni vema akafahamu kuwa kama yeye hahitaji mjadala kuhusu suala la mgao wa umeme,waliomweka madarakani (yaani Watanzania) wana kiu kubwa mno ya kufahamu kulikoni.Anachoogopa ni nini kuhusu wabunge kujadili suala hilo?Kuna nini ambacho hataki Watanzania wakifahamu?Pamoja na kuwa msemaji sana tangu aingie madarakani hajaweza kabisa kugusiana utata uliojitokeza kuhusu kampuni ya Richmond.Kwanini sasa asiwaache Watanzania kupitia kwa wabunge wao wajadili kwa undani suala hilo na kufahamu nani aliyetufikisha hapa na pengine cha muhimu zaidi ni lini nchi yetu itarejea kwenye kanuni za jiografia za mchana kuwa mchana na usiku kuwa usiku badala ya sasa ambapo inaelekea usiku ni mrefu kuliko mchana kutokana na “giza la kulazimisha” linalosababishwa na mgao wa umeme.Tunafahamu kuwa mgao huu unawaumiza wale wasio na uwezo wa kununua jenereta na sio vigogo ambao hawajui hata bei ya mafuta ya taa kwa vile muda wote umeme upo maofisini na majumbani mwao.Pia ni dhahiri kuwa baadhi ya watu wananufaika na mgao huu hasa wale wenye biashara ya majenereta,na si ajabu hili wazo la kununua mitambo ya umeme kutoka nje ikawa kwenye mlolongo huohuo.Kama kweli serikali ilikuwa na nia ya kupunguza makali ya mgao wa umeme kwa kununua majenereta basi ingeweza kuomba msaada kwa balozi za nchi kama Japan,Marekani,Uingereza,nk kuwasaidia kupata kampuni ambazo naamini ndani ya mwezi mmoja zingekuwa zimetekeleza walichoagizwa.Tumeanza kusikia tetesi kwamba iwapo serikali itavunja mkataba na kampuni ya Richmond,inaweza kujikuta inatakiwa kulipa fidia kubwa.Yaleyale ya IPTL.Hivi hawa jamaa wa Richmond wanatoa msaada wa bure au wanatakiwa kutekeleza mkataba halali wa kibiashara ambao unawalazimisha kutekeleza matakwa ya mteja (serikali) ndani ya muda maalum badala ya kuleta mitambo kwa mafungu (na hatuna uhakika lini mitambo hiyo itaanza kazi,kama kweli itaweza kufanya kazi “kutokana na joto la Tanzania”,na iwapo itakongoroka basi wahandisi kutoka Marekani hawatakuja kwa mafungu kama mitambo hiyo).

Mwisho,nawaomba sana wawakilishi wetu huko bungeni wasikubali kuwasaliti Watanzania wanaowawakilisha.Hakuna dhambi kwa kukubaliana na Lowassa kuwa hawataibua hoja hiyo lakini wakamgeuka na kuiibua wakati wa kikao cha bunge.Huko sio kukosa nidhamu bali ndio kuwajibika.Wabunge wetu wafahamu kuwa siku zote serikali itatetea matendo yake hata yakiwa mabaya,na ni jukumu la wabunge kuikosoa na kuiwajibisha pale itapolazimika.Wabunge msituangushe safari hii,mnapaswa kuikalia kooni serikali bila uoga ili muwasaidie mnaowawakilisha angalau wafahamu wahusika wakuu katika hili sakata la mgao wa umeme na mikataba ya utata.Na kwa Waziri Mkuu,wito wangu kwako ni kukuomba uwaruhusu Watanzania kupitia kwa wawakilishi wao watumie haki yao ya kikatiba kufahamu ni lini hiyo ndoto ya maisha bora kwa kila Mtanzania itatimia kwa kuanzia na suala la umeme.

Alamsiki

http://chahali.blogspot.com
http://chahali.livejournal.com

KULIKONI UGHAIBUNI-34

Idd Mubarak (japo nimechelewa kutoa salamu hiyo,nategemea kusikia “minal faidhina” kutoka kwako msomaji mpendwa wa safu hii).

Katika mojawapo ya makala zangu za nyuma niliwahi kuahidi kuwazungumzia jamaa flani ambao ndio kama uti wa mgongo wa uongozi wa Rais George W Bush.Hawa jamaa wanafahamika kama “neoconservatives” au kwa kifupi “neocons.”Msamiati huu uliibuka kwenye miaka ya 60 na 70 na ukapata umaarufu zaidi wakati wa utawala wa Rais Bush mkubwa,Ronald Reagan na sasa kwenye utawala wa huyu Bush mdogo ambaye anaonekana kuwategemea mno jamaa hao kiasi cha watu wengine kuamini kuwa wao ndio wanaendesha nchi hiyo kwa kumtumia Rais huyo.

Wengi wa hawa neocons ni watu ambao “shule imepanda” kweli (ni wasomi).Kwa kiasi kikubwa mafanikio yao ya kisiasa yametokana na elimu yao na sio mbinu chafu za kupata uongozi.Na kama ilivyo kwenye nchi nyingine za magharibi,wengi wa jamaa hawa wako ndani ya vivuli vya taasisi ambazo aidha ni za kitaaluma,ushauri au zile ambazo zinatetea maslahi flani (interest groups) lakini zilizo maarufu zaidi ni hizo zinazoitwa “think-tanks” (nadhani kwa lugha yetu ya taifa tunaweza kuziita “visima vya fikra” japo BAKITA wanaweza kuwa na msamiati bora zaidi).Think-tanks nyingi ni taasisi zinazosikilizwa na kuheshimika hasa kwa vile huwa zinakusanya wasomi waliobobea,wanasiasa wastaafu na watu wengine maarufu kwenye maeneo kama uchumi,sayansi na teknolojia,jamii,nk.Zilizo maarufu miongoni mwa nyingi zinazomsapoti Bush ni “American Enterprise Institute” (AEI) na “Project for the New American Century (PNAC)”.Neocons maarufu ni pamoja na Makamu wa Rais Dick Cheney,Waziri wa Ulinzi Donald Rumsfield,Rais wa Benki ya Dunia Paul Wolfowitz,Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa John Bolton,Balozi wa Marekani huko Irak Zaymal Khalilzad,Profesa wa siasa-uchumi ya kimataifa katika chuo kikuu cha John Hopkins Francis Fukuyama ,Mkurugenzi wa zamani wa CIA James Woolsey,Gavana wa Florida Jeb Bush (mdogo wake George Bush),Mhariri wa gazeti la Weekly Standard na mchangiaji kwenye kituo cha televisheni cha Fox News Bill Kriston na Naibu wa zamani wa Ulinzi na mtetezi maarufu wa siasa za Israel Richard Perle,na wengineo wengi ambao haiwezekani kuwataja wote kwenye makala moja kama hii.

Kimsingi hawa jamaa ndio waasisi wa vita dhidi ya Iraq na wamekuwa wakitumia ujuzi,elimu,umaarufu na nafasi zao kutetea sera za Bush ambazo kimsingi wao ndio vinara wake.Miongoni mwa imani zao ni pamoja na kuimarisha na kutumia “ipasavyo” nafasi ya Marekani kama taifa lenye nguvu zaidi ulimwenguni,kushambulia taifa lolote linaloonekana tishio kwa ustawi wa Marekani,kuisapoti Israel kwa nguvu zote (wengi wao wana asili ya Israel),kubadili “jiographia” ya nchi za Mashariki ya Kati kulingana na matakwa ya Marekani na hili la vita dhidi ya ugaidi.

Nadhani hadi hapa umeshaanza kuchoshwa na maelezo yangu kuhusu jamaa hawa na siasa zao.Tulia kidogo,nataka kujenga hoja muhimu hapa ambayo inawafananisha hawa jamaa na kikundi flani ambacho kinaelekea kushika hatamu kwenye siasa za huko nyumbani.Hapa nawazungumzia wanaoitwa “WANAMTANDAO.”Unajua hadi hivi karibuni nilikuwa naamini kuwa nazifahamu sana siasa za nchi yangu hadi nilipokutana na “mtaalam” flani wa siasa halisi (japo hazionekani waziwazi) za Tanzania.Huyo jamaa yangu aliniambia kuwa kwa sasa kundi la wanamtandao limeshika vilivyo hatamu ya siasa za Bongo,na wanamtandao wamekuwa sehemu muhimu ya maamuzi mbalimbali ya CCM na serikali yake (ya Bara,kwa vile nguvu za wanamtandao huko Visiwani hazijulikani sana japo zinaweza kuwa zipo).Mtaalam huyo alinidokeza kuwa wanamtandao wako kila kona:ndani ya serikali na taasisi zake,vyombo vya habari,taasisi za elimu,mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali,biashara binafsi (mambo ya fedha) na hata kwenye jobless kona za mitaani.Pia alinijulisha kuwa wanamtandao wana nguvu kweli na wametandaa hasa.Hapo ndio nikamkumbuka nilipokuwa huko nyumbani kulikuwa na jamaa mmoja aliyekuwa “akimwaga bia ovyo” kwenye baa flani maeneo ya Kinondoni huku akitamba kwamba “wao wanamtandao ndio wamekamata nchi kwa sasa.”Kwa wakati huo nilidhani huyo jamaa alikuwa anatafuta “ujiko” (sifa) tu,lakini sasa nakiri kwamba pengine alikuwa anaongea ukweli.

Mimi sina ugomvi na wanamtandao alimradi wanayofanya hayaipeleki nchi yetu kusikoeleweka.Wasiwasi wangu mkubwa ni ukweli kwamba ndani ya kundi hilo kuna watu safi na wengine wana sifa zenye walakini.Hawa wa kundi la pili ndio nawahofia zaidi kwa vile inawezekana wakawatumia wenzao walio katika nafasi za kutoa maamuzi kuhakikisha maslahi yao binafsi yanatekelezwa.Kinachoogopesha zaidi ni ukweli kwamba kundi hili limekuwa la siri kwa muda mrefu na karibu wahusika wake wote ni watu ambao tunawahisi tu kwa vile hawatamki hadharani uanamtandao wao.Pia inajulikana kuwa baadhi yao si viongozi wa chama tawala japokuwa wanaweza kufanya matakwa yao kutekelezwa bila ya wao wenyewe kuhudhuria vikao vya chama hicho.

Pengine ni wakati mwafaka kujiuliza hivi hatma ya hawa jamaa ni nini.Wajuzi wa mambo wanasema kuwa hawa jamaa ndio waliotengeneza timu ya ushindi wa Jakaya,kazi ambayo wameifanya kwa zaidi ya miaka 10.Leo wamefanikiwa kumuingiza Jakaya madarakani na pia baadhi yao wamefanikiwa kushika hatamu ndani ya serikali na chama tawala.Na tunafahamu kuwa wanataka kuendelea kuwepo kwa ajili ya chaguzi zijazo.Lakini wasiwasi wangu ni pale watakapokosana na wenzao walio madarakani.Uwezekano huo upo japo sio mkubwa kwa sasa.Upo kwa vile baadhi ya wanamtandao hawako ndani ya chama na serikali,sasa ipo siku yatatolewa maamuzi ambayo yatalenga zaidi maslahi ya chama au Taifa kwa ujumla kuliko maslahi ya wanamtandao walio nje ya uongozi.Niite “conspirancy theorist” (mwanafalsafa mwenye kuhisi “hapa kuna namna”) lakini historia imeonyesha kuwa ni rahisi sana kwa vikundi visivyo rasmi na vinavyoendeshwa kwa usiri kuingia kwenye migogoro hasa kwa vile nidhamu ya uongozi katika vikundi vya namna hii huwa ni haba,wengi wa “wanachama” huwa na matarajio makubwa pengine zaidi ya uwezo wa wanaowategemea kutimiza matarajio hayo na wakati mwingine kuna tabia ya kuoneana “donge” (wivu) kwamba “mbona mie nilifanya kazi kubwa sana kumfikisha flani hapa alipo lakini sithaminiwi kama flani ambaye mchango wake ni mdogo kuliko wangu.”Angalia mfano huu: CCM ikishindwa kuafikiana kuhusu uteuzi mgombea wake ajae watawekana chini na demokrasia ya namna flani itatumika kufikia muafaka kwa maslahi ya chama.Kwenye mtandao je?Hivi mnaoongea na wanamtandao wanawaeleza maslahi yao halisi ni kwenye nini?Chama,mgombea au matumbo yao binafsi?

Neno la mwisho,nimesoma kwenye magazeti kuwa hatimaye kampuni ya Richmond wameanza kuleta mitambo.Lakini badala ya kuomba radhi kwa kuchelewa kutimiza ahadi zao ndani ya muda waliojiwekea wenyewe eti wanalalamika kuwa walikuwa wanapigwa majungu.Enewei,kuna msemo kwamba ahadi haina maana hadi inapotekelezwa.Tunasubiri hizo jenereta zianze kufanya kazi tukitarajia kuwa hii sio miujiza kama ya Mv Alina.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI-33

Asalam aleykum,

Majuzi nilipata barua pepe kutoka Uholanzi ikinieleza kwamba jina langu limepitishwa katika bahati nasibu ya Jumuiya ya Ulaya na “nimebahatika” kuwa mshindi wa Euro milioni moja!Wahusika waliniomba kuwapatia taarifa za akaunti yangu ya benki ili waweze kuingiza kitita hicho.Unaweza kudhani kwamba labda nilipiga kigelegele cha furaha kwamba hatimaye Mndamba mie nimekuwa milionea.Umekosea.Kabla hata ya kumaliza kuiosma barua hiyo niliamua kuifutilia mbali.Utapeli wa namna hiyo umetawala sana huku ughaibuni na wapo “wanaoingia mkenge” na kuwaamini matapeli wa aina hiyo kabla ya kuangua kilio badala ya kicheko baada ya kugundua kuwa taarifa za akaunti zao ziliombwa ili matapeli hao waibe fedha kwa utaalamu wanaoujua wao.

Njia mojawapo ya kubaini utapeli wa watu hao ni kutafuta habari zaidi kuhusu jina la kampuni husika.Na sio kazi ngumu.Kwenye mtandao kuna kitu tunachoweza kukiita “injini ya kutafia habari” (search engine).Maarufu zaidi ni Google,lakini kuna nyingine kadhaa kama Yahoo!,MSN,Ask,nk.Kwa hiyo ukitaka kutafuta habari zangu unataipu “CHAHALI” halafu unabonyeza “tafuta” na hapo utapata habari mbalimbali zinazohisana na jina hilo.Nyingine zitakuwa zinanihusu asilimia 100 na nyingine zitakuwa zinakaribiana na ukweli huku nyingine zikiwa haziusiani nami kabisa.Kwa hiyo nilipotaipu jina la kampuni hiyo ya bahati nasibu nikakuta taarifa kibao kuhusu utapeli wao ambao kwa “lugha ya mama” unaitwa “scam.”Waliobobea zaidi kwenye scamming ni Wanaijeria,na yayumkinika kusema kuwa utapeli wao kwenye mtandao ni maarufu zaidi kuliko timu yao ya Taifa.

Kwanini watu wanaamini scammers hadi kutoa taarifa zao za siri?Jibu jepesi ni kwamba ni rahisi kumtapeli mtu binafsi kuliko kundi la watu.Kosa kubwa wanalofanya scammers hao ni kutuma barua pepe zinazofanana kwa watu wengi,na japo wapo wanaotokea kuwaamini lakini wapo pia watu ambao huwa wanajihangaisha kutafuta ukweli kwenye mtandao kama nilivyofanya mimi.Walengwa na waathirika wakubwa wa vitendo hivyo vya kitapeli ni watu binafsi,na ni nadra sana kusikia taasisi flani imedanganyika na kukubaliana na matapeli hao.

Wanasema maajabu yote yanawezekana katika nchi inayoitwa Tanzania.Matapeli flani wameivaa serikali wakidai wana kampuni yenye makao makuu huko Houston,Texas nchini Marekani na kupata tenda ya kuleta majenereta kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la mgao wa umeme.Hapa naizungumzia kampuni ya Richmond Development Company.Niliposoma habari za kampuni hiyo kwa mara ya kwanza nilikimbilia kwenye Google kutafuta habari zaidi kuhusu waungwana hao.Nikaambulia patupu.Nikajaribu kutafuta habari za makampuni yanayojihusisha na biashara ya majenereta kwenye jimbo la Texas,napo nikaambulia patupu.Hata nilipojaribu kutafuta habari hizo kwa Marekani nzima nikitumia aidha jina la kampuni hiyo,au aina ya shughuli wanazofanya,bado nilitoka kapa.

Sasa hivi serikali yetu hii ya awamu ya nne inataka kutuambia iliingia mkataba na kampuni hiyo bila hata kuhakiki iwapo kweli ipo hai?Tuna mabalozi wawili nchini Marekani,moja akituwakilisha kwenye nchi hiyo na mwingine ikituwakilisha kwenye Umoja wa Mataifa.Kwanini mabalozi hao hawakuulizwa kabla ya kuingia mkataba na kampuni hiyo iliyodai ina makao yake makuu nchini humo?Au kwanini hawakuagizwa kufuatilia ukweli huo baada ya dalili kuanza kuonyesha kuwa jamaa hao ni wababaishaji flani?Hata kama mabalozi wetu walikuwa bize,tuna Watanzania lukuki wanaoishi Houston na hao wangeweza kuwa wa msaada sana kujua habari za kampuni hiyo.Hivi jamani,si majuzi tu Rais alikuwa Marekani na kundi kubwa tu la Watanzania?Sasa kwanini ziara hiyo nayo haikutumika kama mojawapo wa njia za kufahamu iwapo kama kampuni hiyo ipo kweli?

Kwa kweli habari hizi zinasikitisha sana kwa sababu kwa namna flani zinakinzana na ahadi iliyotolewa na serikali ya Awamu ya Nne kwamba itakuwa makini kabla ya kuingia mikataba hasa na makampuni ya kigeni.Hadi leo hatujui nani hasa aliyesaini mkataba na IPTL kwa sababu kila mmoja anamtupia mzigo mwenyewe ilhali kuna mamilioni ya fedha za walipakodi zinazoendelea kumwagwa kwa kampuni hiyo kwa sababu tu kuna mtu alisaini mkataba utadhani alikuwa usingizini.Hivi huyo alompatia taarifa Rais Kikwete kwamba majenereta yangewa sili Jumapili ileee ni nani,na hadi sasa amechukuliwa hatua gani.Je huyo aloingia mkataba na kampuni hiyo (kwa vyovyote atakuwa ni binadamu Mtanzania,na sio kompyuta au jinni) anatueleza nini kuhusu hiki kizungumkuti kinachochafua azma ya “maisha bora kwa kila Mtanzania”?

Yafuatayo ni mawazo yangu binafsi,na naomba atakayeguswa asikimbilie mahakamani kudai gazeti hili limemkashifu.Waziri Msabaha,Naibu wake na maofisa wa ngazi za juu wa Wizara ya Nishati wanawajibika moja kwa moja katika sakata hili,na wana maswali ya kujibu kwa Watanzania.Mabadiliko ya Wizara yanaweza kuwa njia flani ya kuwaokoa watu kujibu maswali magumu lakini kwa vile bado wako katika serikali hii basi ni lazima tuambiwe ukweli na baadaye hatua sahihi zichukuliwe dhidi yao.Karamagi ana majibu mepesi kabisa kwa maswali kuhusu utapeli wa kampuni hiyo, “Mimi sikuwa Waziri katika wizara hii wakati mkataba huo unasainiwa”,na hiyo ni sahihi kwake kusema hivyo japo anaweza kulivalia njuga swala hilo ili kujua lilianzwa vipi,nani alipewa nini na hatimaye nini kifanyke dhidi ya wahusika.

Watanzania wanachezewa kwa vile ni wakimya sana.Hata wakiwa na maswali yanayohitaji majibu lakini wanaopaswa kujibu wanakaa kimya bado Watanzania wataishia kusema chinichini tu.Na hiyo ndio inawapa watu flani jeuri ya kuboronga mambo kwa vile wanajua wananchi watakaa kimya na waliowateaua hawatawawajibisha.Hakuna kauli yoyote iliyotolewa na serikali kuhusiana na sakata la kampuni ya Richmond.Hatujaambiwa hatua gani zimeshachukuliwa dhidi ya wamiliki wake hasa huyo mmoja anayedaiwa kuwa Mtanzania.Wito wangu kwa Rais Kikwete ni kwamba kuwakalia kimya watu wanaochafua jina la serikali yako ni sawa na kuwaomba Watanzania waanze kupoteza imani yao kwako mapema kabla hata serikali yako haijatimiza mwaka mmoja madarakani.Sina kinyongo na mabadiliko ya baraza la mawaziri kwa vile ni haki ya kikatiba ya Rais kufanya hivyo japo sijui kama zile ziara zilizofanywa na Rais kwenye kila wizara (kuwaelekeza mawaziri na watumishi wa wizara hizo nini wanapaswa kufanya) na hatimaye kufuatiwa na semina huko Ngurdoto zimezaa matunda gani.Kama (nasisitiza KAMA) mabadiliko hayo yametokana na dalili kwamba baadhi ya mawaziri wamezidiwa na kasi mpya,nguvu mpya na ari mpya basi ufumbuzi sio kuwabadilishia wizara bali kuwatimua.Kuna maelfu ya Watanzania wenye uwezo ambao hawahitaji kuambiwa “hii ndio nafasi yako ya mwisho,ukiboronga nakutimua” ili wawajibike ipasavyo.

Naamini Jakaya anatambua deni alilonalo kwa Watanzania,na naamini anafahamu kuwa baadhi ya matendo ya aliowateuwa yanawachefua wanaompenda.Chaguo liko kwake:kuwaridhisha waliomchagua au aliowachagua yeye.Ukiniomba nitegue kitendawili hicho,ntakwambia kuwa Jakaya atawarukia kama mwewe hao wanaotaka kuifanya kauli-mbiu ya “maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana” ionekane kuwa kiini macho.

Ramadhan Karim

Kwa makala zilizopita za “KULIKONI UGHAIBUNI” tembelea http://chahali.blogspot.com au http://chahali.livejournal.com

KULIKONI UGHAIBUNI-32


Asalam aleykum,

Kwanza napenda kutoa pole kwa familia za marehemu Walter Mazula na mchumba wake Vonatha Nkya.Kwa namna mazingira ya huku ughaibuni yalivyo,Mtanzania mwenzako popote alipo ni kama sehemu ya familia.Mauaji hayo ya kikatili yamewagusa watu wengi hata kwa sie ambao hatukubahatika kukutana nao wakati wa uhai wao.Kwa mujibu wa wenzetu walio Marekani,kulikuwa na ushirkiano mkubwa na familia ya wafiwa kwa kuwafariji na kuwapatia msaada wa hali na mali,na kwa mara nyingine imeonyesha ni jinsi gani Watanzania tuna moyo wa ushirkiano popte tulipo.Wakati tunaviacha vyombo vya sheria huko Marekani vikiendelea na uchunguzi kuhusu mauaji hayo,tunachoweza kusema kwa sasa ni kuwatakia marehemu pumziko la milele na kuwaombea wafiwa moyo wa uvumilifu na faraja.

Wakati tunazungumzia maisha ya Watanzania hao wawili ambao wamenyang’anywa uhai wao bila chembe ya huruma,pengine ni wakati muafaka pia kuangalia maisha ya Watanzania wengine ambayo yanapotea takribani kila siku huko nyumbani kutokana na ajali za barabarani.Kwa kweli inatia uchungu kusoma habari za ajali kila kukicha huku kukiwa hakuna daliliz zozote kwamba angalau ajali hizo zitapungua.Kuna msemo wa Kiswahili kwamba ajali haina kinga,lakini nyingi ya hizo zinazotokea huko nyumbani zinaweza kuepukika au kupunguzwa iwapo wenye dhamana ya kusimamia usalama barabarani wataongeza jitihada.

Kila mwaka kuna wiki ya “Nenda kwa Usalama Barabarani”.Kama sijakosea,kipindi hiki ndicho ukaguzi wa magari unafanyika japokuwa jukumu la kukagua magari ni la mwaka mzima.Sina tatizo na zoezi hilo kufanyika mara moja kwa mwaka.Ugomvi wangu kwenye zoezi hilo ni jinsi linavyoshindwa kupunguza ajali za barabarani.Lakini ugomvi wangu mkubwa uko kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri ambao wameweka mbele tama ya fedha kuliko uhai wa hao wanaowawezesha kupata fedha hizo kwa njia ya nauli (abiria).Laiti wamiliki hao wangekuwa na ubinadamu wa kutambua kuwa magari yao hayako katika hali nzuri ya kubeba abiria,nadhani hata trafiki wasingekuwa na haja ya kuyakamata magari ya aina hiyo.

Wengine wasioweza kukwepa lawama zangu ni madereva wazembe.Hawa wangeweza kukwepa lawama pale tu wanapokabidhiwa magari ambayo wanafahamu fika kuwa ni “vimeo”.Tunafahamu kuwa wanalinda ajira zao kwa vile ni lazima wamepeleka mkono kinywani lakini hata hivyo ridhiki zao zisiwe sababu ya kuleta vilio kwa wenzao.Kwa utaratibu uliozoeleka,wamiliki wa magari kama daladala huwa wanapatia dhamana madereva wa magari hayo kuhakikisha yanafanya kazi kwa namna inavyopaswa.Kwa mantiki hiyo,inaweza kuwa vigumu kwa mmiliki kumsimamia dereva ahakikishe anasima kwenye traffic lights,hafanyi “ovateki” za kizembe,au anazingatia mwendo unaotakiwa katika barabara husika.Majukumu hayo ni yadereva mwenyewe.Kwa bahati mbaya,uhuru huo wanaopatiwa madereva huishia kutumiwa vibaya,na hawa jamaa wakishakuwa kwenye usukani wanajiona kama wanaendesha magari hayo wakiwa peponi.Na napozungumzia madereva wazembe najumuisha madereva wote,wale wa magari ya abiria na yale yasiyo ya abiria.

Labda hapa nitoe mfano mmoja wa sheria za usalama barabarani za hapa Uingereza.Ni “dhambi” isiyosameheka kwa dereva yoyote yule kukutwa anaendesha akiwa amepata kinywaji.Siku za wikiendi utakuta watu wanaacha magari yao nyumbani pindi wanapoamua kwenda kupata kinywaji.Usafiri unaotegemewa wakati wa kurejea majumbani kwa nyakati hizo za usiku ni taksi na mabasi ya usiku pekee.Haina maana hakuna wakorofi wachache wanaojaribu kuwapima nguvu polisi kwa kuendesha huku wamelewa,lakini kwa ujumla madereva wengi wanazingatia sana sheria hiyo.Kingine ni kudhibiti mwendo wa magari.Hilo linasaidiwa sana na teknolojia ambapo kuna kamera za barabarani zinazorekodi magari yanayoendeshwa zaidi ya spidi inayoruhusiwa kwenye barabara husika.

Kundi la tatu ambalo nadhani haliwezi kukwepa lawama kuhusiana na hiz ajali za kila siku ni wenzetu tuliowakabidhi dhamana ya kuhakikisha usalama barabarani.Hapa nawazungumzia polisi wa kitengo cha trafiki.Hawa jamaa wamekuwa wakisifika (au kulaumiwa?) zaidi kwa “kudai kitu kidogo” badala ya kawadhibiti madereva watukutu.Simaanishi kwamba askari trafiki wote ni wala rushwa lakini hatuhitaji digrii ya upelelezi kufahamu kuwa trafiki wengi wanaendekeza zaidi rushwa badala ya kuzingatia majukumu waliyokabidhiwa.Hatuwashuku kuwa ni wala rushwa kwa vile wengi wao wana miili iliyoneemeka licha ya vilio vya askari wetu kuwa mishahara ni kiduchu,bali ni ushahidi ambao sidhani kama kuna dereva au abiria hajawahi kuuona mchana mweupe ambapo trafiki anamshusha dereva au konda wake na kuelekea “mafichoni” kupatiwa mlungula.Hivi huyu mla rushwa anaweza kweli kulizuia gari bovu lisitembee barabarani?Kwa hakika hawezi,kwa sababu akilizuwia ina maana atakosa “maslahi” yake.Nadhani baadhi yao wanasiktika pindi wanapolisimamisha gari na kugundua kuwa halina tatizo na dereva wake hajavunja sheria yoyote.

Serikali yetu nayo haiwezi kukwepa lawama kuhusu kuzidi kwa ajali za barabarani.Kumekuwa na ahadi nyingi zaidi ya vitendo.Baadhi yetu tumeshasahau kuhusu “spidi gavana” na hatujui huyo “tapeli aliyetuingiza mkenge” (tu aliyekuja na wazo hilo) amechukuliwa hatua gani baada ya kubainika kuwa mradi huo ulikuwa feki na haujaleta manufaa yoyote kwa wananchi.Nasema hivi,nyingi ya ajali za huko nyumbani zinaweza kuepukika iwapo serikali itasimamia na kuhakikisha sheria iliyoziweka zinafuatwa bila utani.Na si ajali za barabarani tu lakini hata kwenye vyombo vya majini (hivi lile suala la Mv Nyamangeni limeishia wapi?).Vivuko vyetu vingi ni sawa na majeneza yanayoelea,na kwa vile sie ni watu tuliozowea kuchukua hatua pale tu tatizo linapotokea,maelfu ya Watanzania wanaendelea kutumia pantoni na feri ambazo kwa kiasi kikubwa usalama wake ni wa hatihati.

Mwisho,ifahamike kuwa tatizo la ajali za barabarani halizoeleki.Kuwa na ajali za kila siku haimaananishi kuwa wananchi wanazizowea.Hawana la kufanya ila kusafiri roho mkononi huku wakiomba dua madereva watumie akili zaidi,trafiki watekeleze majukumu yao vizuri na hatimaye wafike salama huko waendako.Tusisubiri hadi gari la kiongozi lipate ajali kwa kugongwa na dereva mzembe na kufumbiwa macho na trafiki aliyepewa rushwa ndio tufumbuke macho kwamba kumbe kweli ajali ni tishio kwa maisha yetu.Sheria zipo na kwa hakika zinatekelezeka,kinachohitajika ni usimamizi na ufuatiliaji tu.

Ramadhan Karim (heri ya mfungo wa Ramadhan…kwa waliouona mwezi)

KULIKONI UGHAIBUNI-31

Asalam aleykum,

Moja ya mambo ambayo yalikuwa magumu kwangu baada ya kuwasili hapa nilipo ni namna ya kuendana na aina ya chakula kilichozoeleka hapa.Mie ni Mndamba,na kule kwetu Ifakara hadithi ni wali,wali na wali sana.Asubuhi ni chai na kiporo cha wali,mchana ni wali,na usiku hadithi ni hiyohiyo ya wali.Nilipokuwa nawakaribisha rafiki zangu pale Ifakara mama alihakikisha kuwa lazima wapate wali,na japo ugali pia ni mlo lakini kwa tabia za Kindamba kumlisha mgeni ugali ni kama kutompatia makaribisho mazuri.

Sasa nilipokuja hapa Uingereza nikakutana na mambo ya chips samaki,burgers,pizza na kadhalika.Sio kwamba huko nyumbani hakuna vitu hivyo katika zama hizi za utandawazi (kuna Steers,Subway,Nando’s,nk) lakini makoronya hayo kwangu ilikuwa ni ya anasa na pia ladha yake haikuwa sawa na ile ya wali nilouzowea Ifakara.Ukienda huko kwenye mwezi Juni au Julai unakutana na harufu ya mchele mpya ambao unanukia utazani umemwagiwa pafyumu bila kusahau habari za pepeta.

Majuzi nilikuwa naongea na baba yangu mdogo Mzee Magungu ambaye makazi yake ni Kiberege.Alinipa habari ambazo kwa hakika ni za kusikitisha.Labda kwanza niwapatie jiografia ndogo ya bonde la mto Kilombero,eneo ambalo lina rutuba ya asili ambayo kimsingi ndio chemchem ya utajiri wa mpunga na hatimaye mchele kwa maeneo hayo.Sio hadithi za kusifia sehemu ninayotoka lakini ni ukweli usiopingika kwamba kwa namna flani Mungu ameijalia sana wilaya ya Kilombero.Kuna vijito na mito lukuki ambayo mingi yao inaishia Mto Kilombero.Michache kati ya hiyo ni Mto Lwipa,Mpanga,Ruhuji,Mwatisi,Furua,Misima na Kihansi.Kulingana na kitabu cha maeneo yenye unyevunyevu ambayo yana umuhimu wa kimataifa (Directory of Wetlands of International Importance) bonde la Mto Kilombero ni la kipekee kitaifa na kimataifa kwa vile licha ya ardhi yake nyenye rutuba ya mwaka mzima kuna utajiri mkubwa wa misitu, wanyama na ndege asilia.Ndio maana enzi hizo majangili kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakimiminika huko “milima ya Golan” kuwinda tembo na faru,na hadi leo naamini kuwa nyama za nyati,mbawala,swala na nyinginezo bado si adimu.Takwimu zinaonyesha kuwa Bonde la Mto Kilombero ni makazi ya asilimia 75 ya swala waliopo duniani kote.Pia eneo hilo lina takribani aina 20,000 ya ndege wanaopenda maji (water birds) sambamba na aina tofauti 23 za samaki (hapo ndipo kuna akina “mlamu kaliandili”,”perege”,”kitoga”,“mbufu”,nk…nadhani Wandamba wakisikia hivi mate yanawachuruzika).Kuna utani mmoja kwamba Wandamba,Wambunga,Wabena,nk wana uhodari sana wa kula samaki wenye miiba sana halafu wana teknolojia ya kutenganisha nyama ya samaki na miiba hiyo mdomoni,yaani unakuta miiba ya samaki inatoka kwenye pembe ya mdomo kana kwamba kuna mashine inayotenganisha nyama na miiba.Ardhi yenye rutuba ya bonde hilo ndio inayomudu ustawi wa miwa ya sukari (Kilombero Sugar),miti ya mitiki,na mazao lukuki.Pia kutokana na utajiri huo wa maliasili,eneo hilo limekuwa kivutio kwa watalii (kwa mfano kingo za hifadhi ya Udzungwa) japokuwa inasikitisha kuona eneo hilo haliendelezwi ipasavyo.

Kilio cha wakazi wa maeneo yaliyopo kwenye Bonde la Mto Kilombero ni uvamizi wa jamii ya wafugaji ambao wengi wao wanatoka Kanda ya Ziwa na Arusha.Hawa jamaa wana ukorofi wa namna flani.Unajua mgeni sharti uwe na heshima kwa mwenyeji wako,lakini hawa “waungwana” wamekuwa wakitumia siasa za ubabe kulisha mifugo yao,ambapo kimsingi chakula cha mifugo hiyo ni mazao ya wakazi halisi wa maeneo hayo.Licha ya uvamizi huo kwenye mazao,jamii hiyo ya wafugaji inaelekea kutishia vyanzo vya mito vinavyolirutubisha Bonde la Mto Kilombero sambamba na kuathiri mito kadhaa iliyopo maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Mzee Magungu,kilio cha wakazi wa maeneo hayo sio cha hivi karibuni bali kimekuwepo kwa muda mrefu.Ngazi husika katika serikali zimefahamishwa lakini hadi sasa hakuna dalili ya utatuzi wa tatizo hilo.Naomba nisisitize kwamba mimi binafsi nimeshuhudia uharibifu wa mazao na mzingira unaofanya na jamii hizo za wafugaji katika safari zangu tatu nilizofanya nilipokuwa huko nyumbani kwa ziara ya kimasomo.Yaani ukifika Morogoro mjini ukiwa unaelekea Ifakara unakutana na kundi kubwa la jamii za wafugaji wakijiandaa kwenda kulisha mifugo yao maeneo hayo.Na humo njiani unakutana na mifugo lukuki ambayo haichagui kati ya majani na mpunga au mahindi.Sawa,Tanzania ni ya Watanzania wote lakini kuna watu wana maeneo yao binafsi pamoja na mashamba na mito wanayoitegemea kwa kilimo na uvuvi.Sasa uhuru wa kikatiba wanaopatiwa watu wa kwenda popote wanapotaka usitumiwe vibaya kiasi cha kuwaathiri wenzao.

Ombi kubwa la wakazi wa maeneo hayo ni kwa Mheshimiwa Jakaya Kikwete kwa vile wanaamini kuwa walimchagua kutokana na sifa zake za kuwajali wananchi wake.Wanamwomba awabane watendaji wake ambao wanaelekea kulea matatizo hadi pale yanapolipuka.Kama filamu ya mapanki ilimchukiza Rais kwa vile ilikuwa inachafua jina la nchi yetu huku nje basi wanamwomba afahamu kuwa uvamizi wa jamii ya wafugaji sio tu unachafua mahusiano kati ya wakazi wa maeneo hayo na wafugaji bali pia unaathiri jitihada zao halali za kumudu maisha kwa njia ya kilimo na uvuvi.Makala hii inaomwomba Rais Kikwete kuangalia njia za kutatua mgogoro huu ambao ukiachiwa unaweza kuwa mbaya kuliko ile inayotokea huko mkoani Mara.Ardhi ni haki ya kila Mtanzania lakini pia ni muhimu kukumbuka kuwa hakuna haki bila wajibu,na wajibu wa jamii za wafugaji wanaovamia Bonde la Mto Kilombero ni kuelewa kuwa wanawakosea heshima wenyeji wao na vitendo vyao vinaa thri ustawi wa eneo hilo lenye umuhimu si kwa wakazi wake tu bali pia Taifa kwa ujumla.

Alamsiki.

KULIKONI UGHAIBUNI-30:

Asalam aleykum,

Mwaka jana wanamuziki mbalimbali maarufu duniani walifanya matamasha makubwa nchini Uingereza,Marekani,Japan,Italia,Ufaransa,Canada na Afrika Kusini kwa lengo la kukusanya fedha za kupambana na umasikini barani Afrika.Miaka 10 kabla ya hapo kulifanyika matamasha kama hayo kwa lengo hilohilo.Matamasha hayo yalizua mjadala mmoja mkubwa kuhusu iwapo kweli nia nzuri ya kupambana na umasikini barani Afrika inaweza kufikiwa bila kuwaelimisha viongozi wa Kiafrika juu ya umuhimu wa kuthamini maisha ya wanaowatawala.Wapo waliosema kuwa hakuna haja ya kuchanga mamilioni ya fedha ambayo yataishia mifukoni mwa viongozi wabadhirifu,lakini wengine wakasema itakuwa sio vema kuwatelekeza mamilioni ya Waafrika wanaoteseka kwa umasikini kwa vile tu wana viongozi wanaothamini matumbo yao kuliko ya wale wanaowaongoza.Matamasha yalifanyika,fedha zikapatikana na sijui kama ziliwafikia walengwa au la.

Siwalaumu wazungu wanaotushangaa sie masikini wa kutupwa ambao maisha ya kifahari ya baadhi ya viongozi wetu hayalingani hata na yale ya mabilionea wa huku Ughaibuni.Pengine kabla ya kuendelea na hoja hiyo nieleze wasiwasi wangu kuhusu hali ya mambo ilivyo huko nyumbani.Baada ya Rais Kikwete kutangaza baraza lake la mawaziri ulizuka mjadala kuhusu ukubwa wa baraza hilo.Mimi nilikuwa miongoni mwa waliodhani baraza hilo ni kubwa sana kwa nchi masikini kama yetu.Hofu yangu ilimalizwa kwa kiasi flani na kauli aliyotoa Rais kwamba ili kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania kwa kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya,ni muhimu kuwa na timu kubwa ya kutekeleza jukumu hilo zito.Wasiwasi kidogo niliobaki nao ulikuwa kwenye baadhi ya sura zilizokuwamo kwenye baraza hilo.Inafahamika kuwa baadhi ya walioteuliwa walikuwa mawaziri kwenye awamu iliyotangulia,na baadhi yao walikuwa kero kwa wananchi.Sihitaji kuwataja majina kwani sote tunawajua.

Siku za hivi karibuni Waziri wa Miundombinu Basil Mramba amekaririwa akisema kwamba serikali ina mpango wa kununua ndege nyingine ya Rais.Nisichokielewa ni aidha hiyo inayotumika sasa ni mbovu au kuna fedha za kutosha kuwa na ndege mbili za Rais.Kama ni mbovu mbona bado inatumika.Kama imechakaa mbona barabara zetu nazo zimechakaa na bado tunazitumia,mabehewa ya TRC yamechakaa lakini bado yanabeba abiria.Au Mramba anataka kutuambia kuwa maisha ya kiongozi wetu ni bora zaid kuliko ya mamilioni anaowaongoza?Naomba niseme kuwa haya ni maoni yangu binafsi na sio ya gazeti hili,na kama yataamuudhi Mheshimiwa Waziri anivumilie tu kwa vile nami ni mlipa kodi na nina haki ya kuhoji matumizi ya kodi nayokatwa.Nitamke bayana kuwa kauli za Mramba zimekuwa za jeuri kama vile fedha anazopanga kununulia hiyo ndege zinatoka mfukoni mwake.Na sijui jeuri hiyo anaipata wapi!Badala ya kuzungumzia mipango gani aliyonayo kuhusu kuboresha barabara zetu anaturudisha kwenye suala ambalo nina hakika anajua kabisa linawakera Watanzania.Kwanini asielekeze nguvu zake katika kufufua au hata kuanzisha shirika la ndege la Tanzania ambalo pamoja na mambo mengine linaweza kumpatia usafiri Rais wetu?Mbona Tony Blair kuna wakati anatumia ndege za British Airways?Nakubali kwamba Rais wetu hawezi kusafiri kwa kutumia daladala au kwenda ziarani kwenye treni za TRC zilizochoka vibaya.Anahitaji usafiri unaoendana na hadhi yake.Lakini kwa sasa si anao usafiri huo?Kuna haja gani ya kuzungumzia vitu ambavyo hatuvihitaji kwa muda huu?Kwanini,kama fedha za kununulia ndege nyingine zipo,zisielekezwe katika kurejesha uhai wa Shirika la Reli,kwa mfano?Mramba anataka watu waanze kumchukia Kikwete bila sababu ya msingi kwa sababu wakati anazungumzia kununua ndege nyingine ya Rais maelfu kwa maelfu ya Watanzania wanataabika kwa kusafiri kwenye mabehewa chakavu na barabara mbovu kupindukia na baadhi zikiwa na madaraja ambayo yanahitaji dua kadhaa kuyapita kwa usalama.Huyu Mramba anatoka Tanzania hii masikini wa kupindukia au jimbo la matajiri la Texas huko Marekani?

Na ndio maana nilisema hapo mwanzo kuwa nilipatwa na hofu na ukubwa wa baraza la mawaziri la Kikwete,sambamba na baadhi ya sura zilizomo kwenye baraza hilo.Pengine ukubwa wa baraza sio tatizo lakini pia inawezekana ukubwa huo unawapatia nafasi ya kujificha bila kubainika wale wasioendana na falsafa za “maisha bora kwa kila Mtanzania” na “kasi,nguvu na ari mpya”.Nakumbuka nilipokuwa huko nyumbani,mwalimu wangu wa zamani pale UDSM (Mlimani),Dokta Mwami wa Idara ya Sosholojia,aliniambia kuwa baadhi ya nyakati anatoa mihadhara (lectures) kwenye madarasa yalilofurika wanafunzi kiasi kwamba inakuwa vigumu kwa namna flani kumjua kila mwanafunzi aliyemo darasani.Pengine waziri mdhaifu anaweza kupata mwanya wa kujificha kwenye baraza la mawaziri lililo kubwa.Hata hivyo hata kama baraza lingekuwa na mawaziri 100 lakini wote ni wawajibikaji sidhani kama kungekuwa na manung’uniko.Watanzania wanataka maendeleo na hawajali kama yataletwa na kundi la watu watano au mia mbili.

Nakumbuka Rais Kikwete alishonya kuwa watu wasitafsiri sura yake iliyojaa tabasamu kuwa ni dalili ya upole na kuwaachia viongozi wazembe.Kauli zake zimeonyesha kuwa anaweza kumpa mtu kibano huku anatabasamu.Adhabu ni adhabu tu,hata kama anayeitoa anafanya hivyo huku anacheka.Tunafahamu viongozi waliokuwa wakitoa hotuba za ukali huku wamekunja uso na ungedhani kwamba dakika tano baada ya kumaliza hotuba hizo wala rushwa wangejipeleka wenyewe TAKURU au wazembe wangejiondoa wenyewe madarakani,lakini wapi!Sasa,Jakaya aanze kufanya kweli kwa hawa watendaji wake ambao kwa hakika hawaonekani kuelewa lugha anayoongea.Watanzania hawawezi kupata usingizi bora,acha hayo maisha bora,kama kila kukicha wakisikia kauli za kibabe zilizojaa dharau kuhusu matumizi ambayo kwa muda huu si ya dharura ukilinganisha na hali mbaya ya miundombinu yetu.Jakaya anapaswa kuwaonyesha wananchi wake wanaompenda kupindukia kuwa suala la ndege ni kimbelembele tu cha mtendaji wake mmoja,na kwamba ndege anayoitumia kwa sasa inamtosha,na fedha zinazozongumziwa kununulia ndege hiyo zitaelekezwa kwenye mahitaji ya haraka ya miundombinu yetu iliyo hoi bin taabani.Akimwachia Mramba aendelee kutoa kauli zake zisizoeleweka watu wanaweza kudhani kuwa Waziri huyo anatekeleza tu matakwa ya bosi wake (Rais),jambo ambalo naamini litawaumiza Watanzania wenye matumaini makubwa na Rais wao kipenzi.

Hata kama Waheshimiwa wabunge watakasirika lakini naomba niwaambie kuwa nawalaumu kwa kuwaacha watu kama waziri Mramba wamalize kikao cha bunge la bajeti huko Dodoma bila kutambua mahitaji halisi ya waajiri wa wabunge hao (wananchi wanaowawakilisha).Na pengine Mheshimiwa Lowassa asingemkwamua Mramba ili bajeti yake ipite tusingemsikia akitufanya wajinga kuamini kuwa hivi sasa ndege nyingine ya Rais ni muhimu kuliko mahitaji mengine lukuki katika wizara yake.Ni matumaini yangu kuwa kama alivyomkalia kooni Sauper na Darwin’s Nightmare yake kwa vile inachafua jina la Tanzania basi Jakaya atamkumbusha Mramba kuwa kuzungumzia ununuzi wa ndege muda huu ni sawa na kumchafulia jina yeye (Kikwete) kwa sababu anafahamu sana nini wananchi wanataka kusikia kutoka kwa mawaziri wake.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI-29

Asalam aleykum,

Kuna dalili za kutosha kwamba pindi Waziri Mkuu wa hapa Tony Blair atapong’atuka madarakani atarithiwa na Kansela Gordon Brown.Tayari baadhi ya viongozi wa chama cha Conservative kimeonyesha wasiwasi wa namna flani kuhusu Brown ambaye anatoka Scotland kushika nafasi hiyo ambayo ni ya uongozi wa juu kabisa wa serikali ya Uingereza.Pia kuna kipindi flani kulikuwa na mjadala kuhusu wabunge wanaotoka Scotland kuchangia hoja za mambo yanayohusu England pekee.Labda nirudie tena kuelezea kwamba Uingereza au United Kingdom ni muungano wa England,Scotland,Wales na Northern Ireland.Kwa huku nilipo mimi (Scotland) hakuna mbunge kutoka England,na hivyo ndivyo ilivyo huko Wales na Northern Ireland.Wanasiasa wa England wameonyesha kukerwa kwa kiasi flani kuingiliwa na wenzao wasio wa-English katika mambo ambayo ni ya England pekee.

Nizungumzie England na Scotland.Ukifika maeneo ya Cumbria ukiwa unatoka Scotland kwenda England kwa basi utakuta kibao kisemacho “Welcome to England” (yaani Karibu England), na ukiwa unatoka England kuja Scotland utakutana na maandishi “Scotland Welcomes You” yaani (Scotland Inakukaribisha).Sijui kwa wataalam wa lugha kuna tofauti gani kati salamu hizo mbili.Zaidi ya “karibu” hizo hakuna mpaka kama mpaka wala passport haihitajiki.Pengine miongoni mwa tofauti unazoweza kuzigundua ukiwa upande tofauti na mwingine ni lafidhi.Wote wanaongea Kiingereza lakini hiki cha Kiskotishi kama hauko makini unaweza kudhani ni lugha nyingine.Pamoja na tofauti hizo ndogondogo linapokuja suala la Uingereza kama United Kingdom kunakuwa na mshikamano wa mkubwa.Labda niseme hivi,yanapokuja mambo yanayohusu maeneo binafsi,kwa mfano England au Scotland,kunakuwa na hisia za utaifa na uasili,lakini kwa Uingereza kama nchi kuna mshikamano zaidi.Hiyo sio kusema kuwa hakuna kelele za chinichini kuhusu Muungano huu ulio chini ya Malkia Elizabeth wa Pili.Vurugu za huko Northern Ireland ni kati ya wanaotaka kuwa sehemu ya muungano na wale wanaotaka taifa huru.Hapa Scotland kuna chama kama SNP ambacho miongoni mwa ajenda zake ni uhuru wa Scotland japokuwa hoja hiyo haina nguvu sana.Kwa hiyo suala la Gordon Brown kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza linaonekana kama linaweza kuzua hoja ya Waziri Mkuu Mskotishi ambaye pamoja na mambo mengine atashughulikia “mambo yasiyomhusu” ya England.Tony Blair analiepuka hilo kwa namna flani kwa vile England ndio kubwa zaidi ukilinganisha na Scotland,Northern Ireland na Wales.Pamoja na yote hayo kelele za wapinga muungano ni ndogo kulinganisha na wale wanaoupenda.

Pengine ni kawaida kuwapo na kelele kwenye siasa za muungano ambao unajumuisha watu ambao kwa namna flani wana asili tofauti.Lakini nadhani kwa hali ya huko nyumbani mambo mengine yanakera kama si kushangaza.Nilisoma gazeti la Nipashe la tarehe 24-08-2006 ambapo kuna habari yenye kichwa “hakuna kuingia Zanzibar bila kibali maalum.”Gazeti hilo lilimkariri Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Ukaazi,Bw Mohammed Juma Ame,akieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeanzisha utaratibu utakaowalazimisha Watanzania kutoka Bara kuwa na vibali maalum vya kuingia visiwani humo kabla ya kuweka makazi ya kudumu. Alisema,namnukuu, “pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuruhusu Mtanzania kuishi sehemu yoyote atakayo, utaratibu huo umewekwa kwa madhumuni ya kuwatambua watu wote wanaoingia na kutoka Zanzibar kwa sababu za kiusalama”.

Huu ni mlolongo wa kauli za ajabuajabu kutoka kwa wenzetu wa Visiwani ambao kwa baadhi yao wanaona Muungano kama ni kuifanya Zanzibar kuwa koloni la Bara.Inasikitisha zaidi kuona kuwa kauli kama hizi zinatolewa huku kukiwa na jitihada za kuwakutanisha viongozi wa serikali kutoka Bara na wale wa Zanzibar kujadili mambo mbalimbali yanayohusu Muungano.Juzijuzi tumesikia Mamlaka ya Usafiri wa Maji na Majini (SUMATRA) ikitimuliwa bila sababu za msingi.Zikafuatia kauli kadhaa za kujichanganya na hata haieleweki nani anasema nini na kwa niaba ya nani.Katika makala yangu moja iliyopita nililaani kauli ya kiongozi mmoja wa juu wa Visiwani kudai kuwa suala la mafuta ni la visiwa hivyo tu,utadhani kwamba hayo mafuta yashaanza kuchimbwa.

Haiyumkiniki kusema kwamba ni huru kwa Wapemba na Waunguja kuamua kukaa sehemu yoyote wanayotaka Tanzania Bara lakini Mpogoro au Mkwere kutoka Bara lazima awe na kibali maalum utadhani anatoka nje ya Tanzania.Nasemaje,hizi ni hujuma za dhahiri dhidi ya Muungano,na kama viongozi wetu wataendelea kuacha mambo yaende kiholela namna hii basi tunaweza kujikuta mahala pabaya.

Binafsi sijui hizi hisia kuwa Bara inanufaika zaidi na Muungano zinatoka wapi!Tatizo la wenzetu wa Zanzibar ni kwamba mtu anaweza kukurupuka na hisia zake asubuhi na kutoa tamko la serikali na baadaye jioni unaweza kusikia mtu mwingine anamkanusha yule wa mwanzo.Lakini naamini kuwa Rais Karume na serikali yake wanayasikia haya,nisichoelewa ni kwanini hawakemei kauli hizi zisizoisha ambazo zinatufanya sie wa-Bara tujihisi kama tumekuwa mzigo kwa wenzetu wa Visiwani.Haiwezekani tukawa tunadhalilishana namna hii kwa visingizio vya usalama na mambo mengine kama hayo.Je Wazanzibari watajisikiaje wakiambiwa kuwa wanapaswa kuwa na vibali maalum vya makazi huku Bara kwa kisingizio cha kukabiliana na wimbi la ujambazi?Hivi kwa busara za hao wanaopiga kelele na kutoa kauli za ajabuajabu wanadhani tukizingatia hali halisi,Bunge la Muungano lingekuwa na idadi iliyopo ya wabunge kutoka huko visiwani?Idadi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam ni takriban mara mbili ya idadi ya wakazi wote wa Zanzibar,hebu tujiulize kuna wabunge wangapi kutoka Dar kulinganisha na wale wa kutoka Zanzibar.

Siku za nyuma niliwahi kuandika kwamba haya mambo ya kuogopana kwa sababu za kuridhishana kisiasa yatatufikisha mahali ambapo hatuwezi kurekebisha mambo.Kasi ya kutatua matatizo ya Muungano ni ndogo sana licha ya ukweli kuwa serikali ya Awamu ya Nne ina Waziri maalum wa kushughulikia suala la Muungano.Vikao visivyoisha vya kujadili Muungano huku watu flani wakiendelea kutoa kauli zisizoeleweka ni sawa na kuendesha kikao cha harusi mwaka mzima huku wanandoa watarajiwa wakitupiana maneno kuwa mmoja wao yuko kwa ajili ya kumnyonya mwenzie na sio mapenzi ya dhati.

Hitimisho langu linaweza kuwa sio la busara lakini pengine linaweza kusaidia kunyamazisha hizi kelele za kila siku dhidi ya watu na taasisi za Bara.Wazanzibari wapige kura ya maoni kama wanataka Muungano (wapige wao na sio sisi kwa vile hakuna anayelalamika huko Bara) na kama wataona Muungano unawazingua waruhusiwe kupewa wanachokihitaji kwa amani.Kama kauli ya wengi itakuwa wanataka kuendelea na Muungano basi wasilete sheria za kibaguzi kama hii ya vibali kwa wa-Bara wanaotaka kuishi huko.

Alamsiki.

KULIKONI UGHAIBUNI-28

Asalam aleykum.

Mwaka 2003 Mmarekani mmoja aitwaye Dan Brown alichapisha kitabu kiitwacho The Da Vinci Code ambacho baadaye kilipelekea kutengenezwa kwa filamu iliyobeba jina hilohilo.Hadi mwezi Mei mwaka huu zaidi ya nakala milioni 60 za kitabu hicho zimeshauzwa sehemu mbalimbali duniani.Idadi hiyo ni sawa na nakala moja kwa kila Mtanzania na bado nyingine kibao zitasalia.Nayo filamu ya Da Vinci Code iliyotolewa mwaka huu hadi kufikia tarehe 14 ya mwezi Agosti ilikuwa imeshaingiza dola za kimarekani 749,975,451 (sijui ni sawa na shilingi ngapi za huko nyumbani).Vyote viwili,kitabu na filamu,vinazungumzia mambo ambayo kwa namna flani ni kama kashfa dhidi ya Kanisa Katoliki.Brown anadai kuwa Kanisa hilo limekuwa likificha ukweli kuhusu maisha halisi ya Yesu Kristo na kwamba kwa makusudi makao makuu ya kanisa hilo huko Vatican yamekuwa yakifanya hivyo (kuficha ukweli) ili yaendelee kuwa na nguvu za kiutawala ulimwenguni.Huyu jamaa ametengeneza marafiki na maadui wa kutosha kwa utunzi wake huo.Nimekisoma kitabu chake,na mie ni Mkatoliki,kwa hiyo naomba mniruhusu nisieleze “upuuzi” uliomo kwenye kitabu hicho.Si unajua tena,mambo ya dini ni imani,sasa mtu akianza kuleta maswali ya ajabuajabu anakuwa anawakwaza wale wengine ambao utotoni kwenda kanisani hadi watishiwe kunyimwa chakula na wakisinzia kidogo tu wanalambwa na shetani (lugha za kidini hizo…samahani kwa ndugu zangu wapagani).

Ilipotoka filamu ya Da Vinci Code ulizuka mjadala miongoni mwa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Wakristo,hususan Wakatoliki.Kuna wale waliowataka waumini waisusie filamu hiyo kwa vile inamtukuna Yesu.Walisema kwamba kuiangalia filamu hiyo kunaweza kuathiri imani zao hasa kwa vile madai yaliyomo kwenye filamu hiyo ni mazito mno na hayazungumziki katika lugha za kiroho.Wengine wakadai kwamba ili kuweza kuapambana na hoja za mwandishi huyo ni muhimu kwa waumini kuiona filamu hiyo.Walidai kuwa mtu atakaepoteza imani yake kwa vile tu ameamini aliyoyaona katika filamu hiyo basi atakuwa na matatizo yake binafsi…kwa lugha za kanisani wanaita imani haba.Nadhani kundi hili la pili ndio lililopata wafuasi wengi zaidi,yaani watu wenye imani zao thabiti ambao walikwenda kuiona filamu hiyo kwa malengo ya kuelewa madai yaliyomo na kujiweka katika nafasi nzuri kuyakabili.Mimi sijapoteza muda wangu kuiangalia,sio kwa kuhofia kuiyumbisha imani yangu.Ni kwa vile tu nilishasoma kitabu ambacho kimsingi ndicho asili ya filamu hiyo.Kama nilisoma kitabu hicho na msimamo wangu haukuyumba basi ni dhahiri filamu hiyo isingebadili kitu kwangu.

Huko nyumbani tumepata kiji-Da Vinchi Kodi chetu kwa jina la Darwin’s Nightmare.Mengi yameshasemwa kuhusu filamu hiyo na mimi sitaki kuyarudia hapa.Nachotaka kukizungumzia hapa ni unafiki unaozunguka suala hilo.Hivi filamu hiyo si ilirekodiwa huko Mwanza?Hivi samaki si ndio maliasili zetu?Hivi Waziri wa Maliasili na Utalii Anthony Diallo hatoki Mwanza huyo?Alikuwa wapi hadi Rais Kikwete aikemee filamu hiyo?Huyu ni mguswa wa karibu kabisa wa sakata la mapanki.Na isieleweke kuwa namshikia bango.Hapana,ila nashindwa kuacha kushangaa kuwa Diallo ambaye alikuwa Naibu Waziri na Mbunge wakati filamu hiyo inatengenezwa na kutolewa mwaka juzi,angeweza kuwa na kisingizio cha kuakaa kimya katika awamu iliyopita kwa vile hakuwa wizara inayohusika na samaki au mapanki.Sasa ndio yuko wizara husika na yeye anatoka Mwanza.Kwanini alikuwa kimya muda wote huu?Kwanini kwa mfano,wataalam wa kompyuta wa wizara yake hawakuweka msimamo wa serikali alipoingia madarakani badala ya kusubiri kauli ya Rais?Naomba nisisitize tena kuwa namtaja Diallo kwa vile ni wa kutoka Mwanza na Wizara yake ndio inahusika na mambo ya samaki,na Darwin’s Nightmare imegusia maeneo hayohayo:Mwanza na samaki (mapanki).Na Zakia Meghji nae si ndiye alikuwa waziri wakati huo?Japo si mwenyeji wa Mwanza lakini yeye ni Mtanzania,na alipaswa pamoja na watendaji wake kuzuia utengenezaji wa filamu hiyo (iwapo ilikuwa muhimu kufanya hivyo) na iwapo Hubert Sauper alidanganya dhamira yake,basi Meghji na timu yake walipaswa kuwa wa kwanza kuizungumzia filamu hiyo.Waziri wa Maliasili na Utalii ni miongoni mwa wenye dhamana ya kulinda na kutetea vivutio vyetu (maliasili) na kuvutia wanaotaka kutembelea nchi yetu (watalii).Ina maana kabla ya kauli ya Rais Kikwete Mengji na baadaye Dialo walikuwa hawajui lolote kuhusu filamu hiyo?

Kuna mlolongo wa watu wengine kadhaa ambao kimsingi walikuwepo wakati filamu hiyo inatengenezwa na walikuwa wanajua kabisa maudhui yake,lakini hatujawahi kuwasikia wakisema lolote kuhusu filamu hiyo.Hivi viongozi wa serikali ya Awamu ya Tatu walikuwa hawajui kabisa kuwa kuna mtu anatengeneza filamu ambayo inaweza kuchafua jina la nchi?Sauper hakuja kwa kutumia ungo na kutengeneza filamu hiyo usiku wa manane,kisha kuondoka tena kwa ungo alfajiri.Aliomba viza kwenye ubalozi wa Tanzania huko alikotoka,alieleza anachokwenda kukifanya Tanzania,na akapewa viza na maofisa ubalozi ambao pia ni Watanzania.Aliingia Tanzania kupitia sehemu ambazo zinadhibiti wageni,yaani jamaa wa Idara ya Uhamiaji walimruhusu jamaa huyu.Wizara na mamlaka husika huko Mwanza zitakuwa zilimpatia kibali cha kutengeneza filamu hiyo baada ya kuelezwa maudhui ya filamu hiyo.Sasa hawa wote waliohusika wamekuwa wapi siku zote hizi?Kuwalaumu washiriki wazawa kwenye filamu hiyo ni kuwaonea.Wao walikuwa wanataka malipo ya ushiriki kwenye filamu hiyo.Na kwanini wasishiriki kama serikali yao ilimpa ruhusa mtengenezaji kuendelea na kazi hiyo?Eti tovuti ya Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa anakotoka Sauper ndio nayo imezinduka kueleza “ukweli” kuhusu filamu hiyo.Watueleze kwanini walimpa viza huyu jamaa,au ndio wanataka kutueleza kwamba hawana namna yoyote ya kuthibitisha dhamira halisi ya wageni wanaoomba kuja Tanzania?Mungu aepushie mbali,lakini hivi Sauper angekuwa ndio gaidi Osama sijui ingekuwaje!!!

Haiwezekani kila jambo lisubiri tamko la Rais wakati kuna lundo la watu wanaolipwa mishahara minono na kutembelea mashangingi lakini hawawajibiki ipasavyo.Nimesikia kuwa kuna tume imeundwa kufuatilia sakata la filamu hiyo.Bila kuathiri utendaji wa tume hiyo nadhani makala hii itakuwa na msaada kwao,na ni matarajio yetu kuwa matokeo ya tume hiyo hayatamwonea haya mhusika yoyote yule.Ukweli au unafiki wa Darwin Naitimea hautofautiani sana na ule wa kwenye Davinchi Kodi.Inategemea unataka kumwamini nani na nini na kwa sababu gani.Lakini tunaloweza kukubaliana ni kwamba hawa wanaolala mpaka wakurupushwe na kauli za Rais ni watu wanaoweza kukwamisha kasi mpya,nguvu mpya na ari mpya ya serikali ya Jakaya.

Alamsiki

KULIKONI UGHAIBUNI-27

Asalam aleykum,

Hivi karibuni,serikali ya hapa ilitoa idadi ya raia wa kigeni walioingia nchini humu kutoa nchi za Ulaya za Mashariki ambazo ziliingizwa kwenye Jumuiya ya Ulaya mwaka juzi.Wengi wa wageni hao ni kutoka Poland na serikali imekiri kuwa idadi ya walioingia imekuwa zaidi ya matarajio ya awali.Tayari kumeanza mijadala kuhusu athari za kuruhusu wageni hao kuja kwa wingi namna hiyo.Hofu imeongezeka zaidi kutokana na ukweli kwamba siku chache zijazo nchi za Bulgaria na Romania nazo zitajiunga na Jumuiya hiyo na hivyo raia wake kuwa huru kuja hapa kutafuta maisha.Kuna dalili kwamba serikali ya Uingereza itaweka udhibiti dhidi ya raia wa nchi hizo mbili kutokana na hofu kwamba bila kufanya hivyo mambo yatakwenda mrama.

Mjadala huu wa sasa unanikumbusha ule uliojitokeza miaka michache iliyopita kuhusu iwapo nchi hii iache kutumia sarafu yake (Paundi) na badala yake itumie ile ya Jumuiya ya Ulaya (Euro).Kwa nguvu ya hoja za wananchi,serikali ikabidi iendelee na Paundi ambayo ndio inayotumika hadi hivi sasa.Mara nyingi hawa wenzetu wanathamini kusikia hoja za wananchi kabla ya kuchukua maamuzi kuhusu masuala yanayohusu maslahi ya taifa.Japokuwa kuna nyakati sauti ya wengi huwa inapuuzwa-kwa mfano upinzani mkubwa wa Waingereza dhidi ya vita vya Iraq na ukimya wa serikali ya hapa kuitaka Israel iache mashabulizi dhidi ya Lebanon- mara nyingi masuala yanayogusa maisha ya kila siku ya wananchi hutengenezewa mazingira ya mjadala.

Huko nyumbani kuna mambo kadhaa ambayo kwa mtizamo wangu yanahitaji kufanyiwa mjadala kabla hayajachukuliwa maamuzi.Hapa ntayazungumzia mawili,na ntatilia mkazo kwenye moja kati ya hayo mawili.La kwanza,je Tanzania ichague uanachama wa SADC au Jumuiya ya Afrika Mashariki linapokuja suala la mgongano wa kisheria na masuala ya ushuru?Na la pili,je kuna umuhimu kuanza kuzungumzia muungano wa kisiasa wa nchi za Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2010 huku hiyo jumuiya ya ushirikiano kati ya nchi hizo bado iko katika mwendo wa kusuasua na mafanikio ya uanachama wetu hayajawekwa bayana?Kuhusu hilo la kwanza nadhani serikali inapaswa kuangalia faida na hasara za kuwemo au kutokuwemo kwenye aidha SADC au EAC,au pengine kurejea COMESA,lakini pia isisahau kuwa wadau wakuu ni Watanzania,hivyo ni muhimu kuwapatia fursa ya kutoa mawazo yao.Na nikisema kuwapatia fursa wananchi simaanishi kupitia kwa wabunge wao (inabidi niwe makini hapa kwa vile hawa waheshimiwa hawataki kutajwa vibaya).Natambua kuwa kuitisha kura ya maoni ni zoezi linalohitaji fedha nyingi lakini hata mashangingi ya waheshimiwa wetu nayo yametugharimu fedha nyingi.

Kwa mtizamo wangu hili la muungano wa kisiasa wa nchi za Afrika Mashariki halina nafasi kwa muda huu.Pengine badala ya kuzungumzia muungano huo ni vema tukaelekeza nguvu zetu kuboresha Muungano wetu wenyewe baina ya Bara na Zanzibar ambao kwa hakika una matatizo lukuki.Hivi tujiulize,tangu Ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki uanzishwe sisi kama Watanzania tumenufaika vipi.Nikitoa jibu la harakaharaka ni kwamba kumekuwa na Wakenya wengi zaidi hapa nchini waliochukua nafasi za kazi ambazo pengine zingeweza kujazwa na Watanzania,na japo sijafika Kenya au Uganda nasikia kuwa ni nadra kukuta Meneja au Mhasibu wa Kitanzania katika nchi hizo.Msiniite mbaguzi lakini tuwe wakweli.Hivi inaingia akilini kweli kwa mgeni kuwa na kazi wakati mwenyeji anakosa nafasi hiyo?Kukurupuka kuridhishana kisiasa sio jambo la busara.Maamuzi ya kisiasa yameshatugharimu huko nyuma na ni vema tukayaepuka.Haihitaji digrii ya uchumi kuelewa kwamba kwa hali ilivyo sasa washirika wenzetu kwenye EAC wananufaika zaidi yetu.Labda manufaa ya maana tunayopata ni kwa watoto wa vigogo kwenda kujazana kwenye shule za wenzetu.Sasa sijui hilo linawanufaishaje wakulima wa mpunga kule kwetu Ifakara.

Sina maana kwamba ni dhambi kushirikiana na majirani zetu bali cha muhimu ni kwamba ushirikiano huo uwe wa manufaa kwetu.Hebu tuseme ndio tunakubaliana kuwa na muungano wa kisiasa wa nchi hizi tatu,kuna kikubwa gani tutakachokipata ambacho hakipatikani kwenye muungano wetu wa kisiasa na Zanzibar?Tukumbuke kuwa sisi ndio kwanza tunajaribu kuuzowea uchumi wa soko huria ambapo kwa wenzetu wa nchi kama Kenya hilo limekuwa sehemu ya maisha yao kwa miongo kadhaa.Ni dhahiri kuwa wenzetu wanatumia uzoefu wao kunufaika zaidi kwenye ushirikiano wa namna hiyo.Ipo hatari ya kujikuta ni wanajumuiya wenzetu waliojazana kwenye makampuni ya wawekezaji yaliyoko Tanzania hasa katika zama hizi za uwekezaji ambapo mwekezaji habanwi kumpendelea mzawa katika kutoa ajira.Kuna Watanzania wangapi wanaofanya kazi Kenya na Uganda tukilinganisha na raia wa nchi hizo waofanya kazi hapo nchini?Hatuwezi kuwalaumu wao kuja nchini kutafuta maisha kwa vile kama mtu una sifa zinazostahili na mazingira yapo ya kwenda kutafuta maisha nje ya nchi yako,kwanini usifanye hivyo?

Hivi wabunge wa kutoka Tanzania walioko kwenye Bunge la Afrika Mashariki wamekuwa wanafanya jitihada gani za kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika na kuwamo kwenye Jumuiya hiyo?Simaanishi kuwa wanakwenda kwenye vikao vya bunge hili kuchukua posho zao tu bali ninafikiri wana jukumu kubwa la kuwaelimisha wanaowawakilisha kuhusu,kwa mfano,nafasi mbalimbali zinazoweza kuchukuliwa na Watanzania huko Kenya na Uganda,iwe ni katika ajira au kibiashara na hata kutueleza bidhaa zetu zinafanyaje kwenye masoko ya washirika zetu.Jumuiya ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki imekuwa zaidi kwenye kauli za wanasiasa wetu kuliko akilini mwa wananchi wa kawaida ambao kimsingi ndio wanaonufaika au kuathiriwa na uanachama wetu kwenye jumuiya hiyo.

KULIKONI UGHAIBUNI-26

Asalam aleykum,

Hapa ni shwari japokuwa usafiri wa anga umekuwa ni kama adhabu vile tangu zipatikane taarifa kwamba kuna kundi la watu lililokuwa linapanga kulipua ndege kadhaa.Huwezi kuzilaumu taasisi zinazohusika na usafiri na usalama kwa kuchukua hatua ambazo kwa namna flani ni kama bughudha kwa wasafiri kwa vile pindi wakizembea kidogo tu basi kuna hatari ya watu kupoteza maisha yao.Wachambuzi wa mambo wanasema wakati magaidi wanahitaji kosa moja tu kutimiza azma yao vyombo vya usalama vinahitaji kila sekunde kuwa makini kuwazuia magaidi kutekeleza azma yao.

Ni kutokana na kuongezeka kwa matishio ya mashambulizi ya kigaidi shirika la ujasusi la Uingereza (MI6) lililazimika hivi karibuni kuvunja mwiko wake na kutangaza hadharani nafasi za kazi za ushushushu.MI6 ilikiri kwamba inahitaji nguvukazi zaidi ili kuweza kumudu kwa ufanisi zaidi majukumu iliyonayo ya kuilinda nchi hii.Kabla ya hapo shirika hilo lilikuwa na njia zake za siri za kuajiri watumishi wake.Pamoja na MI6 ambayo kimsingi kazi yake kubwa ni kuzuia matishio ya kutoka nje ya nchi,patna wake MI5,shirika la ushushushu wa ndani,kwa pamoja wameanza kujitokeza hadharani zaidi ili kupata sapoti ya wananchi ambao kama ilivyo kwa nchi nyingi duniani huyaangalia mashirika kama hayo kwa wasiwasi na uoga.Sababu kuu ni kwamba wengi hawajui umuhimu wa taasisi hizo muhimu kwa ustawi wa taifa lolote lile.Hali ni tofauti kidogo nchini Marekani ambapo mashirika mawili makuu (wana mlolongo wa taasisi za kishushushu) yaani FBI na CIA yamekuwa wazi kwa kiasi flani ukilinganisha na katika nchi nyingine.

Huko nyumbani,hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alimteua Bwana Rashid Othman kuwa Mkuu mpya wa Idara ya Usalama wa Taifa.Kwa baadhi ya sie tuliopo Uingereza tunamfahamu Mheshimiwa huyo kwa vile alikuwa mwambata kwenye Ubalozi wetu wa London,na Watanzania wengi hapa wameupokea uteuzi wake kwa furaha kwa vile alikuwa mchapakazi na mtu wa karibu kwa wengi.Kingine kilichowagusa wengi ni kauli yake kwamba atakuwa anakutana na waandishi wa habari kubadilishana nao mawazo sambamba na mkwara aliowachimbia majambazi.Baadhi ya vyombo vya habari viliporipoti uteuzi na kuapishwa kwa Bwana Othman vilionyesha kukunwa na dhamira ya kiongozi huyo na taasisi yake kuwa karibu zaidi na wananchi katika harakati za kukabiliana na maovu katika nchi yetu.
Wengi wetu tumekuwa na hisia potofu sana kuhusu Idara ya Usalama wa Taifa.Siku za nyuma wapo waliokuwa wanaamini kuwa maofisa usalama ni watu waliokuwa wakuenda baa kuhesabu visoda vya bia kuwatambua watu wanaotanua (wanaotumia fedha pengine zaidi ya kawaida).Wapo pia wale waliokuwa wanadai kuwa mashushushu ni wanyonya damu (sijui hiyo damu ilikuwa inapelekwa Muhimbili au wapi).Baadhi ya wanaozijua ofisi za taasisi hiyo wamekuwa wanaogopa hata kuziangalia utadhani wakifanya hivyo watapigwa risasi.Kwa kifupi,japokuwa taasisi hiyo ni ya Kitanzania na watumishi wake ni Watanzania wenzetu imekuwa ikichukuliwa kama imetoka nje ya dunia.

Kiutamaduni,taasisi za usalama zinafanya kazi zake kwa siri.Na ni kwa usiri wa aina hiyo ndio unasikia MI6 na wenzake wanaweza kuokoa maisha ya watu waliokuwa wanapanga kulipua ndege pamoja na matukio mengine ambayo laiti yangetokea basi mamia na pengine maelfu ya watu wangepoteza maisha yao.Wapo wanaosema kwamba wakati wa mapambano dhidi ya ukaburu huko bondeni (Afrika Kusini),makaburu walitaka sana kuihujumu Tanzania hasa kutokana na mchango wake katika mapambano hayo lakini Idara ya Usalama wa Taifa ilisimama kidete kukabiliana nao hadi mwisho.Inasemekana pia kwamba japo wengi tunaamini kwamba Watanzania ni watu wa amani kwa asili,mchango wa taasisi hiyo katika kuiweka nchi yetu kuwa kisiwa cha amani ni mkubwa sana.Wachambuzi wa mambo ya usalama wa kimataifa wanabainisha kuwa utulivu katika nchi ni kigezo muhimu cha ufanisi wa idara yake ya usalama wa taifa.

Itakuwa tunawaonea tukiwalaumu wale wanaodhani mashushushu ni wanyonya damu au wale wanaoogopa kuzitazama ofisi au magari ya idara hiyo utadhani wakifanya hivyo watapigwa na radi.Wanapatwa na hisia hizo kwa vile hawajui kinachofanywa na taasisi hiyo.Hatuwezi pia kuilamu idara hiyo kwa kuwaacha watu waiogope kwa vile kazi ya kubadilisha mawazo ya watu inaweza kuchukua karne nzima na pengine bila mafanikio.Hata huko Marekani ambako taasisi kama CIA na FBI ziko wazi kiasi haimaanishi kuwa watu hawana mawazo ya ajabuajabu dhidi ya taasisi hizo.La muhimu hapa sio nani alaumiwe au kuwa na uoga ni kosa au dhambi.La muhimu ni mahusiano bora kati ya taasisi hiyo na wananchi.Wengi wetu tunawaogopa polisi lakini tunapopata matatizo tunakwenda kwenye vituo vya polisi.Pengine badala ya kuendelea na uoga wananchi wanapaswa kuzisaidia taasisi zinazowalinda.Kinachohitajika ni utaratibu tu wa namna mchango wa wananchi wa kawaida unaweza kuwasilishwa.
Yayumkinika kusema kwamba wananchi wengi wana imani kubwa na taasisi hiyo nyeti.Nasema hivyo kwa sababu pindi Rais Kikwete alipotangaza kuwa vita dhidi ya rushwa na ujambazi itaijumuisha pia Idara ya Usalama wa Taifa na kwamba watu wanaweza kupeleka majina ya watuhumiwa kwenye ofisi za taasisi hiyo wananchi wengi walipata imani kuwa sasa mafaniko yanaweza kupatikana hata kama itachukua muda kidogo.Kama alivyosema Bwana Othman baada ya kuapishwa,wananchi wa kawaida wana mchango mkubwa katika ustawi na usalama wa nchi yetu hasa kwa vile wale wanaotunyima usingizi (majambazi),wanaogeuza ndugu zetu kuwa mazezeta na nusu-wafu (wauza unga),wanaokwamisha maendeleo yetu na kuminya haki zetu (wabadhirifu na wala rushwa) ni watu tunaoishi nao.Ni dhahiri basi kwamba ushirikiano kati ya wananchi na taasisi za usalama ni wa manufaa makubwa kwa kila mmoja wetu.

Alamsiki.

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget