TANGU Januari 7 mwaka huu, Rwanda imekuwa katika maadhimisho ya miaka 20 ya mauaji ya kimbari yaliyotokea kati ya mwaka 1994 hadi 1995, na kugharimu maisha ya takriban watu milioni moja.
Maadhimisho hayo yaliyopewa jina la Kwibuka 20 (‘kwibuka’ ni neno la Kinyarwanda lenye maana ya ‘kumbuka’) yanaambatana na kukimbiza ‘mwenge wa kumbukumbu’ ndani na nje ya nchi hiyo, sambamba na mijadala ya kimataifa katika miji mbalimbali duniani.
Kwa bahati mbaya-au pengine makusudi- wakati Wanyarwanda wakijaribu kuionyesha dunia kuwa wanasonga mbele katika umoja na mshikamano, hivi karibuni kumejitokeza propaganda za waziwazi katika baadhi ya vyombo vya habari vya nchi hiyo, ambazo mlengwa mkuu amekuwa Rais Jakaya Kikwete, na pengine, Tanzania kwa ujumla.
Na kama kuna chombo cha habari kinachoweza ‘kushikwa uchawi’ basi ni gazeti linalomilikiwa na serikali ya Rwanda la News of Rwanda. Gazeti hili limekuwa mstari wa mbele kupandikiza chuki dhidi ya Rais Kikwete na Tanzania kwa ujumla.
Kinachokera zaidi ni ukweli kwamba gazeti hilo linamilikiwa na serikali, na kinachoandikwa kinaweza kuwa msimamo wa serikali ya Rwanda.
Katika mlolongo wa propaganda zake chafu, hivi karibuni gazeti hilo lilichapisha habari zilizodai kwamba Rais Kikwete hivi karibuni alikuwa na mazungumzo na viongozi wa vikundi viwili vya waasi wanaoipinga serikali ya nchi hiyo, vya Rwanda National Congress (RNC) na The Democratic Forces for Liberation of Rwanda (FDLR).
Kichekesho ni kwamba wakati gazeti hilo likidai hivyo, Rais Kikwete alikuwa nchini Switzerland kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa uchumi dunia (World Economic Forum). Ni wazi kuwa isingewezekana kwa Kikwete kuwaalika ‘wageni hao’ ilhali yeye mwenyewe yupo nje ya nchi.
Na hata kama habari hizo zingekuwa na ukweli, kwanini basi mlengwa awe Rais Kikwete na si Serikali ya Tanzania? Jibu la wazi ni kwamba News of Rwanda linawakilisha tu chuki inayozidi kukua dhidi ya Rais Kikwete hasa baada ya kutoa ushauri kwa serikali ya Rwanda kukaa chini na waasi kujadili amani.
Sawa, pengine Wanyarwanda hawakupendezwa na ushauri huo, lakini kelele walizopiga baada ya wito huo wa Kikwete zilipaswa kuisha wakati huo na si kuliendeleza suala hilo kana kwamba Kikwete amerejea au kuendelea kutoa ushauri huo.
Ilitarajiwa kwamba wakati Rwanda inaadhimisha miaka 20 ya mauaji ya kimbari kungekuwa na tafakuri kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kujenga au kubomoa amani. Ikumbukwe kuwa miongoni mwa nyenzo zilizotumika kuchochea mauaji hayo ya kimbari ni vyombo vya habari, kwa mfano, gazeti hatari la Kangura.
Lakini ukiangalia kwa makini, kinachofanywa na News of Rwanda kwa Kikwete na pengine Tanzania kwa ujumla hakina tofauti na propaganda hatari za gazeti la Kangura. Kila mara gazeti hilo linapokuja na ‘exclusive story’ kuhusu Kikwete, msomaji hahitaji kuwa na uelewa wa tasnia ya uandishi wa habari kubaini kuwa kilichoandikwa ni porojo tu hasa kutokana na matumizi ya ‘nyenzo za kidaku’ kama vile “kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika” lakini visivyo na majina.
Kwa kiasi kikubwa Watanzania wameendelea kupuuza jitihada za makusudi zinazoendelea nchini Rwanda kuharibu uhusiano kati ya nchi hizi jirani. Pengine kupuuza huko kunatokana na silka ya Watanzania kuwa easy going lakini pia wengi wetu bado tuna kumbukumbu ya Vita ya Kagera na athari zake ambazo zimeendelea kudumu hadi sasa (kwa mfano jinsi vita hiyo ilivyoathiri uchumi wetu).
Lakini pia, Tanzania yetu inakabiliwa na changamoto mbalimbali- umasikini, rushwa, nk- na hata kama jitihada za kukabiliana na changamoto hizo hazijazaa matunda makubwa, kitu cha mwisho ambacho nchi yetu inahitaji ni kuingia kwenye mgogoro usio na tija na jirani zetu wa Rwanda.
Yayumkinika kuhisi kuwa kwa wapenda chokochoko huko Rwanda, kwa mfano News of Rwanda, ukimya na upole wetu unatafsiriwa kama aibu ya “hila zetu dhidi ya nchi hiyo kuwekwa hadharani” au hata uoga. Ukimya wa Tanzania haujasaidia hata kidogo kuwapa akili wachochezi hao kutambua kuwa amani ni muhimu kuliko chokochoko.
Hata hivyo ni muhimu kwa News of Rwanda na wote wanaoendekeza mkakati dhalimu wa kuvuruga mahusiano kati yetu na Rwanda wakatambua mchango wa Tanzania katika kuisaidia nchi hiyo wakati wa mauaji ya kimbari.
Licha ya umasikini wetu, tulijibana na kuhifadhi lundo la wakimbizi kutoka nchi hiyo. Na japo hivi karibuni Serikali ililazimika kuendesha operesheni dhidi ya wahamiaji haramu ambayo kwa kiasi fulani iliwaathiri baadhi ya Wanyarwanda, ukweli unabaki kuwa Rwanda ina deni kubwa kwa nchi yetu kutokana na wema tuliowafanyia licha ya matatizo yetu lukuki.
Naam, mikwaruzano ya hapa na pale katika nyanja za siasa na wakati mwingine kidini inaweza kutoa picha kwamba umoja wa Watanzania upo shakani. Hata hivyo, ni vema kwa yeyote anayedhani kuwa tutaendelea kukaa kimya ilhali Rais wetu anadhalilishwa bila makosa akatafakari upya. Tofauti zetu haziondoi ukweli kuwa sisi ni Watanzania tunaojivunia nchi iliyotoa mchango mkubwa kuleta amani kwa majirani zetu.
Nihitimishe makala hii kwa kukumbushia kuwa japo ni mapema kuzungumzia vita, ni vema kwa kila anayeichokonoa nchi yetu akarejea ufanisi na uhodari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Majuzi tu, mashujaa wetu hao wameonyesha uimara na utaalamu mkubwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambako jeshi letu lilikuwa sehemu ya jeshi la kimataifa la kurejesha amani nchini humo.
Vilevile, ningependa kutoa rai kwa Rais Paul Kagame na serikali ya Rwanda kwa ujumla kukemea vikali propaganda chafu zinazoongozwa na News of Rwanda kumdhalilisha Rais wetu Kikwete sambamba na kuchochea uhasama kati ya nchi hizi mbili.
Ili ‘Kwibuka 20’ izidi kuwa na maana kusudiwa basi ni muhimu pia kuhamasisha amani hata nje ya mipaka ya Rwanda, ikiwa ni pamoja na kukemea jitihada zozote za kuathiri mahusiano kati ya nchi hiyo na Tanzania yetu.
“When we are unified, working together, no challenge is insurmountable” (Tukiwa na umoja, tukishirikiana, hakuna changamoto ya kutushinda) ~Paul Kagame
- See more at: http://raiamwema.co.tz/chokochoko-hizi-na-zilaaniwe#sthash.URpf2wgf.dpuf
0 comments:
Post a Comment