KABLA ya kuanza kuandika makala hii nilikutana na habari moja mtandaoni iliyonifanya nijiulize iwapo Rais Jakaya Kikwete anapata muda wa kuangalia kalenda kufahamu muda uliobaki kabla hajamaliza muhula wake wa pili na wa mwisho wa Urais.
Habari hiyo ilihusu hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa mjini Dodoma kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ambapo aliwataka wanachama wa chama hicho kuacha unyonge na kusema uvumilivu una kikomo chake.
“Tunashindana na wenzetu wagomvi, maana wao ugomvi ndiyo sehemu ya mwongozo wa kufanya kazi ya siasa...Tulizungumza nalo hilo kwenye Kamati Kuu, tulikubaliana kuacha unyonge. Ndiyo, kwenye Kamati Kuu tumekubaliana, tumesema jamani watu wote waende wakaseme tumekubaliana kuacha unyonge,” alinukuliwa Kikwete ambaye licha ya kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.
Kwa kifupi, Rais Kikwete ametoa ruhusa kwa wana-CCM kukabiliana na alichokiita tabia ya ugomvi ya vyama vya upinzani. Kwamba wana-CCM wachukue sheria mkononi pindi wakihisi wanafanyiwa ugomvi na wapinzani. Kwa lugha nyingine, jukumu la ulinzi na usalama katika shughuli zinazokihusu chama hicho zimeporwa kutoka vyombo vya dola na kukabidhiwa kwa wanachama wa chama hicho tawala.
Kwa tafsiri pana, iwapo wana-CCM ‘wataacha unyonge’ na kufanya mashambulizi ya kujihami dhidi ya wapinzani (yaani hata kama wapinzani hawajafanya ‘ugomvi’ wowote) bado watakuwa na ‘haki’ kutokana na ruhusa hiyo waliyopewa na Rais Kikwete.
Kadhalika, vyombo vya dola vitakuwa na wakati mgumu kuchukua hatua dhidi ya wana-CCM watakaowashambulia wapinzani kwa sababu amri ya kufanya mashambulizi hayo ina baraka za Rais ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu.
Hivi kweli Rais Kikwete hatambui kuwa amebakiwa na takriban miezi 20 tu kabla ya kuwa ‘raia wa kawaida tu’ ambaye anaweza kuwa miongoni mwa wahanga wa ruhusa hiyo ya vurugu aliyowapa wana-CCM wenzake?
Na hata kama angekuwa amebakiwa na miaka mingine mitano katika Urais, haihitaji busara kutambua kuwa ni rahisi kuruhusu uvunjifu wa sheria kuliko kuzuwia. Ni rahisi kwa Rais Kikwete ‘kuwapa rungu’ wana-CCM kupambana na wapinzani lakini ni vigumu mno kuwazuwia kutotumia ruhusa hiyo.
Binafsi ninadhani kinachomsumbua Rais Kikwete ni ‘kofia mbili za uongozi katika Taifa,’ yaani Urais na Uenyekiti wa Taifa wa CCM. Na suala hili la ‘unyonge wa wana-CCM’ si pekee linaloonyesha jinsi ‘kofia mbili’ zinavyomtesa Rais Kikwete.
Angalia suala la Katiba Mpya: anapozungumza nje ya hadhara za ki-CCM, Rais anaonekana kuwa na dhamira ya dhati kuona Katiba mpya inapatikana kulingana na matakwa ya Watanzania wote.
Lakini ukisikiliza hotuba zake mbele ya wana-CCM wenzake, inakuwa mwendelezo uleule wa kuweka mbele itikadi za kisiasa hata pale inapohitaji kutanguliza maslahi ya Taifa.
Kimsingi ‘kofia mbili’ hazipaswi kuwa tatizo iwapo kasumba ya kuweka mbele siasa katika kila jambo itaepukwa. Rais anaweza kabisa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria pasipo hofu ya kuathiri nafasi yake kama Mwenyekiti wa Taifa wa chama anachoongoza.
Na kwa kumrahisishia kazi, CCM inafahamika kwa ‘mshikamano’ wake, na ni dhahiri kuwa Rais ana nafasi kubwa ya kuungwa mkono na chama chake katika uongozi wake, na wakati huohuo Rais imara anatengeneza mazingira ya uenyekiti imara ndani ya CCM hivyo kuondoa uwezekano wa upinzani ndani ya chama.
Sitaki kabisa kudhani kuwa baada ya ruhusa hiyo kwa wana-CCM wenzake kuacha unyonge, Rais Kikwete atahamia kwa Watanzania na kuwaruhusu kuacha unyonge dhidi ya mafisadi, wafanyabiashara ya madawa ya kulevya na majangili.
Lakini hata asipotoa ruhusa ya aina hiyo, uamuzi wake wa kuwakabidhi wana-CCM majukumu ya vyombo vya dola unaweza kuvuka mipaka ya kisiasa (yaani CCM dhidi ya wapinzani) na kuchukua sura ya kitaifa, kwani wahanga wa ufisadi, madawa ya kulevya, ujangili, nk ni Watanzania wote pamoja na hao wana-CCM.
Ruhusa hiyo ya Rais Kikwete kwa wana-CCM kuacha unyonge na kukabiliana na wapinzani si tu ni fyongo lakini pia imekuja wakati mbaya. Macho na masikio ya Watanzania wote yameelekezwa Dodoma kufuatilia Bunge la Katiba ambalo limeanza kukiwa na matarajio Katiba mpya itaimarisha umoja na upendo miongoni mwa Watanzania.
Na kwa upande mwingine, kauli hiyo ya Rais Kikwete inaturejesha kwenye suala nililozungumzia katika makala yangu ya wiki iliyopita nikieleza kuwa tatizo kubwa la Katiba tuliyonayo na zilizotangulia huko nyuma ni utekelezaji wake.
Ni wazi kuwa Rais Kikwete anafahamu kwamba wenye jukumu la kukabiliana na ‘wagomvi’ wa CCM si wana-CCM bali vyombo vya dola. Huo ndio utawala wa sheria kwa mujibu wa Katiba. Inapotokea matamshi yetu yakaonyesha kuwa kuna ruhusa kwa wananchi kupora wajibu wa vyombo vya dola katika kulinda amani na usalama, tutarajie nini kutoka kwa mwananchi wa kawaida?
Kutarajia kwamba Rais Kikwete atabadili kauli yake ya ‘ruhusa kwa wana-CCM kuacha unyonge dhidi ya tabia ya ugomvi wa wapinzani wa chama hicho’ ni sawa na kutarajia ujangili utakwisha kwa vile Rais amedai serikali inawafahamu vigogo 40 wanaoendesha biashara hiyo haramu. Labda kinachoweza kutokea ni ‘kucheza na maneno’ na kuwalaumu waandishi wa habari kuwa “walinukuu vibaya.”
Nimalizie makala hii kwa kumkumbusha Rais Kikwete kuwa bado ana nafasi nzuri ya kujitengenezea mazingira mazuri ya ‘kustaafu kwa amani’ pindi atapomaliza muhula wake wa Urais mwakani.
Kuruhusu wana-CCM wachukue sheria mkononi dhidi ya ugomvi kutoka kwa vyama vya upinzani ni kuruhusu uvunjifu wa sheria.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/amri-hii-yaweza-kumfuata-kikwete-uraiani#sthash.9f8lBlwU.dpuf
0 comments:
Post a Comment