Pamoja na kuwa moja ya nchi maskini kabisa duniani, Tanzania yetu bado inaendelea kusifika kwa mambo kadhaa. Ukiachia mbali vivutio vya asili kama Mlima Kilimanjaro, utitiri wa wanyama huko Selous, Mikumi na kwingineko, na “utajiri” wa madini kama Tanzanite,dhahabu, almasi na madini mengineyo,nchi yetu pia inasifika kwa watu wenye uwezo wa kuongea.
Ndio maana jirani zetu wanapenda kututania kuwa “nyie Watanzania iko maneno mingi” wakimaanisha tunaongea sana. Na pengine mahala mwafaka pa kuthibitisha uwezo wetu wa kuongea ni katika vikao vya bunge letu tukufu. Laiti yote yanayoongewa katika vikao hivyo yangekuwa yanatafsiriwa kwa vitendo, basi kwa hakika tungekuwa mbali sana.
Lakini licha ya sifa hiyo ya kuongea sana, Watanzania tuna sifa nyingine ya usikivu na kuamini kirahisi kila tusikiacho hata kama ni “wizi mtupu”. Ndio maana basi watu wenye akili na busara zao walidanganyika kwamba miongoni mwa wabunge wa CCM kuna kundi la WAPIGANAJI DHIDI YA UFISADI.Kundi hilo lililojipatia umaarufu usiostahili linadaiwa kuwa chini ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta.
Na kwa katika kile kinachoweza kutafsiriwa kwamba ni jitihada za kujiongezea sifa za “upambanaji” , Spika Sitta na wabunge wawili kutoka vyama vya upinzani,Dr Wilbroad Slaa (Chadema) na John Cheyo (UDP) walichapisha kitabu walichokipa jina “BUNGE LENYE MENO”. Si lengo la makala haya kurejea yaliyomo katika kitabu hicho, lakini kwa kifupi ni mwendelezo wa sifa tulizonazo Watanzania: maneno meeeengi lakini vitendo SIFURI.
Sijui Sitta wa “wapiganaji” wenzie walikuwa na mawazo gani kurefusha mjadala wa ujambazi wa Richmond kwa takriban miaka miwili lakini tukashuhudia wakilamba matapishi yao walipounga mkono kile kinachoitwa “utekelezaji wa serikali wa maazimio ya bunge kuhusu suala la Richmond”.Kwanini hawakuiunga mono serikali tangu siku ya kwanza badala ya kuwazuga Watanzania kwa muda wote huu?
Binafsi siamini kabisa kuwa Spika Sitta ni mpambanaji dhidi ya ufisadi.Ni usanii tu ambao unaelekea kuwa moja ya sifa muhimu za wanasiasa wetu.Sitta atakuwaje kamanda wa vita dhidi ya ufisadi ilhali ndiye aliyemfungia Zitto Kabwe alipohoji ufisadi wa Buzwagi?Je sio Sitta huyohuyo aliyetishia kumpeleka Dr Slaa kwenye vyombo vya sheria pale (Slaa) alipoibua ufisadi wa EPA?
Spika Sitta,akisaidiwa na vyombo vyetu vya habari vinavyosifika kwa umahiri wa kukariri kikasuku kila kinachosemwa na wanasiasa (badala ya kwenda mbali zaidi na kuchambua kauli hizo), alitambua vema kuwa Watanzania wengi wanahitaji wanasiasa watakaoungana nao kupambana na ufisadi.Kwa lugha nyingine,alifahamu fika kuwa mapambano dhidi ya ufisadi ni mtaji maridhawa kisiasa na ungeweza kuimarisha nafasi yake.
Na kwa vile anafahamu kuwa Watanzania ni wasikivu sana hata kama wanadanganywa,akawa anapita huku na kule akijigamba kwamba “kamwe hatatishwa na wanaomwandama kisiasa kutokana na msimamo wake thabiti wa kupiga vita ufisadi”. Sitta, na wasanii wenzake waliotuhadaa kuwa ni “wapiganaji dhidi ya ufisadi” walibinafsisha ajenda ya vita dhidi ya ufisadi kiasi kwamba “kila aliyeonyesha dalili ya kutamani MAJIMBO YAO alionekana anasukumwa na umahiri ya akina Sitta katika kupambana na ufisadi”.Yaani hawakubinafisha tu hoja ya ufisadi bali wamegeuza majimbo yao kuwa mali zao za urithi ambazo hazipaswi kuguswa na Mtanzani mwengine yeyote yule.
Na Sitta anadai atawania tena kiti cha Uspika katika bunge lijalo.Kuna dalili kuwa anaweza kurejea bungeni kwa vile ametumia vema nafasi yake ya uspika kujiimariusha jimboni kwake Urambo.Lakini kama bunge lijalo litakuwa na wabunge wanaowajali wapiga kura wao basi ni dhahiri Sitta atabaki kuwa historia tu.Hatastahili hata unaibu Spika,pamoja na naibu wake wa sasa Anne Makinda,viumbe wawili waliotumia vibaya sana madaraka yao na kuendesha taasisi hiyo kwa utashi wao huku wakitumia kanuni zilizopitwa na wakati kuwaokoa mawaziri wazembe walioshindwa kutoa majibu sahihi kwenye mijadala bungeni.
“Wapiganaji feki wa ufisadi” wametuchezea shere.Upande mmoja wao ni sehemu ya mfumo wa kifisadi unaoshamiri kwa kulindana,na hawana jeuri ya kujitenga nao kwa vile ni wabinafsi.Lakini kwa upande mwingine wanataka tuwaone wao ni wenzetu,wanaguswa na matatizo yetu na wana uchungu wa dhati na nchi yetu.Wasanii hawa wanatuona sie wajinga tusiojua kuwa mishahara yao minono ni ushahidi tosha kuwa wanaishi dunia nyingine kulinganisha na walimu,madaktari,manesi,wakulima na walalahoi wengine.Wanarefusha vikao vya bunge ili posho zao nonoi ziendelee kutunisha akaunti zao.
Spika Sitta na wasanii wengine waliotudanganya kuwa wao ni wapiganaji dhidi ya ufisadi hawana sababu hata moja ya kuwaacha majambazi wa Richmond wakisafishwa na pasipo kuchukuliwa hatua yoyote.Kuna baadhi yetu tulikuwa tukifahamu tangu mwanzo kuwa hakutakuwa na hatua yoyote dhidi ya Lowassa,Karamagi,Msabaha,Mwanyika ,Hoseah na wengineo waliohishwa na ufisadi huo.Tulifahamu hivyo kwa vile kimsingi,ufisadi huo-kama ilivyo kwenye ishu za EPA,Kiwira,na kwingineko-ni matokeo ya ushirika wa kijambazi uliobuniwa na kufanikishwa kwenye korido za utawala za CCM.Kuwachukulia hatua watuhumiwa hawa kungeweza kabisa kupelekea vigogo wengine kuadhiriwa hadharani.
Hiyo haimaanishi kuwa kuadhirishwa kwa vigogo hao ni kosa,bali ni muhimu kwetu kuelewa kuwa mtandao huu wa kifisadi uliundwa kwa madhumuni ambayo mpaka sasa bado yana umuhimu kwa wahusika.Kwa lugha nyepesi.mfumo wa kifisadi ni matokeo ya moja kwa moja ya kundi la WANAMTANDAO.Na kama walivyoshirikiana kuingizana madarakani,wanaendelea kulindana ili Mtandao huu uendelee kututawala.
Na Watanzania tuna sifa nyingine ya ziada:UPOLE. Ungetarajia kusikia wananchi wakiandamana kupinga majambazi wa Richmond “kuachiwa huru na Bunge” huku wakihakikishiwa kuwa “kuna siku watarejea madarakani”. Yaani tumetapeliwa,tukachezewa akili kwa zaidi ya miaka miwili na sasa tunashuhudia majambazi wakisafishwa bungeni lakini hakuna tumetulia kana kwamba Katiba inatuelekeza tufanye hivyo!Ama kweli hiyo ndio amani na utulivu-sio kwako na kwangu bali AMANI KWA WANAOTAFUNA NCHI YETU NA UTULIVU KWA AKAUNTI ZAO ZILIZESHEHENI MAMILIONI YA FEDHA ZA KIFISADI.
Habari njema kwa mafisadi ni dalili kuwa wengi wao watarejea tena madarakani baada ya uchaguzi mkuu hapo Oktoba.Na habari njema zaidi kwao,ni kuwepo kwa kila ishara kuwa chama kinacholea ufisadi,CCM,kitaunda serikali ya awamu ya tano huku kikilindwa na idadi kubwa ya wabunge.Japo baadhi yetu tungependa kuona mabadiliko lakini ni muhimu kwetu kuwa wakweli kwa nafsi zetu.Hakuna dalili ya CCM kushindwa uchaguzi mkuu ujao kwa vile mazingira yaliyopo yanakwaza mabadiliko ya aina yoyote ile.
Hata hivyo,kama wewe Mtanzania umechoshwa na ufisadi,kulindana,ahadi hewa na ubabaishaji mwingine,una nafasi ya pekee ya kutimiza hasira zako kwa kuinyima kura CCM.Vinginevyo,hali sio tu itaendelea kuwa mbaya bali tunaweza kufika mahala watu wakalazimisha mabadiliko yatakayopelekea kutuathiri sote.Ni muhimu kwako mpiga kura kujisuta kwa makosa uliyofanya 2005 na huko nyuma,lakini kufanya kosa si kosa bali kurejea kosa.Ni mwaka huu au ndio tumeumia milele.Timiza wajibu wako.
0 comments:
Post a Comment