Friday, 10 April 2009

NAOMBA USOME HABARI IFUATAYO KISHA TUSHIRIKIANE KUFANYA TAFAKURI KATIKA MASWALI YANAYOJITOKEZA (katika maneno yenye rangi nyekundu).
Na Salim Said

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa imekikataa kwa mara ya pili kitabu cha hesabu za mapato na matumizi ya Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha baada ya kubaini mapungufu, ikiwa ni pamoja na udanganyifu.

Kamati hiyo pia imewapa adhabu ya kukatwa asilimia 15 ya mishahara ya watendaji sita wa halmashauri hiyo kwa kosa la kuidanganya kamati hiyo ilipowatembelea Januari mwaka huu.

Kamati hiyo ilianza kupitia taarifa za mapato na matumizi ya serikali za mitaa kuanzia Jumatatu wiki hii na imeshapitia hesabu za halmashauri za mkoa wa Dodoma na jana ilipitia halmashauri za mkoa wa Arusha.

Awali kabla ya kukataliwa kwa kitabu hicho, mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Cyprian Oyier alionekana kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kwa wabunge kuhusu makosa waliyofanya na mapungufu yaliyojitokeza katika kitabu chao.

Oyier alikiri mbele ya wajumbe wa kamati hiyo na wageni waalikwa kuwa waliidanganya kamati ilipoenda kuwatembelea wilayani kwao kwa kuwaeleza kuwa halmashauri ilijenga nyumba ya walimu kwa Sh30 milioni, jambo ambalo halikuwa la kweli.

Nyumba hiyo iliyogharimu zaidi ya Sh 30 milioni ilibainika kuwa imejengwa na Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa) na wao kukabidhiwa funguo tu baada ya wajumbe kufanya ziara shuleni hapo.

Baada ya kukitaa kitabu hicho, wakuu wa halmashauri hiyo na waandishi, walitakiwa kutoka nje kwa muda, ili kuwapa nafasi wabunge kupanga adhabu. Baada ya dakika 20, kaimu mwenyekiti wa kamati hiyo, Samuel Chitalilo alisema kuidanganya kamati ni kosa la jinai, lakini kamati imewaonea huruma.

Alisema wangeweza kuwataka kurudi tena mbele ya kamati, lakini wanawasamehe kwa kuwakata asilimia 15 mishahara yao ya mwezi wa tano mwaka huu. “Tunawarudisha mkaandae tena kitabu chenu... hiki tunakikataa kwa mara ya pili. Angalieni wenzenu wa Same walivyoandaa vizuri ili mkija tena tusije kukikataa tena,” alisema Chitalilo na kuongeza:

Mmeidanganya kamati na mmekiri kosa, hili ni kosa la jinai, lakini kamati imewaonea huruma kwa kuwapa adhabu ya kujifunza na ili iwe fundisho kwa wengine”.

“Mkurugenzi wa halmashauri, mhandisi, ofisa mipango, mkaguzi wa ndani, mweka hazina na ofisa elimu aliyekuwapo wakati huo tutawakata asilimia 15 ya mishahara yenu ya Mei.”

Naye mbunge wa Kinondoni na mjumbe wa kamati hiyo, Idd Azzan alisema halmashauri hiyo ilitoa taarifa za uongo kwa kamati na kwamba walipokwenda kuitembelea shule hiyo walipewa taarifa tofauti kutoka kwa mkuu wa shule hiyo.

Alifafanua kwamba wanatoa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa halmashauri zinazotoa taarifa za uongo. “Adhabu hii tunataka iwe fundisho kwa wengine, kwa kuwa fedha za serikali hazitumiki ipasavyo katika ngazi za halmashauri, zinatumika kwa safari na posho za viongozi jambo ambalo ni kinyume na malengo ya fedha hizo,” alisema Azzan.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo alikataa kuzungumza na Mwananchi baada ya kupewa adhabu hiyo, huku mwenyekiti wa halmashauri hiyo, David Pelo akisema kuwa hiyo ni bahati mbaya na hakuna aliyekusudia kutoa taarifa za uongo.

“Tutajitahidi kufuata maelekezo yenu, tunawashukuru kwa kutoturudisha tena katika kamati kwa kuwa fedha za halmashauri zingetumika pia kwa usafiri,” alisema Pelo.

Haya ni ya kawaida na yanaweza kutokea kwa halmashauri yoyote, pia tutarudia kuandika kitabu kama tulivyoelekezwa na tutaenda kwa wenzetu wa Same kwa kuwa wao wamefanya vizuri.”

Kamati mbalimbali za bunge zinaendelea na vikao vyake kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam kuanzia Jumatatu wiki hii.

CHANZO: Mwananchi

TAFAKURI:

KITABU CHA MAHESABU KILIPOKUTWA NA MAKOSA MARA YA KWANZA,WAHESHIMIWA WABUNGE WAKAAMUA KUKITAA ILI KIFANYIWE MAREKEBISHO.KILIPOLETWA MARA YA PILI,WAHUSIKA WAKAAMUA LIWALO NA LIWE,WAKAKIRI KUWA WALIDANGANYA.HIVI TUJIULIZE,WAHESHIMIWA WABUNGE WALIPOTAKA MAREKEBISHO HAWAKUWA WANAKARIBISHA USANII KUTOKA KWA WATENDAJI HAO WA HALMASHAURI?HAIHITAJI ELIMU YOYOTE KUTAMBUA KWAMBA MAHESABU YA TAASISI YA UMMA YANAPOKUWA NA KASORO INAASHIRIA UFISADI WA NAMNA FLANI,HIVYO KUWATAKA WAHUSIKA WAREKEBISHE NI MITHILI YA KUWAPA MUDA WA KUFUNIKA UFISADI HUO.

JAPO NAAFIKIANA NA MANTIKI YA KUWAADHIBU WATENDAJI WASIOTEKELEZA MAJUKUMU YAO IPASAVYO,NAPATWA NA WASIWASI NA NAMNA KAMATI HIYO YA BUNGE ILIVYOJIPA MAJUKUMU YA MAHAKAMA NA KUAMUA KUKATA ASILIMIA 15 YA MISHAHARA YA WATENDAJI HUSIKA.HUU NI UKIUKWAJI WA UTAWALA WA SHERIA KWA VILE KAMA ILIBAINIKA KUWAPO KWA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA UMAA,MAHALA MWAFAKA PA KUSHUGULIKIA SUALA HILO NI POLISI NA MAHAKAMA.

NA JINGINE LA KUJIULIZA NI NAMNA MAKATO HAYO YATAVYOWEZA KUFIDIA FEDHA ZILIZOIBIWA NA USIMAMIZI WA KUHAKIKISHA KUWA MAKATO HAYO HAYAISHII MFUKONI MWA MAFISADI WENGINE.

MHESHIMIWA CHITALILO (rejea HAPA na HAPA) ANATAMKA BAYANA KWAMBA WATENDAJI HAO WAMETENDA KOSA LA JINAI,LAKINI CHA KUSHANGAZA ANADAI ETI KAMATI IMEWASAMEHE NA BADALA YAKE KUWAAMURU WAKWATWE ASILIMIA HIZO 15 ZA MISHAHARA YAO.HIVI INGEKUWA NI FEDHA ZAKE BINAFSI NDIO ZIMEIBIWA ANGEWEZA KUTOA MAAMUZI YA KUSTAAJABISHA NAMNA HIYO?

HIVI KWA UTARATIBU HUU WA KULEA UZEMBE,UBADHIRIFU,UJAMBAZI NA UFISADI KUNA UWEZEKANO WOWOTE WA KUFIKIA MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA?

TUTAFAKARI!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget