Unafiki wa viongozi wetu wa dini
na evarist chahali, uskochi
MADA yangu ya leo, najua dhahiri itawakera wateule wachache wa aina fulani. Lakini kabla ya kuwapasha, naomba nizungumzie suala la imani na dini hapa ninapoishi Ughaibuni.
Nilipofika hapa kwa mara ya kwanza, nilionyeshwa majengo kadhaa ambayo huko nyuma yalikuwa Makanisa, lakini sasa yamegeuzwa kuwa kumbi za disko na klabu za usiku.
Na hao walioyageuza Makanisa hayo kuwa sehemu za starehe, wala hawakujishughulisha kabisa katika kubadili mwonekano wake, bali wameyaacha yatoe ushuhuda kuwa huko nyuma yalikuwa sehemu za ibada.
Nilipofanya udadisi kwa wenyeji, niliambiwa kwamba makanisa hayo yaliuzwa baada ya kuwa matupu kutokana na ukosefu wa waumini. Wengi wa waumini wa makanisa ya mji huu ninaoishi, ni ama wahamiaji waliotoka nje ya nchi hii kama mimi, na au vikongwe vya hapa hapa.
Binafsi, sina majibu ya moja kwa moja kwamba tatizo la hawa wenzetu ni nini. Hata hivyo, ninachofahamu ni kwamba kuna watu kadhaa ambao wanajitambulisha kuwa hawana dini, na au hawaamini kuwapo kwa Mungu.
Imani ni suala la mtu binafsi, na hivyo pengine si mwafaka kuhoji kwa nini fulani anaamini, ama haamini kuwapo au kutokuwapo kwa Mungu.Ingawa binafsi, ni muumini kwa aina fulani, huwa sisiti kuwasifu wale wasiowaumini wa dini yoyote, lakini wasioona aibu kuelezea msimamo wao wa kidini. Kwa lugha nyingine, watu hao si wanafiki. Wanaeleza bayana kile wanachokiamini na kutokiamini.
Kuna tatizo la msingi huko nyumbani, ingawa natambua dhahiri kwamba watu wengi hawapendi kujadili mambo ya dini kwa sababu ile ile ya unafiki!
Baadhi ya viongozi wetu wa dini, wamekuwa mstari wa mbele kukemea wale ambao wanakwenda kinyume na imani zao, lakini viongozi hao hao wakishiriki kwenye maovu wanayoyakemea.
Ndiyo, tunatambua kwamba mara nyingi viongozi wetu wa dini wana wafadhili wao nje ya nchi. Lakini hicho si kigezo cha wao kuishi maisha tofauti kabisa na wafuasi wao.
Utakuta katika kijiji fulani ambacho kimegubikwa kabisa na umasikini, kiongozi fulani wa dini yeye akiishi kama yuko peponi. Na bila huruma, huyo huyo anayeishi maisha kama ya peponi katikati ya waumini masikini, kwa kutumia kisingizio cha maandiko matakatifu, anawashurutisha waumini wake kujipigapiga ili kuongeza sadaka wanazotoa.
Kinachokera zaidi, ni hili suala la baadhi ya viongozi wa madhehebu fulani kuwa na watoto mitaani, huku sheria za madhehebu yao zikiwa haziwaruhusu kufanya hivyo.
Tatizo hili ni sugu sana, hususan maeneo ya vijijini. Kinachosikitisha ni ukweli kwamba waumini wanafahamu kwamba kiongozi wao wa dini, anaishi kinyume na maadili ya huduma yake, lakini hawachukui hatua yoyote zaidi ya kulalamika chini chini.
Binafsi, ninayo mifano hai ya baadhi ya viongozi wa madhehebu yangu ambao wana watoto lukuki mitaani. Baadhi yao wanatoa huduma kwa wazazi wa watoto wao hao, lakini wengine wamewatelekeza kabisa.
Hawa watu ni wanafiki ambao hawastahili kuachwa waendeleze uhuni kwa kisingizio kwamba daraja walilofikia, haliwezi kutenguliwa.
Mitume wetu waliishi maisha ya uadilifu, ambayo yalishabihiana kwa asilimia 100 na kile walichokuwa wakikihubiri. Na si katika suala la uzinzi pekee, bali hata kwenye dili za kibiashara.Majanga kama ya ukimwi yataondoka vipi iwapo baadhi ya wale wanaopaswa kukemea vitendo vya ngono, kwa vile vinavunja amri ya Mungu, nao ni washirika wa vitendo hivyo?
Pamoja na mapungufu waliyonayo baadhi ya viongozi wa dini, hivi karibuni tumeshuhudia wengi wakijitokeza kuungana na Watanzania wenzao kukemea masuala yanayohatarisha umoja wa kitaifa.
Suala ambalo baadhi ya viongozi hao wa dini wanastahili pongezi, ni katika kukemea vitendo vya kifisadi, ingawa tatizo linakuwapo, pale msimamo huo unapokuwa wa kiongozi mmoja zaidi, badala ya kuwa msimamo wa taasisi ya dini.
Katika hili, napenda nichukue fursa hii kumpongeza Askofu Mkuu mpya wa Kanisa la Anglikana Tanzania, ambaye ameweka bayana msimamo wake dhidi ya vitendo vya kifisadi. Hiyo inatia moyo sana!
Licha ya kukemea ufisadi na maovu mengine katika jamii, asasi za dini zinaweza kubadili tabia za waumini wao kwa kuwawekea vikwazo vya aina fulani. Taratibu za aina hiyo, zipo katika baadhi ya imani, kwa mfano, Wakatoliki, ambao muumini akikiuka kanuni fulani, anazuiwa kushiriki baadhi ya sakramenti.
Kwa nini basi tunaendelea kujumuika na mafisadi makanisani, na au misikitini ilhali matendo yao yanalenga kutuumiza kimaisha? Nafahamu kuwa dini zote zinahimiza upendo, lakini hiyo si sababu ya kutowabana wale wasio na upendo kwa Watanzania wenzao.
Inawezekana kwamba kikwazo kikubwa kwa dini zetu kuwa mstari wa mbele katika kukemea maovu na kubadili tabia za wanaokwenda kinyume na maadili ya kimwili na kiroho, ni hofu ya usafi wa baadhi ya viongozi wa dini hizo, kama nilivyoeleza mwanzoni mwa makala haya.Tatizo hilo linaweza kupatiwa ufumbuzi iwapo viongozi wa madhehebu wataepuka mtindo wa kulindana, na hivyo kuchukua hatua kali kwa walio chini yao, ambao wanakwenda kinyume cha kanuni na taratibu za madhehebu.
Ni wazi kwamba viongozi waadilifu wa dini, hawawezi kuogopa kumnyooshea kidole fisadi fulani, kwa kuwa hata kama fisadi huyo atataka kulipa kisasi, atajikuta hana jambo lolote analoweza kulitumia kushusha heshima ya kiongozi wa dini aliyemkemea.
Busara za Kiswahili zinatueleza kwamba kujikwaa si kuanguka, na hata kuanguka si mwisho wa safari. Wito wangu kwa viongozi wetu wa dini, ni kuongeza jitihada za kuwahudumia waumini wao kiroho na kimwili.
Ni muhimu kwa viongozi hao kuishi kama Mitume ambao mafundisho yao yalikubalika na kuvuta watu wengi, kwa vile wao wenyewe walikuwa waadilifu na mifano bora ya kuigwa na wanadamu.
0 comments:
Post a Comment