Thursday, 2 April 2009



Gazeti la Mwananchi linaandika:


MKURUGENZI wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea jana alikuwa kwenye wakati mgumu baada ya wabunge kumhoji uhalali wake wa kuiongoza taasisi hiyo wakati akikabiliwa na tuhuma za kusafisha kashfa ya zabuni ya mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura.

Mkurugenzi huyo, ambaye alitajwa kwenye taarifa ya tume teule ya bunge iliyochunguza kashfa hiyo na serikali kutakiwa kumchukulia hatua, alikumbwa na mtafaruku huo katika semina ya Miundombinu ya Uadilifu iliyoandaliwa na Takukuru na Chama cha Wabunge wa Afrika (APNAC) na kufanyika kwenye hoteli ya Whitesands jijini Dar es salaam.

Ilifikia wakati Dk Hosea alionekana kukerwa sana na maswali kiasi cha kulazimika kuwaonya kuwa anao uwezo wa kuwachafua kama wakiendelea kufanya mambo yanayoonekana kumvua nguo.

Mbunge wa Busega, Raphael Chegeni ndiye aliyeanzisha kizaazaa hicho baada ya kumhoji Dk Hosea akisema ilikuwaje taasisi yake iliisafisha kampuni tata ya kuzalisha umeme wa dharura Richmond Development (LLC) iliyokuwa inakabiliwa na kashfa ya kushinda zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura wakati kamati teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mkataba wake, iligundua kuwepo kwa mazingira ya rushwa.

“Inakuwaje wakati wa mjadala wa Richmond, wewe mkururugenzi wa Takukuru ulikanusha kuwapo rushwa na uchunguzi wa kamati ya bunge ulibaini kuwepo rushwa ndani ya kampuni hiyo? Je ni nani mwenye dhamana ya kukuadhibu wewe na taasisi yako kuhusu rushwa’’ aliuliza Chageni.

Swali hilo halikutegemewa na Dk Hosea na lilionekana kumuudhi na kulazimika kuchukua kipaza sauti na kusitisha maswali na kuanza kujibu kwa ghadhabu.

“Hapa siyo jukwaani hivyo tusilete siasa. Nipo hapa kwa ajili ya kufundisha na kama ni suala la Richmond waziri mkuu alishaliongelea na ndiyo mwenye dhamana ya kujibu hilo. Mimi sina jibu kwa hilo na kama mtu hapendi kuvuliwa nguo kwanini umvue mwenzako,” alisema Dk Hosea.

"Mjadala huu aachiwe Waziri Mkuu Mizengo Pinda na aliyeuliza swali hilo hanitendei haki kwani hakuna hoja nyingine ya maendeleo kwa jamii ambalo inaweza kujadiliwa... mbona mnang’ang’ania kujibu hilo pekee.

“Najua kuna watu wanatumiwa ili niongee halafu nibabaike katika kujibu nanishindwe kufanya kazi yangu. Mbona mnang’ang’ania jambo hilo tu wakati kuna hoja nyingine za maendeleo kwa jamii. Kuhusu suala la Richmond sijibu ng’o.”.



Nalo Tanzania Daima linaripoti:


MKURUGENZI wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Edward Hosea, jana aliwashambulia wabunge katika semina ya kukabiliana na rushwa iliyoandaliwa na taasisi yake na kuwashirikisha wabunge wa Chama cha Kupambana na Rushwa (APNAC).

Akitoa mada katika semina hiyo, Dk. Hosea aliwashambulia wabunge hao hadharani, kwamba wamekuwa wakichangamkia posho za semina wakati hakuna uwajibikaji.

Katika mada hiyo iliyoonekana dhahiri kuwakera wabunge hao, Dk. Hosea alisema baadhi yao wamekuwa wakihudhuria na kusaini posho zaidi ya tatu katika semina tofauti kwa siku moja, huku wakishindwa kuwajibika, jambo ambalo alisema ni aina mojawapo ya rushwa.

“Wapo wabunge wanaohudhuria semina zaidi ya tatu kwa siku moja na kusaini posho, lakini hata baada ya kuwezeshwa kwa posho hizo, hakuna uwajibikaji. Kwa kweli kuna mambo mengi yanayotokea, lakini tunayafumbia macho,” alisema Dk. Hosea.

Mbali na kusaini posho kwenye semina tatu kwa siku, Dk. Hosea pia alisema wapo wabunge ambao wanatumia vibaya ubunge wao kwa kutokaa kwenye foleni wawapo sehemu za huduma kama benki.

Pia aliwapasha wabunge kuwa hivi sasa siri nyeti za serikali ziko wazi, na kwamba inatokana na ukosefu wa maadili miongoni mwao.

Hata hivyo, baada ya kumaliza kutoa mada hiyo, baadhi ya wabunge walionekana dhahiri kukerwa na mada hiyo na kutaka kujibu mapigo kwa kuhoji utendaji wa taasisi hiyo na mafanikio yake tangu ilipoanzishwa.

Mbunge wa kwanza kutoa dukuduku lake, alikuwa Dk, Raphael Chegeni (Busega-CCM) ambaye alihoji utendaji wa TAKUKURU na kueleza kutoridhishwa kwake.

Dk. Chegeni alianza kujibu mapigo kwa kuhoji uwajibikaji wa Dk. Hosea na taasisi yake kuwa, iliwahi kuchunguza kashfa ya zabuni ya kampuni ya kufua umeme wa dharura, Richmond, na kuitangazia jamii kwamba hakukuwa na rushwa katika zabuni hiyo.

Kama hiyo haitoshi, Dk. Chegeni alisema TAKUKURU pia ilishindwa kuchunguza kashfa ya minara pacha ya majengo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na badala yake Kampuni ya nje ya Ernest & Young ilibua ufisadi mkubwa na hatimaye leo baadhi ya watuhumiwa wamefikishwa mahakamani.

Huku akishangiliwa na baadhi ya wabunge, Dk. Chegeni alihoji ujenzi wa gharama wa ofisi za TAKUKURU nchini pamoja na magari ya kifahari wanayotumia wakati haiwajibiki ipasavyo katika kukabiliana na rushwa.

“TAKUKURU mnawajibika nini? Mlisema kwenye Richmond hakuna rushwa, lakini baadaye Bunge lilibaini kuwapo kwa rushwa, kwenye ujenzi wa minara pacha ya BoT mmeshindwa kuchunguza hadi kampuni ya nje ndiyo iliyokuja kuibua kashfa hiyo,” alisema Dk. Chegeni.

Kutokana na hoja hiyo, Dk. Hosea alikuja juu na kuwataka wabunge hao kuacha kuhoji mambo hayo, kwani wakianza kuchambuana, hakuna atakayebaki salama.

“Hapa hatukuja kulumbana, tumekuja kwenye semina, si mahala pake, lakini nyie wabunge ndio mlioamua kupitia Kamati Teule ya Bunge na mapendekezo yenu yapo, kwa hiyo iulizeni serikali, lakini hatuko hapa kushambuliana,” alisema Dk. Hosea.

Hata hivyo, baada ya malumbano hayo makali, wabunge na maofisa wa TAKUKURU, waliendelea na semina yao inayofanyika katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, inayotarajia kumalizika leo.



Wakati huo huo viongozi wawili wakuu wa Chadema,

Freeman Mbowe na Dr Wilbroad Slaa wametoa matamshi mazito kuhusiana na ishu ya Dowans.Gazeti la Mwananchi linaripoti




KATIBU mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kumtetea mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Dk Idris Rashid kinamtia wasiwasi na kuhoji uhalali wa kufunga mjadala wa Dowans.

Dk Slaa alikuwa mmoja wa watu waliohojiwa na Mwananchi kuhusu maoni yao juu ya hotuba ya kila mwezi ya Rais Kikwete aliyotoa juzi kuzungumzia mambo mbalimbali, likiwemo suala la mpango uliokwama wa serikali kununua mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura ya kampuni ya Dowans Tanzania Limited.

Ingawa Dk Rashid alionekana kushutumu wabunge waliopinga kutekelezwa kwa azma hiyo wakati akitangaza uamuzi wa Tanesco kuachana na mpango wa kununua mtambo huo, Rais Kikwete aliipongeza Tanesco kwa uamuzi huo huku akionekana kutaka malumbano juu ya suala hilo yaishe.

Lakini Dk Slaa anaona kauli hizo zinalenga kumlinda Dk Rashid, gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

"Tuna mashaka naye Kikwete kwa kauli yake ya kumtetea Dk Idris ambaye pia sisi tuna mashaka naye kuwa alihusika katikasakata la ununuzi wa rada," alisema Dk Slaa.

"Kikwete hawezi kueleweka kwa kumtetea mtu aliyedaiwa kuhusika na kampuni ya nchini Uingereza, akidai inatuhumiwa kupokea fedha kupitia akaunti inayodaiwa kuwa ya mwanasheria wa zamani."

Dk Slaa alisema hofu yake inakuwa kubwa zaidi kutokana na kile alichodai kuwa wakati sakata la Tanesco na ununuzi wa mitambo ya Dowans likipamba moto, Kikwete alikwenda nje ya nchi na aliporejea alitoa kauli kumtetea mkurugenzi huyo.

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliishauri serikali isinunue mitambo hiyo ya Dowans kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma, ambayo inazuia kununuliwa kwa vitu vilivyotumika.

Hata hivyo, Tanesco na serikali hawakuridhika na ushauri huo wa Bunge na badala yake wakazunguka na kuliwasilisha suala hilo kwenye Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, ambayo ilishindwa kutoa maamuzi hasa baada ya bunge kueleza kuwa maoni ya kamati ya awali ndio msimamo wa chombo hicho cha kutunga sheria.

Kukwama kwa mpango huo kulimfanya Dk Rashid kuitisha kikao na waandishi na kulaumu wabunge, akidai kuwa waligeuza suala hilo kuwa la kisiasa na kudai asilaumiwe iwapo nchi itaingia gizani.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ambaye aliunga mkono mpango wa serikali kununua mitambo hiyo akitaka watu waangalie kwa umakini tatizo lililo mbele, hakuwa na maoni yoyote alipotafutwa na Mwananchi.

"Sina maoni yoyote," alisema Zitto ambaye mkoa wake wa Kigoma uko kwenye matatizo makubwa ya umeme na ambao Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliahidi bungeni kuwa utakuwa umefungiwa mtambo wa megawati 6 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Naye kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Hamad Rashid alisema tatizo la umeme nchini limetokana na serikali kushindwa kufanyia kazi maeneo 15 ambayo iliyaainisha ili kukabiliana nalo na ndiyo inayostahili kubeba mzigo wa lawama.

Alisema serikali inapaswa kulaumiwa kwa tatizo la umeme kwa kuwa imeshindwa kufanyia kazi suala hilo tangu mwaka 2006 na kwamba iwapo maeneo hayo yangefanyiwa kazi, kero ya umeme ingemalizika na wala mjadala kuhusu mitambo ya Dowans usingekuwepo.

“2005/2006 tulikumbwa na tatizo kubwa la ukame na kusababisha mgao mkubwa wa umeme. Katika juhudi za kutafuta njia mbadala, serikali iliainisha maeneo 15 ya kuyafanyia kazi ili kuondoa tatizo hilo,” alisema Rashid.

Alisema moja ya maeneo hayo ni ununuzi wa mitambo ya kufua umeme wa dharura, ambalo ndilo lililosababisha mjadala mkubwa wa kitaifa kutokana na Tanesco kutaka kununua mitambo ya Dowans, ambayo ilirithishwa mkataba wa kampuni ya Richmond Development (LLC) iliyoshinda katika mazingira ya utata zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura.

“Maeneo hayo yapo katika hansard (vitabu maalum vya kuhifadhia kumbukumbu za bunge) na nitayatoa kwa waandishi katika mkutano wangu nao kesho au keshokutwa," alisema Rashid.

Alisema anaunga mkono hotuba ya Kikwete kwa kuwa alichozungumza ndicho alichotaka kukieleza kwa wananchi akiongeza kwamba mkutano wake na waandishi hautakuwa tena wa kutoa msimamo wa kambi ya upinzani kama alivyodhamiria awali bali kuikumbusha serikali kuyafanyia kazi maeneo hayo.

Hata hivyo alisema hotuba hiyo ya Kikwete inathibitisha kuwa serikali iliridhia uamuzi wa bunge juu ya mjadala wa ununuzi
wa mitambo ya kampuni ya Dowans.

Alisema bunge lilitoa maamuzi yake kuishauri Tanesco isinunue mitambo hiyo kutokana na utata uliopo kati ya uhusiano wa Dowans na kampuni ya Richmond na kwamba iwapo haikuridhia ingerudi bungeni na kuliomba bunge libadilishe maamuzi yake.

“Hotuba ya rais ni ushahidi kuwa serikali imeridhia maamuzi halali ya bunge na ndio maana rais akamaliza mjadala wa Dowans na kuwapongeza Tanesco kwa kuachana na nia ya kununua mitambo hiyo,” alisema Rashid.

Lakini Dk Slaa hakukubaliana na kauli ya Rais Kikwete kutaka malumbano kuhusu ununuzi wa mitambo ya Dowans yaachwe.

"Ametumia udikteta kufunga mjadala," alisema Dk Slaa ambaye ni mwanasheria. "Wananchi hawakumpa mamlaka hayo ya kuwazuia kujadili rasilimali zao na nchi yao.

"Siku zote nasema Kikwete asituamulie... wananchi wanazungumza juu ya rasilimali na nchi yao, wanasiasa ni wadau katika maslahi ya nchi, asituamulie juu ya rasilimali zetu.

"Hakupewa mamlaka ya kutuamlia nini cha kujadili. Hatuwezi kukubali... kwa sababu gani analazimisha kufunga mjadala? Lazima kuna kitu."


Nalo Tanzania Daima linaandika:


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kutofunga mjadala wa suala la mitambo ya kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura, Dowans, bila kuwaeleza wananchi ukweli kuhusu wamiliki wake na mahala walipo.

Mbowe aliyasema hayo jana katika mahojiano maalum na Tanzania Daima, akitoa maoni yake kuhusu baadhi ya masuala aliyoyazungumza Rais Kikwete juzi usiku, wakati akilihutubia taifa kwa njia ya
redio na televisheni.

Alisema hatua ya Rais Kikwete kutangaza kufunga mjadala wa Dowans ni ya kuungwa mkono kwa kuwa mjadala huo si jibu la matatizo ya umeme nchini, lakini alimtaka kwanza awaeleze Watanzania ukweli wote kuhusu Kampuni ya Dowans, ndipo aufunge mjadala huo vizuri.

“Tunakubaliana na ushauri wake wa kutaka mjadala wa Dowans uishe. Tunakubaliana naye kwa sababu Dowans si jibu la matatizo ya msingi ya sekta ya nishati nchini. Hata hivyo, Kikwete asikimbilie kufunga mjadala bila kuwaeleza wananchi, Dowans ni nani. Watoe tamko, waueleze umma wa Watanzania, wamiliki wa Dowans ni nani, wako wapi, wanafanya nini, wataje watu wote wanaonufaika na Dowans, kisha ndipo atufungie mjadala huo vizuri. Kikwete anataka kuficha ukweli,” alisema Mbowe.

Akizungumzia tatizo la uhaba wa umeme nchini, alisema si mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kuahidi kumaliza tatizo la umeme, kwani wakati wa sakata la kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond, alishaahidi kuwa tatizo la umeme lingekuwa historia.

“Si mara ya kwanza rais kuahidi kwamba nchi haitakuwa gizani. Ameshaahidi hivyo wakati wa vuta nikuvute ya Richmond, ameshasema hivyo karibu mara tatu. Alishasema kwamba matatizo ya umeme yatakuwa historia, lakini hadi leo nchi haina umeme wa uhakika. Rais anaendelea kutoa maneno matamu, hatuwezi kupata umeme kwa maneno yake….”

“Asitazame tu uchaguzi wa 2010, na kuwapa watu maneno matamu, atazame mbele. Tunahitaji mkakati wa muda mrefu na mfupi. Na si mkakati tu, tunahitaji mpango wa utekelezaji, maana sera ya nishati imeainisha yote hayo, lakini tatizo utekelezaji. Serikali inapaswa kuwa na uhakika wa kulipatia taifa umeme hata kwa miaka zaidi ya 50 ijayo,” alisema Mbowe.

Alisema kwa kiasi kikubwa sekta ya umeme nchini inaathiriwa na wafanyabiashara wakubwa ambao ni maswahiba wa Rais Kikwete na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaoigeuza sekta hiyo kuwa chanzo chao cha mapato, kwa kuanzisha kampuni za kufua umeme wa dharura na kuiuzia TANESCO kwa gharama kubwa.

Alisisitiza kuwa, msingi wa tatizo la nishati ya umeme nchini ni kutokuwapo kwa sera endelevu na mikakati yakinifu na inayotekelezeka, ya muda mrefu na mfupi, ya kuzalisha na kusambaza umeme.

Alisema pamoja na uhaba wa umeme unaozalishwa, bado sehemu kubwa ya umeme huo imekuwa ikiibwa na kusababisha wananchi wengi kukosa haki ya kupata umeme.

“Na tatizo hapa si uhaba wa umeme unaozalishwa tu. Bado kuna umeme mwingi sana unaibwa, lakini serikali halizungumzii hili,” alisema Mbowe.

Alisema tatizo jingine ni umeme unaozalishwa kuwa wa gharama kubwa kiasi cha wananchi wengi kushindwa kuupata na kuutumia.

“Tuna network (mtandao) kubwa sana ya umeme. Maeneo mengi nyaya za umeme zinapita jirani na nyumba za watu, lakini wenye uwezo wa kuunganisha umeme huo kwenye nyumba zao ni wachache sana. Gharama za kufunga umeme majumbani ni kubwa mno kwa Mtanzania maskini kumudu. Gharama za kuutumia, kulipa ankara pia ni kubwa.

“Kwa hiyo Rais Kikwete na serikali yake, wasiishie tu kuzungumzia uzalishaji, lakini pia lazima waeleze ni jinsi gani watapunguza gharama za umeme ili Watanzania maskini nao waweze kuutumia,” alisema Mbowe.

Akizungumzia tahadhari ya Rais Kikwete, kwamba kwenye baadhi ya mikoa kuna uwezekano wa kutokea tatizo la chakula kwa sababu ya kuchelewa kwa mvua za masika, Mbowe alisema ni aibu na fedheha kubwa kwa nchi yenye maji mengi yanayotiririka kama Tanzania, kutangaza njaa ndani ya msimu mmoja wa matatizo ya mvua.

“Sikio la kufa halisikii dawa. Tatizo la chakula ni tatizo la kujitakia. Kukosa mvua msimu mmoja, halafu rais anatangaza njaa, ni jambo la kutia aibu sana. Tuna maji mengi sana yanatiririka, tuna mito na maziwa, ardhi yenye rutuba nzuri sana. Tuna kila kitu, tatizo ni ukosefu wa sera nzuri na uongozi bora,” alisema Mbowe.

Alisema Rais Kikwete anapaswa kumfukuza mara moja Waziri wake wa Kilimo na Chakula kwa kushindwa kusimamia programu za kilimo cha uwagiliaji nchini.

“Walipoingia madarakani walikutana na tatizo la chakula. Kikwete na Lowassa waligawa chakula na kuahidi kwamba njaa ile isingetokea tena, sasa leo wanatuambia nini? Wamefanya nini? Na hii ndiyo kawaida yake, anaahidi halafu anasahau. Nchi hii ikipata viongozi wazuri serikalini, kilimo cha umwagiliaji kinaweza kabisa kumaliza tatizo la njaa za mara kwa mara,” alisema Mbowe.

Alisema serikali inapaswa kuwa na mpango wa makusudi wa muda mrefu wa kuzalisha na kuhifadhi chakula kwa wingi, ili kiwe kinaingia katika mtandao wa matumizi ya wananchi, pindi kunapokuwa na uhaba wa chakula.

Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi uliopita, Rais Kikwete pamoja na mambo mengine, alitaka mjadala wa kununua au kutonunua mitambo ya Dowans, ufungwe baada ya wahusika (TANESCO), kutangaza kuachana na uamuzi wa kutaka kuinunua.

Alisema anashangazwa na malumbano ya baadhi ya viongozi wa siasa kuhusu jambo hilo.

Mjadala wa Dowans, hivi karibuni uliwaingiza katika malumbano makali, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, wote wa CCM





PENGINE DR HOSEA ANA HAKI YA KUWA MKALI KWANI YEYE HAKUJITEUA KATIKA WADHIFA HUO BALI ALITEULIWA...NA PIA KWA VILE KWA MUJIBU WA "UTAMADUNI WETU" KUJIUZULU NI MITHILI YA KUMKOSEA ADABU ALIYEKUTEUA BASI HUENDA KUMSAKAMA DR HOSEA NI KUMWONEA KWANI YAELEKEA ALIYEMTEAU KARIDHIKA NAE.AMA KWA HAKIKA TANZANIA BILA UFISADI INAWEZEKANA!!!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget