Wednesday, 15 August 2012


Kwa sababu zilizo nje ya uwezo wangu,makala yangu katika jarida la Raia Mwema toleo la Jumatano iliyopita (Agosti 8, 2012) haikuwekwa mtandaoni japo ipo gazetini.Kwa faida ya wasomaji,nimelazimika kuiweka hapa (inaweza kuwa na tofauti chache na iliyopo gazetini ambayo imehaririwa)


MAKALA YA RAIA MWEMA TOLEO LA AGOSTI 8
Kwa zaidi ya wiki moja sasa kumekuwepo habari zisizopendeza kuhusiana na tatizo la muda mrefu la mpaka kati ya Tanzania na Malawi.

Ningependa kukiri hadharani kwamba pamoja na kiu yangu kubwa ya ufahamu wa masuala mbalimbali sikuwahi kujibidiisha kufuatilia kwa undani chanzo cha tatizo hilo. Na pengine kuliita suala hilo ‘tatizo’ ni kulipunguzia uzito kwani ukichambua kwa makini kauli mbalimbali kutoka kwa baadhi ya viongozi wetu na wenzao wa Malawi, kinachoendelea hivi sasa kinaweza kabisa kuitwa ‘mgogoro wa mpaka kati yetu na Malawi.’

Katika baadhi ya mitandao ya jamii, ambayo baadhi yetu inatusaidia sana kufuatilia mambo mbalimbali huko nyumbani kumeanza kujitokeza hofu ya vita kati ya nchi hizi ambazo licha ya ujirani zina ukaribu mkubwa kwa sababu ya mwingiliano wa makabila.

Hata hivyo, wakati hofu hiyo ya vita kati yetu na Malawi ikianza kukua, kuna mambo kadhaa yanayopaswa kujadiliwa kwa uwazi. Lakini pia ningependa kuweka wazi msimamo wangu kuwa ninaamini ufumbuzi pekee na wenye manufaa katika mgogoro huu ni kwa njia za amani.

Na moja ya sababu kubwa ya kutaka mgogoro huu utatuliwe kwa njia za amani ni kumbukumbu niliyonayo ya vita pekee nilivyowahi kushuhudia katika uhai wangu hadi sasa. Bado nina kumbukumbu nzuri ya vita ya Kagera kati yetu na Uganda, ambapo wakati huo nilikuwa mtoto mdogo ninayeishi na wazazi mkoani Kigoma.

Moja ya kumbukumbu zinazoniogofya hadi leo ni pale wakazi wa mji huo walipotakiwa kuchimba mahandaki kama hatua ya kujilinda. Kulikuwa na taarifa kwamba ‘swahiba’ wa nduli Idi Amin wa Uganda, aliyekuwa Rais wa ‘Zaire’ (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo-DRC) dikteta Mobutu, alikuwa na mpango wa kumsaidia Amin kushambulia Kigoma hasa kwa vile mkoa huo unapakana na DRC.

Ninakumbuka hofu tuliyokuwa nayo kila tuliposikia mlio wa ndege angani, tukidhani ni ndege za Mobutu zimekuja kutuangamiza. Bahati nzuri hadi vita hiyo inamalizika hakukuwa na shambulio lolote kwa mji huo.

Kwa kuzingatia kumbukumbu hizo, nisingependa kuona Watanzania wenzangu wakirejea kwenye hofu kama hiyo iliyotukumba sie wakati wa vita hiyo kati yetu na Uganda.

Lakini kuna jambo jingine linalonipa hofu zaidi. Katika moja ya shahada zangu za Uzamili nimesoma Stadi za Vita (War Studies), na katika kozi hiyo tulitumia muda mwingi mwanafilosofia mahiri wa masuala ya vita, Mchina Sun Tzu. Moja ya mambo yanayousiwa na Sun Tzu kuhusu maandalizi ya vita ni hili

Sanaa ya vita inatufundisha sio kutarajia kuwa adui hatotuvamia bali maandalizi yetu katika kukabiliana nae, na sio katika uwezekano kuwa (adui) hatoweza kutuvamia bali uimara wa nafasi yetu ‘kutohujumika’ (unassailable).”

Licha ya sote kuwa na mapenzi kwa nchi yetu, tukiangalia mwenendo wa mambo huko nyumbani kwa sasa, jambo tusilotaka kabisa kusikia kwa sasa ni vita. Mmoja wa ukweli mchungu ni kwamba hadi sasa tumeshindwa kukabiliana na maadui kadhaa wa ndani ambao hawana silaha bali fedha na porojo zao. Hapa ninawazungumzia mafisadi na maharamia wengine wanaoifanya Tanzania yetu kuwa katika umasikini tusiostahili.

Lakini pia uimara wetu kukabiliana n adui si wenye kutoa matumaini. Katika siku za karibuni tumeshuhudia migomo ya madaktari na baadaye walimu, wote wakidai kuboreshewa maslahi yao. Wakati watawala wetu wanadai serikali haina fedha za kuboresha maslahi ya watumishi wake, imemudu kupandisha mishahara ya wabunge hadi kufikia shilingi milioni 11 kwa kila mmoja wao.

Je inawezekana chokochoko kutoka Malawi zinachangiwa na uelewa wa nini kinachoendelea nchini mwetu? Lakini hata kama hiyo si sababu, je katika mazingira haya ya kuendekeza anasa kwa tabaka dogo huku wengi wa wananchi wakizidi ‘kupigika’ kutokana na uchumi dhaifu unaozidi kudhoofeshwa na majambazi wanaopora raslimali zetu kila kukicha, tunaweza kweli kukabiliana na adui huku tukiwa na uhakika wa kumshinda?

Ninatambua kuwa ninaweza kuonekana msaliti kwa nchi yangu kwa kubainisha hoja hizo hapo juu lakini kama nilivyotanabaisha hapo awali, ningependa, na ninataraji, mgogoro huu utamalizwa kwa njia za amani.

Nimeeleza hapo mwanzo kuwa sikuwahi kujishughulisha kufuatilia chanzo cha mgogoro ‘wa muda mrefu’ wa mpaka kati yetu na Malawi. Lakini jitihada kidogo tu ziliniwezesha kukutana na makala ya kitaaluma, ambayo licha ya kuwa ilichapishwa mwezi Disemba mwaka 1973, bado ina maelezo muhimu kuhusu mgogoro huo.

Katika makala hiyo, The Malawi-Tanzania Boundary Dispute (mgogoro wa mpaka wa Malawi na Tanzania) iliyoandikwa na James Mayall, na ambayo ni mapitio ya kitabu (book review) kuna taarifa ambazo kwa namna flani zinatoa taswira ya ‘msimamo wa kukanganya’ kwa baadhi ya viongozi wetu, ikiwa ni pamoja na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Kwa mujibu wa makala hiyo, awali viongozi wetu wakiongozwa na Nyerere waliridhia kuwa Ziwa si letu bali la Malawi. Kwa kiasi kikubwa msimamo huo ulionekana kuchagizwa na dhamira ya nchi yetu katika umoja wa nchi za Afrika.

Japo sitaki kuchukulia makala hiyo kama ukweli halisi kuhusu chanzo cha mgogoro huo, mwandishi alijitahidi kwa kiasi kikubwa kubainisha jinsi suala hilo lilivyochukuliwa kuwa la kiutawala zaidi kuliko la kisheria.

Inavyoelekea, kwa mujibu wa Mayall, moja ya sababu zilizopelekea nchi yetu kubadili msimamo wake wa awali kuwa Ziwa hilo si letu ni uhusiano wa karibu kati ya aliyekuwa Rais wa Malawi, dikteta Kamuzu Banda na utawala wa makaburu. Kama ambavyo inaelezwa kuwa moja ya vipaumbele vilivyopelekea Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni sababu za kiusalama, umuhimu wa sehemu ya Ziwa hilo kumilikiwa nasi unaelekea kuchangiwa na sababu kama hizo.

Kadhalika, makala hiyo inajenga picha moja ambayo yayumkinika kuhisi kuwa inaweza kurandana na sababu za sasa za kurejea kwa mgogoro huo. Mwandishi Mayall alieleza kuwa katika wakati flani huko nyuma kulikuwa na hisia kwamba hoja ya Malawi kumiliki Ziwa lote ilihamasishwa na utawala wa Makaburu (waliokuwa wakitawala baadhi ya nchi za kusini kabisa mwa Afrika) na Wareno (waliokuwa wakitawala Msumbiji).

Kisichopendeza kwa Mtanzania yeyote kuhusu makala hiyo ni ukweli kwamba msimamo wa awali wa nchi yetu ulikuwa ni pamoja na kuwaachia Wamalawi waamue wenyewe ‘kutuachia’ sehemu ya Ziwa Nyasa na pia kauli mbalimbali zilizoonyesha kuafiki kuwa Ziwa hilo si sehemu ya nchi yetu, japo baadaye msimamo huo ulibadilika.

  Ningependa sana kuitafsiri makala hiyo nzima kwa Kiswahili lakini nafasi hairuhusu, na pengine kufanya hivyo kunaweza kuwavunja moyo baadhi ya Watanzania wenzangu na pengine kuanza kuamini kuwa sie ndio chanzo cha chokochoko zilizopelekea mgogoro huo kufikia hatua ya sasa. Hata hivyo, iwapo kuna msomaji atahitaji nimsaidie kutafsiri makala hiyo ya Kiingereza, nipo tayari kufanya hivyo.

Wakati ninajipa matumaini kuwa mgogoro huo utamalizwa kwa amani, ninajikuta nikikabiliana na maswali kadhaa ambayo ninachelea hata kudadisi majibu yake. Kwa mfano, itakuwaje iwapo Malawi watapuuza onyo lililotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe kuwa makampuni yanayojihusisha na uchimbaji raslimali katika Ziwa hilo yasitishe kazi mara moja?

Wakati viongozi kadhaa huko Malawi wametoa kauli za kuleta matumaini kuwa kilichopo si mgogoro kwa vile nchi zetu zipo katika mahusiano mazuri, takriban wote wanaonekana kuwa na msimamo unaorandana kwamba Ziwa Nyasa lote ni la nchi hiyo.
Hapo huhitaji uelewa wa mambo ya diplomasia kuhitimisha kuwa kinachoongelewa na viongozi hao ni kupunguza tu hofu kwa wananchi lakini pasipo kurudi nyuma katika msimamo kuwa Ziwa hilo ni lao lote na hawapo tayari kuliachia.

Lakini kuna swali jingine la msingi zaidi. Je jeuri ya Malawi inatoka wapi? Je inachangiwa na makampuni yanayochimba raslimali katika Ziwa hilo? Je inachangiwa na uelewa kuwa nchi yetu kwa sasa inakabiliwa na ‘mizigo mikubwa’ kiasi cha kuiaminisha nchi hiyo kuwa hatuna uwezo wa kuwakabili? Na swali ambalo pengine ni gumu zaidi, je tuna uwezo wa kurejea ‘tulichomfundisha Nduli Idi Amin mwaka 1978-79?

Ili uingie vitani ni lazima uwe na taarifa sahihi dhidi ya adui yako. Je taasisi zetu zinazoonekana kama zimesalimu amri kwa mafisadi wanaotafuna nchi yetu zina uwezo wa kukusanya taarifa muhimu za kiusalama ili pindi tukiamua ‘liwalo na liwe’ dhidi ya Malawi tusiishie kujilaumu?

Vyovyote itakavyokuwa (huku tukiamini kuwa hakutokuwa na haja ya matumizi ya nguvu kutatua mgogoro huo) suala moja muhimu ni kuutumia mgogoro huu kama fursa ya kusaka suluhisho la kudumu.Kama ambavyo matatizo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unavyoendelea kuzalisha matatizo hususan kutokana na kukosekana utashi wa kisiasa kumaliza matatizo yaliyopo, mgogoro huu kati yetu na Malawi ambao umedumu kwa takriban nusu karne sasa unahitaji kumalizwa. Lakini ili hilo liwezekane ni muhimu kwa watawala wetu kuelewa vipaumbele vya taifa letu.

Na kwa vile katika mazingira tuliyonayo tunalazimika kuwa kitu kimoja (na kuweka kando ukweli kuwa baadhi ya wenzetu wameigeuza nchi yetu kuwa kitegauchumi chao) na tunalazimika pia kuwaamini watu walewale ambao ‘wanadai hawajui chanzo cha umasikini wetu’, basi ni muhimu Tuweke kando tofauti zetu na tuwe tayari kulinda na kutetea kile tunachoamini ni halali yetu.

Nimalizie kwa kutoa wito kuwa suala hili nyeti lisigeuzwe turufu ya kisiasa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015.Tusiruhusu wababaishaji wakurupuke na kauli za kusaka umaarufu pasipo kuwa na mikakati ya namna ya kutatua mgogoro huu kwa njia za amani.

Kwa jirani zetu wa Malawi na hususan Rais Banda, wito wangu kwao ni huu: amani ni muhimu kwetu sote, lakini wakati mwingine inalazimu kutumia mabavu ili kuleta amani ya kudumu. Pamoja na matatizo yetu, mie na pengine kila Mtanzania anaamini kuwa kamwe hatutoruhusu Ziwa Nyasa ligeuzwe ‘uwanja wa kutupima ubavu.’ Tulimsambaratisha Nduli Amin kwa sababu nia tulikuwa nayo, sababu tulikuwa nazo, na uwezo pia tulikuwa nao. Hata kama itaonekana kwa Wamalawi kuwa nia, sababu na uwezo wetu ni hafifu kwa sasa, hakuna Mtanzania aliye tayari kuona ardhi ya nchi yake ikimegwa au mipaka yetu ikichezewa.

Mwanafalsafa Sun Tzu anaonya; “gharama ya vita ni kubwa kuliko ushindi wowote utakaopatikana”   na “wanaoingia vitani hufanya hivyo wakiongozwa na ‘miscalculations’ hasa imani kuwa watashinda...lakini vita ikimalizika hujikuta wana hasara kubwa kuliko kabla hawajaingia vitani.

Mungu Ibariki Afrika

Barua-pepe: chahali@about.meBlogu: www.chahali.com   





0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget