KUNA msemo mmoja ninaopenda sana kuutumia kusisitiza hoja katika maongezi, ambao unasema, “Ili uweze kulielewa giza inabidi utoke au uende katika mwanga, na kinyume chake (vice versa).”
Huwa ninautumia msemo huu kubainisha ‘faida’ tuliyonayo baadhi yetu (Watanzania) tulio nje ya nchi yetu. Kwamba, kuwa kwetu huku kwa namna fulani kunatusaidia kuwa kama kile kinachofahamika katika tafiti kuwa ni “participant as an observer,” yaani kwa tafsiri isiyo rasmi ‘mshiriki ambaye pia ni kama mwangalizi.’
Kwa kuwa huku ughaibuni sio tu tunapata fursa ya kulinganisha tofauti ya mambo kati ya hapa na huko nyumbani bali pia tunaweza kuiangalia jamii yetu inayotuhusu lakini tukabaki watazamaji.
Hata hivyo, kuna wakati baadhi yetu tulio nje hukumbanana wakati mgumu kuzungumzia mambo ya huko nyumbani, hususan, kutokana na madai kuwa yanayotokea huku hayatugusi moja kwa moja.
Baadhi ya ‘wapinzani wetu’ hudiriki kwenda mbali zaidi na kutulinganisha na Watanzania ‘tusio kamili’ kwa maana ya kwamba shida au raha za huku hazitukabili katika namna zinavyowakabili wao.
Huu ni mtizamo potofu hasa ikizingatiwa kuwa wengi wetu, kama si sote, bado tuna ndugu, jamaa na marafiki huko nyumbani. Kimsingi, kuwa nje ya Tanzania hakumpunguzii mtu Utanzania wake, isipokuwa tu kwa wenzetu wachache ambao kuwa kwao huku kunamaanisha ‘talaka’ kati yao na asili yao.
Ni katika kuiangalia nchi yetu kwa mtizamo huo wa ‘mshiriki ambaye ni kama mwangalizi’ ndipo nimejikuta nikifikia hitimisho kwamba mwenendo wa mambo huko nyumbani una mushkeli.
Kati ya wiki iliyopita na muda huu ninapoandaa makala hii kumejitokeza matukio kadhaa yanayoweza kuashiria kuwa nchi yetu inakwenda ‘ndivyo sivyo.’
Nitatoa mifano machache. Habari ambayo imetawala katika vyombo vingi vya habari kwa sasa kuhusu mambo yalivyo huko nyumbani ni hili suala la baadhi ya wabunge kutuhumiwa kupokea rushwa.
Habari hiyo inapata uzito mkubwa zaidi pale inapotanabahisha kuwa licha ya baadhi ya wabunge kuandamwa na tuhuma hizo, baadhi ya Kamati za Bunge pia zinatuhumiwa kujihusisha na rushwa, hali iliyopelekea Spika wa Bunge kuamua kuivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.
Lakini tuhuma hizi za rushwa zimefichua kitu ambacho binafsi ninakiona kama tatizo la msingi katika jamii yetu. Katika siku chache zilizopita, nimekuwa nikitumia muda wangu mwingi katika mtandao wa kijamii wa twitter kuzungumzia tuhuma hizo dhidi ya wabunge, hususan, wale wanaodaiwa kupokea mlungula ili kulifisadi Shirika la Umeme (TANESCO).
Jumapili iliyopita mmoja wa tunaoweza kuwaita watu maarufu (celebrities) alionekana kuchukizwa na twiti zangu ambazo kimsingi zilikuwa zinaelekezwa kwa mbunge mmoja wa chama cha upinzani ambaye ametangaza dhahiri kuwa ana nia ya kuwa rais wetu huko mbele.
Katika mazingira ya kawaida tu, mwanasiasa anayetamka hadharani kuwa anataka kuwa rais ni lazima aangaliwe kwa makini ili wapiga kura wapate fursa nzuri ya kumuelewa.
Kwa sababu anazozijua yeye binafsi, celebrity huyo wa kike alinivurumishia maneno makali akidai kuwa tuhuma nilizotoa dhidi ya mwanasiasa huyo zina dalili za chuki binafsi, hasa kwa ile haijathibitishwa kuwa mwanasiasa huyo ni fisadi.
Lakini kabla sijatulia, mwanamama mwingine msomi na mwenye wadhifa kwenye taasisi moja ya umma naye akanihoji ni mahali gani mwanasiasa huyo ametajwa kuwa ni mwizi. Labda hadi hapa msomaji unaweza kujiuliza kwanini ‘utetezi’ dhidi ya mwanasiasa huyo unaonekana kwa jinsia moja tu.
Huyu mtu wa pili kukerwa natwiti zangu kuhusu mwanasiasa huyo ndiye aliyenigusa zaidi, kwa sababu kimsingi, elimu na madaraka yake yanamweka katika kundi la kijamii linalofahamika kama tabaka la kati.
Nilishawahi kuandika katika makala moja huko nyuma kuhusu jinsi tabaka hili la kati linavyoshindwa kuwa kiunganishi cha kupigania maslahi ya tabaka la chini la walalahoi.
Nilieleza katika makala hiyo kwamba tabaka la kati lingeweza kuwa nguvu muhimu ya kupigania maslahi ya tabaka la chini kutambuliwa, na hatimaye kufanyiwa kazi na tabaka la juu (ambalo hujumuisha tabaka tawala).
Nikinukuu maneno ya binti huyo wa pili, alinieleza kuwa “wanamchukia mwanasiasa huyo wajinyonge, kwani njia yake kuelekea Ikulu ipo wazi.” Niliguswa sana na maneno haya kwa sababu wakati mwanasiasa huyo anaonekana kupata utetezi katika tuhuma zinazomkabili kuhusu kuifisadi TANESCO, sio tu kuna watuhumiwa wengine wasiotetewa bali pia hata huko nyuma baadhi ya wanasiasa waliotuhumiwa kuwa mafisadi hawakuwahi kutetewa kiasi hicho.
Japo ninatambua na kuheshimu haki ya kila Mtanzania kumtetea mwanasiasa anayempenda, ukweli ni kwamba licha ya utetezi huo kuwa wa ‘upendeleo’ (kile kinachoitwa na Waingereza kuwa ni haki ya upendeleo-selective justice), kwa maana ya kuwa watuhumiwa wengine kwenye kashfa hiyo hawapati utetezi kama ilivyo kwa mwanasiasa huyo, tunapotetea tuhuma za ufisadi kwa vile tu ‘tuna mahaba’ na tunaowateta, tunaweza kuwafahamasisha mafisadi wengine waendelee kuitafuna nchi yetu wakijua watatetewa.
Moja ya mambo yanayokwaza sana maendeleo yetu ni kile ninachokiita ‘siasa za mahaba.’ Kwamba mgombea uongozi hapimwi kutokana na sifa na/au uwezo wa kutumikia umma bali kinachoangaliwa ni urafiki, haiba na vitu kama hivyo visivyoweza kuwa vigezo vya uongozi bora
Bado ni mapema kutoa hitimisho kuhusu wabunge wanaotuhumiwa kujihusisha na rushwa, hususan hiyo ya kuihujumu TANESCO, ukweli kwamba tuhuma hizo zimewekwa hadharani unaeleza bayana kuwa ufisadi umeingia katika hatua mpya na ya hatari zaidi ambapo baadhi ya watu tuliowakabidhi dhamana ya kutunga sheria (ikiwa ni pamoja na zile za dhidi ya ufisadi) nao ni sehemu ya tatizo la ufisadi.
Nimebainisha hapo mwanzoni kuwa matukio ya hivi karibuni yanaashiria kwamba hali ya mambo si shwari. Jingine lililonigusa ni suala la mgomo wa walimu ambapo japo kumekuwa na taarifa za kukanganya, kuna dalili kuwa mgomo huo unaendelea.
Lakini tukio lililotokea katika shule ya msingi ya Maili Moja, Kibaha, linaweza kutufumbua macho zaidi kuhusu mwenendo wa nchi yetu. Inaelezwa kuwa katika tukio hilo, wanafunzi wenye hasira waliamua kuvurumisha mawe shule yao. Sina hakika kama walifanya hivyo kama ishara ya kupinga mgomo wa walimu wao au kuwaunga mkono, lakini kilicho wazi ni kuwa pindi inapofika mahala wanafunzi wa shule ya msingi wanachukua ‘sheria mkononi’ basi ni wazi kuwa Taifa letu limefika mahali pabaya.
Wanafunzi hawa ndio kizazi cha kesho, ndio mawaziri na wabunge wetu, ndio viongozi wa kesho. Sasa inapofika mahala nao wanaingia katika utamaduni mpya wa ‘vurugu kama ufumbuzi wa matatizo’ sijui huko mbele itakuwaje.
Majuzi tu tulishuhudia mgomo wa madaktari ambao bado unaelekea kuwa haujaisha kwa utimilifu (taarifa kwenye mtandao mmoja wa jamii inaeleza kuwa baadhi ya madaktari wameonyesha dhamira ya kutaka kurejea tena kwenye mgomo). Kabla hatujasahau kuhusu mgomo huo tunasikia jinsi baadhi ya wabunge wanavyoshiriki kuihujumu TANESCO.
Wakati huohuo tunashuhudia baadhi ya walimu wakiamua kutimiza azma yao ya siku nyingi ya kugoma. Lakini pengine kubwa na la kutisha zaidi ni taarifa kuwa mmoja wa viongozi maarufu wa dini amekumbwa na kashfa ya shule yake kuiba uniti za umeme wa TANESCO. Haya yote (na mengine ambayo nafasi hairuhusu kuyataja) yanaashiria kuwa hali si shwari huko nyumbani.
Je, viongozi wetu wanafanya nini kukabiliana na hali hii? Usidhani hiki ni kichekesho lakini siku moja kabla sijaandaa makala hii kulikuwa na taarifa kuwa Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai alionekana anaongea na simu wakati kikao cha Bunge kinaendelea.
Labda ilikuwa ni simu muhimu kutoka kwa Spika au pengine Rais, lakini taswira ilivyotokana na tukio hilo inaweza kutanabaisha ni jinsi mtizamo wangu kuwa hali ya mambo si shwari huko nyumbani ilivyotofautina baadhi ya viongozi wetu, ambapo hata kwenye majukumu muhimu ya kuogoza Bunge wanamudu kuongea na selula zao.
Funga kazi ni uamuzi wa Serikali kulifungia jarida la Mwanahalisi kwa muda usiojulikana kwa madai kuwa jarida hilo limekuwa likiandika habari za uchochezi.
Katika toleo lililopita jarida hilo kulikuwa na habari kuhusu suala la Dk. Steven Ulimboka na mtumishi wa taasisi nyeti ya serikali alihusishwa nayo. Je, serikali haidhani kuwa uamuzi wake kulifungia jarida hilo unaweza kutafsiriwa kama unalenga kulizuia kuibua ‘makubwa zaidi’ kuhusu sakata hiyo?
Hivi isingewezekana kulifikisha jarida hilo mahakamani ili haki si tu itendeke bali ionekane imetendeka? Na je, uamuzi wa kulifungia unasaidiaje kuzifanya habari zilizoandikwa nalo zionekane ni uchochezi tu.
Nimalizie kwa kutoa rai ya haja ya mjadala wa kitaifa kuhusu hatma ya Taifa letu. Tunakoelekea si kizuri. Na hili la mjadala si kuhusu tabaka tawala (walio katika bunge, serikali, nk) bali pia kuna haja ya mjadala wa kitaifa kuhusu nafasi ya tabaka la kati katika kuhamasisha, kutetea na hata kupigania maslahi ya tabaka la chini la walalahoi linaloelekea kuachwa bila mtetezi wala msomaji.
Tanzania ni yetu sote. Tuweke kando siasa za mahaba, tuepuke kutanguliza maslahi binafsi badala ya maslahi ya Taifa, tutatue tofauti zetu (migomo, nk) kwa njia za kidiplomasia, na kubwa zaidi tuungane kwa pamoja kuhangaikia kuipeleka nchi yetu katika mwelekeo sahihi.
Inawezekana, timiza wajibu wako.
0 comments:
Post a Comment