MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge jana alinguruma ndani ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, alipowataka Watanzania kuacha kutafuta mchawi aliyeua mashirika ya umma, akisema kuwa mengi yalikufa yakiwa mikononi mwao na si mwa wageni.
Chenge, mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali, ametoa kauli hiyo wakati wananchi wengi wakilalamikia mikataba mibovu ya uwekezaji na uendeshaji mashirika ya umma kuwa ndiyo iliyochangia baadhi kufa na mengine kuwa katika hali mbaya.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati akichangia Taarifa ya Utekelezaji wa Moboresho ya Shirika la Bima (NIC), Chenge alisema makaburi mengi ya mashirika ya umma yamechimbwa na Watanzania wenyewe.
"Leo (jana) wakati tunamalizia kuadhimisha miaka kumi ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, shirika hili la Bima lilikuwa moja ya malengo yake," alisema Chenge akirejea NIC ambayo ilikua na kutapakaa nchi nzima kabla ya kuanguka kiuchumi kiasi cha kusababisha serikali kuingilia kati na kuitengenezea muundo mpya.
"Lakini shirika hili leo liko hoi; kwa vyovyote vile serikali haiwezi kusimamia shirika hili kwa asilimia 100, lazima likabidhiwe kwa sekta binafsi, lakini Watanzania tumekuwa ni watu wa kupenda kupiga kelele hasa tunapoamua kubinafsisha. Mashirika haya tumeyaua wenyewe wala si wageni."
Chenge alisema: "Watanzania hatupaswi kutafuta mchawi wa mashirika yetu haya. Sisi wenyewe ndiyo tumeyaua na makaburi mengi leo hii yanaonekana."
Alifafanua kwamba, umefika wakati sasa Watanzania wakaachana na dhana ya kulalamika na badala yake wafanye kazi kwa bidii, huku pia akiitaka serikali iondoe dhana ya kuendesha mashirika kijamaa, akitolea mfano uwekaji wa kiwango cha chini cha bei na kutaka bei ya soko ishike hatamu.
Hata hivyo, alionyesha wasiwasi na Kikosi Kazi kinachofanya marekebisho kutokana na kukosa bodi na kuongeza: "Napata shaka kidogo, chombo ambacho kinaandaa taarifa halafu chenyewe pia ndio kijitathmini, nafikiri inapaswa kuundwa bodi."
Akichangia katika kikao hicho cha Kamati ya Fedha na Uchumi, Mbunge wa Tabora Mjini, Juma Kaboyonga aliitaka serikali kuharakisha ununuzi wa nyumba za NIC ambazo thamani yake ni Sh31.7 bilioni.
Mbunge huyo ambaye kitaaluma ni mchumi alisema serikali haipaswi kucheza na NIC, hivyo ni lazima itafute fedha hizo ili kuliwezesha shirika kwenda kwa kasi zaidi.
Kaboyonga alidai kuwa kumekuwa na hujuma dhidi ya NIC na kuhoji kwamba "kama mashirika binafsi yanaweza, vipi NIC ya serikali ishindwe".
Alisema: "Ipo dhana kwamba mashirika ya serikali hayana wenyewe, lakini mimi nasema yana wenyewe na wenyewe ni wananchi, lazima NIC iangaliwe, iwezeshwe na ipewe mtaji."
Akijibu hoja mbalimbali, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Jeremia Sumari alisema serikali imepanga kuendeleza huduma nafuu na zenye ubora kutokana na kuamini NIC inaweza kujiendesha kwa faida zaidi.
Sumari alisema uamuzi huo wa serikali kupanga kutoa huduma bora na za gharama nafuu haumaanishi kuwa nchi inarejea kwenye ujamaa, bali ni kuangalia uwezo wa shirika na mahitaji ya Watanzania.
Kuhusu mtaji na mpango wa kununua nyumba za NIC kwa Sh31.7 bilioni, alisema hilo liko katika hatua nzuri na za mwisho na kuongeza: "Lakini hadi sasa nyumba hizi ni za serikali, kuna mahitaji ya nyumba kwa watumishi wetu kama waheshimiwa majaji n.k."
Dk Abdallah Kigoda, ambaye ni mwenyekiti wa kamati hiyo, alisema katika majumuisho yake kuwa kuna umuhimu wa serikali kulipatia shirika kiasi hicho cha fedha.
Alisema:" Sioni tatizo kwa serikali kutoa au kukopa Sh31.7 bilioni kuokoa shirika kubwa la umma kama hili, nafikiri kuna umuhimu wa kulipatia kiasi cha fedha kwa sasa."
NIC iko katika kipindi cha mageuzi baada ya kuwepo mvutano kati ya serikali na bunge, hasa tathmini ya mali ambayo awali ilikuwa Sh18 bilioni, lakini Kamati ya Fedha ikaikataa na kutaka ifanyike upya.
Tathmini mpya iliyoonyesha kuwa thamani ya mali za NIC ni Sh31.7 bilioni ilikubaliwa na mwezi Februari, Rais Jakaya Kikwete aliunda Kikosi Kazi kilicho chini ya Balozi Charles Mutalemwa kufanya mageuzi ya shirika hilo.
Hadi Februari wafanyakazi waliokuwa nje ya ajira wakati huo walilipwa malimbikizo ya mishahara yao kwa jumla ya Sh1.90 bilioni.
CHANZO: Mwananchi
MBONA MAMBO!?
0 comments:
Post a Comment