KULIKONI UGHAIBUNI-33
Asalam aleykum,
Majuzi nilipata barua pepe kutoka Uholanzi ikinieleza kwamba jina langu limepitishwa katika bahati nasibu ya Jumuiya ya Ulaya na “nimebahatika” kuwa mshindi wa Euro milioni moja!Wahusika waliniomba kuwapatia taarifa za akaunti yangu ya benki ili waweze kuingiza kitita hicho.Unaweza kudhani kwamba labda nilipiga kigelegele cha furaha kwamba hatimaye Mndamba mie nimekuwa milionea.Umekosea.Kabla hata ya kumaliza kuiosma barua hiyo niliamua kuifutilia mbali.Utapeli wa namna hiyo umetawala sana huku ughaibuni na wapo “wanaoingia mkenge” na kuwaamini matapeli wa aina hiyo kabla ya kuangua kilio badala ya kicheko baada ya kugundua kuwa taarifa za akaunti zao ziliombwa ili matapeli hao waibe fedha kwa utaalamu wanaoujua wao.
Njia mojawapo ya kubaini utapeli wa watu hao ni kutafuta habari zaidi kuhusu jina la kampuni husika.Na sio kazi ngumu.Kwenye mtandao kuna kitu tunachoweza kukiita “injini ya kutafia habari” (search engine).Maarufu zaidi ni Google,lakini kuna nyingine kadhaa kama Yahoo!,MSN,Ask,nk.Kwa hiyo ukitaka kutafuta habari zangu unataipu “CHAHALI” halafu unabonyeza “tafuta” na hapo utapata habari mbalimbali zinazohisana na jina hilo.Nyingine zitakuwa zinanihusu asilimia 100 na nyingine zitakuwa zinakaribiana na ukweli huku nyingine zikiwa haziusiani nami kabisa.Kwa hiyo nilipotaipu jina la kampuni hiyo ya bahati nasibu nikakuta taarifa kibao kuhusu utapeli wao ambao kwa “lugha ya mama” unaitwa “scam.”Waliobobea zaidi kwenye scamming ni Wanaijeria,na yayumkinika kusema kuwa utapeli wao kwenye mtandao ni maarufu zaidi kuliko timu yao ya Taifa.
Kwanini watu wanaamini scammers hadi kutoa taarifa zao za siri?Jibu jepesi ni kwamba ni rahisi kumtapeli mtu binafsi kuliko kundi la watu.Kosa kubwa wanalofanya scammers hao ni kutuma barua pepe zinazofanana kwa watu wengi,na japo wapo wanaotokea kuwaamini lakini wapo pia watu ambao huwa wanajihangaisha kutafuta ukweli kwenye mtandao kama nilivyofanya mimi.Walengwa na waathirika wakubwa wa vitendo hivyo vya kitapeli ni watu binafsi,na ni nadra sana kusikia taasisi flani imedanganyika na kukubaliana na matapeli hao.
Wanasema maajabu yote yanawezekana katika nchi inayoitwa Tanzania.Matapeli flani wameivaa serikali wakidai wana kampuni yenye makao makuu huko Houston,Texas nchini Marekani na kupata tenda ya kuleta majenereta kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la mgao wa umeme.Hapa naizungumzia kampuni ya Richmond Development Company.Niliposoma habari za kampuni hiyo kwa mara ya kwanza nilikimbilia kwenye Google kutafuta habari zaidi kuhusu waungwana hao.Nikaambulia patupu.Nikajaribu kutafuta habari za makampuni yanayojihusisha na biashara ya majenereta kwenye jimbo la Texas,napo nikaambulia patupu.Hata nilipojaribu kutafuta habari hizo kwa Marekani nzima nikitumia aidha jina la kampuni hiyo,au aina ya shughuli wanazofanya,bado nilitoka kapa.
Sasa hivi serikali yetu hii ya awamu ya nne inataka kutuambia iliingia mkataba na kampuni hiyo bila hata kuhakiki iwapo kweli ipo hai?Tuna mabalozi wawili nchini Marekani,moja akituwakilisha kwenye nchi hiyo na mwingine ikituwakilisha kwenye Umoja wa Mataifa.Kwanini mabalozi hao hawakuulizwa kabla ya kuingia mkataba na kampuni hiyo iliyodai ina makao yake makuu nchini humo?Au kwanini hawakuagizwa kufuatilia ukweli huo baada ya dalili kuanza kuonyesha kuwa jamaa hao ni wababaishaji flani?Hata kama mabalozi wetu walikuwa bize,tuna Watanzania lukuki wanaoishi Houston na hao wangeweza kuwa wa msaada sana kujua habari za kampuni hiyo.Hivi jamani,si majuzi tu Rais alikuwa Marekani na kundi kubwa tu la Watanzania?Sasa kwanini ziara hiyo nayo haikutumika kama mojawapo wa njia za kufahamu iwapo kama kampuni hiyo ipo kweli?
Kwa kweli habari hizi zinasikitisha sana kwa sababu kwa namna flani zinakinzana na ahadi iliyotolewa na serikali ya Awamu ya Nne kwamba itakuwa makini kabla ya kuingia mikataba hasa na makampuni ya kigeni.Hadi leo hatujui nani hasa aliyesaini mkataba na IPTL kwa sababu kila mmoja anamtupia mzigo mwenyewe ilhali kuna mamilioni ya fedha za walipakodi zinazoendelea kumwagwa kwa kampuni hiyo kwa sababu tu kuna mtu alisaini mkataba utadhani alikuwa usingizini.Hivi huyo alompatia taarifa Rais Kikwete kwamba majenereta yangewa sili Jumapili ileee ni nani,na hadi sasa amechukuliwa hatua gani.Je huyo aloingia mkataba na kampuni hiyo (kwa vyovyote atakuwa ni binadamu Mtanzania,na sio kompyuta au jinni) anatueleza nini kuhusu hiki kizungumkuti kinachochafua azma ya “maisha bora kwa kila Mtanzania”?
Yafuatayo ni mawazo yangu binafsi,na naomba atakayeguswa asikimbilie mahakamani kudai gazeti hili limemkashifu.Waziri Msabaha,Naibu wake na maofisa wa ngazi za juu wa Wizara ya Nishati wanawajibika moja kwa moja katika sakata hili,na wana maswali ya kujibu kwa Watanzania.Mabadiliko ya Wizara yanaweza kuwa njia flani ya kuwaokoa watu kujibu maswali magumu lakini kwa vile bado wako katika serikali hii basi ni lazima tuambiwe ukweli na baadaye hatua sahihi zichukuliwe dhidi yao.Karamagi ana majibu mepesi kabisa kwa maswali kuhusu utapeli wa kampuni hiyo, “Mimi sikuwa Waziri katika wizara hii wakati mkataba huo unasainiwa”,na hiyo ni sahihi kwake kusema hivyo japo anaweza kulivalia njuga swala hilo ili kujua lilianzwa vipi,nani alipewa nini na hatimaye nini kifanyke dhidi ya wahusika.
Watanzania wanachezewa kwa vile ni wakimya sana.Hata wakiwa na maswali yanayohitaji majibu lakini wanaopaswa kujibu wanakaa kimya bado Watanzania wataishia kusema chinichini tu.Na hiyo ndio inawapa watu flani jeuri ya kuboronga mambo kwa vile wanajua wananchi watakaa kimya na waliowateaua hawatawawajibisha.Hakuna kauli yoyote iliyotolewa na serikali kuhusiana na sakata la kampuni ya Richmond.Hatujaambiwa hatua gani zimeshachukuliwa dhidi ya wamiliki wake hasa huyo mmoja anayedaiwa kuwa Mtanzania.Wito wangu kwa Rais Kikwete ni kwamba kuwakalia kimya watu wanaochafua jina la serikali yako ni sawa na kuwaomba Watanzania waanze kupoteza imani yao kwako mapema kabla hata serikali yako haijatimiza mwaka mmoja madarakani.Sina kinyongo na mabadiliko ya baraza la mawaziri kwa vile ni haki ya kikatiba ya Rais kufanya hivyo japo sijui kama zile ziara zilizofanywa na Rais kwenye kila wizara (kuwaelekeza mawaziri na watumishi wa wizara hizo nini wanapaswa kufanya) na hatimaye kufuatiwa na semina huko Ngurdoto zimezaa matunda gani.Kama (nasisitiza KAMA) mabadiliko hayo yametokana na dalili kwamba baadhi ya mawaziri wamezidiwa na kasi mpya,nguvu mpya na ari mpya basi ufumbuzi sio kuwabadilishia wizara bali kuwatimua.Kuna maelfu ya Watanzania wenye uwezo ambao hawahitaji kuambiwa “hii ndio nafasi yako ya mwisho,ukiboronga nakutimua” ili wawajibike ipasavyo.
Naamini Jakaya anatambua deni alilonalo kwa Watanzania,na naamini anafahamu kuwa baadhi ya matendo ya aliowateuwa yanawachefua wanaompenda.Chaguo liko kwake:kuwaridhisha waliomchagua au aliowachagua yeye.Ukiniomba nitegue kitendawili hicho,ntakwambia kuwa Jakaya atawarukia kama mwewe hao wanaotaka kuifanya kauli-mbiu ya “maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana” ionekane kuwa kiini macho.
Ramadhan Karim
Kwa makala zilizopita za “KULIKONI UGHAIBUNI” tembelea http://chahali.blogspot.com au http://chahali.livejournal.com
Monday, 13 November 2006
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment