Hivi karibuni Tume ya Uchaguzi ilieleza kwamba inaangalia uwezekano wa kuongeza idadi ya majimbo ya uchaguzi.Niende moja kwa moja kwenye hoja yangu: ni rahisi kwa Tume hiyo kuwa na wazo kama hilo kwa vile halina athari zozote kwenye mishahara au posho zao.Kinyume chake,tunaambiwa zoezi la tathmini linatarajiwa kugharimu mabilioni ya shilingi.Unadhani zinakwenda wapi hizo kama si kwa haohao wanaokuja na wazo la kuongeza majimbo?
Mzazi mwenye busara hawezi katu kufikiri kuongeza idadi ya watoto wakati hao alionao sasa "wanampelekesha" linapokuja suala la kumudu gharama za matundo/malezi.Ni katika mantiki hiyohiyo,Tume ya Uchaguzi,ilipaswa kutambua kuwa uwezo wetu kiuchumi hauwezi kumudu majimbo zaidi ya hayo tuliyonayo sasa.
Lakini jingine lililo muhimu zaidi ni kuangalia ufanisi wa wawakilishi tulionao sasa.Naamini wengi tutaafikiana kwamba idadi kubwa ya wabunge hadi sasa haijasaidia kumkomboa Mtanzania kutka kwenye lindi la umasikini wa kutupwa.Tunashuhudia jinsi Bunge na Serikali wanavyotunishiana misuli kuhusu mazingaombwe ya Richmond,Kiwira,nk.Je kuongeza idadi ya wabunge kutaongeza "misuli zaidi" kwa Bunge.Jibu la haraka ni HAPANA.
Wengi wa wabunge wetu ni wabinafsi wanaoangalia maslahi yao binafsi.Umuhimu wa wapiga kura wao na majimbo wanayowakilisha unakuja pale tu kunapojiri uchaguzi.Wabunge,hususan wa CCM,wameweka mbele maslahi ya Chama kuliko wananchi wanaowawakilisha.Hilo lisingekuwa tatizo kama CCM ingekuwa chama kinachowajali wananchi badala ya mafisadi.
Na kwanini wazo la majimbo mapya lije mwaka huu tunapotarajia uchaguzi mkuu?Kwanini sio mwaka jana,juzi au 2007?Jibu jepesi ni kwamba wazo la majimbo mapya halina uhusiano na kukuza demokrasia au kuongeza uwakilishi bali ni kuwatafutia ulaji vigogo wanaonyemelea ubunge au wale ambao ubunge wao uko hatarini kutokana na upinzani kwa wanaotaka nafasi hiyo.
Nihitimishe kwa kueleza kuwa kuongeza idadi ya majimbo si moja ya vipaumbele vyetu kwa sasa.Pengine badala ya wazo hilo la kuwatengenezea watu ulaji,Tume ingetafakari ni namna gani wapiga kura watawezeshwa kuwabana wawakilishi wasiotekeleza wajibu wao majimboni.Tume pia inapaswa kuelewa kwamba wabunge watakaoongezwa pindi wazo la majimbo mapya likikamilika watapaswa kuongoza watu "hai",na ili "uhai" wa watu hao uwe na uhakika wa kuwepo ni muhimu kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa kurekebisha hali ya uchumi wetu,sambamba na kuwabana mchwa (mafisadi) wanaotafuna kila kidogo tulichonacho.
0 comments:
Post a Comment