Uskochi
NIANZE makala hii kwa kutoa pongezi za dhati kwa mmoja wa watoto wa Rais Jakaya Kikwete, Miraj, kwa kauli yake kuhusu vurugu zilizotokea hivi karibuni katika baadhi ya maeneo nchini.
Gazeti moja huko nyumbani lilinukuu kauli ya Miraj kwenye ukurasa wake wa mtandao wa jamii wa Facebook akisema kwamba ni makosa kukihusisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na vurugu hizo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, mtoto huyo wa Rais alieleza kwamba CHADEMA si nchi bali ni chama cha siasa na si wanachama wa chama hicho pekee wenye shida na matatizo bali ni Watanzania wote.
Nimelazimika kutoa pongezi hizi kwa sababu kwa kiasi kikubwa siasa za vyama vingi zimezua mazingira ya uadui na uhasama kwa misingi ya kiitikadi. Na katika hili, chama tawala CCM ambacho wengi wetu tunakiangalia kama kiongozi kwenye ulingo wa siasa, si tu kwa vile kimekuwa madarakani kwa muda mrefu bali pia ndicho kilichoridhia mageuzi ya kisiasa nchini, kimekuwa kinara wa siasa za chuki.
Miraji si mwanasiasa, lakini si tu ni mtoto wa Rais ambaye ametokana na CCM bali pia baba yake ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho tawala. Na japo Kikwete mwenyewe si mahiri sana kwenye siasa za uhasama kati ya CCM na vyama vya upinzani, ukimya wake pindi baadhi ya viongozi wenzie wanaofanya kila jitihada kujenga picha kuwa vyama vya upinzani havina tofauti na wahaini unaweza kuashiria kuwa naye ni muumini wa siasa za aina hiyo.
Mtoto huyo wa Rais alinukuliwa akitukumbusha kuwa, “Tofauti ni harakati na sera... tupendane Watanzania, tutafika mbali kwa umoja na mshikamano wetu na wala si kwa kejeli na matusi…, wenye haki tuwasimamie wote na penye haki tusimame sote.” Sote tunatambua kuwa tofauti zetu za kiitikadi haziongezi au kupunguza Utanzania wetu.
Japo habari hiyo haikuvuma sana lakini uzito wake unaweza kuwa na umuhimu mkubwa kwa mustakabali wa taifa letu. Wiki iliyopita tumeshuhudia jinsi baadhi ya mawaziri na wabunge wa CCM, wakiongozwa na Spika Anne Makinda, wakiwakebehi wabunge wa CHADEMA na NCCR-Mageuzi kama vile uamuzi wao wa kutoka nje ya Bunge kupinga uendeshaji wa mjadala wa mabadiliko ya Katika ni uhayawani.
Hivi kuna ugumu gani kuendesha mijadala muhimu kwa taifa kwa kutumia hoja za kiutu-uzima na mantiki badala ya vijembe na kebehi ambazo hazisaidii lolote? Hivi kama mtoto wa Rais ambaye ni kijana wa umri wa kati tu anaweza kuwa na busara za kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya unazi wa kisiasa, inakuwaje vigumu kwa wanasiasa watu wazima ambao baadhi yao wamekuwa kwenye fani hiyo miaka nenda miaka rudi?
Baada ya pongezi hizo na mafunzo kwa wanasiasa wanaoendekeza siasa za uhasama, nigeukie kwa ufupi kuhusu mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Sitajadili kwa undani sana kwa sababu ubabe uliofanywa na CCM kuilazimisha hoja ambayo kimsingi haikuwa yao, umeikoroga akili yangu kiasi kwamba siwezi kujadili suala hili kwa ufasaha.
Lakini kwa kifupi tu, ninapenda kuwakumbusha CCM kwamba wanaweza kutumia ubabe kulazimisha matakwa yao pasipo kujali athari za ubabe huo kwa umma lakini kwa hakika ipo siku watajutia kufanya hivyo.
Kimsingi, moja ya mambo yanayolalamikiwa sana na wapinzani, wanaharakati na baadhi ya wananchi kuhusu muswada huo ni madaraka makubwa ya Rais. Nashukuru angalau, suala la Rais kupewa madaraka ya kuandaa hadidu za rejea limeondolewa kutoka mikononi mwake, katika mjadala uliopitishwa na Bunge wiki iliyopita.
Kuna mambo makubwa mawili yanayowasukuma CCM kutaka mwendelezo wa Katiba mithili ya hii inayolalamikiwa. Kwanza, Katiba hiyo imekisaidia sana chama hicho kushinda chaguzi mbalimbali na hivyo kuendelea kuwa madarakani. Chama hicho tawala kinafahamu kuwa Katiba inayokidhi mahitaji ya demokrasia ya kweli ni sawa na kitanzi kwake.
Lakini la pili ni ukweli kwamba kwa wana-CCM wengi wazo kwamba kuna siku chama hicho kinaweza kung’olewa madarakani na kuwa chama cha upinzani ni ndoto ambayo kamwe haitotimia. Maana laiti wangeamini kuwa hilo linawezekana basi wangekuwa makini kubariki muswada wenye mwelekeo wa kuzaa Katiba inayompa Rais madaraka makubwa kupita kiasi. Wangefanya hivyo kwa kuelewa kuwa laiti wakiingia kuwa chama cha upinzani, madaraka hayo yanaweza kabisa kutumika kuwakandamiza.
Na mjadala huo wa muswada wa mabadiliko ya Katiba unatoa picha ya changamoto kubwa zinazovikabili vyama vya upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao hapo mwaka 2015. Tulichojifunza katika sokomoko hilo ni kwamba chama tawala kipo tayari kufanya lolote lile kuhakikisha kinaendelea kuwa madarakani.
Japo sijapata fursa mwafaka ya mwendelezo wa makala zangu kuhusu changamoto mbalimbali kwa vyama vya upinzani katika uchaguzi huo, kilicho wazi ni ukweli kuwa kikwazo kikubwa cha demokrasia ya kweli nchini ni CCM - chama ambacho kinapenda kutuaminisha kuwa kiliridhia mageuzi ya kisiasa pasi na hofu wala kinyongo.
Vyama vya upinzani vinaweza kabisa kufanikiwa kuuza sera zao vizuri na vikafanikiwa pia kuwashawishi Watanzania watoe ridhaa kwao kuirithi CCM. Lakini kwa mwenendo huu wa siasa za kibabe ambao unarutubishwa na wingi wa wabunge wa CCM bungeni itakuwa vigumu sana kwa vyama hivyo kufanikiwa.
Na hapa tunazungumzia utaratibu wa kisiasa ambao kila mwenye macho anaouna na mwenye masikio anausikia (nikimaanisha kuwa jitihada za CCM kukwaza upatikanaji wa Katiba “safi” zimeshuhudiwa bayana). Sasa kama chama hicho tawala kinaweza kufanya mambo haya hadharani hali ikoje kwa mambo yasiyoonekana hadharani?
Kama ambavyo nimekuwa nikibainisha mara kadhaa, tatizo si CCM kuendelea kuwa madarakani. Laiti chama hicho kingeendelea kuwa cha wakulima na wafanyakazi (na si cha kulea mafisadi wanaofanya alama za jembe na nyundo zionekane kama kijiko na bunduki-kuashiria ulaji na ufisadi), basi tungekesha tukiomba kiendelee kututawala milele.
Lakini kwa vile ni wazi kuwa CCM si tu kimeshindwa kukidhi matarajio ya Watanzania bali pia kimeishiwa mbinu bora zaidi za uongozi wa taifa, kuna kila sababu ya kutoa fursa kwa wengine kutuongoza na kutukomboa kutoka katika lindi la umasikini linaloigubika nchi yetu.
Ukisoma ripoti ya Bunge kuhusu sakata linalomhusu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Davidi Jairo (na swahiba wake Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, sambamba na Waziri na Naibu wake, William Ngeleja na Adam Malima, pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utoh) unawezakujiuliza tena; “kama ufisadi mmoja uliowekwa hadharani uko hivi, mambo yakoje kwingineko ambako yanayoendelea huko hayajawekwa hadharani?”
Ni matukio ya ufisadi kama huo yanayowatia wasiwasi CCM kuwapa Watanzania Katiba inavyoweza kabisa kukiweka chama kingine madarakani. Wanafahamu kuwa laiti wakiondolewa kwenye utawala kwa njia halali za kidemokrasia, madudu mengine chungo mbovu ambayo yayumkinika kuamini kuwa yanaendelea hadi muda huu, yatawekwa hadharani.
Si kama nimekata tamaa lakini kuna kila dalili kwamba kutarajia kwamba CCM watajenga mazingira ambayo yanaweza kuwa chanzo chama hicho kung’oka madarakani ni ndoto ya mchana. Kila mpenda demokrasia angetamani kuona tunakuwa na chaguzi huru na haki lakini hilo ni vigumu kutokea kwa mwenendo huu.
Wakati naandaa makala hii, CCM walikuwa wanakutana huko Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine wanatarajiwa “kukaliana kooni” kuhusu suala la “kuvuana magamba.” Japo pengine si njia mwafaka, lakini misukosuko inayokikabili chama hicho inaweza kuwa ndio njia pekee inavyoweza kukisambaratisha na hatimaye kutoa fursa isiyotarajiwa kwa wazalendo wengine kuongoza taifa letu.
Sikiombei mabaya chama hicho tawala lakini kama njia za kistaarabu za kutaka mazingira mwafaka ya kidemokrasia yanayoruhusu mabadiliko zinakwamishwa na chama hicho hicho basi sioni ubaya kutamani mpasuko mkubwa utakaofanya kiishiwe pumzi ya kubaki madarakani au kuhujumu chaguzi zijazo.
ipo siku ccm inajutia. ingekua ni chama chenye akiri ingejiuliza kwanini tz tu ndo imebakiza chama cha uhuru mpaka sasa. ingejifunza yanayotokea kwingineko duniani. lakini kwa vile inafaindi ujinga na kulala kwa wa tz inadhani itakaa milele.
ReplyDelete