JUMAMOSI Februari 2 mwaka huu itabaki katika kumbukumbu zangu kwa muda mrefu, pengine katika uhai wangu wote.
Majira ya saa 3 asubuhi nilikurupushwa usingizini na kelele za mlango uliokuwa ukigongwa kwa nguvu. Wakati ninajiandaa kwenda kufungua mlango, nikasikia sauti yenye dharura ikisema, “bwana Chahali, polisi hapa, tafadhali fungua mlango.”
Nilichanganyikiwa kwani tangu nifike nchi hii zaidi ya miaka 10 iliyopita sijawahi kufanya kosa lolote au kukwaruzana na vyombo vya dola/sheria.
Baada ya kufungua mlango, askari waliovalia kiraia walijitambulisha na kuonyesha vitambulisho vyao. Pia walinisihi kuwa nisiwe na hofu ya kudhani kwamba nimefanya kosa lolote.
Kwa kifupi, walinieleza kuwa wamepewa ujumbe kutoka moja ya taasisi za intelijensia za hapa kuwa kuna tishio la uhakika dhidi ya maisha yangu. Hata hivyo, walieleza kuwa kwa vile wao walipewa tu ujumbe huo na kutakiwa kuuwasilisha kwangu, hawakuwa na maelezo ya ziada. Walisisitiza kuwa nichukue tahadhari muhimu na kunipa maelekezo ya mawasiliano ya dharura.
Kwa vile nilikurupushwa usingizini, awali taarifa hiyo ilionekana kama ndoto iliyokuwa inaendelea hata baada ya kutoka usingizini. Ilinichukua takriban saa tatu kuzinduka kutoka katika mshituko huo, na kutambua uzito wa taarifa niliyopewa na polisi hao.
Nikaamua kwenda kituo kimoja cha polisi kupata ufafanuzi zaidi. Mara baada ya kujitambulisha, mazingira ya namna suala hilo lilivyokuwa likishughulikiwa kituoni hapo lilinipa picha kuwa jambo hilo lina uzito. Kwa kifupi, baada ya kitambo nilipewa ufafanuzi ambao haukutofautiana na maelezo niliyopewa awali na polisi walionitembelea katika makazi yangu.
Kikubwa ni kuwa taarifa hiyo ilionyesha kuwa tishio hilo dhidi ya maisha yangu linatokea huko nyumbani. Swali linaloendelea kunisumbua kichwa ni KWA NINI iwe hivyo.
Wakati si vigumu kwangu kuhisi wahusika wa mpango huo wa kijahili, napata shida kuelewa kwanini wahusika hao watumie fedha za walipakodi kuandaa operesheni ya kutaka kunidhuru ilhali ninaamini kwa asilimia 100 kuwa mimi si tishio kwa usalama wa Taifa letu.
Ndiyo, baadhi ya ninayoandika kwenye makala zangu na tweets zangu huko kwenye mtandao wa kijamii wa twitter yanaweza kuwachukiza baadhi ya watu, lakini kwa hakika kuchukizwa huko si sababu ya kutaka kunidhuru.
Hadi wakati ninaandika makala hii nimekuwa nikiishi kwa tahadhari kubwa. Faraja kubwa kwangu inatokana na sababu tatu za msingi. Kwanza, kwa vile nilizaliwa na kukulia katika familia inayomtanguliza Mungu katika kila jambo, nina imani kubwa kuwa mamlaka pekee kuhusu uhai wangu (yaani kuwa hai au kufa) ni Mungu pekee. Hakuna mwanadamu anayeweza kupora jukumu hilo la Mungu na kufanikiwa kufupisha uhai wa yeyote.
Pili, nina imani kubwa na taasisi za usalama za hapa Uingereza. Kimsingi, wenzetu hawa wanathamini sana usalama na uhai wa binadamu pasi kujali mhusika ni mzaliwa wa hapa au ni ‘mgeni’ kama mimi. Ushauri na sapoti ninayoendelea kupata inanipa matumaini makubwa kuwa nipo kwenye ‘mikono salama.’
Lakini tatu ni ukweli kwamba takriban miaka mitano sasa nimekuwa nikiishi na uelewa kwamba kuna baadhi ya watu huko nyumbani wanaoniona kama kimelea cha maradhi hatari ambacho kikiachwa bila kudhibitiwa kitazua balaa.
Kwa sababu hiyo, tangu wakati huo nimekuwa nikiishi kwa tahadhari japo si kubwa kama hii ninayolazimika kuichukua sasa. Lakini ili uweze kuchukua tahadhari ni lazima uwe na mbinu na ujuzi wa kuchukua tahadhari husika. Kwa bahati nzuri, watu hao wanafahamu fika kuwa nina ujuzi wa kutosha na kuelewa na kumudu fika mbinu za kuishi kwa tahadhari.
Hata hivyo, kumudu mbinu ni suala moja na kuishi kwa kutumia mbinu hizo ni kitu kingine. Si jambo la kupendeza hata kidogo kuishi ukiwa na uelewa kuwa siku moja, mahala fulani unaweza kukumbana na madhara fulani. Lakini kadri unavyolazimika kuishi kwa namna hiyo inakuwa kama sehemu muhimu ya maisha yako, na ndivyo ilivyo kwangu.
Pamoja na kuchukulia kwa uzito taarifa hizo za tishio dhidi ya uhai wangu, nimechukua hatua nyingine kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwafahamisha watu ninaohisi kuwa ndio wahusika wa mpango huo dhalimu kwamba ni ukosefu wa busara wa hali ya juu kupoteza fedha za walipa kodi kutaka kunidhuru.
Ingekuwa vema raslimali zinazotumika kufanikisha mpango huo zikaelekezwa kwenye uchunguzi wa mabilioni ya fedha za Watanzania yaliyofichwa kwenye mabenki nchini Uswisi huku nchi yetu ikikabiliwa na deni kubwa la ndani na nje la zaidi ya shilingi trilioni 30!
Licha ya kuwa na mwangaza kuhusu mahala linakoanzia tishio hilo kutoka huko nyumbani, sina hakika kama ni mkakati wa kitaasisi au ndiyo yaleyale niliyowahi kuandika katika makala yangu moja huko nyuma juu ya kuwapo kwa rogue elementskatika taasisi zetu nyeti.
La muhimu kwangu kwa sasa ni kuhakikisha kuwa majahili hao hawafanikiwi katika azma yao. Pia sioni haja ya kuvifahamisha rasmi vyombo vya dola huko nyumbani. Itoshe tu kusema hapa kwamba mipango kama hii katika zama hizi haina tena tija.
Hakika suala hili limenikera sana lakini ninajitahidi kuzingatia busara za mwandishi wa Laws of Power, Robert Greene, ambapo kanuni ya 21 inausia kuwa “Play a Sucker to Catch a Sucker – Seem Dumber than your Mark” (yaani, kwa tafsiri isiyo rasmi, jifanye mjinga kumnasa mjinga).
Kanuni hii inasema, ninanukuu, “No one likes feeling stupider than the next persons. The trick, is to make your victims feel smart – and not just smart, but smarter than you are. Once convinced of this, they will never suspect that you may have ulterior motives” (hakuna mtu anayependa kuonekana mpumbavu zaidi ya mtu mwingine. Ujanja ni kumfanya mlengwa wako ajione mwerevu, na si mwerevu tu bali mwerevu zaidi yako. Pindi akaamini hivyo, hatohisi kuwa una nia kubwa zaidi yake).
Nimalizie makala hii kwa kusisitiza kuwa vitisho kama hivi kamwe havitonizuwia kusimamia ukweli na kuuhubiri pasi kumhofia mtu au taasisi.
Ninatambua yaliyowakumba baadhi ya waandishi wa habari wa nyumbani.
Kwangu hizo ni chachu za kuendeleza walichoanzisha.
Kadhalika, ni vema walioandaa mpango huo dhalimu wakatambua kuwa licha ya kitendo hicho kuwa na uwezekano wa kuharibu ‘mahusiano ya kiusalama’ kati ya nchi yetu na Uingereza (kwa kuwatwisha mzigo usio wa lazima kuhakikisha mimi kama mkazi wa nchi hii sidhuriwi), lakini pia kinakwaza kiapo changu cha utii kwa nchi yangu (nilipokuwa mtumishi wa umma) ‘kuyaacha mambo fulani yaendelee kubaki yasiyopaswa kuongelewa hadharani.’ Laws of Power ya 19 inasisitiza, “Never offend a wrong person” (kamwe usimkorofishe mtu asiyestahili).
"If you're not ready to die for it, take the word 'freedom' out of your vocabulary" ~ Malcom X
Ni habari ya kutisha kweli jamani..pole sana kakangu Mungu atakulind na hao watu watashindwa ...
ReplyDelete