Thursday, 2 January 2014


HERI ya mwaka mpya wasomaji wapendwa wa safu hii na gazeti hili kwa ujumla. Kumaliza mwaka si jambo dogo na kuanza mwaka mpya pia kunahitaji tafakuri nzito, hasa tukizingatia yaliyojiri katika mwaka uliopita 2013.
Katika makala hii nitajaribu kurejea nilichokifanya mwanzoni mwa mwaka 2012, yaani kubashiri mwelekeo wa masuala mbalimbali, hususan huko nyumbani.
Mwanzoni mwa mwaka jana sikufanya hivyo kwa sababu mbalimbali za msingi, mojawapo ikiwa dalili kuwa mengi ya yaliyojiri 2012 yangejitokeza tena 2013
Mwaka huu 2014 unatarajiwa kuwa na tofauti za msingi kulinganisha na mwaka jana, kubwa zaidi likiwa harakati za kuelekea katika Uchaguzi Mkuu hapo mwakani.
Mara kadhaa nimeandika kuwa ukweli una tabia moja kuu: kuuchukia hakuufanyi uwe uongo. Na moja ya ukweli mbaya kuhusu mwaka huu ni uwezekano wa kushuhudia vihoja ambavyo huenda havijawahi kutokea katika historia ya taifa letu.
Vihoja ninavyobashiri kutokea vitahusu mtifuano mkubwa ndani ya chama tawala CCM, chama kikuu cha upinzani CHADEMA, na kwa kiasi fulani katika baadhi ya vyama 'vidogo' vya upinzani kama vile CUF, NCCR-Mageuzi, TLP na UDP.
Ninabashiri kwamba takriban vyama vyote hivyo vitayumbishwa na migogoro ya wazi au ya siri, aidha kati ya viongozi au wanachama wenye nia ya kuteuliwa kuwa wagombea urais kupitia tiketi za vyama vyao au makundi yao (hili la makundi ni kwa CCM zaidi).
Wakati ninabashiri mtifuano ndani ya CCM kuwa wa dalili zaidi kuliko kujitanabaisha hadharani, kwa CHADEMA na vyama vingine vya upinzani hali inatarajiwa kuwa tofauti ambapo baadhi ya wanasiasa wataweka kando maslahi ya vyama hivyo na kupambana hadharani.
Kubwa zaidi ninalotarajia kuliona ni mwendelezo wa mgogoro uliopo ndani ya CHADEMA, ambapo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe ataendelea kuwa 'tatizo' kwa viongozi wenzake, hususan Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dokta Willbroad Slaa.
Japo hili sina hakika nalo sana lakini kuna uwezekano wa aidha Zitto kufukuzwa au yeye mwenyewe kujiondoa katika chama hicho. Yoyote kati ya hatua hizo halitasaidia kumaliza mgogoro ndani ya chama hicho kwani kuna uwezekano wa 'masalia ya Zitto' kuendeleza harakati za 'mageuzi' aliyoyaasisi.
Ni vigumu kutabiri hatma ya CHADEMA siku kama leo hapo mwakani lakini ninabashiri kuwa chama hicho hakitakufa bali kuna uwezekano wa kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na mgogoro huo, kiasi cha kutokuwa tishio la kubwa kwa CCM.
Kwa upande wa vyama vingine, ninatabiri uwezekano wa kuwepo harakati za kuwang'oa "wagombea urais wa kudumu" yaani Seif Sharrif Hamad na Ibrahim Lipumba kwa upande wa CUF, John Cheyo kwa UDP na Augustine Mrema kwa TLP. Harakati hizo zinaweza kusababisha vyama hivyo kudidimia zaidi ya ilivyo sasa. Binafsi sioni dalili za vyama hivyo kuimarika hata kama vitapata safu mpya za wagombea au viongozi.
Moja ya matukio makubwa yanayoweza kutokea ni kuibuka kwa chama kipya ambacho kitaimarishwa na kujiunga kwa wanasiasa maarufu. Kuna uwezekano pia kuwa chama hicho kisiwe kipya bali ni miongoni mwa vyama vilivyopo, huku ubashiri wangu ukiiona NCCR - Mageuzi kama yenye uwezekano wa kunufaika na hali hiyo.
Kwa upande wa CCM, sioni dalili ya 'machafuko' tofauti na hali ilivyo sasa. Uwezekano mkubwa ni kuongezeka na kushamiri kwa kile kinachofahamika kama siasa za majitaka ambapo maovu ya kweli au ya kusingiziwa yatawekwa hadharani ili kupunguza kasi za baadhi ya wenye nia ya kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho.
Kuna uwezekano, japo pengine si mkubwa, wa baadhi ya vigogo wa chama hicho kuhama baada ya kubaini kuwa wana nafasi finyu ya kuteuliwa kumrithi Rais Jakaya Kikwete kwa tiketi ya CCM. Moja ya wanasiasa wanaoweza kuachana na chama hicho ni Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye.
Inaniwia vigumu kufanya ubashiri wa kueleweka kuhusu CCM kwa vile hadi ninapoandaa makala hii bado kuna dalili ya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri. Ni wazi, iwapo Rais Jakaya Kikwete ataamua kumwondoa Waziri Mkuu Mizengo Pinda (sidhani kama hilo litatokea) yeyote atakayemrithi anaweza kuwa na nafasi nzuri ya kuleta changamoto mpya kwenye kinyang'anyiro cha kumpata mrithi wa Kikwete.
Kwa upande mwingine, ninabashiri kuwa safari mfululizo za Rais Kikwete nje ya nchi zitaendelea kuwepo. Kadhalika, ninabashiri kuwa tutaendelea kusikia habari za ufisadi wa kutisha unaoweza kusababisha Rais Kikwete kufanya mabadiliko mengine katika Baraza lake la Mawaziri.  Uwezekano wa ufisadi zaidi unachangiwa na ukweli kuwa baadhi ya viongozi watakuwa na hakika kuwa hawatorejea bungeni mwaka 2015 na hivyo wataongeza kasi ya ulaji (ufisadi) kwa staili ya 'chukua chako mapema.'
Kadhalika, kutokana na mapambano ndani ya CCM ya kuwania nafasi ya urais mwaka 2015 kwa tiketi ya chama hicho, kuna uwezekano wa kuibuka 'wazalendo feki' watakaoibua taarifa za ufisadi. Ninasema 'feki' kwa sababu kitakachowasukuma kuibua taarifa hizo sio mapenzi yao kwa nchi yetu bali kujisafishia nafasi zao kumrithi Rais Kikwete.
Kwa upande mwingine, ajali zitaendelea kuteketeza maisha ya Watanzania wenzetu na kama ilivyokuwa mwaka jana, habari hizo zitaendelea kuishia kuwa vichwa vya habari vikubwa au ‘breaking news’ pasipo jitihada ya kukabiliana na tatizo hilo la ajali.
Vilevile ninatabiri kuwa tutaendelea kusikia majina ya watu maarufu, hususan wasanii yakihusishwa na biashara ya dawa za kulevya. Japo ninaombea hili lisitokee, kuna uwezekano wa angalau msanii mmoja kututoka kutokana na matumizi ya dawa za kulevya ilhali wasanii kadhaa wanaweza kukamatwa nje ya nchi (hususan Mashariki ya Mbali) wakiwa na shehena za mihadarati.
Kisichonipa shida kubashiri ni uwezekano wa wazi kuwa hakuna kigogo yeyote wa biashara hiyo ya dawa za kulevya atakayekamatwa japo kuna uwezekano wa majina makubwa kufahamika kuwa yanajihusisha na biashara hiyo haramu.
Vilevile, matukio ya utekaji, utesaji na hata vifo dhidi ya wanahabari na watetezi wa haki za jamii au binadamu yataendelea kusikika. Kuna uwezekano wa kujitokeza wanahabari au wanaharakati watakaojitoa mhanga kuripoti kwa uwazi kuhusu ufisadi na uhalifu wa masuala kama biashara ya mihadarati au ujangili lakini, japo natamani Mungu aepushe, wanaweza kuishia kukumbana na yaliyowakuta Absalom Kibanda, Dk. Steven Ulimboka au Daudi Mwangosi. Ninaomba kusisitiza kuwa uwezekano wa majanga hayo usiwavunje moyo wanahabari na wanaharakati.
Jingine ambalo halinipi shida kutabiri ni mwendelezo wa mgawo wa umeme pasipo maelezo ya kueleweka kutoka serikalini au Tanesco, sambamba na Bunge letu tukufu kuendelea kuwa ukumbi wa mipasho, matusi na hata vurugu, huku kila kikao kikitanguliwa na vichwa vya habari magazetini "Bunge kuwaka moto" (moto huo utaishia kuchoma fedha za walipakodi kwa maana ya maslahi manono kwa wabunge, na si moto wa kutetea maslahi ya wananchi wanaowakilishwa na wabunge hao).
Ninaomba kuhitimisha makala hii kwa kueleza kuwa ninatarajia kufanya utabiri mwingine katika toleo lijalo kuhusu masuala ya kimataifa. Vilevile ninaomba kutoa angalizo kuwa utabiri huu umezingatia mwenendo wa mambo ulivyokuwa mwaka jana na 'hauna mwamana' (guarantee) kuwa kila nilichotabiri kitakuwa hivyo.
Kwa mara nyingine, ninawatakia heri ya mwaka mpya 2014



0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget