“TUMEROGWA na aliyeturoga naye karogwa, kisha kafariki.”
“Hapana, hatujarogwa ila nadhani bongo zetu zimefungwa, na funguo zimetumbukia chooni.”
Hizo ni baadhi ya kauli zinazoanza kuzoeleka masikioni mwa Watanzania wanapojadili mustakabali wa nchi.
Ukisikia kauli hizo unaweza kuishia kucheka kwa kuzitafsiri kuwa ni utani tu. Lakini ukichukua muda kuzitafakari, unaweza kujikuta unaungana kimtizamo na watu hao.
Hivi katika mazingira ya kawaida unawezaje kuelezea ‘busara’ za Kamati ya Olimpiki kujaza viongozi wengi zaidi wa wanamichezo kwenye msafara wa wawakilishi wetu kwenye mashindano ya Olimpiki ya majira ya joto yaliyomalizika juzi jijini London, hapa Uingereza?
Wakati wenzetu Wakenya wakirejea na medali kadhaa huku Waganda wakijivunia medali ya dhahabu, sisi tumeendelea kupigilia mstari ‘sifa’ yetu ya kuwa kichwa cha mwendawazimu.
Lakini ukidhani uhuni huo katika ushiriki wetu kwenye Olimpiki unachefua, basi sikiliza hii ‘kali kubwa’ kutoka kwa Bunge letu tunaloliita ‘tukufu.’ Wiki iliyopita, Naibu Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai aliwaeleza Watanzania kuwa baadhi ya wawakilishi wao bungeni (wabunge) wamekuwa wakiingia kwenye vikao vya chombo hicho cha kutunga sheria wakiwa wamelewa pombe na sigara zisizo za kawaida.
Kabla hatujaenda mbali kujadili taarifa hii ya kuogofya ni vema tukakumbushana kuwa kwa mujibu wa marekebisho ya hivi karibuni, waheshimiwa wabunge wanalipwa shilingi milioni 11 kwa mwezi. Ni muhimu kutaja kiwango hicho ili tunapowajadili watu hawa tuwe na uelewa kuwa pamoja na umasikini wa nchi yetu tumejikamua na kuwapatia waheshimiwa hawa maslahi manono kabisa.
Kwa namna fulani ninampongeza Naibu Spika Ndugai kwa kutufungua macho kuhusu swali ambalo ninadhani wananchi wengi wamekuwa wakijiuliza, “kwanini baadhi ya waheshimiwa huonekana wamelala bungeni huku kikao kinaendelea?”
Mitandaoni kumejaa picha za ‘wachapa usingizi bungeni’ na kuna waheshimiwa wengi tu wanaopenda kuligeuza Bunge kuwa sehemu ya kulala.
Baadhi yetu tulipoona picha za aina hiyo tulijaribu kujipa matumaini kuwa labda waheshimiwa hao wanazidiwa na usingizi kwa vile ‘wanakesha wakitafakari jinsi ya kuwatumikia wapigakura wao, na pengine nchi kwa ujumla, kwa ufanisi mkubwa zaidi.’
Kadhalika, kauli ya Ndugai imetusaidia pia kutupa mwanga kuhusu michango ya baadhi ya wabunge ambayo mwananchi hawezi kulaumiwa akihisi mchangiaji anatafuta nafasi ya ushiriki wa Bongo Star Search kwa kipaji cha mipasho. Inakera lakini ndio ukweli wenyewe, baadhi ya waheshimiwa hutumia fursa ya kuchangia hoja kuonyesha umahiri wao wa kukebehi, kudhihaki na hata kutusi.
Lakini kilichonikera katika maelezo ya Ndugai ni ‘utetezi wa kitoto’ kuwa, (ninamnukuu) “Wabunge ni watu kama watu wengine, wana tabia kama walivyo wanadamu wengine, wapo ambao kwa namna ninavyohisi wanaingia bungeni hasa vikao vya kuanzia mchana wakiwa wamepiga bia.”
Kwanza, wabunge wetu si sawa na ‘watu wengine.’ Ni ‘watu wengine’ wangapi wanaitwa ‘waheshimiwa’? Na ni wangapi wanaolipwa posho kwa kutimiza wajibu wao (licha ya kulipwa mshahara kwa nyadhifa zao)? Na ni ‘watu wengine’ wangapi wanaolipwa mishahara minono japo kwa kiasi kikubwa ufanisi wao upo zaidi kwenye mipasho, kukashifiana na porojo nyingine zisizomsaidia Mtanzania?
Ndugai hayupo sahihi kudai kuwa wabunge wanaoingia bungeni wamelewa ‘wana tabia kama walivyo binadamu wengine.’ Mimi kama mwanafunzi siruhusiwi kuingia darasani nikiwa nimelewa. Hata kwenye sehemu za vinywaji ‘baamedi’ haruhusiwi kuingia kazini amelewa. Sasa hao ‘binadamu kama wengine’ anaotueleza Naibu Spika wametoka sayari gani?
Halafu cha kuchukiza zaidi ni ukweli kwamba Naibu Spika anafahamu kuwa kuna wabunge wanaingia kwenye vikao vya Bunge wakiwa wamelewa lakini hachukui hatua zozote bali anasubiri hadi apate nafasi ya kumwaga jambo hilo kwenye mahojiano na kituo cha runinga.
Huyu ni kiongozi dhaifu. Japo tunaweza kumpongeza kwa ‘kutuibia siri ya yanayojiri bungeni’ lakini dhamana aliyokabidhiwa si kunyooshea watu vidole (kwa maana ya kubainisha kuna wabunge walevi) bali kuchukua hatua stahili dhidi ya ‘wahalifu’ hao.
Na si kama nimetumia neno ‘wahalifu’ kwa bahati mbaya. La hasha. Mtu anayelipwa shilingi milioni 11 kama mshahara wa kumwakilisha mwananchi, kisha akaamua kufanya uwakilishi huo akiwa amepata bia kadhaa, au amevuta sigara isiyo ya kawaida (bangi?) au amelamba vitu fulani (‘unga’-madawa ya kulevya?), hana tofauti na mhalifu.
Ni jambazi anayesababisha watu waishi kwa shida ili wamudu maslahi yake kwa matarajio kuwa maslahi hayo manono yataleta ufanisi katika kazi lakini yeye anaishia kutekeleza majukumu yake akiwa na ‘faida kichwani’ (kalewa)!
Katika moja ya makala zangu huko nyuma niliweka wazi msimamo wangu kuwa mishahara mikubwa kupita kiasi ya wabunge wetu ni ujambazi wa mchana kweupe (daylight robbery) kwa sababu haiendani na hali mbaya ya uchumi watu. Na sasa ujambazi huo unajidhihirisha bayana kwa uhuni wa baadhi ya waheshimiwa wanaopuuza kanuni za Bunge na wajibu wao, na kutinga bungeni wamelewa.
Lakini kuna swali moja la msingi ambalo kila Mtanzania anapaswa kujiuliza, “IMEKUWAJE TUMEFIKA MAHALA BAADHI YA WABUNGE WANATINGA BUNGENI WAKIWA WAMELEWA?”
Msomaji mmoja wa jarida hili, Omary Abdallah, Mtanzania anayeishi nchini Ujerumani alinitumia ujumbe kupitia mtandao wa facebook akishauri kuwa badala ya kuendelea kuwalaumu viongozi wabovu inabidi sisi Watanzania wenyewe tuangalie mapungufu yetu yanayotufanya kuchagua viongozi wasiofaa (kwa mfano hao walevi).
Kwa kifupi, msomaji huyo anahitimisha kuwa Taifa limegubikwa na utapeli na uvivu. Rejea kwenye kampeni za ubunge. Utaona mgombea ‘anatoka jasho mwilini na mapovu mdomoni’ kuwahadaa wapigakura jinsi anavyowajali. Na kwa uvivu wetu wa kufikiri, wala hatuhoji iwapo ‘uchungu’ wa mgombea huyo ni kwa ajili ya maslahi yetu au ya tumbo lake (na pengine ‘nyumba ndogo’ zake). Matokeo ndio hao tunaoambiwa wanatuwakilisha wakiwa wamekunywa, kuvuta au kulamba kilevi.
Lakini pia, katika skandali hii ya ulevi wa baadhi ya wabunge, ninaona kipato cha waheshimiwa hao kuwa miongoni mwa vichocheo vya kuwasahaulisha wajibu wao.
Katika mazingira ya kawaida tu, mtu anayepewa fedha nyiiingi zaidi ya mahitaji yake anaweza kuishia kufanya mambo ya ajabu kabisa. Kwa huku Ughaibuni tunashuhudia baadhi ya wanasoka, kwa mfano, ambao wanalipwa mamilioni ya fedha, na kuna aina ya mwafaka wa kimtizamo kuwa ‘madudu’ yanayofanywa na baadhi yao yanachangiwa na wingi wa fedha usiowiana na mahitaji yao ya kawaida.
Suala la nyongeza ya mishahara ya wabunge linaonekana kama limeridhiwa na umma. Wakati madaktari na walimu wakiambiwa serikali haina fedha za kuboresha stahili na mazingira ya kazi zao, hatujapewa sababu za msingi za kuongeza mishahara ya wabunge ambao tayari walikuwa na mishahara mikubwa kabisa.
Utendaji kazi wa wengi wao hauendani na hata ‘kidogo’ walichokuwa wanapewa kabla ya mishahara mipya. Ikumbukwe kuwa mamilioni hayo kwa wabunge wetu ni fedha za walipakodi ambao wengi wao ni masikini wa kupindukia. Kuna kila sababu ya si tu kulaani ‘unyonyaji’ huu bali pia kuupinga kwa nguvu zote.
Sasa, kwa vile tumeruhusu ubunge uwe njia ya mkato ya kukwaa utajiri basi tutarajie kuona chaguzi zetu huko mbele zikiandamana na kila aina ya vituko na vioja miongoni mwa wanaotaka kuwa sehemu ya ‘mradi huu wa utajiri wa chap chap’ (get-rich-quick scheme).
Katika hali ya kawaida tu, nani asiyetaka kulipwa japo shilingi elfu kadhaa tu kwa kazi ya kulala huku una bia mbili tatu kichwani? Ni kama kwenda baa kisha unalipwa kwa kulewa.
Naomba ieleweke kuwa si kila mbunge hatimizi wajibu wake. Kuna wazalendo wachache wanaotambua majukumu yao. Baadhi yao, wameishia ‘kuumbuliwa’ na Kiti cha Spika kwa ‘kukiuka kanuni za Bunge (isomeke: kutetea maslahi ya wapigakura katika namna isiyokubalika kwa watawala).
Mashujaa hawa wachache wana ujasiri wa ziada kwani wakati wao wanatolewa nje kwa kutimiza wajibu wao, wanashuhudia baadhi ya wanaoachwa waendelee na vikao wakiwa wamelala kutokana na kinywaji, sigara zisizo za kawaida au kulamba vitu flani.
Nimalizie kwa kurejea maswali niliyoyanukuu mwanzoni mwa makala hii. Tumerogwa na aliyeturoga nae karogwa kisha kafariki, au akili zetu zimefungwa kisha ufunguo umepotea? Naomba usinijibu bali jibu lako liwe kwenye sanduku la kura katika uchaguzi ujao.
Penye nia pana njia
0 comments:
Post a Comment