BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA
(TEC)
Mpendwa Msomaji,
Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania inayo furaha kukuletea Ilani hii.
Madhumuni ya matini hii ni kukualika tutafakari pamoja juu ya masuala muhimu yanayotukabili kama Taifa.
Tunawashukuru Wanataaluma Wakristo wa Tanzania walioandaa hati hii.
Kwasababu chaguzi za mwaka 2010 haziko mbali mnaona ni muhimu kupendekeza vipaumbele vyetu kama jamii tukiwaambia viongozi wetu wajao yale ambayo tungependa yafanyike kwa ajili ya jamii yetu. Katika uchaguzi hatupigi kura tu, tunapaswa kueleza makusudio yetu kwa yale tunayofikiri kuwa muhimu sana kwa Taifa.
Kwa kuchapisha Ilani hii tunataka kutekeleza haki yetu ya uzalendo ili kujenga maisha yaliyo mema zaidi kwetu sote katika siku zijazo.
Askofu Mkuu P. Ruzoka
Askofu Mkuu wa Tabora
MWENYEKITI
Tume ya Haki na Amani - TEC
WANATAALUMA WAKRISTO TANZANIA (CPT)
ILANI
MAPENDEKEZO YETU YA VIPAUMBELE VYA KITAIFA
A: Fikra Msingi
Maswali ya msingi
Uchumi na Siasa vipo kwa madhumuni gani?
Chimbuko la uwepo wa mfumo wa kisiasa ni nini?
Dira yetu
Maadili ndio dira yetu msingi ambapo kiini chake ni wanadamu walioumbwa katika sura na mfano wa Mungu, wakiwa na hadhi katika utu wao, haki yao na wajibu zao. Watu ndio kusudio na sababu ya shughuli zote za kiuchumi na kisiasa. Tunu za Ujamaa ambazo ndizo zilizojenga utamaduni wa nchi yetu zinakubaliana kabisa na maoni haya ya kimaadili. Tunu hizo ambazo ni umoja mshikamano, maelewano, mtazamo wa kifamilia (familyhood) zinabeba maana pana zaidi ya itikadi ya kisiasa. Uamuzi wetu wa kuchagua kufuata uchumi wa ujamaa wa kisoshalisti kulituletea matokeo mazuri na mabaya (chanya na hasi), kwa hiyo basi sio vema kudharau na kutupilia mbali kila kitu.
Marekebisho ya sera yanayofanyika sasa ni mengi, na baadhi ni ya lazima na ni mazuri. Lakini sio yote ambayo ni ya kujenga jamii yetu. Tunaweza kuona kuna ukuaji mzuri wa uchumi, lakini panakosekana usawa kwa kiwango kikubwa katika kunufaika na ukuaji huo wa uchumi. Kimsingi kanuni za uchumi wa soko huria sio tu kwamba zina kasoro za kiuchumi na kijamii tu, bali pia kasoro zake zinajionyesha katika maisha ya watu kiutamaduni na kimaadili. Watu wanaona mabadiliko haya kuwa yameingizwa kwa nguvu kutoka nje na hivyo yananufaisha matajiri na wenye uwezo.
Kumekuwa na ongezeko kubwa mno la tofauti/pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho, wanaosonga mbele kimaendeleo na wanaoachwa nyuma. Sera zetu nyingi za sasa zinajiridhisha kuwa msukumo wa maendeleo ni katika ukuaji wa uchumi kwa kutazama fedha taslimu (monetary terms). Kwa hiyo tunatilia mkazo shughuli na mambo yanayoonekana kusaidia ukuaji uchumi. Mtazamo huu ni wa kibepari kabisa.
Matokeo ya kubaki katika mtazamo wetu finyu, kutengeneza sera zetu kwa kuzingatia sekta chache zenye kulenga ukuaji uchumi tu, kumewaacha nje watu wetu wengi. Kuweza kuwachukulia watanzania wote kuwa ndio msingi wa sera zetu za kiuchumi na maendeleo yetu, sio suala la kimaadili tu bali pia inaleta maana kamili kiuchumi. Ni pale tu taifa zima litakaposhiriki katika uzalishaji na katika matumizi ya bidhaa na huduma (faida ya ukuaji uchumi) ndipo tu soko litakapopanuka.
Nchi za Magharibi zimeweza kupiga hatua mbele katika maendeleo ya kiuchumi pale tu walipoweza kupanua na kuimarisha soko lao la ndani, katika maana ya uzalishaji na matumizi. Vile vile kwa uzingatiifu huo huo nchi za Mashariki zimefanikiwa (kama vila Japani, Korea, Vietinam) na hali hiyo hiyo inaonekana wakati huu katika nchi za China, India, Brazil.
Katika Tanzania sisi tunaonekana kufanya kinyume chake. Kuweza kufanya maboresho yenye manufaa, ni lazima tubadili mtazamo wetu kutoka ule wa kukazania ukuaji uchumi tu na badala yake lengo liwe kuinua maisha ya watu wa kawaida: wake kwa waume. Hatuwezi kuwa na matumaini ya kutatua tatizo la umaskini kwa kufikia ukuaji katika sekta chache tu kama ya utalii na madini. Mtindo tunaotumia sasa hauwezi kutusaidia kupunguza kiwango kikubwa cha umaskini uliopo ambao pia umeenea nchi nzima.
Kuzungumzia sekta rasmi na isiyo rasmi ni mfano mmoja wa fikra finyu tuliyo nayo ya kugawa katika matabaka mfumo wetu wa kiuchumi. Kwa kuwa wengi miongoni mwa watanzania wamo katika sekta isiyo rasmi, kwa sababu hiyo wamegeuzwa kuwa watu wasio na umuhimu, ambao kiuchumi thamani yao ni ndogo.
Kitendawili msingi cha Tanzania
Tanzania ni tajiri katika rasilimali na bado watanzania wengi ni maskini. Kwa nini? Hiki ni kitendawili kikubwa ambacho tunapaswa kukijibu.
Umaskini katika Tanzania sio ugonjwa ambao tiba yake haipatikani kwa urahisi. Kwa kweli umaskini tulionao huku tukiwa tumejaliwa rasilimali nyingi na utajiri mwingi unaotokana na mchakato wa mambo mengi yanayokuwepo kwa wakati mmoja.
Hali tuliyo nayo imeletwa na mchanganyiko wa mambo mengi. Tunapaswa kuchunguza na kuchanganua mambo hayo na hasa tukijiangalia sisi wenyewe, mienendo yetu, na kisha tuelewe ukweli wetu, mazuri na kasoro zetu. Kuondokana na umaskini, ni lazima kufuata mchakato wa kubadilika. Mwenye wajibu katika kuongoza mchakato huo ni sisi wenyewe. Ni lazima tuwe viongozi wa mchakato huo. Haifai kuwaachia watu wa nje, wafadhili, ama fedha kutoka kwingine popote. Hatuwezi kufaulu kwa kujifunza na kupokea njia zilizosaidia nchi nyingine. Kikwazo cha maendeleo yetu ni utegemezi na kukosa uwajibikaji miongoni mwa mawakala katika jitihada za kuleta maendeleo. Kukosa uwajibikaji ndio sababu kuu na jambo kuu linalosababisha umaskini wetu. Ni lazima, kwa hiyo, tujiwajibishe wenyewe katika kujinasua na mtego huu. Lazima tujisumbue na tuhangaikie kutafuta ufumbuzi wa matatizo yetu tukitumia ubunifu wetu wenyewe na rasilimali zetu wenyewe.
Madhumuni/Lengo la Ilani
Mipango tunayo, sera, taratibu na kanuni tunazo na pia mikakati mingi imewekwa. Licha ya hayo, ujuzi wa kinadharia juu ya ufumbuzi wa matatizo yetu tunao. Na bado hatufanyi vizuri katika kupambana na matatizo yetu. Kimsingi kinachokosekana ni uwajibikaji wetu katika utekelezaji wake. Tunakosa ujasiri na utashi katika utendaji, kujitoa kweli na kufanya kazi kwa bidii: kutimiza majukumu na kujitoa katika kutoa huduma yetu kwa ajili ya manufaa kwa wote; kuwa mawakala na wafanyakazi wazalendo waaminifu kwa jamii yetu. Tukubali kuukabili ukweli kuhusu sisi wenyewe. Alisema Mtume Yohane “Ukweli utawaweka huru” (Yh. 8: 32).
Kwa ilani hii, tunatoa mwaliko kwa wote na kuwasihi watanzania wote kufikiri kwa makini changamoto kuu zinazokabili nchi yetu na wananchi wake wengi ambao ni maskini wa mali, waliotengwa na wasio na uwezo. Kuzishughulikia changamoto hizi kunahitaji kuweka vipaumbele sahihi na njia sahihi za ufumbuzi ambazo zinashughulikia kikamilifu matatizo ya umaskini, utenganisho wa kijamii na hali ya kukosa uwezo kwa watanzania wengi. Ilani hii itakuwa mwongozo kwa mtu binafsi kuchagua chama na mgombea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2009 na Uchaguzi Mkuu wa 2010.
B: Vidokezi vya vipaumbele katika sera
Katika kuzingatia maoni yetu ya msingi juu ya jamii yetu, na uchunguzi wetu wa jumla juu ya utendaji na mfanikio, hapa sasa tunawasilisha mawazo yetu juu ya vipaumbele kwa taifa letu. Huu ni mchango wetu kwa ajili ya watu kutafakari na kuchangia katika mijadala kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2010.
1) Hadhi ya Utu wa Mwanadamu
Lengo na sababu ya mahusiano yote katika jamii ni kumpa kila mtu hadhi ya kiutu ambayo ni stahili yake. Maana yake ni kwamba, kila mtu apatiwe mahitaji msingi kumwezesha kuishi maisha yanayostahili mwanadamu. Hicho ni kipaumbele namba moja. Watu wote wameumbwa na Mungu katika usawa. Kwa hiyo kila mtu ni sawa na mwingine.
Hapa tunapendekeza:
- Lazima tunu za kimaadili ziwe ndio msingi wa taifa letu, haya yakiwa yamehifadhiwa katika Katiba na kuongoza kanuni na taratibu zote za uendeshaji na utendaji.
- Kutengeneza na kutekeleza programu ya elimu ya uraia kwa watu wazima wengi juu ya haki msingi za binadamu na wajibu kwa kila raia.
- Kuwafundisha watu umuhimu na njia za uchunguzi wa malalamiko ya watu ili kusukuma huduma ambazo ni stahili ya watu zitolewe kikamilifu. Huduma hizo ni pamoja na zile za utawala wa umma. Hapo ni pamoja na kuwapa watu nafasi na kuweka njia fanisi za kupeleka malalamiko yao ngazi za juu.
- Ni haki ya msingi kwa kila raia kupatiwa fursa ya kutoa malalamiko yake na kusikilizwa. Haki hii lazima iweze kutendeka kwa kuiwekea mifumo ya kisheria na kiutawala.
- Kanuni na taratibu za kimaadili na weledi (meritocracy) viwe ndio vigezo au sifa za kuwapa watu kazi na kupandishwa cheo.
2) Marekebisho ya Katiba
Katiba inaeleza Mkataba Msingi wa Kijamii wa watu kuhusiana na namna ya kujipanga katika maisha yao ya pamoja. Katiba ni zaidi ya hati ya kisheria. Ni dira ya kimaadili na maelezo ya kifalsafa ya tunu na kanuni watu wanazotaka kuzizingatia katika maisha yao ili kuwahakikishia amani, haki na vile vile kuheshimiana na kuvumiliana katika kuwa na maoni tofauti. Hakuna chama cha kisiasa wala serikali ya wakati huu wanaoweza kihalali kutumia Katiba kwa faida zao za kisiasa.
Katiba inamilikiwa na watu na ni ya watu katika anuwai (diversity) na katika upokeaji wa watu wenye tofauti mbalimbali (plurality). Kwa kuwa taifa ni kitu kinachoishi ni jambo la kiasili na la muhimu hivyo ni sharti kuruhusu mapitio ya vipindi kwa vipindi yafanyike ili kuwapa watu fursa kueleza maoni yao. Haifai kuachia kundi moja kushinikiza au pande/kundi/chama chenye maslahi (kijamii, kiuchumi au kidini) kuchochea mabadiliko. Tangu Tume ya Nyalali imetoa ripoti yake (1991), ombi la marekebisho ya Katiba halijapokelewa kwa namna na kiwango cha kuridhisha. Kuhusiana na suala hili tungependa masuala haya yapewe kipaumbele:
- Tamko dhahiri juu ya tunu msingi za maadili ya kitaifa ambayo yapasa yazingatiwe katika mchakato wa kurekebisha Katiba.
- Pana haja ya kuunda Baraza la Mapitio ya Katiba. Katika mifumo mbalimbali ya kisiasa, kuna njia kadhaa za kuwezesha suala kutekelezwa: Mahakama ya Kikatiba, Chamba ya pili katika Bunge, Mkutano wa Katiba.
Tunapendekeza paundwe baraza la wazee, wanaoteuliwa na sekta za kijami, ama wanaochaguliwa na taasisi mbalimbali za kijamii, kidini na wanazuoni. Chombo hiki kingechaguliwa na kuhakikishiwa uhuru watendaji wake kulingana na Katiba yenyewe. Kiwe huru, na kisibanwe na serikali.
- Kanuni za marekebisho na udhibiti (regulations) na kuwezesha uwazi kisheria kuhusiana na upatikanaji wa fedha za chama ama mgombea.
- Kanuni za udhibiti na marekebisho ya kuchagua wagombea kutoka ndani ya chama kwa lengo la kusaidia mchakato mzima. Kufanyika kwa uwazi na kwa kidemokrasia zaidi.
- Kuanzisha mfumo wa kiuwiano katika uwakilishi badala ya huu wa sasa wa mwenye kupata kura nyingi kuwa ndiye mshindi.
- Kuruhusu wagombea binafsi (isipokuwa katika nafasi ya Urais).
- Kuheshimu kanuni ya kuwa Serikali haina dini na kutoruhusu taasisi za kidini kuwa sehemu ya mfumo wa nchi (mfano. Mahakama ya Kadhi na uanachama wa OIC).
- Kulinda haki ya watoto ambao hawajazaliwa.
3) Uongozi wa Umma
Kwa kiongozi, huduma kwa umma ni dhima muhimu sana kwa jamii yoyote ile ya wanadamu. Ndio maana lazima pawepo uangalifu mkubwa kwa jamii yoyote katika njia na namna (means) inavyochagua viongozi wake na namna inavyoweka taratibu za kusimamia na kudhibiti mienendo ya viongozi wao. Mamlaka mikononi mwa wanadamu kwahitaji uangalifu mkubwa ikiwa tunataka madaraka hayo yasiegemee upande mmoja yawe na uwiano, yasitumike vibaya na hata kuwa ya rushwa.
Kwa wakati huu, tumesikia matukio mengi ya ufisadi, maamuzi yanayopendelea upande fulani kwa sababu ya maslahi ya kiuchumi (kwa watu wa nje na wa ndani). Hapa tunaweka kipaumbele katika yafuatayo:
- Uwazi zaidi katika michakato yote ya uteuzi katika huduma na ofisi za umma, Tume za umma na bodi za utawala.
- Kufanya mapitio ya mamlaka ya Rais katika kuwateua mawaziri, idadi ya wizara, na pia uwezo na uhuru zaidi wa bodi za usimamizi wa mashirika ya huduma za umma.
- Kanuni na taratibu za uongozi ikiwa ni pamoja na kutafuta njia za kuondoa wale wanaothibitika kutumia vibaya nafasi zao.
- Kuhimiza na kuunga mkono kazi halali ya uandaaji wa ripoti zilizofanyiwa uchunguzi na kutafuta taarifa juu ya utendaji fanisi katika huduma za umma kama huduma msingi kwa raia wote.
- Kuhimiza utamaduni wa kufanya tathmini makini juu ya utendaji fanisi wa viongozi, kwa kuweka njia ya kuwezesha wasomi, vyombo vya habari, jumuiya za kiraia na vikundi vya kiraia kushiriki katika tathmini hiyo ya umma.
4) Mfumo wa Kisheria
Kutenda haki ni zaidi ya kufuata sheria na taratibu. Sifa ya uadilifu kwa wale wanaosimamia uendeshaji wa taasisi za sheria na taratibu, na msingi wa mawakala hao wa kuheshimu utu wa kila mtu na kwa ajili ya manufaa kwa wote na kutunza amani na utulivu na maelewano, ni mahitaji ambayo kamwe hayapaswi kupuuzwa, na yafaa liwe ni somo la kila mara katika malezi yao endelevu.
Polisi, maafisa wa mahakama, mawakili, maofisa magereza, watunga sheria, na watawala sio “mabosi” mbele ya watu. Wao ni walinzi wa taratibu nzuri za jamii yetu.
Lazima hawa wajali sana wigo mpana wa mahitaji ya jamii yetu, na sio wawe na ufinyu wa kujiona kuwa wasimamia sheria tu. Kwa ulingo huu tunaleta vipaumbele hivi:
- Lazima kuweka na kudumisha uwiano mzuri zaidi katika mgawanyo wa madaraka katika mihimili mikuu mitatu ya Dola, Serikali, Bunge na Mahakamu. Ilivyo sasa uwiano hakuna na kuna uegemeo upande wa mkono wa Utawala/Utendaji (Executive). Sio kweli kudhani kwamba kudhibiti uwezo wa maamuzi ya madaraka kutaleta ucheleweshaji na kukosa ufanisi, bali kinyume chake ndio kweli. Maamuzi mengi mabaya na ubishani wenye mvutano yangeweza kuzuilika. Ni muhimu pia kuachia madaraka ya maamuzi katika masuala ya kiutawala kwa ngazi za kati na chini yakiandamana na haki ya kukata rufaa kwa ngazi za juu.
- Dhima ya Bunge ya kudhibiti Serikali Kuu inapaswa kuiimarishwa. Pamoja na hatua njema iliyopigwa hapa karibuni, udhibiti makini unatakiwa kwasababu Bunge likiwa ndilo mwakilishi wa majimbo yote linatarajiwa kutoa tathmini yakinifu ya maamuzi yanayofanywa na Serikali.
Wabunge nao wawe na mawasiliano ya karibu na wapiga kura wao wakiwa na ziara zilizopangiliwa majimboni mwao ambako watu wataweza kukutana nao. Wabunge wajizuie kujipendelea kwa kujipangia marupurupu na mapato maalumu pamoja na bonasi nyingi.
- Kupunguza usiri katika mchakato wa maamuzi yanayofanya katika ngazi za juu. Uwazi huboresha maamuzi yanayofanyika.
- Maamuzi yanayofanywa na utekelezaji unaohitajika vinazuiwa na kukosekana matumizi ya kanuni ya auni, badala yake mfumo unategemea maamuzi ya viongozi wa juu wanaohusika. Watu wa chini yake wanaweza kukatishwa tamaa katika uwajibikaji. Kwa hiyo wakubwa lazima wajifunze kugawa madaraka yao kwa walio chini yao. Kwa kufanya hivi, mfumo wa kisiasa unaweza kufikia maboresho makubwa.
- Kupunguza kiwango cha wanasiasa kuingilia mambo ya utawala na huduma.
- Hasira ya kijamii yapasa ishughulikiwe na taasisi za kisiasa na wakala wa sheria na taratibu. Tunaunga mkono sera ya ulinzi shirikishi na kupendekeza kuongeza idadi ya njia mbadala ya adhabu kwa watenda makosa madogo madogo (mfano; huduma kwa jamii, kulipa fidia, kemeo/karipio/onyo rasmi la umma). Pia kuanzisha vituo zaidi kwa ajili ya majaribio kwa wakosaji vijana kuishi bila kufanya kosa.
- Magereza yetu yanapaswa kuendesha programu za mafunzo kwa ajili ya marekebisho ya wafungwa kimaadili, kutoa fursa kwa wafungwa kuwa na mawasiliano na upande wa pili (mshtaki/mhanga) kwa lengo la kufikia usuluhishi.
- Mfumo wetu wa kisheria uchunguzi na kutafiti, na kutekeleza nyenzo na taratibu zinazoongeza ufanisi na utendaji wenye kuleta mafanikio yanayotakiwa kufikia matarajio ya watu. Ucheleweshaji na uzembe/uchovu (lethargy), kukosa uwajibikaji na kukosekana utendaji mzuri wa mahakama kunawafanya wananchi wakose matumaini na kukatishwa tamaa (frustrating) na kuwakosesha imani katika mahakama kama chombo cha kuwasaidia kupata haki kwa njia ya mfumo wa kisheria. Watu hawaoni uwezekano wa kushughulikiwa kesi zao kwa wakati na hivyo kujenga mazoea ya kujichukulia sheria mkononi.
Lazima mfumo wenyewe wa sheria uanzishe njia za kujinidhamisha na kujitathimini utendaji wake na kutumia kanuni za kisasa zaidi za kusimamia utendaji.
- Mahakama inapaswa kutumia sehemu kubwa ya fedha na mali zake zilizopo kwa ajili ya Mahakama za Mwanzo na za Wilaya na za Hakimu Mkazi (kwa mishahara, majengo, kutengeneza ofisi ziwe za kisasa na vifaa na huduma nyinginezo, kuongeza idadi na ujuzi wa mahakimu na makarani). Ni kweli kwamba ni katika ngazi hizi za mahakama ndipo watanzania wengi wanapoijua (wanapofika) mahakama.
5) Viwanda, Biashara na Fedha.
Ni vivutio vingi mno vinatolewa kwa wawekezaji wakubwa na hakuna jitihada na kujali vya kutosha wawekezaji katika uzalishaji mdogo. Wawekezaji wa nje pamoja na makampuni makubwa sio ufumbuzi katika kupunguza umaskini wa watanzania wengi. Upande mwingine wanataaluma wengi wanavutiwa na “mambo makubwa na ya kisasa na ya ughaibuni.” Wanakimbilia mitaji ya nje na njia za nje ya nchi wakati fedha ya ndani inabaki tu pasipo kutumika vizuri katika taasisi zetu za fedha.
Hatua hizi tunazipendekeza ziwekewe kipaumbele:
- Kabla ya yote kabisa, lazima tuangalie suala la utu katika kazi na wajibu wa kimaadili wa kila mmoja kuchangia katika jamii na sio kuwa mnyonyaji wa jamii. Kukaa bure bila kufanya kazi na uvivu ni dhambi mbele ya Muumba na pia ni kosa mbele ya macho ya jamii. Uzururaji ni kosa kisheria. Kutofanya chochote ni tabia isiyoridhisha, malipo sio kitu pekee kinachosukuma mtu kufanya kazi. Utu wa mtu wenyewe unamtaka mtu afanye kazi.
- Kuhusisha taasisi zinazosaidia uwekezaji (huduma za mikopo, miundo mbinu na huduma za ushauri, utafiti wa masoko) kwa ajili ya sekta ya uzalishaji mdogo.
- Kuweka kipaumbele katika kutengeneza soko la ndani na kuongeza uwezo wa watumiaji wa ndani na hapo tutawezesha uzalishaji wa ndani kuwa ndio nguvu ya kukuza uchumi wetu. Viwanda na biashara zetu lazima zikue kutoka ndani ya nchi yetu.
- Kuingilia kati uzalishaji katika sekta ya kilimo ili kuwahakikishia mapato wakulima wadogo wadogo kwa kuweka sera za bei ambazo zinawapa wazalishaji wadogo kipato cha uhakika kutokana na mazao yao. Njia za kuwalinda wakulima dhidi ya anguko la bei ya soko la dunia lazima ziwekwe.
- Maslahi ya wafugaji, haki zao na wajibu wao yanahitaji kufikiriwa kwa makini zaidi na kuwekewa njia nzuri zaidi za kisheria na kiutawala ambazo zitawahakikishia haki zao msingi na uhuru kwa mujibu wa Katiba.
- Kuweka njia imara za marekebisho ya kifedha kwa ajili ya faida ya wawekezaji na kunufaika na upendeleo zaidi kwa watu wetu badala ya kuwajali zaidi wawekezaji wa nje.
- Kufanya mapitio makini ya kuongoza vigezo vya vivutio kwa wawekezaji wa nje. Ni lazima tusiwachukulie kama wahisani wetu.
- Serikali iingilie katika kudhibiti soko la fedha ili kuwajali wakopaji wadogo. Kuna haja ya kuchukua hatua za kusaidia huduma za mikopo na akiba kuwafikia watu vijijini.
- Waendesha maduka madogo yasiyo rasmi sio kero kwa jamii. Tunakubaliana kuwa sekta hii inahitaji mabadiliko, lakini sio kwa njia ya polisi, bali kwa njia ya kuweka jitihada za kiuchumi zinazowawezesha watu wawe mawakala wenye thamani na faida. Hivyo lazima kuwaingiza katika sekta nzima ya biashara ikiwa ni pamoja na mambo ya huduma za mikopo, kuchangia kodi, huduma zilizo katika kiwango, utoaji leseni na mahala pa kuendeshea biashara ndogo ndogo na sio tu katika bustani za majumba makubwa.
- Kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kuishi. Kuanzisha sera ya dhamana au rehani kwa kuwalinda na kutoa upendeleo kwa wenye kipato cha kawaida. Ujenzi wa majengo na barabara ni kichochea muhimu katika kukuza uchumi wan chi.
6) Uchumi
Kwa kuangalia changamoto za sasa kufuatana na ukubwa wa tatizo la umaskini, kuangalia mahitaji ya kiuchumi katika upeo mpana zaidi ya ukuaji uchumi. Tunahitaji kuweka mkazo katika watu wengi zaidi kuzifikia fursa, hasa kwa watu maskini na wasio na uwezo. Ukuaji uchumi lazima unufaishe watu kwa kuangalia walio maskini zaidi, kunufaisha wengi badala ya kuangalia wachache tu wenye kupewa upendeleo.
Kwa hiyo watu yapasa wapewe fursa ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji na katika mchakato wa ukuaji ili wanufaike kwa njia ya ushiriki wao wenye kuleta tija na kuweza kufikia maendeleo ya jumla ya nchi yetu. Watu wanahitaji kuwezeshwa ili ushiriki wao uwe wa tija. Uwezeshaji huu unaweza kufanyika kwa njia ya kuwekeza katika elimu, afya, miundo mbinu n.k.
Panahitajika mfumo sahihi uandaliwe kuhakikisha matumizi mazuri na ya kisheria juu ya urithi wa pamoja wa rasilimali zetu. Hapa panahitajika kuimarisha uwezo wa utawala na taasisi zenye wajibu huo. Pawepo uwiano kuhusiana na dhima ya Dola na soko.
Lingine muhimu ni juu ya namna tunavyojenga mahusiano yetu na jumuiya ya kimataifa. Ushirikiano wenye tija lazima uwekwe na kulindwa kwa misingi ya kuheshimiana, na maslahi ya taifa lazima yawe ndio yanaongoza ushirikiano huo. Hivyo umiliki wa nchi yetu na uongozi katika kutengeneza sera, mikakati, programu na menejimenti ya mchakato wa bajeti yapasa ziwe ndio kanuni zinazoongoza.
Sasa tunaelewa kwamba kinachotupatia lengo la uchumi na sera za kiuchumi sio tu uzalishaji na upatikanaji wa bidhaa na huduma. Uchumi lazima uwe chombo cha kutuhakikishia ubora wa maisha ya raia wote, ukiwa unahudumia manufaa kwa wote na uhalali na usawa wa kupata mali na huduma zilizopo. Sera yetu ya kiuchumi inaangalia mno upande mmoja, upendeleo ukiwa ni kwa wale ambao wana uwezo tayari. Masuala ya kijamii yanahitaji kutiliwa mkazo upya. Hapa maoni yetu ni haya:
- Tunapendekeza kwamba huduma ya afya na elimu ziwe ndio kipaumbele namba moja katika kupanga uchumi wetu.
Rasilimali kubwa ya taifa letu ni watu wake. Kushughulikia afya na elimu ya watu, kwanza kabisa ni wajibu wa kimaadili, kutunza maisha na kuongeza ustawi wa watu. Lengo hili hili yapasa liwe ndilo la kwanza katika mipango yote ya kisiasa na kiuchumi. Kuacha kujali afya na elimu kwa watu wetu ni kosa kimaadili.
Kwa maoni ya kiuchumi kuzungumzia gharama za huduma hizo ni kupotoka. Ni bora kuzungumzia kuwezesha ubora wa rasilimali watu ili uwezo wao uongezeke. Gawio linalotokana na uwekezaji huu tu linatokea haraka mara tu na ni la muda mrefu na huongeza kiwango cha jumla cha tija katika nchi.
- Watu wanaofanya kazi katika huduma ya afya na elimu wako katika taaluma za kiwito. Ubora wa elimu na afya unatokana kwanza kabisa na kujitoa kimapendo na uwajibikaji wa kitaaluma.
Tunatoa changamoto kwa dhana msingi ya mtazamo wa uchumi wetu wa sasa ambao mkazo wake ni kwamba lazima nia iwe ukuaji uchumi, kisha tutaweza kuongeza matumizi katika huduma za jamii. Maoni yetu ni kwamba tunahitaji kuwekeza zaidi katika afya na elimu ili tija ya kiuchumi na ukuaji wake vitokane na uwekezaji/matumizi hayo.
- Tunapendekeza mapitio katika sera ya kuchangia huduma za jamii. Sera hii ya ushirikiano wa Umma-Binafsi (UBIA) inaleta mambo mengi yasiyoridhisha na inachangia moja kwa moja katika kuyumbisha na kuzidi kuongeza mgawanyo wa matabaka katika jamii yetu, kwa kuwa baadhi wanazimudu gharama za huduma hizo na wengine wanashindwa kwa hiyo hawawezi kupata huduma hizo msingi.
• Sera ya Elimu
Mkazo lazima uwe katika kiwango cha juu katika elimu cha shule zote na kuondoka na kiwango cha chini kwa watu maskini na kwa shule za vijijini.
Ubora huu wa kiwango kizuri na sawa kwa wote, lazima kikubalike katika ufundishaji na kujifunza na vile vile katika usimamizi na utawala wa shule katika ngazi zote za elimu: msingi, sekondari na vyuoni.
Katika ngazi ya shule ya msingi elimu iwe bure na gharama zibebwe na kodi inayolipwa Serikali kuu na Serikali za Mitaa.
Kwa ngazi ya Sekondari na vyuo sera nzima ya elimu inahitaji kufanyiwa mapitio na mpango lazima uongozwe na Serikali na hivyo hapatakuwa na mwingiliano wa programu kama ilivyo sasa. Pia hali ya mazingira ya kazi kwa waalimu yafanyiwe mapitio. Tuisheni/mafundisho ya ziada yafanyiwe mapitio pia, ulipaji ada na viwango vyake lazima udhibitiwe, mfumo wa mikopo uwe wazi zaidi na iwe ni juu ya mfumo mzima wa kodi na sio mzigo umwangukie mzazi pekee yake.
Mapitio katika mfumo wa mitihani na kupima wanafunzi kwa kutumia maendeleo yake, na sio tukio moja la kufanya mtihani.
• Sera ya Afya
Tunapendekeza kurudi katika huduma bure ya tiba kwa mahitaji msingi ya kiafya katika zahanati na hospitali ngazi zote na kuanza mtindo wa kuzipiga faini hospitali za Serikali ngazi za chini ikiwa huduma hizi za msingi hazipatikani katika eneo lao.
Kushirikisha kikamilifu hospitali na zahanati zinazotoa huduma bila kujitafutia faida, nazo ni zile zinazoendeshwa kwa kujitolea ama zile za mashirika ya kidini. Hizi ziingizwe katika mfumo wa uendeshaji wa zahanati na hospitali za umma na zipate misaada sawa.
Kuifanya huduma ya bima ya afya kuwa ni hitaji msingi na la lazima kwa kila Mtanzania.
• Sera ya Kazi na Ajira
Sera hii inahitaji kufikiriwa upya haraka. Jambo hili limekuwa kitendawili cha hali za kihistoria na maoni na upendeleo na imeathiri sekta mbalimbali na makundi ya watu wa namna mbalimbali. Msingi ungekuwa pato la mshahara ambao unamwezesha mtu kuishi na sio mshahara wa kima cha chini. Malipo ya ziada kama zawadi kwa mafanikio mazuri (bonus), marupurupu (allowances) ya kila namna, gharama maalum sasa yamekuwa sambamba na kipato na wala hayatozwi kodi wala kudhibitiwa. Wale walio katika nafasi za kujipangia upendeleo huu wanafanya hivyo kwa makusudi na hawako radhi kujipunguzia au kujiondolea upendeleo huo. Na hii ni kuanzia na ngazi za juu za nafasi za umma.
Sio tu kwamba sera ya ajira sio ya haki, bali pia sio nzuri na inaleta mtikisiko na hali ya kutoridhika katika jamii kama ambavyo migomo ya waalimu na watumishi wa afya ilivyodhihirisha hivi karibuni. Na njia ya kutumia nguvu iliyotumika kukabili migomo hiyo ni jambo la aibu.
• Mtazamo wa jumla wa sera ya kiuchumi – kijamii
Lazima tuwe na ujasiri na tuthubutu kutambua mahitaji yetu na kuweka vipaumbele na kujua namna ya utekelezaji wenye kuleta kilichokusudiwa. Wafadhili, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), nchi wahisani wanaweza kuwa na la kusema. Lakini wasiwe ndio wanatuamulia namna ya kupanga mahitaji na vipaumbele vyetu na kuwa ndio wasimamizi (take charge) katika mchakato wa maboresho ya kimaendeleo kama ambavyo imeonekana kuwa.
Kwa haya lawama zinatuangukia sisi wenyewe. Kila mara tunavutwa na pesa na hivyo tunakuwa tayari mno kukubali masharti yoyote bila kufikiria matokeo yake na bila kujali sura kamili; bila hata kujifunza mahusiano yaliyomo baina ya hali mbalimbali ya nchi yetu kiuchumi na kimuundo. Mara nyingi mno tunakuwa na mtazamo katika mradi tu (project – focused) na tunashindwa kuwa na mtazamo kamili katika kupanga maendeleo yetu.
Kilimo na ufugaji yapasa vipewe uzito na kipaumbele kadiri inavyostahili, kwa kuwa bado ni muhimili/uti wa mgongo wa uchumi wetu. Mazao ya kilimo na biashara yanayostawi katika kila sehemu (mkoa au wilaya) yapasa yatambuliwe kisayansi na watu wasaidiwe kushughulikia kilimo kwa njia ya kuwezeshwa kuwekeza katika viwanda vya kusindika mazao ya kilimo na ufugaji, huduma za ugavi wa pembejeo, mashine za kilimo (agri-machinery), masoko na huduma za ugani kwa kulenga kupata mazao mengi na yenye ubora.
7) Hifadhi ya Jamii
Njia ya moja kwa moja inayoweza kuisaidia Tanzania kupunguza umaskini ni kuhakikisha huduma ya hifadhi ya jamii kwa walengwa na makundi ya wasio na uwezo. Sera hii inaweza kupunguza umaskini uliokithiri kwa nusu ndani ya muda mfupi na kwa kutumia gharama tunayoimudu.
• Tunapendekeza:
- Mpango wa mafao ya uzeeni kwa watanzania wote walio na umri wa zaidi ya miaka 60.
- Kuwapatia watoto wote wa shule za msingi chakula cha mchana bure/bila malipo.
- Malipo ya kila mwezi kwa kila mtoto mlemavu.
- Zaidi ya hayo tunapendekeza kuimarisha mfumo wa kijamii wa ustawi (welfare): hifadhi ya jamii inahitaji mambo mengine zaidi ya pesa. Hali ya kukosa uwezo na ulemavu vinahitaji raia wote kumjali mtu huyo. Jamii haiwezi kuwa imestaaribika na kuwa na msimamo wa kimaadili ikiwa inawadharau wale wasio na uwezo ama walio na ulemavu. Kuheshimu hadhi ya utu wao ni sehemu ya kuonyesha mwenendo na tabia ya kiutu. Kuwatendea kwa kiwango kilicho chini ya utu wa mwanadamu ni tabia ya kiuhalifu (criminal) na vile vile ni dhambi kimaadili.
Tunapotoa wito wa kuimarisha mfumo wa ustawi wa kijamii (social welfare) tunapendekeza kupanua ushirikiano baina ya jitihada za vikundi vya kujitolea kama vile vya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo na vya Mfumo wa zakat kwa waislamu na vile vya Serikali kuu na Serikali ngazi za chini. Hii inaleta hitaji la kuongeza wafanyakazi (social workers) ambao wataunganisha jitihada za vikundi vya kujitolea na zile za taasisi za Serikali. Kushughulikia na kutunza watu wasio na uwezo na walemavu sio kazi rahisi, na hivyo ili kuweza kufaulu tunahitaji kushirikiana wote miongoni mwetu.
Ni lazima tushawishike kwamba hii ni kazi yenye thamani na maana kubwa. na kwa kweli matokeo mazuri ya jitihada kama hizo za jamii ni kwamba jamii yetu itakuwa ya kiutu zaidi, yenye msimamo wa kimaadili na itaonyesha sifa nzuri ya ubora wa kujali, ambayo itameza au kuondoa tabia na mienendo mibaya kama uchoyo, ubinafsi na rushwa/ufisadi. Kutunza kwa kujali watu wasio na uwezo yapasa, na hatimaye kunaifanya jamii yetu kuwa nzuri zaidi kimaadili na ya kiutu zaidi.
HITIMISHO
Mwisho kabisa tunapendekeza tafakari ya kina juu ya nini na nani wanaongoza uchumi wetu na maslahi ya taifa letu. Na kwa hiyo kwa uwezo mkubwa tuhimize mijadala juu ya kama uchumi wetu unavutiwa na ongezeko la mahitaji ama na kuwezesha ongezeko la upatikanaji vitu? Nini kinasukuma/kuongoza uchumi wetu? Je, ni uwekezaji, au ni ongezeko la fedha, kuongeza ajira na bidhaa na miundombinu? Tuna nia ya kuongeza mahitaji na matumizi ya ndani ili kuchochea uzalishaji wa ndani kukamilisha mahitaji ya ndani na hapo tuweze kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha bidhaa zenye thamani zaidi badala ya kuwa na bidhaa za malighafi.
Kwa kusikiliza mjadala huu kuwa mahitaji yetu hasa sio pesa, bali tunachohitaji ni utashi, mawazo na kufanya kazi kwa bidii. Kuna tabia imejijenga katika jamii yetu, nayo ni ile ya kutojishughulisha, na watu wana kiu ya kutaka fedha bila kufanya kazi. Mwenendo huu hautatuletea maendeleo ya kweli.
Naam, nchi ina utajiri mkubwa wa rasilimali na utaalam, na pia kuna fursa nyingi ambazo hazijatumika. Na bado nchi ina vikwazo vingi vya kiurasimu ambavyo huruhusu wachache kunyonya kwa faida yao binafsi. Tunahitaji kuweka mfumo wa kuweka mikakati na kuanzisha chombo cha kujitoa kweli katika kuhamasisha na kulinda manufaa kwa wote na mafanikio mazuri kabisa kwa ajili ya urithi wa kitaifa.
Tunahitaji kufufua maadili, kurudi katika tunu msingi za kimaadili na matashi ya kujenga maelewano, mshikamano, kujali manufaa kwa wote na kumpatia kila mmoja mahali, nafasi, fursa na wajibu.
KAMATI YA TAIFA
CPT
MPANGO WA KUHAMASISHA HUDUMA YA KICHUNGAJI KATIKA JAMII KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2010
Idara ya Kichungaji
TUME YA HAKI NA AMANI - TEC
MPANGO WA KUHAMASISHA HUDUMA YA KICHUNGAJI
KATIKA JAMII KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2010
DIRA
Mungu anakuita, anakuhitaji.
Dunia imeumbwa na Mungu ili iendelee kuwa mahala panapodhihirisha Ufalme wa wake. Ukuu wa uumbaji huu ni mwanadamu ambaye ndiye kiumbe aliyekirimiwa utashi na uelewa ili awe mshiriki na mdhamini wa kazi ya Mungu. Mungu ametuchagua tuchukue wajibu huu, na pamoja naye tupunguze uovu na taabu, na kujenga dunia ambamo upendo na maelewano vinamhakikishia kila mmoja kufurahia utu wake.
Kama wakristo, tunapokea mwaliko wa Kristu uwe mwaliko wetu. “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa” (Lk 4: 18 – 19).
Kwa kutilia mkazo mwaliko huu, tunaelezwa kuwa Mwana wa Mtu atakaporudi atayahukumu mataifa kwa kigezo cha huduma tuliyotoa kwa wenye njaa, kiu; walio wageni, uchi, wagonjwa na wale walio kifungoni (rej. Mt. 25: 31 – 46).
Mungu alipomuumba Mwanadamu alimpa wajibu wa pekee, sio tu kuwa mlinzi na mdhamini wa dunia/uumbaji, bali pia kuwa mshiriki katika kuumba, na kutunza. Ni wito wa kushirikiana na Mungu katika kupambana ili kuuondoa uovu katika jamii yetu na kujenga ulimwengu ambamo kila mmoja ana wajibu wa kutekeleza na wakati huo huo ana haki ya kufurahia matunda ya dunia yetu.
Programu yetu ya kulihamasisha Kanisa kutekeleza wito wa kichungaji katika mambo ya kijamii ni kuwatia moyo waamini wote kutambua na kukubali wito wao wa Kikristo, wito wa kuwapelekea watu habari njema ya Yesu katika mambo ya kijamii na ya kitaifa. Kutakatifuza malimwengu, kuifanya nchi yetu na watu wetu kuishi pamoja huku manufaa ya kila mmoja yakiwa yanatimizwa: kupata huduma msingi za maisha na kuheshimiwa utu wa kila mmoja. Hapa maslahi na manufaa ya wote na ya kila mmoja katika jamii yanapaswa kuzingatiwa. Huu ni wajibu wa kila mmoja.
Mungu anakuhitaji, haya si maneno tu, bali ni uamuzi wa makusudi wa Mungu anayetukabidhi wajibu huu. Kutopokea mwaliko huu unaotoka kwa Mungu ni kushindwa kutimiza wajibu wetu, ni dhambi ya kutotimiza wajibu wa wito wetu wa Kikristo. Wito wa kutimiza wajibu wa kijamii, ambao ni kutia chachu ya tunu za injili na Mafundisho ya Kristo katika masuala na shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa ya taifa letu.
Wito huu haujaeleweka vema na jumuiya zetu. Watu wengi wanadhani kwamba mambo ya umma sio sehemu ya majukumu yetu ya kidini na kiimani, na hivyo Kanisa halipaswi kujishughulisha na mambo hayo. Kinyume chake Kristo anatualika kuleta mafundisho ya Mungu, maadili ya asili yetu ya kibinadamu kama tulivyoumbwa na Mungu. Tunaalikwa kuyafanya hayo yawe ndio msingi na mwanga unaoongoza maamuzi na sera zetu.
Tunaona kwamba ikiwa maadili hayo yatakuwa sio msingi wa maisha yetu ya pamoja na kuyashuhudia katika utendaji wetu na mienendo yetu, hapo tutaingia haraka katika uovu na ubinafsi na uchoyo, mambo ambayo yanaangamiza jamii yetu.
Katika miaka ya hivi karibuni sote tumeshuhudia haya yakitokea na tumepata madhara yake katika amani na utulivu katika taifa letu. Kumekuwa na mgawanyiko miongoni mwetu, kumejengeka matabaka ya wenye mali nyingi na watu wengi ambao wana mali kidogo sana, maskini na fukara hasa . Mwelekeo huu unatishia na kuhatarisha amani na moyo wa ujamaa tuliokuwa nao na kushamiri kwa utengano na chuki kati yetu.
Sote tunawajibika kwa nchi yetu na taifa letu. Ndio maana Mungu ametujalia sote kuenzi hadhi ya utu wetu sawa. Kwa hiyo tusiruhusu nchi yetu Tanzania ikawa na watu ambao thamani ya utu wao ni zaidi ya wengine. Tusisahau kila mmoja wetu ameumbwa katika sura na mfano wa Mungu (Taz. Mwa 1: 28).
Ni kwa sababu hiyo tunazindua programu hii ya kuhamasisha jumuiya zetu kuelewa wito wao wa kijamii, kuinjilisha na kuifanya jamii yetu iwe ya kiutu kulingana na mpango wa Mungu wa uumbaji na haswa kwa jamii ya wanadamu. Msingi wa utu wa mwanadamu ni asili yetu ya kwamba tumeumbwa na Mungu. Huu ndio msingi ambao dini zote zinausadiki na kuuheshimu. Kwa hiyo tunaweza kushirikiana na waislamu, wahindu, na watu wenye kufuata dini za jadi. Sote kwa pamoja tujenge dunia yetu kulingana na mpango wa Mungu.
WITO
Tumetumwa katika jumuiya zetu, Parokia na jumuiya ndogo ndogo, kuwahamasisha watu wafanye tafakari juu ya hali halisi ya maisha na kujua ni kwa namna gani mafundisho ya Kanisa na Injili yanatupatia mwanga wa namna ya kuboresha maisha yetu na katika Taasisi za jamii yetu. Tunachukua hatua katika kurekebisha mambo yanayokwenda vibaya na kuimarisha mambo mazuri. Ni mwaliko wa kuwasaidia watu katika kutekeleza maamuzi yaliyothibitishwa katika ahadi yao waliyoweka wakati wa ubatizo.
Hatua zifuatazo zinapendekezwa kutumika katika utekelezaji:
- Kuchunguza hali, kutambua na kubaini tatizo.
- Kutumia Mwanga wa mafundisho ya Kristo na kutoka katika Mafundisho ya Kanisa kuhusu Jamii.
- Kuamua hatua ya kuchukua na namna ya kufuatilia utekelezaji.
UTARATIBU WA KUZINGATIA (METHODOLOJIA)
Programu hii ya kichungaji inahitaji uongozi mzuri na hatua madhubuti za ufuatiliaji. Hapo tutaweza kufanikiwa na kuleta matokeo katika maisha ya Jumuiya ya Kanisa na ya taifa letu.
Katika hatua ya utekelezaji wa programu hii tunapendekeza:
1) Kufanyika mikutano ya makleri na viongozi wa halmashuri walei. Ni lazima katika mkutano huu ijadiliwe programu hii katika ngazi ya Jimbo na kupewa umuhimu unaostahili.
2) Wajumbe wa Mkutano huu: Wakurugenzi wa Kichungaji na Wajumbe wa Tume ya Haki na Amani watakuwa wakufunzi – kueleza na kufafanua mada za programu yetu.
3) Katika kazi ya kuongoza mkutano (no. 1), wajumbe wa CPT na wawakilishi wa Serikali waalikwe kutoa maelezo juu ya hali halisi pale watu wanamoishi.
4) Inapendekezwa paundwe timu ya Jimbo kwa ajili ya ufuatiliaji wa programu hii.
5) Katika ngazi ya Parokia programu ilenge kufundisha wanavijiji/watu mitaani na katika Jumuiya Ndogo Ndogo ili waweze kujadili masuala yaliyomo katika programu.
6) Ripoti za majadiliano hayo zitumwe Parokiani (Paroko na Halmashauri) kila baada ya miezi mitatu. Ripoti hizo zionyeshe mambo yaliyojadiliwa na maamuzi yaliyofikiwa.
Kwa kupata uelewa zaidi mada zilizojadiliwa katika mkutano wa Wakurugenzi wa Kichungaji na Wajumbe wa Tume ya Haki na Amani (TEC) ni:
1) Vipaumbele kwa mujibu wa Mafundisho ya Kanisa kuhusu Jamii.
2) Umuhimu wa uongozi wenye maadili katika kuleta mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kidini katika Tanzania.
3) Mfumo wa Sheria Tanzania: Nguvu na Changamoto.
4) Haki za Binadamu katika sera za biashara na fedha.
5) Mtazamo wa kimaadili katika mfumo wa kisiasa na kiuchumi.
6) Hifadhi ya jamii.
Mada hizi zinapatikana kwa kiswahili na kiingereza, kama unazihitaji wasiliana na:
- Ofisi ya CPT - St. Josephs Cathedral Dar es Salaam
Tel: 022-2127675/0713-329984
E.mail: cptprofessionals@yahoo.co.uk
Tunaweza pia kukusaidia kupata Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa utatujulisha mahitaji yako.
MADA KUU ZA TAFAKARI
Agenda hizi ndizo zilizoazimiwa katika Mkutano wa Wakurugenzi wa Kichungaji na Wajumbe wa Tume ya Haki na Amani TEC uliofanyika tarehe 20 – 22 Januari, 2009.
1. UTU
Utu aliokirimiwa kila mwanadamu bado haujawa ndio kiini na msingi wa mienendo yetu kama watu binafsi, katika vikundi na kama jamii. Kasoro hii tunaiona katika jumuiya za kidini, katika mila, desturi na tamaduni zetu, katika shughuli zetu za kiuchumi na katika uwanja wa kisiasa.
Kila mwanadamu ana utu sawa na utu wa mwingine na kwa hiyo lazima utu wa kila mmoja uheshimiwe na wengine: watu binafsi, taasisi na utawala. Ikiwa mwanadamu anapewa hadhi kutokana na utu wake, na haki zake atajengeka na kuwa na utu kamili, na yeye mwenyewe atajenga uwezo wake kikamilifu.
Vile vile bila kufanya hivyo jamii yetu haiwezi kamwe kukua na kuwa jamii yenye watu wenye kuenzi ukweli, utu na usawa. Kuigawa jamii katika matabaka ni kosa na ni dhambi, licha ya kuwa huko ni kuzuia jamii kufikia uwezo wake kamili na kuwa jamii yenye furaha. Katiba ya Jamuhuri imeweka bayana kwamba haki, wajibu na uhuru wa binadamu lazima vilindwe, viheshimiwe na kutolewa sawa kwa wote.
Kwa hiyo tunapaswa kufundisha watu dira hii katika:
- Ngazi ya familia, katika ujirani na Jumuiya ndogo ndogo. Ni hapa ndipo msingi wa jamii na kanisa unapojengwa.
- Katika mashule, tuangalie upya sera zetu za elimu na malezi na upande wa kimaadili tuchunguze yaliyo katika mitaala na ratiba katika mashule. Kwa sasa hakuna msisitizo wa kutosha katika malezi ya ubora/sifa za kiutu.
- Katika mambo ya kisiasa na kiuchumi: heshima na utu wa mtu sio suala la kubaki katika maneno na hotuba nzuri na matamko. Taasisi na sheria zetu lazima zikumbuke kuwa kanuni za kimaadili yapasa ziongoze kazi yao.
- Katika ngazi za Kanisa: mkazo zaidi uwekwe katika kuwajenga watu katika mambo ya kiroho ambayo ni ya lazima katika kuongoza tabia ya kijamii. Hapa ni zaidi ya kuweka kanuni na taratibu. Kinachohitajika hasa ni roho ya kiinjili na wito wa kinabii.
Mambo yanayopendekezwa kufanywa katika kufundisha na kuhamasisha utu ni:
- Mafungo katika ngazi ya Parokia na taasisi za Kanisa.
- Mikutano na wazazi ili kuwahamasisha na kutafakari namna ya kufundisha maadili katika ngazi ya familia.
- Semina na Waalimu.
- Kujadili na mamlaka ya elimu ngazi ya wilaya na mkoa.
- Tathmini ya kiroho ili kupima mambo ya kiroho na kupendekeza dhamira za kichungaji ambazo zinaweza kutumika katika mahubiri na miongozo ya katekesi.
- Kufanya utafiti katika ngazi ya Parokia ili kujua nini vijana wanapendelea na kutafuta njia ya kuwajengea hadhi ya utu wao kwa kutumia mambo yanayowavutia vijana.
- Kuchunguza vitabu vinavyotumika mashuleni kama vinahimiza au vinachochea maadili mema.
2. UONGOZI
Dira
Suala la uongozi ni pana. Kuna aina nyingi za uongozi (kiroho, kiutamaduni, kielimu, kiutawala, kisiasa, kiuchumi). Vile vile zipo ngazi mbalimbali za uongozi (familia, ujirani, vijiji, taasisi, kidini, kitaifa). Uongozi unahitaji watu wenye sifa ya huduma, wanaojali, walio wazi, wanaowajibika, wanyenyekevu, wenye hekima na upendo. Uongozi kila mara unashawishika kutenda kinyume na hayo na kuwa na uchoyo na kutumia madaraka vibaya. Kwa hiyo ni muhimu kuandaa viongozi, kushirikiana nao na kushikamana nao na kuwadhibiti kwa lengo la kuwasaidia kuwa jasiri walio waaminifu katika kazi zao.
Hali yetu inadhihirisha kuwa:
- Katika miaka ya hivi karibuni tumeona matatizo mengi ya uongozi. Kwanza kabisa yapasa tujadili kiini chake na kisha tutafute tiba yake.
- Katika uwanja wa kisiasa tunapaswa kuangalia namna wagombea wa na vyoteuliwa na vyama vyao. Tunahitaji kutafuta taarifa ya njia na vyanzo vya upatikanaji wa fedha za vyama vya siasa na namna wanavyozitumia. Watu wajadili kama mfumo wa uwakilishi kiuwiano (proportional representation system) haungeweza kuwa bora kuliko ule wa sasa. Kuna haja kubwa pia ya kusaidia watu kuijua Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
- Ni lazima katika mambo ya kijamii tuwahimize watu kueleza matatizo wanayokumbana nayo katika maisha yao na kuyatolea taarifa katika ngazi ya Parokia hadi Jimbo/Wilaya. Tuwasaidie kushiriki katika utawala tangu ngazi ya Serikali za kijiji/mitaa hadi ngazi ya halmashauri ya wilaya na kutafuta taarifa kisha kufuatilia nini watumishi wa umma wanafanya katika kuhudumia watu. Njia nzuri ni kuanza na kundi mahalia kushughulikia matatizo ya hapo walipo.
- Katika Kanisa tuhimize watu kutoa maoni yao katika Jumuiya ndogo ndogo na kusaidiana kuwa waaminifu katika wito wa Kikristo. Jumuiya ya Kanisa ni mahala ambapo mtu anakuwa na nafasi ya kutimiza wajibu wake wa kushiriki vilivyo katika shughuli za jumuiya. Hiarakia ya Kanisa haimaanishi kuwa ni kutoa amri tu kwa watu wa ngazi ya chini, bali kazi ya Hiarakia ni kuongoza namna ya kutimiza ahadi tuliyoweka wakati wa ubatizo.
Kwa agenda hii tunapendekeza:
Katika ngazi ya kisiasa: kuunda timu ya CPT na wajumbe wa halmashauri kutengeneza maswali maalum, kuendana na hali mahalia, watu wajadili na ili kutoa mawazo na maoni mazuri, wapatiwe habari zinazohitajika kwa ajili ya tafakari. Hapa tusiwape nafasi wale ambao ni wagombea wa kisiasa kutawala mjadala.
Kijamii: Watu watafute ni mashirika gani yapo hapo na huduma zipi hutolewa, na wangeweza kupata msaada gani katika kutatua matatizo yao. Ni taarifa gani tunapaswa kuwapatia watu ili waweze kufanya tafakari katika Jumuiya ndogo ndogo.
Kanisa: Tunawezaje kuimarisha tafakari katika jumuiya juu ya namna Parokia inavyoendeshwa. Halmashauri inafaa iwe chombo ambamo tathmini hiyo inaweza kufanyika. Ikumbukwe Parokia sio chombo cha utawala, bali lazima iwe ni jumuiya hai ya kusaidiana katika kuleta ubora wa maisha ya kiimani, matumaini na mapendo. Kwa pendekezo hili tufanye tathmini ya kiroho katika dhamiri na kuweka ahadi ya uwajibikaji katika kuwa zaidi mashahidi wa ujumbe wa Kristo katika hali halisi ya Tanzania leo.
3. HAKI
Dira
Lazima mfumo wa sheria uwe ni kwa ajili ya jumuiya ya watu katika kulinda na kudumisha amani, ukweli, haki, uhuru, mshikamano na usalama. Mfumo huu unapoleta ukosefu wa haki, watu wanapoteza imani nao.
Tutafute:
- Kwa njia gani tutawasaidia watu kujua haki zao na kuelewa sheria zinazoathiri maisha yao.
- Kuona kama shule zetu zinafundisha Katiba ya nchi na umuhimu wake.
- Tuone kama Wabunge wanawasiliana na majimbo yao na kuwa kweli wawakilishi wao. Kujadili kama wanadhibiti ya kutosha utendaji wa serikali. Ni kwa vipi watu wanapeleka masuala yao katika vyombo vya serikali na kusikilizwa?
- Mahakama za mwanzo zinahudumia watu wengi lakini ziko katika hali mbaya. Je, tunaweza kuziboresha vipi?
- Watu wanaona adhabu zinatolewa kwa makosa madogo, lakini wenye makosa makubwa, wanaachwa tu. Kwa nini watu wanafikiri hivi?
- Lazima tufikiri njia mbadala ya kutoa adhabu na kuona wafungwa kama watu wenye haki pia. Vile vile kutambua kuwa lengo la magereza ni kujenga amani na kurekebisha watu waliofanya makosa.
- Kila mara mfumo wa sheria unafanya kazi taratibu na hivyo watu husubiri mno haki kutendeka. Kukosa ufanisi na utaratibu wa utekelezaji vinasababisha ukosefu mwingi wa haki. Tunawezaje kuboresha hali hii?
Katika mjadala tulenge kuona kwamba “Mamlaka za siasa zichaguliwe na uamuzi wa hiari wa raia, nazo lazima zijali kanuni ya “utawala wa sheria,” ambamo ukuu ni wa sheria na si wa matashi ya watu wasio na sheria.”1
4. BIASHARA NA FEDHA
Dira
Hizi ni taasisi za biashara na fedha na shughuli nyingine zinazotoa huduma katika jumuiya. Biashara zinazotoa mahitaji ya vitu/bidhaa na kubadilishana na bidhaa hizi. Taasisi za fedha zinatunza thamani ya fedha, kwa kuweka kiwango cha kubadilisha fedha.
- Katika biashara, motisha haipaswi kuwa katika faida tu. Biashara inawafikishia watu bidhaa, hivyo isiendeshwe kiunyonyaji.
- Ni vipi tunaweza kuwasaidia watu kutetea maslahi yao na kuzuia wasinyonywe.
- Moyo wa ushirika umepungua mno na matokeo yake watu wameathiriwa na biashara zilizokosa uwaminifu. Tunawezaje kusaidiana.
- Mfumo wetu wa benki unafikisha huduma kwa watu wachache tu, na hasa kwa watu wa mijini na kwa wale wenye kiwango kizuri cha kipato. Lazima tusaidiane, hasa wale ambao hawana kipato cha kutosha, kuunda SACCOS na vikundi vya kusaidiana. Kanisa lazima lifanye bidii kuhamasisha hayo.
- Wachache walio katika mamlaka au katika nafasi za juu za utawala wana marupurupu mengi mno. Tusukume kupunguziwa hayo ili wawe na maisha ya kawaida.
- Tuwe makini na uporaji wa ardhi unaofanywa na makapuni makubwa na watu binafsi, matajiri. Tukumbuke ardhi ni ya thamani na ni hitaji la lazima kwa kila mmoja.
- Rushwa katika biashara, huduma duni, bidhaa duni vinaleta sifa mbaya, na hii ni tabia iliyo dhambi. Miongoni mwa watu hali hii inawajengea hasira na kukosa uaminifu na vile vile watu hujitetea kwa nguvu na kujengea watu fikra ya kulipiza kisasi.
- Udanganyifu katika biashara ni kushusha sifa mmiliki kwa wateja.
- Serikali iwe makini katika kuweka mikataba na wawekezaji wa umma na watu binafsi. Imekwishabainika kuwa katika mikataba hiyo maslahi ya wananchi hayalindwi kikamilifu badala yake wawekezaji hupewa unafuu mkubwa kwa kisingizio kuwa ni kivutio kwao.
- Makapuni ya ndani ni lazima yatiwe moyo na kuungwa mkono ili yaweze kuboresha utendaji wao uwe wenye tija.
5. UCHUMI.
Dira
Uchumi ni kwa ajili ya kuhudumia watu ili wawe na maisha mazuri: wapate mahitaji msingi na walindwe dhidi ya hali zinazowakuta na kutishia usalama wao na majanga mengine yanayoadhiri ubora wa maisha. Maadili katika shughuli ya kiuchumi na kuhakikisha mahitaji haya muhimu katika kumpatia mtu maisha mazuri yanapatikana. Sera za kiuchumi ni lazima ziweke kipaumbele kwa kuzingatia maadili na hivyo kufikia manufaa kwa wote na kulinda utu wa kila mmoja. Kwa hiyo tujadili pamoja na kama jumuiya za kanisa ni lazima tujifunze kuhimiza mahitaji yetu yazingatiwe na wenye maamuzi. Maoni yetu yasikilizwe na kufanyiwa kazi, tunu za kikristo tunazosimamia zionekane katika sera na katika mgawanyo wa bajeti ya serikali.
- Tunaweza kupunguza umasikini kwa kiasi kikubwa katika nchi yetu ikiwa watu wataelewa wajibu wao na kushiriki katika kutatua matatizo yetu: kwa mfano: kushiriki katika namna ya kupata huduma ya maji vijijini, namna ya kudhibiti matumizi ya fedha zinazotumwa katika serikali za mitaa.
- Ni kwa njia gani madiwani watafikisha maombi ya watu wao katika mgawanyo wa bajeti ngazi ya wilaya.
- Je, matumizi katika serikali ngazi ya chini yanawekwa wazi kwa wananchi kujua?
- Wabunge na viongozi katika ngazi ya Mkoa wanatoa fursa ya watu kuwauliza na kuwaeleza mahitaji yao? Tunawezaje kuboresha hali hiyo?
- Je, wakristo wetu wanazielewa fursa zilizopo; huduma zinazotolewa na serikali, mipango ya kusaidiana kama SACCOS, MVIWATA, vyama vya ushirika, jitihada za TASAF. Kwa nini wakristo wetu hawafanyi bidii kuanzisha vikundi/mipango ya kusaidiana? Pia parokia zetu ziwajibike vema katika kujenga ushirikiano na kujenga uwajibikaji wa kijumuiya ili kuboresha maisha.
- Kwa nini watu wetu hawaaminiani? Na tunawezaje kujenga moyo wa uaminifu miongoni mwetu?
- Kwa nini wakristo wetu wanaogopa kuzungumza na wenye mamlaka na walio katika huduma za utawala ili kupeleka malalamiko na kufuatilia utekelezaji wa maamuzi yaliyofanyika. Pia tutafakari namna ya kupambana na tabia ya uvivu.
- Tuna mali nyingi, lakini kila mara tunasubiri “wengine “ au “Serikali” kufanya kitu au kutuletea fedha. Lazima tujifunze kutumia vipaji vyetu na uwezo wetu katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo yetu. Kusaidiana kwa kuunganisha nguvu zetu na uwezo wetu ni wajibu wa kikristo. Mungu ametupa vipawa, lazima tuvitumie.
- Umaskini wa fikra, umaskini wa utashi duni na uwajibikaji ndio hasa husababisha umaskini. Ni kwa vipi jumuiya ya wakristo wanaweza kuwa mahala pa uwajibikaji ili kuweza kuboresha hali yetu.
6. HIFADHI YA JAMII
Dira
Mungu ametujalia uhai na anatupa mwaliko wa kutunza maisha na kuongeza ubora wa maisha. Mungu pia anatutaka kujali kwa namna ya pekee watu wasio na uwezo katika jamii yetu: yatima, wajane, walemavu, wagonjwa, watoto wa mitaani na wazee.
Hifadhi ya jamii maana yake ni kuweka mipango ya kuwahakikishia watu mahitaji na huduma ili wasiishi katika hali ya kukosa hifadhi/ usalama. Tunapozungumzia hifadhi ya jamii haswa tunamaanisha mifuko ya pensheni, elimu, bima ya afya na misaada ya kijamii.
Watu wengi miongoni mwetu hawafikiwi na huduma hii na familia zao zinakwama wanapoingia katika kuhitaji huduma hizo. Tunapaswa kuwa na mtazamo fikiriki ili kuweza kupata njia za kusaidiana. Mipango rasmi iliyoanzishwa na serikali au mashirika ya umma ama makampuni binafsi zinawafikia watu wachache tu ambao ni kama asilimia sita (6%) ya kundi la wafanyakazi.
- Jumuiya ndogondogo wangeweza kuwa chombo cha kusaidiana katika mahitaji ya kila siku ya wanajumuiya wao. Tunawezaje kuzifanya jumuiya zetu zitimize wajibu huu?
- Kutoaminiana ni kikwazo kikubwa katika kuwa na mipango na mifuko endelevu ya jumuiya. Tunawezaje kujenga moyo wa uaminifu? Viongozi wazuri walio tayari kuhudumia wanawezaje kupatikana na tutawawajibishaje viongozi wabovu?
- Lazima tutafute taarifa juu ya huduma na fursa zilizopo. Katika ngazi ya Parokia iundwe timu kwa ajili ya kutafuta taarifa na kuzifikisha katika Jumuiya ndogo ndogo. Taarifa hizo ni pamoja na zihusuzo mfuko wa afya ya jamii, sera ya serikali juu ya karo ya shule, sheria zinazohusu huduma ya tiba kwa mama na mtoto, wazee.
- Katika jamii yetu kuna watu walemavu wengi: Takwimu zinaonyesha kuwa walemavu ni 10% ya watu wote. Hawa ni wenye ulemavu wa namna moja ama nyingine. Kwa kawaida wahitaji hawa wanabaki kutegemea wanafamilia wao wachache, hasa mama au bibi. Kundi hili ndio maskini kupindukia kwa sababu jitihada za kuwainua ni ndogo sana.
Tatizo hili sio rahisi kulitatua. Lakini kwa kutegemea mifumo rasmi ya hifadhi ya jamii tu haitoshi na huduma hii kwao haitakuwa endelevu. Kwa hiyo tunapaswa kutafuta njia ambazo misingi yake ni katika njia za kizamani za kusaidiana, tuzitumie katika mazingira yetu ya leo kwa namna ya kisasa. Wazo hili linaweza kutekelezekaje?
PROGRAMU YA KUHAMASISHA HUDUMA YA KICHUNGAJI KATIKA JAMII KUELEKEA
UCHAGUZI MKUU 2010
(2009 - 2011)
TUKIO
WALENGWA
WAPI/NGAZI
LINI
MHUSIKA/MWEZESHAJI
Mkutano wa Taifa wa kutengeneza Programu
- Wakurugenzi wa Kichungaji
- Wajumbe wa Tume ya H & A (Majimbo)
TEC
20 – 22 Januari, 2009
- Katibu wa Idara ya Kichungaji TEC
- Katibu Tume ya Haki ya Amani – TEC
+ CPT (T)
Kukamilisha programu (booklet form)
TEC
Februari 2009
,,
Kutuma Programu Majimboni
- Maaskofu
- Wakurugenzi wa Uchungaji – Majimbo
- Viongozi wa Tume Majimbo
TEC
Machi 2009
,,
Mkutano wa Jimbo kuzindua Programu
- Mapadre, Watawa
- Halmashauri na vyama vya Kitume
- Taasisi
Jimbo
Aprili 2009
I. Kuanza Mapadre na Watawa, wa
II. Walei
- Askofu
- Mkurugenzi
- Tume (Jimbo)
Mkutano wa Makatekista
Makatekista
Jimbo
Aprili 2009
- Mkurugenzi Uchungaji
- Tume/Mkurugenzi Katekesi
Semina/Mikutano ya Walei/Vyama
Halmashauri (Viongozi wa JNN & Vyama, Kamati)
Parokia
Mei - Juni 2009
- Paroko/mjumbe kutoka Jimboni
- Kamati Tendaji, Viongozi wa vyama
Kufikisha Programu JNN
Waumini/Wakazi
JNN
Julai – Sept. 2009
- Paroko
- Halmashauri ya Parokia
Mijadala na utekelezaji
,,
- JNN
- Vyama vya Kitume
Okt – Des. 2009
- Paroko, Kamati tendaji
- Viongozi wa Jumuiya
Mkutano wa Taifa
(Tathmini ya I)
- Wakurugenzi wa Kichungaji
- Wajumbe wa Tume
TEC
Januari 2010
- Katibu Mtendaji Idara ya Kichungaji
- Katibu Tume – TEC
+ CPT (T)
Mwendelezo wa Mijadala na utekelezaji
Waumini na Wakazi
- Jimbo
- Parokia
- JNN
Febr. – Sept. 2010
- Askofu
- Paroko
- Walei
Kushiriki Uchaguzi kwa tathmini
Waumini na Wakazi
- Taifa
- Jimbo
- Parokia, JNN
Okt – Des. 2010
,,
Mkutano wa Taifa (Tathmini ya II) + kubainisha agenda
- post election
- post synodial
- Wakurugenzi wa Kichungaji
- Wajumbe wa Tume
TEC
Januari 2011
- Katibu Mtendaji Idara ya Kichungaji
- Katibu Tume
+ CPT (T)
Mwendelezo wa Programu
- Post Election
- Post Synodial
Waumini na Wakazi
- Jimbo
- Parokia
- JNN
Febr. - Sept. 2011
- Askofu
- Paroko
- Walei
Kuandaa Ripoti ya Majimbo na kutuma Taifa
Jimbo
Oktoba 2011
- Mkurugenzi wa Uchungaji
- Viongozi wa Tume
Kuandaa Ripoti ya Kitaifa ya utekelezaji wa Programu.
TEC
Novemba 2011
- Katibu Mtendaji Idara ya Kichungaji
- Katibu Tume ya H & A – TEC

Kingunge Ngombare Mwiru - kutoka mwanasiasa mkongwe anayeheshimika, Mjamaa halisi, Mkereketwa nambari wani mpaka Baba wa Taifa wa Mafisadi. Fall from grace au ndiyo the real Kingunge anajionyesha sasa. Hivi Nyerere kweli alikuwa na wafuasi wa siasa zake za Ujamaa au alikuwa amezungukwa na kondoo wa bandia tu? Ndiyo maana siasa zake ziligonga mwamba...Hii inasikitisha!
ReplyDeleteKuna baadhi ya wanasiasa wanapata kichefuchefu kutokana na huu waraka
ReplyDeletejamani tusichanganye dini na siasa ni vitu viwili tofauti, ya kaisali mwachieni kaisali na ya mungu muachieni Mungu.
ReplyDeleteNi muhimu sana kwa vyombo vya dini kutoa muongozo kwa mambo muhimu kwa jamii maana hivi ndo mhimili wa nchi yetu havipaswi kukaa kimya tu. Napongeza sana waandaaji wa waraka huu na pia napenda kila wakati vyombo vya dini visisite kutoa mchango katika jamii iwe kisiasa, Kiuchumi au katika nyanja zingine zozote. Vyombo hivi vya dini ndio wadau wakubwa wa maendeleo katika nchi yetu, tukiangalia mashule, huduma za afya na mambo mengi sana ya maendeleo ndo yamewezashwa na vyombo vya dini.
ReplyDeleteJamani, Mi mnanichanganya. Ina maana Haya makanisa na Watumishi hawa wa Mungu hawakuona wala kupendekeza lolote kwenye serikali zilizopita kuanzia Nyerere, Mwinyi na Mkapa?? Au wao walijua wanafanya nini? Tatizo ni huyu Mkwere ndiyeSisi tumezoea kuyapata haya kwa viongozi wa siasa tena wapinzani. Sasa kama chama chetu cha kanisa cha Chadema mnaona kimechemsha, basi Muungano wa Makanisa anzisheni Chama cha siasa.Sisi Tunakuwa waumini wa kanisa na wanasiasa.
ReplyDeleteIt’s difficult to find knowledgeable people for this subject, but you sound like you know what you’re talking about! Thanks
ReplyDelete