Saturday, 25 January 2014


YAYUMKINIKA kuhitimisha kuwa Tanzania yetu ni moja ya nchi rahisi kuongozwa duniani. Japo wakati mwingine urahisi huo unachangiwa na sheria dhalimu au matumizi ya ubabe yanayofanywa na dola, kwa kiasi kikubwa Watanzania ni wapole kiasi kwamba hata wakitendwa visivyo kwa muda mrefu, kwa wengi wao si jambo la kuwaamsha kudai stahili zao.
Na pengine hakuna mfano rahisi wa urahisi wa kuingoza Tanzania kama katika adha ya mgawo wa umeme wa milele. Hapa nakiri ukweli kwamba moja ya mambo yanayonikera niwapo mtandaoni ni kukumbana na watu wanaolalamikia mgawo wa umeme (wengine kwa lugha isiyoandikika gazetini) kila kukicha.
Kulalamika si tatizo na wanaolalamika wana haki ya kufanya hivyo. Tatizo ni ukweli kwamba malalamiko yao ambayo nyakati nyingine huambatana na matusi mazito dhidi ya TANESCO hayajamsaidia kwa namna yoyote angalau kupunguza tatizo la mgawo wa umeme.
Kimsingi, atakayehitimisha kuwa Watanzania wameridhia kutopewa huduma ya uhakika ya umeme, hatakuwa amekosea. Nimewahi kutumia mfano huu wa hamasa mara kadhaa, kwamba mkoloni hakuamua tu kutupatia uhuru kwa vile hatukupenda uovu aliotufanyia, Nduli Idi Amin hakusalimu amri katika Vita ya Kagera kwa vile tulimwita kila aina ya jina baya, na makaburu huko Afrika Kusini hawakuamua tu kuacha mfumo wa ubaguzi kwa vile sio wa kibinadamu. Zilifanyika jitihada kubwa za kuwafikishia ujumbe wakoloni, Amin na makaburu kuwa ‘imetosha,’ sambamba na harakati za vitendo za kumaliza uovu wao.
Pengine mfano mwingine wa karibu ni malalamiko ya wananchi wengi kuhusu huduma zisizokidhi matakwa za baadhi ya kampuni za huduma huko nyumbani, hususan kampuni za simu. Utakutana na mtu anaitukana kampuni ya simu, ilhali hajashikiwa mtutu wa bunduki kuendelea kuwa mteja wa kampuni hiyo. Wengi wa watumiaji wa huduma ya simu huko nyumbani ni wa ‘malipo kabla’ (pre-payment) na hawabanwi na mikataba yenye masharti kama wale wa ‘malipo baada’ post-payment).
Binafsi, nipo katika mkataba wa miezi 24 wa huduma ya simu ya mkononi, na katika kipindi hicho, nikiamua kuachana na kampuni inayonipatia huduma nitalazimika kulipa fidia ‘kubwa tu.’ Lakini huko nyuma niliwahi kuwa mteja wa huduma za ‘pay as you go’ (lipa kadri unavyotumia) na kila nilipoona siridhishwi na huduma ya kampuni husika niliachana nayo.
Lengo la makala haya si kujadili tatizo la mgawo wa umeme, huduma mbovu za TANESCO na baadhi ya kampuni za huduma au hata upole wa Watanzania. Badala yake, wiki hii ninatupia jicho ‘matumaini hewa ya Watanzania wengi’ wakati walipokuwa wakisubiri mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyotangazwa Jumapili iliyopita.
Kama ilivyo kabla ya kila kikao cha Bunge ambapo vyombo mbalimbali vya habari hupambwa kwa vichwa vya habari kama ‘Bunge kuwaka moto’ au ‘Wabunge kuikalia kooni serikali,’ kisha vikao hivyo vya Bunge kuisha bila lolote la maana, kama ilivyotokea katika vikao vilivyotangulia, ndivyo vyombo vingi vya habari vilifanya bidii kubashiri ‘makubwa’ katika mabadiliko hayo ya Baraza la mawaziri.
Sijui matumaini hayo ‘hewa yalitoka wapi hasa ikizingatiwa kuwa taratibu za uteuzi ambazo huko nyuma zimeonekana kuzaa wateuliwa wabovu ni zilezile.
Nikiri kwamba nilikuwa ‘mhanga’ wa matumaini hayo  lakini angalau matumaini yangu hayakuwa ‘hewa’ kwani yametimia kwa kiasi fulani. Nilitaraji aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, awe Waziri kamili, na hilo limetokea. Niliandika katika makala yangu moja huko nyuma kwa nini ninamwona mwanasiasa huyo kama mwenye sifa kadhaa za kuigwa na wanasiasa wenzie, kubwa zaidi ikiwa ni uzalendo kwa mantiki ya kujiepusha na kasumba ya kutanguliza itikadi za kisiasa mbele ya maslahi ya taifa.
‘Kilichonitibua nyongo’ katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue (kuna wanaohoji kwa nini mabadiliko hayo hayakutangazwa na Rais Jakaya Kikwete kama ilivyozoeleka) ni uteuzi wa Mwigulu Nchemba kuwa Naibu Waziri wa Fedha. Pengine hisia zangu baada ya kusikia habari hizo zinaelezeka vizuri ‘andiko’ nililotundika katika blogu yangu kwamba uteuzi huo ni ‘utani mbaya’ (a bad joke).
Akiwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Mwigulu alifanya kila aliloweza kujenga uhasama mkubwa miongoni mwa Watanzania kupitia kauli na matendo yake dhidi ya vyama vya upinzani na baadhi ya viongozi wake, hususan CHADEMA. Kuthibitisha upungufu wake wa busara, kuna wakati Mwigulu alionyeshwa katika pichani akiwa na mbwa aliyevishwa bendera ya CHADEMA. Kitendo hicho ni zaidi ya ‘utoto wa kisiasa’ (political immaturity).
Lakini pamoja na kushtushwa na kukerwa na uteuzi huo wa Mwigulu kuongoza Wizara hiyo nyeti,  binafsi nimeelewa mantiki ya Rais Kikwete (angalau kwa hisia zangu tu). Kwanza, sasa tunaelewa kuwa yale yote yaliyokuwa yanatukera wengi katika kauli na matendo ya Mwigulu yalikuwa na baraka za Mwenyekiti wake, yaani Rais Kikwete, na sasa amezawadiwa unaibu waziri kwa ‘kazi nzuri aliyofanya.’
Pili, sote tunafahamu kuwa moja ya changamoto zinazoikabili CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu hapo mwakani ni upatikanaji wa fedha (kihalali au isivyo halali). Japo ninaweza kuwa sipo sahihi, ninashawishika kuhisi kuwa uteuzi wa Mwigulu kwenda Hazina una uhusiano na jitihada za chama hicho tawala kujitengenezea mazingira ya kupata fedha kwa ajili ya kampeni za uchaguzi huo. Je, tutarajie ‘EPA’ nyingine? Ni muda tu unaoweza kutupa jibu.
Tatu, uteuzi wa Mwigulu ni mwendelezo wa tatizo sugu la kuweka mbele itikadi badala ya maslahi ya taifa. Kila anayefuatilia siasa za nchi yetu anatambua kuwa mwanasiasa huyo ni nguli wa siasa za uadui, na japo katika utendaji wake wa kazi anapaswa kuzingatia taratibu na kanuni, ni wazi kuwa vyama vya upinzani vitaendelea kumwona kama adui yao.
Vinginevyo, vihoja lukuki alivyofanya dhidi ya wapinzani vilikuwa ni sehemu ya mkakati makusudi wa CCM, yayumkinika kujiuliza; “kama mtu alifanya madudu kwenye ulingo wa siasa, atawezaje kuleta ufanisi kwenye sekta nyeti ya uchumi (katika Wizara ya Fedha)? Tuwe wa kweli, wakati hata mimi ninaweza kubainisha kwa nini mtu kama Nyalandu alistahili kupanda ngazi, ni nani anayeweza kusimama hadharani kutueleza japo sababu moja tu ya Mwigulu kupewa wadhifa huo?
Kwa upande mwingine, ni muhimu kutambua kuwa ‘shangwe’ za kuona baadhi ya mawaziri wakipumzishwa baada ya mabadiliko hayo, kwa mfano aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo, Philip Mulugo (atakayekumbukwa zaidi kwa ubabaishaji wake wa “Muungano wetu ni kati ya visiwa vya Pemba na Zimbabwe”) sio tu zinaambatana na gharama kubwa kifedha, lakini pia haitakuwa jambo la kushangaza kusikia waliopumzishwa wakipewa ukuu wa mikoa au ubalozi.
Nimalizie makala haya  kwa kurejea nilichotanabaisha mwanzoni kuwa nchi yetu ni rahisi sana kuongozwa, na pengine ndio maana tunashuhudia hata wanasiasa wenye vihoja kama Mwigulu wakipewa unaibu waziri katika wizara nyeti. Kwa nini mtawala achelee matokeo ilhali anatambua fika kuwa anaowaongoza sio tu ni wapole kupindukia lakini ni mahiri kwa mtizamo wa kwa nini tujali?

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget