Monday, 7 September 2009


Unaweza kupatwa na hasira nikikuambia kuwa wewe (na mie) kwa namna flani tunahusika na kushamiri kwa biashara ya filamu za ngono, au kwa lugha mwafaka sekta ya filamu za ngono.” Najua utakuwa tayari kushika kitabu kitakatifu kuapa kwamba kamwe hujawahi kujihusisha na “uchafu wa aina hiyo.”

Katika sehemu ya pili ya kipindi cha BBC2 nilichokizungumzia wiki iliyopita kuhusu Utandawazi na Filamu za Ngono kumebainishwa mambo ambayo kwa hakika yanatuhisisha wengi wetu na kukua kwa sekta ya filamu za ngono. Tukiweka kando namna tunavyohusishwa kwa kuwa wateja wa makampuni yanayonufaika kwa ushiriki wao katika sekta hiyo (kwa mfano makampuni ya simu za mikononi, vituo vya runinga vyenye idhaa za filamu za ngono, mahoteli yanayotoa huduma ya “luku” ya filamu za ngono, nk) kuna uthibitisho kuwa baadhi ya taasisi za dini, hususan za Kikristo, zinawekeza fedha zao katika sekta ya ngono, japo sio moja kwa moja (directly).

Tunafahamu kuwa makanisa mengi yanategemea ufadhili kutoka mashirika mbalimbali ya kidini hapa Ulaya na huko Amerika.Lakini ili wafadhili hao waweze kuendelea na usamaria wema huo ni lazima wawekeze fedha zao katika mifuko au makampuni katika mfumo wa hisa.Mfano hai ulioonyeshwa katika kipindi hicho ni namna shirika moja kubwa la kidini huko Marekani lilivyowekeza mamilioni ya dola kwa mfumo wa hisa katika kampuni moja maarufu ya simu za mikononi, ambayo kama zilivyo kampuni nyingi za aina hiyo, hufanya biashara ya kuonyesha filamu za ngono kwa mfumo wa kulipia premium content.

Kwa lugha nyingine, misaada inayotolewa na shirika hilo inatokana na sehemu ya faida iliyopatikana kwa kuwekeza kwenye kampuni ya simu inayotengeneza sehemu ya faida yake kwa kuonyesha filamu za ngono. Naamini kwamba hadi hapo si vigumu kwako msomaji kuona uhusiano kati ya shirika hilo la kidini na filamu za ngono.

Lakini kuna namna nyingine ambavyo wengi wetu tunahusishwa na ustawi wa sekta ya filamu za ngono pasipo kuelewa waziwazi.Chukulia mfano huu mwepesi wa huko nyumbani. Vyama vingi vya kuweka na kukopa (Saccos) huzalisha faida zao kwa kuwekeza hisa kwenye mabenki, mifuko ya jamii (kama NSSF) au makampuni yaliyoandikishwa kwenye soko letu la “kichovu” la hisa.Kadhalika, Saccos hizo huwa na akaunti katika mabenki mbalimbali kwa vile sote tunafahamu kuwa kulaza mamilioni katika ofisi ya Saccos ni mithili ya kutangaza tenda ya kuvamiwa na majambazi.

Sote tunafahamu katika kutoa mikopo, mabenki mengi hayajihangaishi na maadili ya biashara ya mkopaji as long as ametimiza masharti ya kupata na kurejesha mkopo.Na hapo ndipo fedha zako kule Saccos zinapoweza kujikuta zikiishia kwenye akaunti ya mkopaji anayejishughulisha na filamu za ngono.

Lakini mfano mwepesi zaidi kwa mabenki ni akaunti zetu. Fedha tunazoweka katika akaunti hizo hazikai kama matangazo huko benki bali hutumika kibiashara aidha kwa kuwekeza au kukopesha.Na miongoni mwa wakopeshwaji hao ni haohao wanaojihusisha na filamu za ngono. Kwa huko nyumbani, fedha zako unazoweka benki zinaweza kabisa kuishia kwenye akaunti ya mkopaji mwenye gesti bubu wanakotengeza filamu za ngono kama sio gesti hiyo sio danguro bubu.

Njia nyepesi ya “kuua” makampuni ya filamu za ngono ni aidha kususia bidhaa zao (jambo ambalo ni rahisi kufikirika lakini almost impossible kutekelezeka kwa vile kilicho haramu kwako na kitakatifu kwa mwenzako) au kuyakatia mirija ya fedha, yaani kwa mfano kwa mabenki kukataa kutoa mikopo au kwa makampuni yanayowekeza huko kuacha kufanya hivyo au kwa biashara zinazotumia huduma za makampuni ya filamu za ngono kuachana na mtindo huo.

Ili hayo mawili ya mwisho yawezekane kunahitajika kitu kiitwacho uwekezaji wa kimaadili (ethical investment).Lakini hilo si rahisi kwa vile lengo kuu la uwekezaji, kama yalivyo maudhui ya ubepari, ni kutengeneza faida.Ni dhahiri basi kuzingatia maadili kutakwaza upatikanaji wa faida “rahisi” kama hiyo inayopatikana katika mahusiano ya kibiashara na makampuni ya ngono.

Na kwa masikini kama sie tunaotarajia misaada katika ustawi wa takriban kila sekta ya maisha yetu, ni dhahiri hatuna jeuri ya kuhoji msaada tuliopewa umepatikana kutokana na fedha za baishara ya filamu ya ngono au la.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget