Sunday, 13 March 2011


TIBA inayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa KKKT (Babu), Ambilikile Mwasapile katika kijiji cha Samunge, Loliondo, imeendelea kuonyesha maajabu yake baada ya wagonjwa kadhaa wa hospitali mbili kubwa nchini kukutana na madaktari wao kwenye foleni, kila mmmoja akitafuta uponyaji.
.

Wakati hayo yakiendelea, Mbunge wa Kilindi mkoani Tanga, Bi. Beatrice Shellukindo ametoa ushuhuda tiba hiyo ya Babu si jambo la mzaha bali inaponya, yeye amenufaika nayo, pamoja na ndugu zake 18 alioongozana nao.

Wakizungumza na majira kwa nyakati tofauti siku chache baada ya kurudi walikokwenda kufuatilia tiba hiyo, baadhi ya wanachi walithibitisha wagonjwa hao kupigana vikumbo na madaktari wao kwenye foleni kila mtu akijaribu kutatua tatizo lake.

“Sisi tulikwenda baada ya kushauriwa na daktari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambaye anamtibu ndugu yangu. alitwambiwa moja kwa moja ya kwamba tumpeleke mgonjwa wetu kwa Babu,” alisema Timothy Ndalichako, mkazi wa Njoro, mjini Moshi.

Alisema siku chache baada ya kupewa ushauri huo ambao ulitiwa chumvi na kuenea kwa taarifa za huduma ya Babu, walitafuta taratibu za kumpeleka ndugu mgonjwa huyo Loliondo na kufanikiwa kuipata baada ya siku mbili kwa kuwa wakati huo msongamano ulikuwa haujawa mkubwa.

“Tukiwa kwenye foleni siku ya pili, ndipo tukamuona daktari aliyetushauri akiwa ameandamana na wenzake kwenye gari, nao wakiwa wanaingia eneo la tiba Loliondo,” alisema.

Aidha alisema alichogunduwa ni kwamba madaktari wengine kutoka hospitali hiyo maarufu hapa nchini na nje ya nchi pamoja na wale wa hospitali nyingine za mjini Moshi, walishafika na wengine walikuwa wakiendelea kufika eneo hilo kufuatia tiba hiyo mbadala.

Kwa upande wake, Bw. Manase Kiara, alidai kukutana na daktari bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, aliyekwenda Loliondo kufuatia tiba hiyo.

“Niliondoka na wenzangu baada ya kujipanga kwenda kupata tiba baada ya kuhangaikia kwa muda mrefu Muhimbili. Kufika huko mimi na wenzangu tulikutana na dokta wetu ambaye baada ya kusalimiana naye tu alituambia mpeni Mungu yaliyo yake Mungu na ya Kaisari mpeni Kaisari,” alisema.

Wakati huo huo baadhi ya wananchi wa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro wameipongeza serikali kwa tamko lake kuwa haijazuia huduma ya tiba inayotolewa Mchungaji Mwasapile kwa miezi kadhaa sasa.

Shellukindo atoa ushuhuda wa tiba

Mbunge wa Jimbo la Kilindi mkoani Tanga, Bi. Beatrice Shelukindo amesema akiwa na ndugu zake 18 wakiwa na matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwemo yeye mwenyewe kusumbuliwa na magonjwa mbalimbali kwa muda mrefu, wamefika kwa Babu na kupata tiba.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu akiwa Arusha jana baada ya safari iliyomchukua wiki nzima, Bi. Beatrice alisema sio jambo la mzaha, dawa ya Babu inaponya.

Bi. Shelukindo alisema walifika katika Kijiji cha Samunge wilayani Ngorongoro Machi 7, mwaka huu, lakini kutokana na wingi wa wagonjwa walipata tiba Machi 11 yeye na ndugu zake, na baada ya hapo kila mtu akajisikia amepona, wakiwemo waliokuwa wanasumbuliwa na saratani.

"Mimi mwenyewe nilikuwa nasumbuliwa na presha na vidonda vya tumbo kwa muda mrefu, lakini baada ya kunywa kikombe kile cha dawa nilipona, tangu Ijumaa sijagusa kabisa kidonge cha aina yeyote, iwe kwa ajili ya vidonda vya tumbo au presha.

"Lakini maajabu yapo kwa mtoto wangu wa kike, akiwa na miaka 37 tulimpeleka hajiwezi na hajaweza kula wala kusema kwa miezi sita, zaidi ya kunywa uji tu kwa vile alikuwa anasumbuliwa na kansa, lakini baada ya kutoka hapo, kwanza tulishangaa baada ya kutaka tumpe chakula.

"Na kutokana na shida ya safari, wakati wa kurudi tulimuandalia ndege ya kurudi Dar es Salaam alikataa na jana Jumamosi (Machi) amerudi kwa basi. Mwingine ni mama mdogo alikuwa anasumbuliwa na presha mbaya, lakini ghafla amepona," alisema Bi. Shelukindo.

Bi. Shelukindo alisema pia alikwenda na ndugu yake mwanaume, yeye alikuwa anaumwa macho kiasi ambacho moja lilipasuka, lakini alipofika kwa Babu na kunywa dawa amepona, na ndugu zake wote aliokwenda nao wanaendelea vizuri.

"Yusuph (mwandishi) nakusihi sana uende kwa yule mchungaji. Sio vitu vya kubuni, dawa yake inaponya. Hakika ndugu zangu wote wamepona. Ni kweli imani pia ni muhimu katika kutumia dawa hiyo, lakini yenyewe bado inaponya, na inaanza kufanya kazi siku moja mpaka saba tangu unywe dawa hiyo," alimaliza kwa kutoa ushuhuda huo Bi. Shelukindo.


Mazingira yaanza kuwekwa sawa

Hofu ya usalama ilikuwa imetanda kwenye Kijiji cha Samunge imeanza kuondoka baada ya serikali wilayani Ngorongoro
imesema kuanza uboresha wa miundombinu, usafi wa mazingira na kuweka utaratibu mzuri wa wagonjwa kupata tiba.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Elias Wawa Lali alisema jana kuwa
siku chache tu zijazo wananchi watapata tiba hiyo kwa muda mfupi na katika mazingira safi na salama kwa kuwa tayari wameanza jitihada za kukamilisha mpango huo kwa kushirikiana na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati.

Kwa mujibu wa DC huyo kanisa hilo limesema kuwa watahakikisha wananchi hawapati tena taabu walizokuwa wakizipata siku kadhaa zilizopita za kukaa siku zaidi ya tano bila tiba huku wakitishiwa na hatari ya kimazingira kwa afya zao.

“Kila mmoja anazungumza habari ya Loliondo hata yule ambaye hana taarifa sahihi za huko, lakini uhakika ni kwamba tayari mipango yetu inakwenda vizuri tunachozubiri na
wataalamu hao wa ujenzi kutuletea tathimini nzima ya kinachohitajika huko,” alisisitiza DC.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Askofu Thomas Laiser alisema kanisa hilo katika kuhakikisha azma yao inatimia linatarajia kutumia zaidi ya sh milioni 75
katika kuboresha mazingira ya tiba hiyo.

Fedha hizo ni kwa ajili ya kujenga majengo maalumu yenye uwezo wa kuhudumia watu zaidi ya 600 kwa wakati moja, huku kukiwa na huduma bora za matundu ya vyoo na maji safi na salama ya kutosha.

Aliongeza wachoraji na wasanifu wa majengo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi hiyo, Bw. Ezrael Kariyongi hivi sasa wapo kijijini Samunge wakifanya tathimini ya mradi huo.

Alisema kuwa hata hivyo bajeti hiyo itategemea taarifa ya mchanganuo wa ujenzi huo ambapo utekelezaji wake utafanyika ndani ya wiki mbili zijazo ambapo mchungaji huyo ataendelea na tiba hiyo.

Imeandaliwa na Yusuph Mussa, Korogwe; na Heckton Chuwa,
Moshi; na Said Njuki, Arusha

CHANZO: Majira

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget