Sunday, 13 May 2012


Unga unavyouzwa nje nje Kinondoni
Saturday, 12 May 2012 10:08

Mwandishi Wetu
KATIKA manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam yapo maeneo kadhaa ambayo mbali na kukaliwa na watu, yamebeba siri kubwa ambazo ni uihalifu wenye athari kubwa kwa maisha ya watu hasa vijana.

Kinondoni ni eneo maarufu ambalo si tu kwamba ni kubwa kwa wingi wa vitongoji vyake au wingi wa watu pekee, lakini hata kwa nyumba za starehe, maduka ya urembo na mavazi.

Kila unapotembea hatua kadhaa, utakutana na ama duka la nguo au baa.  Lakini si hivyo tu, bali katika hatua hizo inawezekana ni tano, kumi, ishirini au zaidi ya hizo, aghalabu utakutana na mtu ambaye ana dalili za ulevi.

Wengi  wa watu wanaoonekana kuwa wamelewa si kwa kunywa pombe, la hasha, bali ni ulivi wa dawa za kulevya. Huu ndio uhalifu ambao tunauzungumzia, kwani unaharibu sana maisha ya vijana kiasi cha kutisha.

Vyombo vya dola vipo na vinaona, viongozi wapo na wanaona, lakini hakuna kinachofanyika ni kama uhalifu huu umehalalishwa. Kutoka na hali hii gazeti hili lilisukumwa kufanya utafiti mdogo tu katika eneo la Kinondoni , kujua wapi kilipo chanzo cha umaarufu wa dawa hizi haramu.

Haikuwa kazi rahisi kwani kwa siku tatu mfululizo ilikuwa ni kazi ya kusoma mazingira ya baadhi ya maeneo yanayotajwa kutumika kuendesha biashara hiyo. Ilibidi zitumike mbinu mbalimbali kwani tuliambiwa kwamba ni hatari sana kufuatilia uhalifu huu.

Ni maeneo yapi?
Eneo la kwanza kugundulika lilikuwa ni lile lililoko maeneo ya karibu na hospitali ya Mwananyamala, nyumbani kwa maarufu, ambaye hata hivyo kwa sasa ni marehemu.

Watu wanavyoingia na kutoka ndani ya nyumba hiyo ni mithili ya nyuki wanavyoingia na kutoka kwenye mzinga wao. Hali hii inatupa ishara kwamba lazima kuna kinachofanyika ndani. 

Nje ya nyumba hiyo, kuna miti kadhaa aina ya mwarobaini, magurudumu ya magari ambayo hutumiwa na wavutaji wa dawa za kulevya kujipumzisha nyakati zote na duka ndogo. 

Ubavuni mwake zipo ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) na mbele yake kuna soko dogo la wauzaji wa viazi mviringo na mikokoteni ya maji. Mpango wa kuingia ndani ya nyumba hiyo ulikamilika baada ya wiki moja, lakini tulipofanikiwa kuingia, tulibaini kuwa ina vyumba sita, vitatu kulia na vitatu kushoto.

Hata hivyo kuna baadhi ya vyumba vya uani ambavyo vinaonekana kuwa vimepangishwa. Ni vigumu kutambua nani anaishi chumba kipi kutokana na muingiliano, pia wingi wa watu.

Mara unapoingia unakaribishwa, maana wenyeji wanajua kwamba kila anayefika ni mteja wa bidhaa hiyo haramu. Hivyo baada ya kuketi, muuzaji anaitwa,  anatoka ndani ya chumba cha pili kulia, kisha anauliza, “Unahitaji wa shilingi ngapi?”

Mwananchi linatoa noti ya Sh10,000 na yeye anahoji tena, “wa hela yote?.”
Muuzaji anatokomea na kurudi na karatasi lililosokotwa na kulikabidhi kwa mnunuzi.

Tunatoka nje ili kuondoka katika weneo hilo maana tumejawa na hofu kwamba huenda tukagundulika kwamba sisi siyo wateja, mara mmoja wa watu ambaye anaonekana kuwa mtumiaji aliyekubuhu wa dawa hizo anatutahadharisha kwamba  tuwe makini kwani wakati mwingine tunaweza kuuziwa dawa ambazo si ‘kokaine au heroin.’

Tunapohoji ni dawa zipi ambazo zinaweza kuwa za kuchakachua, anatueleza kuwa, wakati mwingine wauzaji husaga mchanganyiko wa tembe za valium, fenegan, hamoxylin au piliton na kuziuza kama dawa za kulevya!.

“Wanachanganya na kusaga hizo dawa na wakikupa kama huujui unga halisi … utaingia mkenge, lakini unapata ‘stimu’ (unalewa) kama kawaida,” anasema.

Kazi nyingine
Katika nyumba hii si uuzaji wa dawa za kulevya pekee unaofanyika, bali pia zinafanyika shughuli za upakiaji na ufungaji wake tayari kwa kuuza.

Chanzo chetu cha habari  kinaeleza kuwa, kila mara mzigo unapowasili,  wapo vibarua ambao hutumiwa kufunga na kwamba wafungaji hawa mara nyingi ni watumiaji. 

Anabainisha kuwa mfungaji hulipwa Sh200,000 kwa kufunga kete 50 na Sh400,000 kwa wanaoweza kufunga kete 100 za dawa hizo.

“Kufunga kwake ni kazi, ndiyo maana wanalipa bei ndefu (kubwa), kwa sababu, ule unga hauji kama unga, bali huja kama donge, kwa hiyo unatakiwa ulisage ili uuingize katika pakiti zake,” kilisema chanzo hicho.

Alisema, kuweka unga katika pakiti 50, huweza kumchukua zaidi ya saa sita.  Chanzo hiki, bila kufahamu kinazungumza na nani, kilitoboa kuwa:
“Juzi nilitumwa nipeleke mzigo wa zaidi ya milioni sita kwa mzee anayeishi Mbezi, nilienda kwa pikipiki, nikalipwa laki moja na nusu,” alisema.

 Akifafanua ni kwa namna gani yeye anaepuka kutumia dawa hizo, hasa wakati wa ufungashaji, alisema, huvaa gloves na kuufunika uso wake kwa kitambaa ili unga usiingie puani mwake.

Kikosi kazi Manyanya
Mwananchi lilibaini kuwa, kikosi kazi chenye mtandao mkubwa hufanya kazi katika kituo cha basi cha Manyanya kinachotumiwa na mabasi yanayoelekea Posta mpya.

Katika baadhi ya vibaraza vya maduka ya eneo hili, ndimo wanamoketi wauzaji. Ni vigumu kuwagundua wauzaji, lakini wanunuzi au watumiaji wanaonekana kwa macho kutokana na kulewa. 

Kituo cha daladala cha Manyanya, kina idadi kubwa ya walioathirika na dawa hizi pengine kuliko kituo chochote hapa Dar es Salaam.

Utafiti wa Mwananchi ulibaini kuwa, baadhi ya maduka yaliyo pembezoni mwa kituo hiki ndimo zinapohifadhiwa dawa hizo. Ilibainika kuwa, dawa hizo huhifadhiwa katika maduka hayo, ili kurahisisha ununuzi kwa watumiaji.

Chanzo kingine kilibainisha kuwa: “Hapa wanafika watu wengi. Usifikiri wanakuja hawa wapiga debe tu. Hata wazee wenye heshima zao na magari yao, akina mama wenye familia, na watu wenye hadhi katika jamii,”  anasema.

Wakati akieleza hayo, anatokea mwanamke wa makamo, anashuka katika gari. Chanzo chetu kinatupasha kuwa, huyo naye ni mtumiaji na aliwahi kuwa mke wa raia wa Uingereza.

Mwananchi liliendelea kuangaza na kuwaona baadhi ya vijana wakisaga dawa hizo kwa kutumia moto, vibati na kigae. Wengine wakiuvuta katika sigara na baadhi, wakinusa katika karatasi. 

Aina mpya ya uvutaji 
Mtoa habari mwingine aliliambia  Mwananchi juu ya uvutaji mpya wa dawa za kulevya, ambao pengine waweza kuwa ni wa hatari zaidi kiafya.

Alisema, mtumiaji huchukua chupa tupu ya maji, kisha hujaza maji aidha nusu au robo ya chupa ile kisha hutumbukiza unga ndani ya maji yale.

Baada ya hapo, huchukua bomba la kalamu na kutoboa chupa, juu kidogo ya yalipoishia maji.Karatasi la foili au nailoni hufungwa katika mdomo wa chupa,  bomba jingine la kalamu huchomekwa juu ya foili au nailoni.

“Ukimaliza unachoma moto bomba la kalamu, moto ukishika kasi na  moshi ukianza kuingia ndani ya chupa, unavuta kwa kupitia bomba la chini,” alisema. Aliutaja mtindo huo kuwa unaitwa "wa kidosi/kitajiri' na wanaovuta dawa za kulevya kwa mtindo huo, hulewa kiasi cha kutojitambua na hujisaidia haja kubwa na ndogo.

“Siku hizi watu hawajichomi sindano, wanatumia njia hiyo, kunusa au kulamba,” alisema na kuongeza: "Huu mtindo unaleta raha ya ajabu, kiasi kwamba mtumiaji huweza kutumia hadi Sh 100,000 kwa siku moja tu."

Halikadhalika chanzo hicho kilikubali kutuuzia kete za dawa za kulevya kwa kutuahidi kutuletea hadi tulipoahidiana kukutana.
Wamiliki wa nyumba 
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, mwenye nyumba hiyo alifariki miaka ya 80, aliacha wake wawili na watoto tisa, ingawa baadha wamekwishafariki. 

 “Mke mmoja wa yule mzee amefariki, lakini mwingine sijui habari zake,” kilisema chanzo hicho. Chanzo hicho kiliongeza kuwa, baada ya mzee huyo kufariki, nyumba hiyo ilibaki mikononi mwa watoto hao.

Miaka ya 90 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, watoto hawa  walijikita zaidi katika biashara ya pombe haramu ya gongo, baadaye bangi.Chanzo hicho kiliongeza kuwa, baadaye waliamua kuachana na uuzaji wa pombe na wakahamia katika uuzaji wa dawa za kulevya pamoja na bangi.

“Kaka yao mkubwa mwanzoni alikuwa analetewa kama msambazaji  na kisha kuwauzia mateja, lakini baadaye akaanza kusafiri yeye mwenyewe,” kilisema chanzo hicho. Vyanzo hivyo vilidai kuwa, ndugu wote zaidi ya 10, wanafanya biashara hiyo, wakiwa na familia zao, na baadhi wakiwa ni watumiaji wakubwa.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Minazini, Juma Katogolo alikiri kuifahamu nyumba na familia hiyo ingawa alikana kufahamu biashara hiyo.

"Ninawafahamu, baadhi yao nimesoma nao, kwa mfano, huyo kijana mkubwa, (anamtaja jina) nimesoma naye darasa moja, lakini kujua biashara wanayofanya, siwezi kuthibitisha hilo," alisema Katogolo.

"Unajua hizi biashara hufanyika kwa usiri wa hali ya juu, siwezi kusema nina uhakika na hilo." Katogolo alisema amekuwa hapandezwi na tabia na vitendo vya vijana wa Wilaya ya Kinondoni kujitumbukiza katika utumiaji wa dawa hizo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyella alisema hana taarifa na nyumba hiyo, isipokuwa polisi imekuwa ikifuatilia na kukamata dawa za kulevya kila siku.

“Ni ngumu kusema naifahamu nyumba hiyo lakini nisema tu kwamba Kinondoni kuwa sehemu ya jiji la Dar es 
Salaam, tatizo la dawa za kulevya lipo kwa kuasi kikubwa,” alisema Kenyella.

Kamanda huyo aliendelea kueleza:”Polisi imekuwa ikifanya uchunguzi wake wa kiintelijensia na kwa kutumia msako wa kawaida na kufanikiwa kukamata aina mbalimbali za dawa kila siku.”Cocaine, “Tumekuwa tukikamata bangi, mirungi, heroine na cocaine kwa nyakati tofauti na kuzipeleka kesi hizo mahakamani.”

Hata hivyo Kamanda Kenyella alisema jitihada hizo zinarudishwa nyuma na baadhi ya watu ambao hawataki kushirikiana na polisi katika kuwafichua wahalifu hao.

“Wito wangu kwa jamii ni kwamba mjenga nchi ni mwananchi na mharibu nchi ni mwananchi mwenyewe. Naomba watu watusaidie kupata taarifa na sisi polisi tumekula viapo, tutazifanya taarifa hizo kuwa siri kabisa,” alisema

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget