Mishahara mipya kwa wabunge ni ujambazi
Uskochi
AWALI, nilitaraji wiki hii ningeendelea na uchambuzi wangu kuhusu changamoto mbalimbali zinazovikabili vyama vyetu vya siasa nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2015. Lakini wakati najiandaa kuingia kwenye mada hiyo nikakutana na habari ambayo siyo tu ilinitia hasira bali pia ilinichefua.
Habari yenyewe inahusiana kwa namna fulani na mada niliyozungumzia wiki iliyopita katika safu hii, yaani suala la unafiki. Wakati unafiki niliouchambua ulihusu sakata la ushoga (kufuatia tamko la Waziri Mkuu wa Uingereza kwamba nchi yake inafikiria kuzikatia misaada nchi zinazominya haki za mashoga), unafiki ninaouzungumiza leo unahusu baadhi ya wabunge wetu.
Wiki iliyopita, vyombo mbalimbali vya habari huko nyumbani viliripoti kwamba baadhi ya wabunge wetu wamekumbushia “kilio chao cha siku nyingi” wakidai posho na mishahara yao viongezwe. Naomba nitamke mapema kuwa huu ni ujambazi wa mchana kweupe (daylight robbery).
Ninatambua kuwa waheshimiwa wetu wamezoea kusifiwa tu hata pale wanapoongea masuala yasiyo na msingi na sitashangaa iwapo hitimisho langu kwamba madai yao ya kuongezewa posho na mishahara ni ujambazi, likaibua malalamiko makali kutoka kwao.
Lakini kwa vile Tanzania haiwezi kuendelea kufanywa shamba la bibi la walafi wachache (ambao zama za Mwalimu Nyerere tuliwaita kupe wanaoishi kwa kutegemea jasho la wengine) ni lazima tuwakemee watu hawa pasipo uoga wala aibu.
Ili kuelewa kwa nini nimeandika kuwa wanachofanya wabunge wanaodai nyongeza ya posho na mishahara ni unafiki wa hali ya juu (na kuufananisha na ujambazi) ni muhimu kusikia hoja zao za ovyo ovyo zinazojaribu kuhalalisha wanachodai.
Mbunge wa Rombo kupitia CHADEMA, Joseph Selasini, alinukuliwa na gazeti moja akidai kuwa eti “uwakilishi umekuwa mzigo kwani wakati mwingine amekuwa akitumia fedha anazopata kwenye vyanzo vyake binafsi kuwatumikia wananchi.”
Gazeti hilo liliendelea kumnukuu mbunge huyo akisema kwamba “Hapa nina mialiko 26 ya kwenda kuchangia ujenzi wa shule na shughuli nyingine za maendeleo kule Rombo, zote hizi zinanihitaji kama mbunge nitoe fedha, sasa jamani fedha hizi zinatoka wapi?”
Swali analopaswa kuulizwa Selasini na wabunge wenzie wenye mawazo kama yake ni hili: “kama uwakilishi ni mzigo, nani alimshikia mtutu wa bunduki kwamba lazima agombee uwakilishi huo? Na kama wakati anagombea ubunge hakufahamu kuwa kutumikia umma ni jukumu linalohitaji kujitoa muhanga kwa nini basi asitue mzigo huo?
Haihitaji japo kozi ya saa chache ya jinsi ya kutumia busara zetu ipasavyo kutambua kuwa kama umewania nafasi fulani na kuipata lakini hatimaye unagundua kuwa nafasi hiyo ni mithili ya mzigo mzito wa gunia la misumari, kinachopaswa kufanywa siyo kudai (tena kwa ubabe badala ya unyenyekevu) usaidiwe bali kuacha nafasi hiyo kwa wenye uwezo wa kuimudu.
Kwa hiyo kama Selasini anaona jukumu la uwakilishi linamfilisi basi kuna shughuli nyingi tu za kufanya ambazo hazitamfanya alalamikie “mshahara na posho kidogo.” Anaweza kabisa kuachana na ubunge na akabaki na jukumu dogo la kuhudumia familia yake pasipo kutaka kuwabebesha walipakodi wa Kitanzania mzigo mkubwa zaidi ya wanaoubeba sasa kuhudumia maisha ya kitajiri ya wabunge wetu.
Lakini katika kuonesha kuwa tuna tatizo kubwa na baadhi ya watu tuliowakabidhi dhamana ya kutuwakilisha, Selasini ananukuliwa na gazeti hilo akikiri kwamba “...wabunge hukutana na kero ya wananchi kuomba fedha ili wakatatue matatizo yao mbalimbali na kwamba ni vigumu kukwepa jukumu hilo kutokana na hali ya maisha ilivyo sasa nchini.”
Ahaa, kumbe wakati anaomba kuongezewa posho na mshahara anafahamu fika kuwa wanyonge anaotaka wakamuliwe zaidi ili posho na mishahara ya wabunge iongezwe si tu wana matatizo mbalimbali bali pia wanakabiliwa na hali ngumu kutokana na hali ya maisha ilivyo sasa nchini.
Sijui tatizo la wabunge kama Selasini ni kuishi katika sayari nyingine ambayo wenye haki ya maisha ya anasa ni wao tu au ni ulafi tu wa kutaka kila kidogo tulichonacho kikusanywe na kukabidhiwa wao wenye mahitaji muhimu kuliko wanyonge “wanaopigika” tangu mawio hadi machweo.
Naye Mbunge wa Mtera kwa tiketi ya CCM, Livingstone Lusinde alinukuliwa akiitaka Ofisi ya Spika, Anne Makinda, kufanya jitihada za kuwaelimisha wananchi kuhusu wajibu wa mbunge ili wafahamu kazi nyingine wanazofanya wawakilishi hao wa wananchi ni nyongeza nje ya majukumu yao ya msingi.
Lusinde alidai kwamba “Malipo yetu ni kidogo sana, hayatoshelezi kabisa lakini wananchi tunaowawakilisha hawatuelewi katika hili, maana wanadhani tuna fedha nyingi, sasa hapa kuna tatizo. Nadhani kuwapo utaratibu wa kuwaelimisha, wajue hata kazi nyingine tunazofanya siyo wajibu wetu ila tunajitolea na nyingine hizi zina gharama kubwa.”
Huu ni zaidi ya unafiki. Ni matusi kwa Watanzania masikini. Hivi Lusinde anafahamu pato la Mtanzania wa kawaida ni kiasi gani? Hivi kigogo huyu ana taarifa zozote kuhusu kuporomoka kwa kasi thamani ya shilingi yetu? Na anaposema hayo mamilioni wanayolipiwa ni kidogo anataka kutuambia kiasi gani ndio stahili kwa mbunge wa nchi yetu masikini kabisa duniani?
Ni hivi, Lusinde sio kwamba wananchi mnaowawakilisha hawawaelewi kwa nini mnadai marupurupu zaidi ya hayo makubwa kabisa mnayopata sasa. Wasichowaelewa ni mnaishi sayari gani? Hivi mnapolalamika kuwa mamilioni mnayolipwa hayawatoshi, watumishi wengine wa umma kama vile walimu, madaktari na wengine waseme nini?
Tatizo la waheshimiwa hawa wakishapata kura wanageuka viumbe tofauti kabisa na wale waliokuwa wakijifanya wana uchungu kweli na wapiga kura wao. Wanasahau kuwa wengi wa wananchi waliowapigia kura waheshimiwa hao kuingia bungeni ni masikini wa kutupwa na hawana wa kumlalamikia (na hata wakilalamika ni kazi bure maana wawakilishi wao nao wapo ‘bize’ kulalamikia mishahara na posho).
Labda msomaji mpendwa unaweza kuwa unajiuliza ninapoandika waheshimiwa hawa wanapata mishahara ya mamilioni ninazungumzia kiasi gani hasa. Kwa hesabu za haraka haraka, mshahara wa mbunge ni Sh milioni 2.3 kwa mwezi na pamoja na posho kiwango cha juu anachopokea kwa mwezi kinafikia takriban shilingi milioni saba.
Hivi mtu anayelipwa shilingi milioni saba kwa mwezi lakini bado “analilalia” kuwa fedha hizo hazitoshi tumwite jina gani? Binafsi nimehitimisha hapo awali kuwa huu ni ujambazi wa mchana kweupe kwa sababu wanachofanya wabunge wanaodai maslahi zaidi ya hayo lukuki wanayopewa ni matusi kwa mamilioni ya Watanzania ambao, wastani wa pato la kila mmoja wao kwa mwaka ni dola za Marekani 500 (takriban shilingi 870,000). Kwa maana hiyo, kwa wastani, pato la Mtanzania kwa mwezi ni shilingi 70,000.
Sasa kuna uhalali gani kwa wabunge kutoridhika na mshahara ambao ni takriban mara 100 ya “mshahara” wa Mtanzania wa kawaida (yaani pato la wastani kwa mwezi)? Ninafahamu kuwa waheshimiwa wabunge hawatopenda kusikia nikihitmisha kuwa neno pekee mwafaka la kuelezea hali hii ni ujambazi lakini huo ndio ukweli wenyewe.
Kwa lipi hasa wanalofanya huko bungeni hadi wadai kuwa malipo mara 100 zaidi ya Mtanzania wa kawaida hayawatoshi? Kama ubunge umekuwa mzigo basi waachie ngazi. Kuna haja gani ya kuwa na watu zaidi ya 300 wanaolipwa mamilioni ya fedha huku nchi ikizidi kuwa masikini tena siyo kwa bahati mbaya bali ni matokeo ya wengi wa wabunge hao kutanguliza mbele maslahi ya chama (na matumbo yao) badala ya yale ya walalahoi waliowatuma kuwawakilisha?
Nimalizie kwa kutoa rai kwa Watanzania wenzangu kufuatilia kinachoendelea hivi sasa kwenye nchi tajiri kama Marekani, hapa Uingereza na kwingineko ambapo umma umeamua kuingia mtaani katika kile kilichoanza kama “Occupy Wall Street” na sasa kinaelekea kusambaa sehemu mbalimbali duniani. Lengo la harakati hizo ni kupinga tamaa na ulafi wa taasisi za fedha hususani benki. Lakini lengo kubwa zaidi ni kupambana na mfumo wa kiharamia ambao mwenye nacho si tu anaongezewa bali anafanya ujambazi kuwapora wale wasio nacho.
Nanyi wabunge nawasihi muache matusi dhidi ya mamilioni ya walalahoi wa Kitanzania ambao licha ya mzigo mkubwa mnaowabebesha kumudu kuwalipa ninyi posho na mishahara yenu ya kufuru, muda huu hawajui watamudu vipi mlo ufuatao, achilia mbali mlo wa siku inayofuata.
Msipoacha kebehi zenu kuwa mamilioni mnayolipwa hayatoshi na mnataka zaidi, ipo siku mtashitukia mkipita mitaani mkiwa ndani ya magari yenu ya kifahari mnakumbana na makelele ya “mwizi, mwizi...” Labda hiyo ndio itawashitua mtambue kuwa ninyi ni wabunge wa nchi masikini kabisa duniani na mishahara na posho mnazopewa sasa haziendani hata chembe na umasikini wetu.
0 comments:
Post a Comment