HOJA YANGU
Mkuu wa Usalama wa Taifa ang’oke
Lula wa Ndali MwananzelaToleo la 282
20 Feb 2013
KWA muda mrefu sasa nimekuwa nikiandika masuala ya usalama na jinsi gani ipo haja ya haraka ya mabadiliko ya muundo wa baadhi ya vyombo vyetu vya usalama. Leo naomba nizungumzie Idara ya Usalama wa Taifa na kwa nini ninaamini ndicho kiungo kinachokosekana (missing link) katika harakati za kupambana na vitendo vya uhalifu wa aina mbalimbali na hasa huu wa siku hizi wa utekaji nyara na mauaji yenye mwelekeo wa kidini au kisiasa.
Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa sasa hivi na tangu Kikwete aingie ni Bw. Rashid Othman. Kuingia kwake kwenye idara ilichukuliwa na baadhi yetu kama ‘asante’ ya Kikwete kwa Rashid Othman (maarufu kama RO) kutokana na urafiki wao wa karibu hasa wakati Kikwete akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na RO akiwa Ubalozi wetu pale London, Uingereza.
Kupewa Ukurugenzi kulikuja kama habari ya kushangaza kwa wakongwe wa idara hiyo.
Tangu kuingia kwake kwenye idara, mojawapo ya mambo ambayo yameonekana kuendelea ni ile hali ya mgawanyiko wa ndani ya idara ambao kwa kweli ulifikia pabaya sana wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010.
Lakini siyo kugawanyika kwa kawaida tulikoona bali ni kugawanyika ambako ndani yake imeingizwa siasa na hata kufanya wanasiasa wahusishwe na usalama wa taifa.
Lakini mambo makubwa matatu yametokea na ambayo kwenye nchi nyingine yenye kujali usalama wa taifa, Mkurugenzi wake angekuwa ameshang’oka. Mauaji ya albino, utoroshwaji wa wanyama kwenda Qatar na mauaji ya kidini na kisiasa. Mambo haya matatu ninaamini yanatosha kabisa kufanya Bw. Othman aamue mwenyewe kuondoka au afukuzwe kazi.
Mauaji ya albino
Mojawapo ya mambo ambayo sikumbuki kama yamewahi kutokea kabla ni mauaji ya Watanzania wenye upungufu wa rangi ya ngozi (maalbino).
Ndani ya mwaka mmoja hivi tulishuhudia watu zaidi ya arobaini wakiuawa, viungo vyao vikinyofolewa na wengine wakibakia na vilema vya maisha. Sasa hili liliendelea hadi Waziri Mkuu akalia bungeni kwa uchungu.
Lakini liliendelea hivyo kwa kiasi kikubwa na kufichua mojawapo ya udhaifu mkubwa wa Usalama wa Taifa chini ya RO – kukosekana kwa watoa taarifa za siri (informants) kwenye ngazi za chini kabisa.
Kwa wanaokumbuka usalama wa taifa wakati wa Nyerere watakumbuka jinsi ambavyo kila Mtanzania alikuwaa najiona kuwa ana sehemu katika kulinda taifa. Wenyewe tulikuwa tunajivuna – kwa stori za kweli na uongo – kuwa makaburu walijaribu mara kadhaa kujipenyeza nchini (infiltrate) lakini mara zote walishindwa. Walijaribu kwenye kambi za jeshi na kote walishindwa kwa sababu maafisa wetu wa usalama walikuwa wameenea kila sehemu.
Hili lilikuwa kweli hata kwenye ofisi na shule mbalimbali ambapo kulikuwa na mtandao mkubwa sana wa mawakala wa Usalama wa Taifa ambao walikuwa wanafuatilia mambo na walikuwa wameingizwa humo kwa umakini mkubwa. Sasa mauaji ya Albino ambayo yamerudi tena huku matukio matatu yakiwa yametokea kabla ya mwezi wa pili haujaisha yamefichua upungufu huo wa Usalama wataifa.
Utoroshwaji wanyama kwenda Qatar
Mojawapo ya kashfa za ajabu sana za utawala wa Kikwete ni hili lililotokea miaka kama miwili nyuma ambapo ndege ya kijeshi ya Qatar ikiwa na watu wenye pasi za Kibalozi iliweza kuingia nchini na kutua KIA na baadaye kuweza kuondoka na wanyama hao bila vyombo vyetu vya usalama kujua.
Inashangaza kuwa uwanja wa kimataifa kama KIA hauna maafisa wa usalama wa taifa ambao wangeweza kuzuia ndege hiyo kuondoka.
Lakini wanyama waliondoka na Qatar imekataa kuwarudisha na nina uhakika kuna watu humu humu kwenye serikali yetu waliopewa walichopewa na sasa wako kimya. Rashind Othman alipaswa kujiuzulu wakati ule ule. Unaweza vipi kuongoza usalama wa taifa na kuacha jeshi la nchi nyingine linaweza kuingia nchini? Na pamoja na RO bila ya shaka Mkuu wa Usalama wa JWTZ naye angepanguliwa!
Mauaji ya kisiasa na kidini
Lakini kubwa zaidi na ambalo naamini linatosha zaidi kumfanya RO kuondolewa na TISS kufumuliwa ni matukio ya utekaji nyara, mashambulizi dhidi ya watu mbalimbali na mauaji ya kisiasa.
Tumeshuhudia vurugu za ajabu kwenye chaguzi zetu huku wanasiasa wakipanda majukwaani na bastola lakini bado wakaendelea kuwa wanasiasa; tumeshuhudia watu wakiuawa katika chaguzi ndogo lakini usalama wa taifa unashindwa kufanya kazi vizuri.
Lakini hakuna kushindwa kubaya kama matukio ya mashambulizi dhidi ya viongozi wa kidini huko Zanzibar na hata usambazaji wa “vipeperushi” vya uchochezi.
Inashangaza sana kuwa Zanzibar kuna vipeperushi vya kichochezi kwa miaka sasa na TISS wameshindwa kujua vinachapwa wapi, na ni nani na vinasafirishwa vipi. Inashangaza (na kuudhi kwa wakati mmoja) kuwa idara ambayo Othman anaiongoza imeshindwa kuwapatia polisi taarifa za wahusika hawa.
Kwenye eneo dogo kama Zanzibar inawezekana vipi watu wakafanya mambo, kuyapanga na kuyafanikisha bila kuweza kugundulika? Marekani taifa kubwa sana duniani liliweza kumpata Osama Bin Laden miaka kama kumi hivi tangu ianze kumsaka; lakini haikufanya hivyo kwa kuombea na kusubiria bali kwa kuwekeza katika kutafuta taarifa.
Kweli idara hii ambayo inajitegemea mno (haiku chini ya Katibu Mkuu Kiongozi) inashindwa kukusanya taarifa namna hii?
Sasa hadi nani auawe ndipo watawataka hawa watu wawajibishwe? Hofu yangu ni kuwa kwa kadiri hali ya mgongano wa kisiasa inavyoendelea na kwa kadiri tunavyoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015 uwezekano wa mauaji zaidi ya kisiasa na kidini unaongezeka.
Hofu yangu ni kuwa tusipoangalia mwaka huu huu tutashuhudia siyo mauaji ya mapadre tu na wachungaji bali tunaweza kushuhudia mauaji ya wanasiasa maarufu. Siwezi kushangaa wala sitoshtuka.
Idara inahitaji mabadiliko na inahitaji mabadiliko ya kiuongozi, kifikra, kimtazamo na mwelekeo. Na mabadiliko hayo yataanza baada ya kuondolewa kwa Rashid Othman na uongozi wake na pamoja na hilo kufanyia mabadiliko makubwa Sheria ya Usalama wa Taifa ya 1996. Lakini kama analindwa ataondoka vipi?
0 comments:
Post a Comment