Friday, 3 July 2009


Mufti Simba aagiza Waislamu waikatae CCM

Mufti Issa bin Shaaban Simba, amekasilishwa na uamuzi wa serikali kuhusu Mahakama ya Kadhi.

Na Ummy Muya

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limesema kutokana na serikali kutupilia mbali ombi la kunzisha Mahakama ya Kadhi, Waislamu hawataipigia kura CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Katika taarifa yake, Bakwata ilifikia hatua ya kusema Waislamu wasimchague Rais Jakaya Kikwete iwapo atasimamishwa na CCM kugombea urais, ikiwa ni pamoja na wabunge na madiwani watakaosimamishwa na chama hicho tawala kutokana na kitendo cha serikali kutupilia mbali hoja ya Mahakama ya Kadhi.

Kauli hiyo imetolewa jana wakati Mufti Issa bin Shaaban Simba alipokuwa akitoa tamko kupinga uamuzi wa serikali kutaka kutumia sheria za dini ya Kiislamu katika mahakama za kawaida badala ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi, kitu ambacho alisema anaamini kitawanyima haki Waislamu.

Alisema serikali imedhihirisha kuwa inaendeshwa na Wakristo na si kweli kama serikali haina dini na akamtaka Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kubatilisha kauli hiyo kwa kuwa inamchafua Rais Jakaya Kikwete mbele ya umma wa Waislamu.

Waziri ametuthibitishia kama Rais Kikwete alikuwa akitulaghai ili tumpigie kura kwa kigezo kuwa suala hilo litashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi na sio kuchanganywa kama ilivyokuwa mwaka 1970 katika Sheria ya Ndoa na kuwanyima haki Waislamu,alisema.

Alisema kwa muda mrefu sana Waislamu wamekuwa kimya wakitumia hekima na busara kudai haki zao, lakini katika hatua hii ambayo serikali imefikia hawapo tayari kuendelea kudhalilishwa na kuwa kitendo hicho ni dhalimu.

Mufti alisema wamekuwa wakiiomba Mahakama ya Kadhi kwa zaidi ya miaka 20 na hivyo hawezi kuendelea kuwa kimya na kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa kwa kuwa mahakama hiyo ni haki yao.

Alisema kauli ya Waziri Chikawe imedhihirisha kuwa serikali ina wenyewe na Waislamu wamewekwa katika tabaka la pili pamoja na Rais Jakaya Kikwete kuwatuliza kwa ahadi kuwa watalipatia ufumbuzi suala hilo.

Natoa wito kwa Masheikh wote nchini na Waislamu wa madhehebu yote kupinga vikali kauli iliyotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na kwamba Waislamu waige mfano wa Waislamu wa Afrika Kusini,alisema Mufti na kuhoji:

Kwa nini iwe Afrika ya Kusini na isiwe Zanzibar, Uganda na Kenya ambazo zipo ndani ya Afrika Mashariki? Kwa niaba ya Waislamu nasema serikali haikututendea haki na imetuchukiza sana,alisema.

Alisema lengo la kuomba mahakama hiyo ni kuhakikisha Waislamu wanashughulikia masuala yao ya ndoa na mirathi na si vinginevyo, hivyo waziri asipotoshe jamii kwa kutumia mifano ambayo haiko sahihi.

Mahakama hii haitawakata wezi mikono kwa kuwa nchi hii ina katiba na sheria na sisi tutazirudisha kesi zote za jinai mikononi mwa serikali. Sifahamu hiyo kamati ambayo waziri alisema alikuwa amekaa na kutoa tamko hilo ilikuwa na watu gani,alihoji.

Aliongeza kuwa kutokana na mapungufu hayo waziri arudi tena na kukutana na masheikh ili apate muongozo wa nini Waislamu wanahitaji na sio kuzungumza bila kuwa na usahihi wa kile anachosema.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya tamko la Bakwata, masheikh walikuwa na mitazamo tofauti. Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum Mussa alisema wapo baadhi ya Waislamu ambao watakubali kutokana na ufinyu wao wa elimu ya dini.

Mussa alisema haoni sababu ya serikali kufanya njia ya mkato katika suala hilo kwani Waislamu wanahitaji Mahakama ya Kadhi kama ilivyo kwa wafanyabiashara ambao wana mahakama yao.

Hukumu inayotolewa katika Mahakama ya Kadhi ni ibada kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume Muhammad (S.A.W) hivyo ni lazima kwa atakayetoa hukumu hiyo awe Muislamu na si vinginevyo,alisema.

Namshanga waziri anapotaka sheria hizi zitumiwe katika mahakama za kawaida. Aliona wapi John akawa imamu,alihoji sheikh huyo wa mkoa wa Dar es Salaam.

Naye katibu wa Bakwata wilayani Ilala, Sheikh Issa Ausi alisema historia iko wazi. Waasisi na wanaharakati ambao waliitoa Tanganyika mikononi mwa wakoloni walikuwa Waislamu, na akahoji sababu za serikali kuwa mstari wa mbele kuwafunga midomo leo.

Bakwata imezinduka sasa Waislamu wote tumeungana katika kupigania haki zetu na kutetea maslahi yetu na serikali itambue kuwa Bakwata iko hai hao Wakristo walikuwa wapi wakati sisi tukipigania uhuru,alihoji.

Wakati huohuo, Sheikh Salum Rwambo alisema anawashangaa wabunge Waislamu ambao baadhi ni mahajat na malhaj wanakaa kimya na kushindwa kutetea hoja za msingi na kudai kuwa huo sasa ndio mwisho wao wa kuwaita masheikh na kutaka waombewe dua ili wasipate wepesi katika kampeni zao.

Sheikh Rwambo pia alimsifia mbunge wa Nzega Lucas Selelii kwamba ni miongoni mwa wabunge katika Bunge hilo wanaozungumza ukweli na kwa kujiamini tofauti na wengine ambao wanaenda kukaa bila kufanya kazi zilizowapeleka .


CHANZO: Mwananchi


KWA MWENENDO HUU SI AJABU KUSIKIA HATA WATANZANIA WALIOAHIDIWA MAISHA BORA NAO WAKAJITOKEZA KUDAI HAWAITAKI CCM....HOJA IKIWA MAISHA BORA YALIYOAHIDIWA YAMEISHIA KWA KUNDI DOGO LA MAFISADI PEKEE!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget