CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SALAAM ZA RAMBIRAMBI NA POLE KWA WANAFAMILIA NA WANANCHI KUHUSIANA NA JANGA LA MAFURIKO YALIYOKUMBA JIJI LA DAR ES SALAAM, MBEYA NA DODOMA .
Usiku wa kuamkia tarehe 20.12.2011 Maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es Salaam, Mbeya na Dodoma yamekumbwa na maafa makubwa ya mafuriko ambayo yamesababishwa na mvua kubwa ambazo zimeendelea kunyesha mfululizo katika maeneo hayo.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapenda kutoa pole za dhati kwa wanafamilia na wananchi wote ambao wamekumbwa na janga hili kubwa , kwani limesababisha maafa makubwa sana ya vifo, kupoteza mali na miundombinu mbalimbali kuharibiwa vibaya kwenye maeneo husika. Tunapenda kuwahakikishia wananchi hawa kuwa tutakuwa nao pamoja katika kipindi hiki kigumu katika maisha yao kutokana na madhara waliyopata yaliyosababishwa na maafa haya.
Kutokana na janga hili limetukumbusha jambo moja kuwa kama Taifa hatujajiandaa kikamilifu kuweza kukabiliana na majanga kama haya pindi yanapotokea na hata vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeonyesha dhahiri kuwa havijaandaliwa kimfumo na kinyenzo katika kuweza kukabiliana na majanga kama haya na huu ni udhaifu mkubwa sana kwa taifa lenye miaka 50 baada ya uhuru wake .
Mathalani mpaka sasa hatujaona jitihada zozote ambazo zimechukuliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa katika kuonyesha juhudi za kukabiliana na janga hili kubwa kwa taifa letu,hii inaonyesha wazi kuwa kitengo hiki hakijaandaliwa kuweza kukabiliana na maafa kama ambavyo majukumu yake yanavyopaswa kuwa . Na hii ni hatari kwani kama chombo cha kukabiliana na maafa hakiwezi kufanya hivyo kwa wakati ni kuendelea kuwaacha wananchi waendelee kupata madhara makubwa zaidi. Na haswa ikizingatiwa kuwa idara ya hali ya hewa ilishatahadharisha kuhusiana na mvua hizi.
CHADEMA tunapenda kuikumbusha serikali kuhusiana na ilani yetu ya uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo ilieleza wazi kuhusiana na kukosekana kwa mifumo thabiti ya kujulisha umma kuhusiana na majanga mbalimbali katika miji yetu (Early Warning Systems) kama ambavyo ipo katika nchi nyingi , mfumo huu ni muhimu sana katika kuweza kuufanya umma uwe na elimu ya jinsi ya kuweza kujikinga na majanga haya kwa lengo la kupunguza madhara yasiwe makubwa kama ambavyo taifa hivi sasa linashuhudia.
CHADEMA inapendekeza hatua zifuatazo ziweze kuchukuliwa haraka na serikali ili kuweza kukabiliana na majanga/maafa mbalimbali hapa nchini yanapojitokeza;
I) Kuandaa mfumo wa awali wa kutahadharisha umma juu ya ujio wa majanga (Early Warning Systems) kwa kutumia vyombo na nyenzo mbalimbali ili kuepusha madhara makubwa kwa watu na mali zao.
II) Kutunga sheria mpya ya ujenzi na kuweka viwango vya ujenzi viwe vyenye hadhi ya kimataifa na haswa ujenzi wa kuta mbalimbali na majengo marefu na kuhakikisha kuwa ujenzi holela haujitokezi kwenye miji na majiji yetu hapa nchini.
III) Kuhakikisha kuwa kwenye miji yote mikubwa mtandao wa mabomba ya maji ya dharura unawekwa ili kuweza kukabiliana na majanga ya moto pindi yanapotokea.
IV) Serikali ijiandae mara moja kukabiliana na magonjwa ya milipuko kama vile kuhara ,kipindupindu na mengineyo ambayo yatajitokeza kutokana na mafuriko haya kuharibu miundombinu ya kusambaza maji, makazi ya watu n.k.
V) Kitengo cha maafa kiwe na vifaa wakati wote , na haswa vifaa kwa ajili ya uokoaji na wawe na utaratibu wa kutoa elimu kwa umma jinsi ya kuweza kutumia vifaa hivyo kuweza kujiokoa na sio kuacha hali iwe kama ambavyo imejionyesha Dar Es Salaam jana baada ya baadhi ya majaketi okozi kufikishwa kwa wahanga na kushindwa kuyatumia kikamilifu.
VI) Serikali itoe elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa ya milipuko kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko haya ili kuepusha wananchi wengi kukumbwa na magonjwa hayo pindi yakijitokeza.
Mwisho tunapenda kuendelea kutoa pole kwa wanafamilia wote na wananchi kwa ujumla kutokana na madhara makubwa waliyoyapata , Mungu awajaze nguvu katika kipindi hiki kigumu.
Tamko hili limetolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu CHADEMA .
……………….
DR. Willbroad P. Slaa.
Katibu Mkuu –CHADEMA.

22/12/2011.