Thursday, 19 April 2012


CAG na madudu ya taasisi zetu

Raia Mwema Ughaibuni
Uskochi
NIANZE kwa kutoa samahani kutokana na safu hii kutoonekana katika matoleo mawili yaliyopita. Hali hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo.
Makala ya wiki hii inalenga kuamsha tafakuri kuhusu taifa letu na hatma yake. Na pengine njia mwafaka ya kuanzisha tafakuri hiyo ni kwa ‘mchapo’ ufuatao (ambao nilishawahi kuutumia huko nyuma).
Miaka machache iliyopita nilipokuwa safarini kutoka jijini London kuja huku Uskochi nilipata nafasi ya kuzungumza na babu mmoja wa Kiskochi ambaye aliwahi kuishi huko nyumbani Tanzania pamoja na sehemu nyingine mbalimbali za Bara la Afrika.
Maongezi yetu yalilenga zaidi katika tofauti zilizopo kati ya nchi za Afrika na Ulaya, na hususan kati ya Tanzania na Uingereza. Na moja ya maswali aliyonidadisi babu huyo, na ambalo linaendelea kunigusa hadi leo, ni hili: kwa nini nchi yangu ni masikini licha ya utajiri mkubwa ilionao?
Katika ‘kujitetea’ nilikimbilia hoja ya kuwalaumu wakoloni, nikajitutumua na kudai kwamba laiti mkoloni asingekuja Afrika basi huenda bara hilo lingeweza kuwa na kiwango sawa (au zaidi) cha maendeleo kulinganisha na nchi kama Uingereza.
Lakini ‘utetezi’ wangu haukuwa na uhai mrefu kwani babu huyo alizidi kunitupia maswali yaliyopelekea nikose majibu ya maana. Kwa mfano, alikiri kwamba ni kweli ukoloni ulichangia kudumaza maendeleo ya Afrika lakini kwa nini hoja hiyo iendelee kutumiwa kama kisingizio takriban nusu karne tangu nyingi za nchi za bara hilo zipate uhuru?
Baada ya kuniona ‘ninatapatapa’ na sina majibu ya kueleweka, mzee huyo akaamua kunipa msaada kwa kubadili ‘maswali na majibu’ kuwa mjadala wa pande mbili. Alidai kwamba kwa mtizamo wake, tatizo kubwa linalozikabili nchi nyingi za Kiafrika lipo kwenye uongozi na wanaoongozwa (yaani wananchi).
Alieleza kwamba pengine atakuwa hawatendei haki viongozi wa Afrika kwa kuwalaumu  kwa kudumaa maendeleo ya nchi zao. Hoja yake ilikuwa kwamba wengi wa viongozi hao walifanikiwa kuingia madarakani kwa ridhaa za wananchi.
Kimsingi,  alikuwa anawalaumu wananchi wanaohadaika kuwachagua viongozi wabovu lakini badala ya kuwang’oa madarakani kila zinapojitokeza fursa za kufanya hivyo, wananchi hao wanaendelea kuhadaiwa. Babu huyo alidai kuwa takriban kila Mwafrika anayekutana naye analalamika kuhusu viongozi wa nchi yake, lakini ni nadra kusikia mtu mwenye angalau ufumbuzi wa tatizo la kulalamikia. Alieleza bayana kuwa matatizo ya nchi kama Tanzania hayawezi kuisha kwa lawama.
Akaeleza kuwa Uingereza ‘ya kisasa’ tuliyonayo leo ni matokeo ya jitihada zilizofanyika miaka mingi iliyopita. Mzee huyo akatanabaisha kuwa kwa mtizamo wake anaona nchi nyingi za Kiafrika zinaendeshwa kwa mihula ya utawala wa kiongozi (yaani kwa vipande vya muda) kiasi kwamba ni vigumu kubashiri hali itakuwaje kwa mfano miaka 50 ijayo.
Akanipa mfano wa jinsi mifumo ya reli za ardhini mijini (underground railways) na ule wa reli ya chini ya bahari unaounganisha Uingereza na Bara la Ulaya kupitia Ufaransa (Eurotunnel) ilivyotokana na mtizamo ya kuangalia miaka kadhaa mbele.
Akaeleza kuwa wengi wa Waingereza walioshiriki kubuni na kutekeleza miradi hiyo hawakuwa wakifikiria kizazi chao tu bali vizazi vingi vijavyo mbeleni.
Akaendeleza mjadala kwa kutupa lawama kwa viongozi wengi wa Afrika ambao aliwaita walafi na wasio na chembe ya uzalendo. Alibainisha kuwa ulafi wa viongozi hao huonekana bayana katika maisha yao ya anasa licha ya kuzungukwa na mamilioni ya wananchi ambao ni masikini kupindukia.
Kuhusu kukosa uzalendo alitoa mfano wa rafiki yake mmoja aliyejitolea kupelekea mradi mmoja wa maendeleo barani Afrika lakini serikali ya nchi husika ikamkwamisha kwa vile hakukubali kuwapa rushwa (haingii akilini kudai rushwa ili uruhusu usaidiwe).
Tukiweka kando maongezi yangu na babu huyo wa Kiskochi (ambaye tunaendelea kuwasiliana kujadili masuala mbalimbali ya Afrika, na hususan Tanzania), ni muhimu kwa kila mwenye uchungu na nchi yetu ajaribu kuangalia ni kwa namna gani anaweza kuchangia kubadili mwenendo wa mambo.
Majuzi, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh, aliwasilisha ripoti kwa Rais Jakaya Kikwete, ambapo kama ilivyokuwa huko nyuma, imethibitika kuwa kuna ufisadi wa kutisha unaoendelea huko nyumbani.
Kilichonigusa zaidi ni changamoto aliyotoa Utoh kuhusu deni la Taifa ambalo limepanda kutoka shilingi trilioni 10.5 mwaka wa fedha 2009/10 hadi shilingi trilioni 14.4 kwa mwaka 2010/11, na misamaha ya kodi ambayo imeongezeka kwa takriban asilimia 49.
Ni vema tukafahamishana kuwa deni hilo la Taifa lina madhara kwetu na kwa vizazi vijavyo hasa ikizingatiwa kuwa badala ya kuwekeza nguvu kwenye kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, watawala wetu wanachuana kutuongezea mzigo huo.
Moja ya maeneo yanayoongeza mzigo huo  ni safari za viongozi wetu nje ya nchi. Tusiume maneno, moja ya mizigo mikubwa anayobebeshwa mlipakodi wa Tanzania inachangiwa na hizi safari zisizoisha za viongozi. Haiingii akilini hata kidogo kuona viongozi wa moja ya nchi masikini kabisa duniani wanakuwa ziarani nje ya nchi mara nyingi zaidi ya viongozi wa mataifa tajiri duniani kama Marekani, Uingereza, Ujerumani, Japan.
Hata kwa majirani zetu ambao wanatajwa kama ‘matajiri wanaochipukia Barani Afrika’ yaani nchi kama Rwanda na Msumbiji, viongozi wao hawasafiri mfululizo kama wa kwetu.
 Sawa, hata tukiafiki porojo kuwa inabidi wasafiri kwenda kutembeza bakuli huko nje. Lakini kama hilo ni la muhimu zaidi basi tufunge balozi zetu. Maana hata hizo balozi nazo zinatajwa katika takriban kila Ripoti ya CAG kama vinara wa matumizi yanayokiuka taratibu.
Awali niliposikia kuwa misamaha ya kodi imeongezea takriban mara dufu nikahisi labda ni katika utekelezaji wa sera ya Kilimo Kwanza (ambapo ni muhimu kutoa misamaha kwenye pembejeo zinazoingizwa nchini kuinua sekta ya kilimo) au katikaimports zinazolenga sekta muhimu za elimu, afya, nk. Kinachokera ni ukweli kwamba asilimia kubwa ya misamaha hiyo ilitolewa kwa mawaziri na wabunge.
Jamani, hawa watu wanaopata mishahara minono na posho lukuki wanapewa misamaha hiyo ili iweje? Au ndiyo yale yale ya ‘mwenye nacho ataongezewa na yule asiyenacho ataporwa hata kile kidogo alichonacho’?
Kama ambavyo yule babu wa Kiskochi alivyotahadharisha, tunaweza kukesha tukimlaumu huyu na yule lakini hali yetu inazidi kuwa mbaya huku wenzetu kama Rwanda wanamudu kutoka ‘kwenye majivu’ (mauaji ya kimbari) na kufikia hatua ya kuitwa economic tiger wa Afrika.
Tafakari. Chukua hatua.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget