Thursday, 29 December 2011




Tatizo Serikali au wanaoishi mabondeni?

Maafa ya mafuriko Dar
Mafuriko Dar es Salaam
Mafuriko Dar es Salaam
NIANZE kwa kutoa pole kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kutokana na janga la mafuriko ya wiki iliyopita. Inasikitisha kuona tunamaliza mwaka 2011 kwa majonzi, badala ya furaha (hata kama tuna vitu vichache vya kufurahia).
Kwa hakika si jambo jema kutumia janga kama hili kunyoosheana vidole, hususan katika kipindi hiki ambacho hata hatujafahamu kiwango cha athari kilichosababishwa na mafuriko hayo.
Hata hivyo, tunaweza kuendelea kusononeka na kuomboleza milele lakini pasipo kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa huko mbele tunajiandaa ipasavyo kukabiliana na majanga kama haya basi ni dhahiri tunaweza kujikuta tena katika hali kama hii inayotukabili sasa.
Ni ukweli usiofichika kuwa nchi yetu inaendeshwa kwa mtindo wa zimamoto. Tunasubiri litokee balaa kisha watawala wetu wapite huku na kule wakijifanya kuguswa na kusononeshwa na maafa yaliyowakumba watawaliwa.
Jiji la Dar es Salaam kama yalivyo maeneo mengine ya nchi yetu ni kama bomu linalosubiri kulipuka. Japo mafuriko ni janga la asili kwa maana hakuna namna ya kuyazuwia, kwa hakika kuna njia kadhaa za kujiandaa kukabiliana nayo na hata kupunguza madhara yake.
Kimsingi haya si mafuriko ya kwanza kuwakumba wakazi wa Jiji la Dar es Salaam au kusababisha madhara katika sehemu nyingine nchini.
Tofauti na mafuriko yaliyotangulia ni kiwango cha madhara ambacho yayumkinika kuhisi kwamba inaweza kuwa vigumu kufahamu kutokana na uzembe, ubabaishaji na kutowajibika ipasavyo kwa wahusika.
Janga hili la mafuriko jijini Dar es Salaam limeibua tena mjadala wa miaka nenda miaka rudi kuhusu makazi ya mabondeni. Swali ambalo limejitokeza katika mijadala mbalimbali ni nani alaumiwe kati ya Serikali na wakazi wa mabondeni.
Pengine cha muhimu si lawama bali kuangalia chanzo na utatuzi wa tatizo hili ambalo likiachwa liendelee litasababisha vilio vingine huko mbele (hata kama tunaombea isiwe hivyo).
Ni rahisi kuwalaumu wakazi wa mabondeni kwa hoja dhaifu kama “nani awalazimishe kuhama mabondeni kama wenyewe hawataki au hawajali maisha yao?”
Unaweza kutoa lawama hizo kirahisi kama hujui ugumu wa kupata sehemu ya kuishi jijini Dar es Salaam, achilia mbali ugumu wa kupata kiwanja cha kujenga nyumba mpya.
Ripoti kadhaa kuhusu utawala bora zimekuwa zikizitaja mamlaka za ardhi kama kiongozi wa muda mrefu katika rushwa. Na kama inavyoeleweka, waathirika wakubwa wa rushwa ni walalahoi wasio na uwezo wa kuhonga. Sitaki kabisa kuamini kuwa wakazi wa mabondeni wanaendelea kuhatarisha maisha yao katika maeneo hayo kwa vile wanapenda iwe hivyo.
Nani asiyeogopa kifo? Nani anayetaka kuishi sehemu ambayo kufikika kwake hata wakati wa kiangazi ni kwa shida? Nani anayependa kukaa eneo ambalo mvua kidogo tu ikinyesha basi inaweza kusababisha wakazi wa eneo husika kujifungia ndani kutwa nzima au usiku kucha kwa vile kila eneo limejaa maji?
Hawa ni watu wanaohitaji kusaidiwa. Lakini kwa vile sote tunajua kuwa si Serikali kuu wala mamlaka za Jiji zinazoguswa kwa dhati na tatizo hili, ni muhimu kuwaelimisha wakazi hao kudai haki zao za kibinadamu kuhusu makazi bora na usalama wa maisha yao kwa ujumla.
Mwaka unamalizika na janga hili la mafuriko, na japo nisingependa kuwa “nabii wa majanga” (prophet of doom) yayumkinika kubashiri kuwa safari yetu huko mbele si salama. Ni wazi kuwa laiti yakitokea mafuriko mengine iwe Dar es Salaam au kwingineko nchini, tutarejea katika hali hii ya huzuni na majonzi kwa vile mfumo wa kuzuia na kukabiliana na majanga ni sifuri.
Viongozi wetu ni wepesi kumbebesha Mungu mzigo wa lawama kwa kauli maarufu ya “ni mapenzi ya Mungu.” Kuna nyakati ninatamani Mungu apandwe na hasira na kuwaumbua viongozi wa aina hiyo kwa umma kwa yeye (Mungu) kujivua lawama hizo na kuwafumbua macho watawaliwa waelewe kuwa tatizo ni watu waliopewa jukumu la kuongoza lakini wasiotekeleza jukumu hilo ipasavyo.
Kuna janga jingine kubwa la kiuchumi. Kwa sisi tunaoishi kwenye nchi kama Uingereza ambayo ni miongoni mwa wafadhili wakubwa wa Tanzania tunaona kila dalili kuwa muda si mrefu wanaweza “kubwaga manyanga” kusaidia nchi masikini na kuelekeza nguvu kwenye kujisaidia wao wenyewe.
Hali ya uchumi wa dunia ni mbaya sana lakini pengine kinachoweza kusababisha msione hivyo huko nyumbani ni ukweli kwamba hali huko ni mbaya karibuni kila siku.
Sasa kama hali ni mbaya wakati huu ambapo wafadhili wanaendelea kumwaga misaada yao (huku sehemu kubwa ya misaada hiyo ikiishia kwenye mifuko na akaunti za mafisadi), ni wazi kuwa hali itakuwa mbaya zaidi pindi wafadhili hao wakilazimika kupunguza au kukata kabisa misaada hiyo.
Tofauti na mafuriko ambayo ni janga la asili (natural disaster), tatizo hili la uchumi ni la kibinadamu. Na wakati wenye jukumu la kujiandaa na kukabiliana na majanga ya asili wanaweza kuwa na kisingizio kwamba “sie ni masikini sana kumudu kuwa tayari muda wote kujiandaa na kukabiliana na majanga ya asili,” kwenye tatizo hili la uchumi hakuna kisingizio hasa kwa vile tuna raslimali za kutosha za kujiandaa kukabiliana na mtikisiko wa uchumi wa dunia.
Wanasema “kufa kufaana.” Janga hili la mafuriko linaweza kutoa nafasi nzuri kwa watawala wetu kukwepa kutueleza kwa nini tupo katika hali mbaya kiasi hiki katika kipindi hiki tunachoelekea mwisho wa mwaka huku ikiwa ni siku chache tu baada ya kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wetu.
Watawala wamepata kisingizio cha “tupo kwenye kipindi cha majonzi na si vema kuanza kunyoosheana vidole kuhusu masuala mengine.” Na kwa vile Watanzania wengi sio tu ni wepesi wa kusahau lakini pia hawapendi kuunganisha mlolongo wa matukio (chain of events) basi ni wazi kuwa janga hili la mafuriko litawanusuru watawala wetu kutupatia majibu kuhusu matatizo mengine mengi ambayo pasi na shaka tutaingia nayo mwaka ujao 2012.
Sawa, kwa sasa tunapaswa kufanya kila linalowezekana kuwasaidia Watanzania wenzetu walioathirika kwa mafuriko. Lakini wakati tunafanya hivyo ni lazima tutambue kuwa laiti tungepata ufumbuzi wa matatizo yaliyokuwepo kabla ya janga hili la mafuriko ni wazi kuwa pindi wahanga hao wakishasaidiwa hawatakuwa na hofu nyingine za kukabiliana na matatizo hayo “ya kudumu.”
Tunamaliza mwaka huku Ripoti ya Bunge kuhusu sakata la akina Jairo likiwa limenyamaziwa na Rais Jakaya Kikwete. Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo bado hajachukuliwa hatua kama ilivyo kwa Waziri William Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima, sambamba na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Utoh.
Hivi Kikwete haelewi kuwa katika mazingira ya kawaida tu uwepo madarakani wa watu hawa unaweza kusababisha madhara makubwa zaidi ya hayo yaliyosabisha Bunge liwachunguze?
Hapa ninamaanisha kuwa kwa vile wahusika hawa wanaweza kujiona wapo “mguu ndani, mguu nje” basi ni bora “wachukue chao mapema” kabla hawajawajibishwa.
Tunamaliza mwaka huku ahadi zilizozoeleka za Rais Kikwete kuhusu utatuzi wa tatizo sugu la umeme zikiendelea kuwa ahadi hewa. Mwaka unaelekea ukingoni lakini ahadi ya Rais kuwa ifikiapo mwezi huu Desemba, mpango wa dharura wa kuongeza nishati ya umeme (megawati 572) katika gridi ya taifa ungekamilika inabaki kuwa ndoto ya alinacha.
Mpango huo wa Serikali uliowasilishwa bungeni mwezi Agosti, mwaka huu ulieleza kuwa kati ya megawati hizo, 150 zilikuwa zizalishwe kupitia makubaliano kati yake na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Mgawanyo wa megawati hizo ulionyesha kungeingizwa megawati 50 kwa kila mwezi, kati ya Septemba na Desemba 2011.
Hadi sasa hakuna hata megawati moja ya umeme iliyozalishwa na NSSF na taarifa zinaonesha kuwa mamilioni ya fedha za umma yamepotea kwa “safari za kutalii” kwenda Marekani na Ufaransa “katika mchakato huo” lakini mgawo wa umeme unazidi kudumisha makali yake.
Nimalizie makala hii kwa kurejea pole zangu kwa waathirika wa mafuriko ya Dar es Salaam, sambamba na kuwatakia wasomaji wote wa Raia Mwema na makala hii heri ya mwaka mpya 2012.
Wakati mwaka huu 2011 unamalizika huku tukiwa na mengi ya kulalamikia kuliko kupongeza au kujidai nayo, ninaomba kutoa wito kwa kila Mtanzania mwenye uchungu na nchi yetu kuukaribisha mwaka mpya kwa kauli ya “Enough is enough”(Imetosha); aidha tuendelee kuwaruhusu viongozi wazembe na mafisadi waipeleke nchi shimoni au tusimame kidete na kudai haki zetu za msingi za kuwa na maisha bora na salama.
Kama alivyowahi kutuasa aliyepata kuwa Waziri wa Fedha wakati wa Awamu ya Pili, Marehemu Profesa Kighoma Ali Malima (namnukuu); “haki haitolewi kama zawadi. Haki hudaiwa, hata kwa nguvu inapobidi.” (Atakayeniita mchochezi kwa nukuu hii lazima atakuwa fisadi asiyetaka kuona Watanzania “wanaamka”).
Mkoloni hakuondoka kwa vile tulikuwa tunanung’unika, Nduli Idi Amin hakuacha uharamia wake kwa vile tulimwita kila jina baya. Kilicholeta mwisho wa udhalimu wa mkoloni na Amin ni harakati za dhati za kukomesha maovu yao.
Manung’uniko na majina mabaya kwa mafisadi na wazembe hayawezi kutuletea “ukombozi” wetu. Kinachohitajika ni mwamko na jitihada za dhati za kukomesha uharamia huo.
Heri ya mwaka mpya  2012.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget