Thursday, 3 September 2009


Kikwete awapa mafisadi ahueni

Asaini marekebisho yaliyopitishwa na Bunge kimya kimya

Ufisadi sasa si uhujumu uchumi

Kesi za ufisadi kuwa kiini macho?

RAIS Jakaya Kikwete amesaini kuridhia mabadiliko ya sheria zinazohusu rushwa na uhujumu uchumi, hatua ambayo wanaharakati wa vita dhidi ya ufisadi nchini wanaitafsiri kwamba ina lengo la kupunguza makali kesi za uhujumu uchumi na rushwa zinazowakabili baadhi ya vigogo nchini, RAIA MWEMA limeambiwa.

Katika hatua hiyo, inayoashiria kupunguza makali ya sheria zinazotumika kuendesha kesi za uhujumu uchumi na rushwa nchini, kesi ambazo baadhi zinaendelea kusikilizwa mahakamani zikiwahusisha waliowahi kuwa viongozi wa kitaifa, Rais Kikwete, Machi, mwaka huu, alisaini marekebisho hayo ya sheria yaliyopitishwa na Bunge katika kikao chake cha Januari mwaka huu.

Hatua hiyo inatokana na kuwasilishwa bungeni kwa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali, ndani yake kikiwamo kipengele kinachoingiza makosa ya rushwa katika Sheria namba 200 ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002 (Economic and Organized Crime Act Cap 200 R.E. 2002).

Kwa kutia saini kwa Rais Kikwete kuridhia marekebisho hayo, rushwa sasa si kosa la kuhujumu uchumi.

Raia Mwema imefahamishwa kwamba mabadiliko hayo ya sheria yaliyopitishwa na Bunge Januari, yalisainiwa na Rais Jakaya Kikwete, Machi 12, mwaka huu na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Machi 20, 2009. Habari kwamba Rais ameridhia marekebisho hayo kwa kutia saini zilifahamika hivi karibuni tu kwa wanaharakati wa vita dhidi ya ufisadi nchini.

Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kwamba Mabadiliko hayo ya Sheria hiyo yamewashitua wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ambao wanasema wakati sheria hiyo inapitishwa walipata nafasi ya kuchangia maoni, hali ambayo haikujirudia wakati wa kuifanyia mabadiliko.

“Tulikuwa tunafikiria Serikali iongeze makali katika sheria ili tuweze kuwadhibiti zaidi mafisadi na wahujumu uchumi, badala yake sasa tunalegeza sheria ili kuwasaidia, ” alihoji mdau wa mapambano dhidi ya ufisadi aliyeko serikalini ambaye anasema ameshitushwa na mabadiliko ya sheria hiyo.

Mabadiliko hayo yamo katika kifungu cha 38 na 39 cha Sheria namba 3 ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali ya mwaka 2009, kifungu kinachofuta kifungu cha kwanza na cha pili katika jedwali la kwanza la makosa ya uhujumu uchumi kinachoingiza makosa ya rushwa na ufisadi.

Vifungu vilivyofutwa vilikuwa vinasomeka hivi:“Mtu yeyote atakuwa ametenda kosa (la uhujumu uchumi) ikiwa atakuwa ametenda kosa chini ya Sheria ya Kuzuia Rushwa” na “atakuwa ametenda kosa (la uhujumu uchumi) ikiwa atakuwa ametenda kosa la rushwa zaidi ya makosa yanayotajwa katika kifungu cha nne cha Sheria ya Kuzuia Rushwa.”

Kuondolewa kwa vifungu hivyo kunatoa nafuu kubwa kwa watu ambao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa makosa ya ufisadi, lakini pia mabadiliko hayo yanawavunja nguvu wapambanaji wa ufisadi ikiwa ni pamoja na vyombo vya dola vikiongozwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Habari za ndani ya Serikali zinaeleza kwamba hakuna uhakika wa moja kwa moja kwamba TAKUKURU ilishirikishwa katika mchakato wa kuifanyia mabadiliko sheria hiyo ambayo ndiyo imekuwa kwa muda mrefu msingi wa mashauri mengi inayopeleka mahakamani na kwa ajili hiyo marekebisho hayo yanagusa moja kwa moja utendaji kazi wa kila siku wa taasisi hiyo inayopigana dhidi ya rushwa nchini.

“Kama TAKUKURU wameshirikishwa basi itakuwa ni juu juu sana, lakini ninavyofahamu ni kwamba hawajashirikishwa katika hili bali Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliandaa muswada na kuupeleka bungeni kimya na wabunge wetu bahati mbaya sana hawakugundua hilo,” ameeleza mdau mmoja muhimu wa mapambano dhidi ya rushwa.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Dk. Edward Hosea, hakuweza kupatikana kuzungumzia Mabadiliko hayo ya Sheria yanayoipunguzia ofisi yake ‘makali’ kutokana na kile Raia Mwema ilichoambiwa ya kuwa amekuwa na vikao na kufanya kazi za nje ya ofisi.

Mabadiliko hayo ya Sheria ndogo ndogo yaliwasilishwa bungeni yakiwa na marekebisho katika sheria mbalimbali 11 ikiwamo hiyo ya uhujumu uchumi na inawezekana kwamba wabunge wengi walikosa nafasi ya kupitia sheria zote zilizoguswa na mabadiliko hayo.

Sheria nyingine zilizounganishwa katika muswada huo ambao tayari umekuwa sheria ni pamoja na ya Administrator-General (Powers and Function) Act, ya Usajili wa Vizazi na Vifo, ya Chuo cha Sheria (Law School of Tanzania), Utumishi wa Umma, Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Afya, National Prosecution Service Act, Sheria ya Uchawi, Penal Code, Sheria ya Leseni za Usafirishaji na Sheria ya Ardhi.

Madhumuni ya awali ya kutungwa kwa sheria ya rushwa yalikuwa ni pamoja na kukuza na kuchochea utawala bora na kutokomeza rushwa na ufisadi kwa kutoa msingi wa kitaasisi na kisheria ambao ni muhimu katika mapambano hayo.

Mabadiliko haya yamekuja baada ya hatua kadhaa za Serikali ya Awamu ya Nne iliyofungua, baada ya muda mrefu, kesi kadhaa, zikiwagusa vigogo mbalimbali, karibu zote zikitumia kipengele cha makosa ya uhujumu uchumi ambacho kilisababisha wengi wao kukwama kupata dhamana.

Miongoni mwa walioshitakiwa kwa makosa hayo ni pamoja na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, mawaziri wa zamani, Daniel Yona na Basil Mramba na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha kwa muda mrefu, Gray Mgonja.

Mbali ya viongozi hao waandamizi, kuna mlolongo wa watuhumiwa wengine wa ufisadi ambao TAKUKURU imewashitaki kwa kutumia Sheria ya Uhujumu Uchumi, wakiwamo watuhumiwa wa EPA na ujenzi wa majengo pacha ya BoT, wote wakibanwa na sheria hiyo katika kupatiwa dhamana.

Wakati kesi hizo zikifunguliwa hasa baada ya vigogo kuanza kupandishwa kizimbani, baadhi ya watu walisema kwamba kesi hizo zimefikishwa mahakamani kama njia ya kufunika baadhi ya mambo ya ndani ya serikali.

Japo baadhi ya Watanzania walifurahia hatua hiyo ya Serikali kufikisha mahakamani baadhi ya vigogo, kumekuwa na maoni kwamba hakukuwa na mantiki ya kuwatia nguvuni watu ambao maamuzi yao yalikuwa ni ya kimchakato na kwamba kesi hizo zilikuwa ni kama mzaha katika utendaji kazi wa serikali.

“Nashangaa ninyi mnafurahia (vyombo vya habari).. Tena inaelekea kila mara wanapopelekwa mahakamani mlikuwa mnajulishwa mapema. Huu ni mzaha. Ni masuala ya kisiasa. Ni kesi zilizojaa siasa. Ukitaka kuwashitaki watu kama hawa basi itabidi ama ushitaki baraza la mawaziri au kundi zima la makatibu wakuu wa wakati huo,” alisema msomaji mmoja wa Raia Mwema.

Aliongeza: “ Haya ni matumizi mabaya ya sheria kwa maslahi ya kisiasa. Nadhani hizi ni jitihada za kufunika kesi nyingine nyeti. Nia ni wananchi wazisahau hizo.

Mramba, Yona na Mgonja, walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu wakishtakiwa kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh 11,752,350,148 kutokana na kile kilichodaiwa mahakamani kwamba walitumia madaraka vibaya kwa kusababisha kusamehewa kodi Kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayer) Government Business Corporation.

Makosa yote hayo yaliegemea zaidi katika Notisi za Serikali (GN) zilizotangazwa kati ya mwaka 2003 na 2005, notisi ambazo ndizo zilihalalisha msamaha wa kodi kwa kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayer) Government Business Corporation.

CHANZO: Raia Mwema

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget