HATIMAYE mchakato wa kupata Katiba mpya unaelekea kufikia hatua nzuri baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya uteuzi wa wajumbe 201 wa Bunge la Katiba.
Hata hivyo, wakati uteuzi huo ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu hasa kwa minajili ya kujua wateuliwa, hatua inayofuata ya Bunge lenyewe la Katiba ni ngumu zaidi.
Kabla ya kuingia kiundani, ningependa kuweka bayana msimamo wangu kuhusu Katiba mpya: japo ninatambua umuhimu wa kuwa na Katiba mpya, bado sijaona jinsi itakavyoweza kuwa na msaada kwa mwananchi wa kawaida. Kwa mkulima wa mpunga kule kwetu Ifakara, muundo wa Muungano si suala la kumnyima usingizi kulinganisha na upatikanaji wa soko la uhakika la mchele, sambamba na udhibiti dhidi ya uhuni wa vyama vya ushirika ambavyo ni mahiri kwa kukopa mazao lakini wagumu kulipa.
Lakini suala jingine ambalo linanifanya nisiguswe sana na uwezekano wa kupata Katiba mpya ni ukweli kwamba tatizo kubwa linaloikabili Tanzania yetu si kuwapo kwa sheria, bali ni utekelezaji wake. Sambamba na hilo ni kasumba inayozidi kujengeka kwamba sheria huonekana msumeno pale tu inapohusu walalahoi lakini si kwa vigogo na maswahiba zao.
Sasa, ni hili ni swali la kuamsha tafakuri tu, kama sheria zilizowekwa wazi kwenye Katiba iliyopo na zilizopita hazikuheshimiwa, kipi cha kuleta matumaini kuwa sheria zilizomo katika Katiba mpya zitazingatiwa?
Tukiweka kando mtizamo wangu huo binafsi kuhusu nafasi ya Katiba mpya katika maisha ya mwananchi wa kawaida, tuangalie hekaheka zinazotawala safari ya kuelekea kwenye upatikanaji wa Katiba hiyo mpya.
Kati ya masuala yanayotarajiwa kutawala mjadala ndani ya Bunge la Katiba ni muundo wa Muungano. Lakini kwa wanaojua kusoma alama za nyakati, tayari wana jibu kuhusu hatma ya suala hilo.
Akihutubia mkoani Mbeya katika maadhimisho ya miaka 37 ya CCM mapema mwezi huu, Rais Jakaya Kikwete aliweka wazi alichokiita msimamo wa chama tawala kuhusu muundo wa Muungano, kuwa ni serikali mbili. Japo Kikwete aliyasema hayo kama Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, ukweli unabaki kuwa pia alitoa kauli hiyo akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sasa huhitaji kuwa mjuzi sana wa siasa za nchi yetu kuelewa kuwa ni nadra kwa ‘mtizamo wa Rais’ kupingwa, na pale inapoonekana kuwa huenda Rais akaumbuka endapo msimamo wake hautofanikiwa, basi mbinu mbalimbali zitatumika kuepusha ‘fedheha’ hiyo.
Lakini suala la serikali mbili si msimamo wa Kikwete pekee bali wa CCM nzima kama alivyobainisha huko Mbeya. Na kwa kila anayeielewa CCM vizuri ataafikiana nami kuwa chama hicho kina historia ndefu ya kulazimisha matakwa yake yawe hivyo, hata kama si kwa maslahi ya Watanzania.
Tatizo kubwa la CCM ni kujipa hakimiliki ya Tanzania: licha ya jumla ya wanachama wake kuwa asilimia ndogo tu ya Watanzania wote, chama hicho kimeendelea kutenda mambo kana kwamba kila Mtanzania ni mwana-CCM.
Kana kwamba hiyo haitoshi, CCM itaingia kwenye Bunge la Katiba ikijivunia wingi wa wajumbe wake: wabunge wake Bara na Visiwani na miongoni mwa hao wajumbe walioteuliwa na Rais. Na kwa vile chama hicho tawala ni sugu wa kuweka mbele maslahi ya kiitikadi kuliko maslahi ya taifa, ni wazi kuwa uwezekano wa Bunge hilo kuridhia muundo wa Muungano wa serikali tatu ni mdogo mno.
Kwa sisi wengine, muundo wa Muungano ukibaki wa serikali mbili kama ilivyo sasa, serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Warioba au hata ukiwa wa serikali moja haitusumbui sana, alimradi nchi inaendeshwa kwa kuzingatia sheria, yenye viongozi wanaojali maslahi ya nchi badala ya maslahi yao binafsi na marafiki zao, mapambano ya dhati dhidi ya umasikini unaoigubika nchi yetu na si porojo za majukwaani, na masuala mengine muhimu kama hayo.
Kuna suala jingine ambalo kwa hakika limenishtua sana, nalo ni taarifa zilizochapishwa katika gazeti moja la kila siku kwamba posho za wajumbe wa Bunge la Katiba ni shilingi 700,000 kwa siku. Ninatambua kwamba demokrasia ina gharama zake, lakini kwa kiwango hicho ni zaidi ya gharama mahsusi ya demokrasia.
Kama ni kweli zitalipwa hizo kwa kila mjumbe, hizo ni fedha nyingi mno ambazo mlipa kodi wa Tanzania atalazimika kuzitoa. Na huyu ni mlipakodi masikini wa Kitanzania ambaye japo yawezekana ana haja ya Katiba mpya lakini umasikini unaomghubika hauruhusu kabisa matumizi ya anasa kiasi hicho.
Japo taarifa hizo za kiwango hicho kikubwa cha posho kwa wajumbe wa Bunge la Katiba hazijatolewa ufafanuzi na mamlaka husika, uzoefu unaonyesha kuwa mara nyingi posho nono kwa wajumbe ni nyenzo mwafaka ya kulainisha msimamo wowote imara wa wajumbe husika. Kwa lugha nyingine, posho nono ni mithili ya rushwa kwa minajili ya mamlaka husika kupata inachohitaji.
Licha ya tetesi zilizozagaa kwamba baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wana ajenda binafsi (kubwa zaidi ikiwa ni kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya uchaguzi mkuu hapo mwakani), ninahitimisha makala hii kwa kuwasihi wajumbe wote kuzingatia ukweli huu: maamuzi yao yatakuwa na faida au hasara kwa vizazi vingi vijavyo. Iwapo maslahi ya taifa yatawekwa mbele ya maslahi binafsi au ya kiitikadi, basi wajumbe hao watawatendea haki Watanzania kwa kuwapatia kile walichopendekeza kwa Tume ya Warioba.
Mungu Ibariki Tanzania
0 comments:
Post a Comment