DANADANA KUHUSU SUALA LA RICHMOND IMEZIDI KUENDELEA.BINAFSI SIDHANI KAMA SUALA HILI LITAPATIWA UFUMBUZI UNAOSUBIRIWA NA WATANZANIA WENGI.KUPATA UFUMBUZI,KWA MAANA YA KUWEKWA BAYANA UKWELI WA UTAPELI NA UJAMBAZI HUO UTAMAANISHA WATU MUHIMU KUPOTEZA NYADHIFA ZAO.SIO KWAMBA HILO NI BAYA BALI HALIWEZEKANI KATIKA MAZINGIRA YA SIASA ZETU ZA KUJIKOMBA,KUOGOPANA NA BORA LIENDE.
PENGINE HII NI SABABU NYINGINE MUHIMU KWA WAPIGAKURA KUIHOJI CCM COME THE 2010 ELECTION.HEBU SOMA KWANZA HAPA CHINI:
Mazingaombwe tupu Richmond
• Shellukindo anuna, akataa kuulizwa maswali
na Deogratius Temba
KWA mara nyingine tena, serikali jana ilishindwa kuwasilisha maelezo ya utekelezaji wa maazimio 23 ya Bunge kuhusu hatma ya kashfa ya Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Licha ya kauli thabiti iliyotolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, William Shellukindo mwanzoni mwa wiki kwa waandishi wa habari kuwa, serikali ingetoa maelezo hayo kwa kamati yake jana, hali ilikuwa tofauti baada ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kutotokea katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, ambako kamati mbalimbali za Bunge zinaendelea na vikao vyake.
Kwa mujibu wa ratiba mpya ya vikao vya kamati hiyo vinavyoendelea katika ofisi hizo, jana kamati ilipanga kupokea taarifa hiyo na kuanza kuijadili kwa muda wa siku mbili, baada ya wiki iliyopita kuahirishwa kwa kile kilichoelezwa kuwa Waziri Ngeleja alikuwa nje ya nchi.
Habari ambazo Tanzania Daima Jumatano lilizipata kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini zilieleza kuwa, walipokea ombi la serikali la kuahirishwa kwa mjadala huo ili ijipange sawasawa.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alieleza kuwa, serikali katika ombi lake kwa kamati, iliitaka kuliweka suala hilo pembeni hadi baadaye itakapoarifiwa, na ilitaka kuendelea na ratiba zake nyingine kama zilivyopangwa.
“Ni kweli leo (jana) tulikuwa tuipokee taarifa ya serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge, lakini haya ni masuala yanayoihusu serikali zaidi, wameomba tuendelee na kazi nyingine, wanaweza kuiwasilisha kesho (leo) au keshokutwa (kesho),” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliyeomba jina lake lisitajwe kwa sababu si msemaji.
Alieleza zaidi maelezo kamili ya kuahirishwa kwa upokeaji maelezo ya serikali yanaweza kutolewa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Shellukindo, ambaye ndiye aliyepokea ombi hilo la serikali.
Shellukindo alipoulizwa kuhusu hali hiyo, aligeuka mbogo kwa waandishi wa habari kwa kuwataka wasimuulize maswali kuhusu Richmond. Kwa ukali aliwataka waulize maswali yanayohusiana na kampuni ya kuzalisha umeme wa gesi ya Songas, ambayo ilikuwa ikijadiliwa na kamati yake jana.
“Nataka kuwaeleza tulichozungumza na watu wa Songas, lakini nikimaliza nitakaribisha maswali ambayo yatahusiana tu na suala hili la Songas, nje ya hapo sitajibu,” alisema Shellukindo.
Msimamo huo wa Shellukindo uliwafanya waandishi wa habari waliokuwa na shauku ya kutaka kujua sababu za serikali kushindwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji maazimio ya Bunge ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na watu wengi, kushikwa na butwaa na kushindwa kuuliza maswali kwa muda.
Baada ya dakika chake, Shellukindo ambaye alionekana kutokuwa katika hali ya kawaida, alieleza kuwa kamati yake imezungumza na uongozi wa Kampuni ya Songas kuhusu utengenezaji wa mashine ya kuzalisha umeme wa megawati 20 iliyoharibika wiki iliyopita na upatikanaji wa gesi nchini.
Hata hivyo katika hali ambayo haikutarajiwa na waandishi wa habari, wakati Shellukindo akiendelea kutoa maelezo, wajumbe wa kamati walianza kusimama mmoja mmoja na kuondoka na walipoulizwa sababu ya kuondoka katika kikao hicho, walidai kuwa wana majukumu mengi ya kufanya.
Kabla ya Shellukindo kuanza kuongea na waandishi wa habari, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye ni kinara wa kashfa hiyo, alisimama na kutoka nje. Mwakyembe amekuwa hazungumzi lolote na waandishi tangu kuanza kwa vikao vya kamati hiyo.
Awali Tanzania Daima Jumatano lilielezwa kuwa, taarifa hiyo haitawasilishwa kwa kamati hiyo ikiwa jijini Dar es Salaam kwa sababu za kiusalama na badala yake itawasilishwa mjini Dodoma.
Taarifa hizo zilieleza kuwa, wajumbe wa kamati ya Shellukindo watapata nafasi ya kuijadili wakiwa Dodoma na endapo watairidhia wataruhusu serikali iiwasilishe bungeni katika mkutano wa 17, utakaokuwa ukiendelea. Mkutano huo unatarajiwa kuanza Oktoba 27.
Taarifa nyingine zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa, serikali ina hofu kuwa, iwapo itaitoa taarifa hiyo kwa kamati ya Shellukindo mapema, inaweza kuvuja na kutoa mwanya kwa baadhi ya watuhumiwa wa Richmond kujipanga namna ya kujisafisha au kupoteza baadhi ya vielelezo.
Mmoja wa viongozi wa serikali aliyezungumza na gazeti hili katika eneo la ofisi ndogo za Bunge jana, alisema serikali imekuwa ikisita kuiwasilisha taarifa yake kwa kamati hiyo kwa sababu inaweza kuvuja na kuvuruga mwenendo wa mambo.
“Hofu yetu ni kwamba, serikali ikiwasilisha taarifa hii mapema, hadi kufikia siku ya kuijadili bungeni itakuwa imezagaa mno, taarifa kuenea si jambo jema, watuhumiwa wanaweza kujipanga, inatakiwa iwe ya kushtukizia,” alisema ofisa huyo.
Katika mjadala huo uliokamiwa na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, wajumbe pamoja na mambo mengine wataangalia kama serikali imejibu maswali na maagizo ambayo Bunge liliipa serikali.
Wakati Bunge likitaka watu zaidi waliohusika wawajibishwe, tayari mmoja wa wawakilishi wa Kampuni ya Richmond, Naeem Adam Gire, ameshafikishwa katika Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam Januari 13, mwaka huu na kusomewa mashtaka matano ya makosa ya jinai.
CHANZO: Tanzania Daima
MAAMUZI YA KUIPA TENDA RICHMOND HAYAKUFANYIKA KWENYE KIJIWE CHA KAHAWA BALI KWENYE OFISI NYETI.SASA KWANINI KILA ALIYEHUSIKA KWENYE MAAMUZI HAYO ASIWEKWE HADHARANI?JIBU JEPESI NI KWAMBA KUFANYA HIVYO KUNAWEZA KUPELEKEA "KUISOGEZA 2010 KABLA YA MUDA WAKE" (READ BETWEEN THE LINES,PLZ).
Ndugu Evarist,
ReplyDeleteMimi nimesoma katikati ya mstari. Nakubaliana na wewe kwamba hii skandali kufikia mwisho wake, ni mpaka watu waamue kujilipua, kuamua liwalo na liwe almuradi mafisadi wasiachwe wakitamba watakavyo. Mambo haya yanaudhi na kukera isipokuwa kama tutakuwa tunaongozwa na ushabiki wa kijinga chama fulani kisiojulikana kinapindua nini mpaka leo.
Ukifuatilia kwa nidhamu suala hili, kuna maswali mengi ya kuudhi yanajitokeza. Kwanza kabisa mtu unajiuliza, ni kwa nini serikali inaonekana kunywea linapokuja suala la kuwashughulikia hawa mabwana ambao Bunge lilikubaliana kwa azimio rasmi kwamba wawajibishwe? Kwa nini inakuwa ngumu? Ni kwa nini serikali katika Bunge lililopita iliamua kutugeuzia kibao kwa kujaribu kuwasafisha wahalifu hawa? Hivi hii haimaanishi kwamba serikali nayo ina maslahi fuylani fulani katika uhalifu huu? Nasema hivyo kwa sababu haiingii kabisa akilini kwamba watu ambao IMETHIBITIKA kuwa wana hatia na kuitambua hatia hiyo kumefanyika kupitia vyombo vilivyopewa dhamana kama Bunge, bado wanaendelea kubembelezwa mpaka leo.
Inachekesha unaposikia eti leo wanapewa likizo ya kustaafu kwa raha zao kwa namna ambayo inaleta picha kwamba hilo limekuwa kwa mujibu wa mabadiliko ya kawaida ya ofisi.
Halafu kama hiyo haitoshi na kwa kwa kweli, kinacholeta wasiwasi zaidi, kila mpiga kelele anapojaribu kupaza sauti kuhusu ujambazi huu, maadamu anaonekana kuwa na nia ya kweli kweli kuwasulubishwa wahalifu hawa, wakubwa (kwa maana hasa ya ukubwa) wanafanya jitihada za kuwanyamazisha kwa mlango wa nyuma. Why? Kuna nini hapa tusichokijua?
Mimi nisingependa kuamini kwamba skandali hii iliasisiwa na wenye madaraka makubwa serikalini waliyoyapewa kama dhamana na wananchi ambao leo wanawadharau. Sipendi kuamini hivyo maana ikiwa hivyo, inatisha.
(Nashindwa kuelewa kwa nini watu wa ile ofisi ya magogoni mara zote wamejitokeza kukanusha habari ambazo hakuna aliayeziulizia. Nasisitiza sijui.)
Nashindwa kuelewa pia kwa nini wananchi hatuandamani tuambiwe nani hasa ni jambazi wa Richmond. Inaniwia vigumu kuelewa ni sababu ipi hasa inayotufumba macho kiasi cha kuwaacha watawala watuchezee kwa kiasi hiki.
Kama watu hawa waliotajwa na kamati teule ya Bunge hawana hatia (na ndivyo inavyotaka kuonekana kwa namna ambavyo tamthlia inavyoendelea) basi tuambiwe nani hasa yuko nyuma ya Richmond ambaye tunamwogopa sana kiasi kwamba akijulikana jua halitachomoza alfajiri ya pili yake? Maana kwa jinsi mwenendo wa mambo ulivyo, mtu anaweza kushawishika kwmaba siku mambo yakijulikana kwa ukamilifu wake, tunaweza kufa kwa kihoro.
Nashauri jambo moja hapa. Kwa kuwa chama chenye serikali kimeendelea kutuzunguka mchana kweupe, kwa kuwakumbatia wahalifu wa kila skandali la ufisadi tulilowahi kulisikia; na kwa kuwa chama hiki kimeonekana kinajitahidi kuwatisha wawakilishi wetu wanaotusemea kuhusu ujambazi huu wa kuchefua wasiokubaliana na mwenendo wa chama chao; na kwa kuwa chama hiki ndicho kilichounda serikali ambayo haitaki kabisa kushughulikia hata vivuli vya mafisadi ambao inawakumbatia kwa lazima; na kwa kuwa uwezo tuliobaki nao ni kuwakataa kupitia sanduku la kura; basi watanzania tuna kila sababu ya kukipindua chama hiki kilichochoka na kulewa madaraka kwa njia za kistaarabu za kupiga kura zetu kwa bidii ifikapo 2010 (kama haitatokea basi uchaguzi ukawahishwa kabla.)