Hivi karibuni niliandika makala flani kuhusu milipuko ya mabomu huko Mbagala, jijini Dar es Salaam. Kwa kutambua kuwa blogu yangu haina idadi kubwa ya wasomaji (japo nawathamini sana wachache wanaotumia muda wao kuitembelea) niliamua kuisambaza makala hiyo kwa bloga wenzangu wawili ambao “nyumba” zao hupata “wageni” wa kutosha kila siku.
Kwa bahati mbaya, bloga hao waliamua kuiweka makala hiyo kapuni.Siwalaumu,kwa sababu kadhaa. Kwanza, blogu ni mali ya mmiliki, na hilo linampa haki ya kuchagua nini kiwepo kwenye blogu yake na nini kisiwepo.Pili, kila bloga ana mtazamo wake kuhusu mambo mbalimbali yanayotuzunguka, iwe siasa, dini au nyanja nyingine za maisha ya binadamu. Kwa maana hiyo, kama ataletewa makala inayokinzana na mtazamo huo, ana haki ya kuipuuza. Kuna sababu nyingine za kibinafsi lakini sidhani kama zina umuhimu sana.
Makala husika (isome hapa) haikuwa ya matusi, kashfa au utovu wa nidhamu kwa watawala japo ilikuwa ikizungumzia uzembe na kutowajibika kwa baadhi ya viongozi wetu unavyohusika na janga hilo la milipuko ya mabomu.Nilishauri katika makala hiyo kwamba wakati umefika kwa Watanzania kudai haki zao hasa pale zinapopuuzwa makusudi. Kwamba ripoti ya milipuko ya kwanza inaozea katika makabrasha ya Wizara husika, kisha mlipuko mwingine unatokea lakini hakuna anayewajibika, jambo linalohitaji shinikizo la kudai haki na uwajibikaji.
Naamini kwamba laiti makala hiyo ingechapishwa laiti ingekuwa ya kumsifia kiongozi flani au kukumbushia tarehe yake ya kuzaliwa. Au laiti ingekuwa ni tangazo binafsi. Yote hayo ni mazuri kwa vile ni huduma kwa umma. Hata hivyo, harakati tunazohangaika nazo wengine kuboresha future ya nchi yetu ni muhimu pia na hazipaswi kupuuzwa.
Ni rahisi kwangu kuhitimisha kwamba kinachokwanza makala za aina hiyo kuchapishwa ni uoga wa mabloga husika wakihofia kuwaudhi watawala. Japo huo ni uhuru wao kibinadamu, madhara yake kwa jamii ni makubwa kwa vile historia inaonyesha kwamba uoga ni kitalu mwafaka kwa ushamiri wa tawala dhalimu.
Lengo langu si kulaumu bali kushauriana.Kukimbilia kuweka picha za kiongozi akihutubia au akirejea Dar akiwa bukheri wa afya lakini kuchelea kujumuisha maelezo kwamba pia alikumbwa na dhahama ya kiafya ni kutowatendea haki wasomaji wetu. Hapa narejea tukio lililotokea jijini Mwanza hivi karibuni ambapo baadhi ya wenzetu walitonyesha “picha nzuri” za JK lakini “wakabania” maelezo kuhusu mkasa uliomkumba wa kushindwa kuendelea na hotuba yake katika kile kilichoelezwa kuwa “uchovu wa safari.”
Ushirikiano wetu jumuiya iliyojibebesha dhamana ya kuujulisha umma kuhusu mambo mbalimbali usiishie kwenye yanayopendeza machoni pekee bali pia yale yanayoudhi au kukera.
0 comments:
Post a Comment