Thursday, 3 November 2011



Waziri Membe asema kama ni misaada yao basi
Raymond Kaminyoge 
TANZANIA imesema ipo tayari kukosa  misaada yote kutoka Serikali ya Uingereza  na kamwe haiwezi kuruhusu sheria inayotambua mashoga na kuhalalisha ndoa za jinsia moja.Msimamo huo mzito wa serikali umekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kutamka kwamba nchi yake ina mpango wa kusitisha misaada yake kwa nchi ambazo sheria na katiba zao, hazitambui mashoga na ndoa za jinsia moja.

Cameron alikaririwa akithibitisha kuwa tayari amewajulisha juu ya suala hilo Wakuu  wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola waliokuwa wakihudhuria mkutano wa Jumuiya hiyo uliomalizika siku nne zilizopita,  mjini Perth , Austaralia ambao pia ulihudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete.

Waziri Mkuu huyo kutoka chama cha Conservative ambacho kilishinda uchaguzi Mei mwaka jana, alisema  suala hilo la mashoga na ndoa za jinsi moja ni moja ya mambo yanayoongoza sera ya serikali yake kuhusu misaada kwa mataifa mbalimbali na kwamba tayari imeanza kutekelezwa katika maeneo kadhaa duniani.

Kauli ya Cameron imechukuliwa kama kielelezo cha ukoloni mamboleo ambao Uingereza inajaribu kuupandisha daraja  kwa mataifa yanayoendelea kwa kigezo cha misaada  

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe,  alisema pamoja na umasikini wake, Tanzania kamwe haitaruhusu upuuzi huo kwa kigezo cha misaada.

“ Tanzania ni nchi maskini lakini hatutakubali kuruhusu upuuzi huo eti kwa sababu ya misaada yake na fedha zao, lakini ushoga si utamaduni wetu, hata sheria zetu zinakataa,” alisema Membe.

Alifafanua kuwa katika kuonesha msimamo wa kutokukubaliana na masharti hayo, Tanzania imeshikilia msimamo thabiti kupinga  upuuzi huo ambapo  Januari mwaka huu,  ilimkataa balozi shoga ambaye aliteuliwa na nchi yake kuja kuiwakilisha hapa  nchini. Hata hivyo Waziri Membe hakutaja jina la balozi huyo wala nchi  anayotoka.
“Niwape siri moja ambayo tuliificha lakini leo ngoja niwaambie, mwanzoni mwa mwaka jana nililetewa barua  kunijulisha ujio wa balozi mmoja anayekuja kuiwakilisha nchi yake, mwanamume mwenye ndoa ya jinsia moja. Nilikwenda kumweleza Rais Jakaya Kikwete kuhusu wasifu wa balozi huyo mtarajiwa naye akajibu kwa maneno matatu, yarabi toba! Mkatae!” 
Waziri Membe alifafanua kuwa serikali ilimkataa balozi huyo kwa kuwa ni kinyume cha utamaduni wetu na sheria za nchi kuwa na watu wenye tabia hizo.

Alisema alimjulisha waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kwamba balozi huyo haruhusiwi kuja kufanya kazi nchini kwa kuwa ni kinyume na utamaduni wetu.  “ Waliendelea kuniomba kwamba balozi huyo akija hatatoka kwenye makazi yake akiwa na mwenza wake hivyo watu hawatamuona lakini tulimkataa kabisa, wakatuelewa,” alisema Membe.

 Alieleza kuwa  tamko hilo la Waziri Mkuu Cameron linaweza kusababisha hatari ya kuvunjika kwa uhusiano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola na koloni mama  Uingereza na waziri huyo atabeba lawama hizo

 Akisisitiza msimamo huo wa serikali, Membe,  alisema  Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha tisa, kinatambua ndoa ya jinsia mbili tofauti,  yaani mume na mke.  “ Sheria hizi tunazozitumia hivi sasa tumezirithi kutoka Uingereza ambako leo wanatukuza ndoa za jinsia moja na ushoga,” alisema Membe.
Suala la kile kinachoitwa haki za binadamu kuhusu ushoga ilikuwa moja ya ajenda ambazo viongozi kadhaa walishindwa kuafikiana katika mkutano  Perth .
Hoja ya  kukomesha vizuizi dhidi ya ushoga na ndoa za jinsi moja lilikuwa moja ya mapendekezo yaliyokuwamo katika ripoti ya ndani kuhusu matarajio ya baadaye ya Jumuiya hiyo ya Madola.
  
Itakumbukwa kwamba, Malawi tayari imeathirika na mpango huo wa Uingereza kwa sehemu ya misaada yake kusitishwa kutokana na msimamo wa nchi hiyo kuhusu kile Uingereza na nchi za Magharibi zinazokiita haki za mashoga. Ikumbukwe pia kuwa, mjadala mzito ulioibuka katika Bunge la Uganda mwaka 2009 kuhusu ndoa za jinsi moja ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa sera hiyo ya Uingereza na washirika wake.
CHANZO: Mwananchi

1 comment:

  1. Mkazo huu wa waziri isiwe mdomoni tu bali ni kwa vitendo ili hata Mashoga waliokuwepo nchini waonyeshwe ya kuwa hatupendezi na tabia zao na ni vitendo vya aibu licha ya kuwa ni kinyume na utamaduni wetu.
    Iweje tuende kinyume na M'Mungu kisa misaada!!??

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget