Makaburu hawakufurukuta, kwa nini mnalea mafisadi?
Usalama wa Taifa
Uskochi
KATIKA kubainisha baadhi ya changamoto zinazolikabili taifa letu baada ya miaka 50 tangu tupate uhuru, nilielezea katika makala yangu ya wiki iliyopita kuhusu ulegevu wa kiusalama na kutoa mfano hai wa namna akaunti ya twitter ya mke wa Rais, Salma Kikwete, ilivyohujumiwa (ilikuwa hacked).
Katika kipengele hicho nilihoji watendaji wa kitengo cha Idara ya Usalama wa Taifa kinachohusika na teknolojia ya habari na mawasiliano walikuwa wapi kwa takriban saa 24 za kushuhudia akaunti ya twitter ya Mama Salma, ikiwekwa habari zisizoandikika gazetini.
Kuashiria kuwa wahusika waliguswa na nilichoandika, hatimaye kasoro hiyo ilirekebishwa na siku hiyo hiyo kuliwekwa taarifa ifuatayo;
“Angalizo: Kwa muda wa takribani siku 10 handle hii ya Twitter ilipata tatizo lililosababisha urushwaji wa taarifa zisizo sahihi na za kukanganya. Tatizo hili limekuwa likishughulikiwa na kufikia leo usiku lilikuwa tayari limetatuliwa. Tunatoa pole kwa usumbufu uliojitokeza na tunashukuru wote waliokuwa nasi wakati wa kutatua tatizo hili kuanzia utoaji taarifa. Tuendelee kutumia mitandao hii ya kijamii kujenga jamii zetu zaidi na zaidi hasa katika harakati za kumkomboa mtoto wa kike kielimu na kiuchumi."(WAMA Foundation - Kitengo cha Mawasiliano)”
Taarifa hii ilinisaidia kufahamu kuwa kumbe kasoro hiyo ilidumu kwa takriban siku 10, na si saa 24 kama nilivyoelewa mwanzoni. Na hii inazidisha wasiwasi kuhusu uwajibikaji wa watendaji wenye jukumu la kuhakikisha usalama wa viongozi wetu na watu mashuhuri(VIPs).
Haingii akilini kuona watendaji wanaolipwa vizuri kufuatilia taarifa mbalimbali zinazohusu usalama wa taifa letu (sambamba na usalama wa viongozi wetu na VIPswengine) wanashindwa kubaini tatizo jepesi kama hilo (lakini lenye madhara makubwa).
Kwa kuzingatia mwenendo wa namna “taarifa za kiintelijensia” zinavyopatikana na kufanyiwa kazi, ni wazi kwamba laiti hacking ya akaunti ya Mama Salma ingekuwa ni wito wa CHADEMA kuhamasisha maandamano basi suala hilo lingeshughulikiwa haraka sana.
Haya ndio madhara ya kutanguliza zaidi siasa na kuweka kando utaalamu na taaluma. Laiti nguvu inayotumiwa na vyombo vya usalama kufuatilia mienendo ya majukwaa ya mtandaoni yanayoelemea kwenye mijadala ya mambo muhimu ya taifa letu (hususan Jamii Forums) ingeelekezwa pia katika kuhakikisha usalama wa mtandaoni wa VIPs wetu basi fedheha iliyosababishwa na hacking ya akaunti yaTwitter ya mke wa Rais ingedhibitiwa mapema badala ya kuachwa idumu kwa takriban siku 10.
Na huenda hadi muda huu hali ingeendelea kuwa hivyo hivyo laiti kasoro hiyo isingezungumzwa nami katika makala ya wiki iliyopita.
Ninatambua kuwa huenda waliozembea katika suala hilo wanakerwa na jinsi “ninavyowashikia bango” lakini lengo langu si kubainisha uzembe wao bali kuwasaidia katika utendaji kazi wao.
Kama nilivyoeleza katika makala iliyopita, suala hili linaweza kuonekana dogo na lisilohitaji kujadiliwa kwa undani. Lakini kimsingi, kasoro ndogo kama hiyo inaweza kutufumbua macho na kuanza kujiuliza maswali muhimu hasa tukizingatia kuwa baada ya uhuru wetu kutimiza miaka 50, ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha taifa letu sio tu linasonga mbele bali pia lina uhakika wa usalama katika safari hiyo.
Kutokana na asili ya kufanya kazi zake kwa usiri, ilikuwa vigumu kwa Idara ya Usalama wa Taifa kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wetu kwa kuueleza umma mafanikio yake katika kipindi hicho.
Lakini kama inavyofundishwa kwenye stadi za usalama (security studies), moja ya vipimo vya ufanisi katika utendaji kazi wa idara yoyote ile ya usalama duniani ni kiwango cha amani-iwe amani kamili (absolute peace) au ile ya kuridhisha (relative peace).
Tukiweka kando matukio ya kusikitisha ya ubabe wa polisi dhidi ya raia wema (ambao mara nyingi kosa lao kubwa ni kutumia haki yao ya kidemokrasia kuandamana), maelfu ya vifo vinavyotokana na ajali (huku nyingi ya ajali hizo zikiwa zinazoweza kuepukika laiti sheria za usafiri zingezingatiwa na wenye mamlaka ya kuzisimamia) na matukio mengine yanayoashiria mmomonyoko wa amani yetu (kwa mfano mauaji dhidi ya maalbino, migongano ya hapa na pale kati ya waumini wa dini mbalimbali), kwa ujumla tumeendelea kuwa na amani ya kuridhisha (hasa tukijilinganisha na jirani zetu).
Lakini unaweza kujiuliza inawezekanaje watu waliomudu kuliwezesha taifa kuwa na amani ya kuridhisha katika kipindi chote cha miaka 50 tangu tupate uhuru wanashindwa kubaini kwa takriban siku 10 kuwa akaunti ya Twitter ya mke wa Rais imekuwa hacked, na kibaya zaidi, aliyei-hack anachapisha mambo yanayodhalilisha utendaji kazi wa Rais na kuaibisha familia yake.
Unaweza kwenda mbali zaidi ya tukio hilo la hacking na kuhoji matukio mbalimbali yanayoendelea kulisumbua taifa hususan skandali lukuki za kifisadi. Je, inawezekana kuwa kinyume cha kanuni za stadi za usalama kuwa uwepo wa amani (japo ya kuridhisha) ni uthibitisho wa ufanisi wa utendaji kazi wa Idara ya Usalama wa Taifa, wanaostahili sifa ni Watanzania wanaosifika kwa upole hata pale wanapopelekeshwa mrama?
Je, inawezekana taasisi hiyo muhimu kwa ustawi wa taifa lolote lile duniani ni dhaifu kuliko tunavyodhani na ndio maana mafisadi wanaligeuza taifa letu kuwa “shamba la bibi” na kulihujumu watakavyo bila uoga wowote ule?
Je, inawezekana kuwa ukaribu wa Idara hiyo na chama tawala umewawezesha mafisadi kufahamu udhaifu wake na hivyo kuwa na jeuri ya kufanya uharamia wao bila hofu?
Nayumkinisha hivyo kwa vile inafahamika kuwa chama tawala kimekuwa kama kimbilio kuu la mafisadi, na uwepo wao ndani ya chama hicho si tu unawatengenezea kinga dhidi ya kuchukuliwa hatua za kisheria bali pia unawasaidia kuwaweka karibu na taasisi za serikali zinazoundwa na chama hicho (ikiwa ni pamoja na Idara ya Usalama wa Taifa).
Kwa uelewa wangu, taasisi hiyo kama haina tatizo basi kinachoikwamisha katika kutekeleza wajibu wake ipasavyo ni kuruhusu nguvu za kisiasa zifunike taaluma na utaalamu ya usalama.
Tatizo hilo la kuruhusu siasa ikwaze matumizi ya taaluma na utaalamu limechangia sana mengi ya matatizo yanayolikabili taifa muda huu. Laiti viongozi wa Idara ya Usalama wangeamua kuweka mbele maslahi ya taifa (au kuzingatia taaluma na utaalamu wao) wangeweza kabisa kuusambaratisha mtandao uliokuwa ukihangaika huku na kule kuingiza mtu wao Ikulu mwaka 2005.
Ni wazi kuwa maofisa usalama wetu walifahamu jinsi fedha za umma zilivyokuwa zinaibiwa na kuingizwa kwenye kampeni za uchaguzi (na nyingine zikiishia kwenye akaunti za wapambe) lakini kwa vile ndani ya Idara hiyo nako kulikuwa na migongano wa kimaslahi (ya nani aingie Ikulu), hakuna kilichofanyika na sasa tunavuna matunda ya uzembe huo.
Kama alivyotuasa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kiongozi anayeingia madarakani kwa fadhila za watu fulani ni lazima ataendelea kuwa mtumwa wa watu hao. Wasifu usiopendeza wa wengi wa wanamtandao ulipaswa kuwa kigezo kinachojitosheleza kwa Idara hiyo kutangaza vita dhidi ya kundi hilo, si tu kwa vile ushindi kwa kundi hilo ungekuwa sawa na tishio kwa usalama wa taifa kwa ujumla bali pia ungeiongezea Idara hiyo mzigo wa majukumu (kwa maana ya mhalifu wa leo akiwa kiongozi kesho basi vyombo vya dola vinalazimika kuwa macho zaidi kuhakikisha kuwa uongozi huo hautumiki kuendeleza uhalifu aliokuwa akifanya kiongozi huyo kabla ya kukwaa uongozi).
Nimalizie makala hii kwa kurejea ushauri wangu kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa kuhakikisha inabaki kuwa taasisi inayozingatia utaalamu na taaluma ya usalama hasa kwa kupinga kwa nguvu zote siasa kuingilia utendaji kazi wao.
Kuna sauti chache nje ya Idara hiyo zinazodiriki kuwanyooshea kidole maofisa wake pale wanapoboronga. Sauti hizo zisitafsiriwe kuwa zina lengo la kuichafua taasisi hiyo muhimu bali cha muhimu ni mantiki ya hoja zinazotolewa.
Na kwa vile Idara ya Usalama wa Taifa legelege hupelekea taifa husika nalo kuwa legelege basi jukumu la kila mzalendo anayeitakia mema nchi yetu kuchangia kwa hali na mali kuhakikisha taasisi hiyo inafanya kazi zake kwa ufanisi kama ilivyokuwa katika zama za “kuhesabu visoda vya bia kwenye mabaa” (uvumi uliozoeleka lakini usio na chembe ya ukweli) na kufanikiwa kuwazuia kabisa makaburu kutekeleza azma yao ya kuiangamiza Tanzania yetu.
Kama Idara iliweza kuwamudu makaburu ambao licha ya uwezo wao mkubwa kiujasusi walikuwa wakisaidiwa pia na mataifa makubwa duniani, kwa nini basi ishindwe kuwamudu mafisadi ambao silaha yao kubwa ni fedha wanazotuibia kila siku?
0 comments:
Post a Comment