WAKATI bajeti ya Serikali inasuasua kutokana na uhaba wa fedha za ndani, familia moja ya Dar es Salaam inayomiliki kampuni inayojihusisha na biashara ya bidhaa za nyumbani imejiingiza katika uwakala wa forodha kwa staili ya aina yake ikiwa ni pamoja na kujikita katika kuwasaidia wafanyabiashara wengine kukwepa kodi; huku wahusika wakijiwekea kinga kwa wanasiasa, Raia Mwema imeelezwa.
Biashara hiyo ya aina yake ya uwakala wa ukwepaji kodi, imeelezwa kuipotezea serikali mabilioni ya shilingi ambazo zilistahili kukusanywa kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali wanaoingiza bidhaa mbalimbali kutoka China na Dubai; huku baadhi ya wanasiasa wenye nguvu serikalini na familia zao wakiwa nyuma ya uhalifu huo.
Vyanzo vya habari ndani ya serikali vimelieleza Raia Mwema kwamba familia hiyo yenye vijana watatu wenye asili ya kiasia ilirithi biashara ya wazazi wao ya kuuza plastic carpets (mazulia ya plastiki), door mats (mikeka ya milangoni), taulo, mapazia na mashuka na baadaye kuamua kuingia katika “uwakala wa ukwepaji kodi”.
Habari za ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zimeeleza kwamba mamlaka hiyo imekuwa ikifuatilia kwa makini suala hilo pamoja na kuwapo taarifa za uhakika kwamba maofisa waandamizi wa mamlaka hiyo wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara hao kukwepa kodi.
Mbali ya kuwahusisha watumishi wazito ndani ya TRA, vijana hao wameelezwa kuingizwa katika orodha ya “wachangiaji wakubwa” wa Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kuwa karibu na wanasiasa binafsi ndani ya chama hicho tawala.
Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa maelezo kwamba hayuko katika nafasi ya kufahamu kila kitu kinachoendelea ndani ya mamlaka hiyo kwa nafasi yake kwa kuwa kila eneo linaongozwa na kamishna wake na “kwa suala hilo anayepaswa kuzungungumzia ni Kamishna wa Forodha.”
Pamoja na kuelezwa kwamba TRA wanazo taarifa za ukwepaji kodi huo na kwamba wamekwisha kuanza uchunguzi, Kitilya alisema: “hilo suala liko chini ya Kamishna wa Forodha na mwenzake Kamishna wa Uchunguzi ambao ndio wanapaswa kulitolea ufafanuzi.”
Raia Mwema ilipomweleza Kitilya kwamba habari za kampuni hiyo kukwepa kodi zimeshawahi kumfikia na ofisi yake kuzitolea maelekezo, alisema, “Ndio kwanza leo unanieleza kuhusu kampuni hiyo, mimi sina taarifa kabisa labda uwatafute Kamishna wa Forodha na wa uchunguzi.”
Hata hivyo, maofisa wa ndani ya TRA wamelieleza Raia Mwema kwamba wafanyabiashara hao vijana wakiongozwa na kaka yao (jina tunalihifadhi kwa sasa), walikuwa wakiagiza bidhaa hizo kutoka nje kupitia bandari ya Tanga kati ya mwaka 2000 hadi 2004 mahali ambako walianza kuwa “mawakala wa ukwepaji kodi”.
“Kutokana na kuzoeleka kwao kwa maofisa wa forodha katika bandari ya Tanga wakati huo, walianza pia kupokea nyaraka za waingizaji wengine wa mizigo tofauti, na kuwasaidia kuivusha kwenye ofisi za Forodha kwa njia za ujanja ujanja.
“Wakati huo hawakuwa na kampuni ya uwakala, walitumia kampuni mbalimbali za kukodi na kutokana na kukua kwa biashara yao na ‘uwakala wao pori’, walijizatiti wakaanzisha mtandao wa kazi kwa kunyoosha au kusafisha njia tangu mizigo inapotoka Tanga hadi kwa wateja Dar es Salaam,” anasema mtoa habari wetu ambaye anafahamu kwa kina mitandao ya ukwepaji kodi.
Imeelezwa kwamba katika ‘kusafisha njia’ walitumia fedha kujitambulisha kwa maofisa forodha na polisi waliokuwa barabarani kudhibiti magendo kwenye vituo muhimu vya udhibiti kama Segera na Kabuku mkoani Tanga; Chalinze na Kibaha mkoani Pwani na kuendelea hadi wakaguzi wengine ndani ya jiji la Dar es Salaam.
“Lakini mwaka 2004 hali ya hewa ya bandari ya Tanga ilibadilika kwa Idara ya Forodha kuziba mianya ya rushwa lakini kwa kuwa vijana hawa walikwisha kuzoea kudanganya katika ulipaji ushuru, ilibidi wahamishie shughuli zao kwingine. Wakaelekeza nguvu zao zote Holili, Kilimanjaro, wakifanya yaleyale waliyokuwa wakiyafanya bandarini Tanga,” anasema mtoa habari wetu.
Imeelezwa kwamba wafanyabiashara hao waliendelea kutoa mizigo Holili kwa muda kati ya mwaka 2004 na 2006 mwishoni walipohamia rasmi bandari ya Dar es Salaam ambako sasa wamekita mizizi.
“Mtandao wao wa Dar es Salaam ni mkubwa wakiwa wameteka mamlaka zote zinazohusika na kodi. Ni mtandao ulioenea kutoka Dar es Salaam hadi nje ya nchi. Zimefunguliwa ofisi Hong Kong na Guanzhou, China na Dubai. Ofisi za nje hutumika kupokea mizigo inayoingia nchini.
“Mwagizaji wa mali yoyote kama nguo, hardware au vifa vya umeme hufanya manunuzi kwenye maeneo hayo na hupewa gharama zote za kufikisha mzigo Dar es Salaam pamoja na ushuru wa forodha na gharama nyinginezo hadi kweye bohari yao iliyopo Dar es Salaam,” kinaeleza chanzo kingine ndani ya serikali.
Imeelezwa kwamba mwagizaji anakabidhi mzigo ofisini China na anakabidhiwa mali yake Dar es Salaam baada ya siku kadhaa kati ya wiki tano hadi sita.
Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini viwango vya gharama zao kwa baadhi ya mali ni kama ifuatavyo:
Kusafirisha na kutoa bandarini vifaa vya ujenzi hutoza Dola za Marekani 350.00 kwa meta moja ya ujazo(1 cbm).
Kusafirisha na kutoa bandarini bidhaa za nguo ni Dola za Marekani 450.00 kwa meta moja ya ujazo (1 cbm).
Kusafirisha na kutoa bandarini bidhaa za umeme kama swichi, circuit breakers na viginevyo ni usd Dola za Marekani 500.00 kwa meta moja ya ujazo (1 cbm).
Mizigo maalumu kama vitenge-mazungumzo hufanyika na bei maalumu hukubaliwa.
“Kinachotisha katika utaratibu huu ni kwamba wakati gharama za usafiri wa meli hupatikana kutegemea uzito na ujazo wa mali, wao wamefika mbali zaidi kwa kukadiria ushuru na kodi za Serikali kwa ujazo (yaani cubic measurements). Kwa kawaida ushuru wa forodha hutozwa kwenye Thamani halisi ya Manunuzi, Bima na Gharama za Usafiri hadi nchini (Cost, Insurane and Freight) na si vinginevyo,” anasema mtumishi mmoja wa TRA mwenye ufahamu wa biashara hiyo akidai kwamba biashara hiyo huwa na ulinzi wa ‘wakubwa’.
Ofisa huyo wa TRA ameendelea kwa kusema, “(wafanyabiashara hao vijana)... hutoza kwa kukadiria na kwa ajili hii wanapata faida kubwa kwa kuwa mfumo mzima umewabeba kuanzia mashirika kama Tiscan ambako nyaraka hupelekwa kuthamishwa (jukumu walilopewa Tiscan kwa mujibu wa mkataba na TRA) hadi bandarini ambako mizigo huruhusiwa kutoka baada ya taratibu zote kukamilika.”
Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kwamba waagizaji wanaopitia mkondo wa vijana hao wamekuwa wakishangaa jinsi mizigo yao inavyoweza kutolewa bandarini bila wao kudaiwa ankara za manunuzi (invoices) wanazokabidhi katika ofisi za China na Dubai.
Wanachoulizwa China na Dubai ni orodha ya mali (packing list) jambo linaloashiria uhalifu wa kutisha kutokana na kudhihirika kwamba ankara za mizigo zinazopelekwa Idara ya Forodha ni za kughushi na hazina uhalisi wowote.
“Kwa kawaida mali au mizigo ya thamani ya manunuzi ya Dola za Marekani 10,000.00 na zaidi (FOB Cost) huwa inauliziwa bei na ubora wake kwenye nchi ilikotoka. Kwa hiyo kwa mteja anayepata huduma kwa hawa watu, nyaraka zake zikifikishwa Tiscan ambayo ni kampuni tanzu ya Cotecna International, wanaulizia kwenye hiyo nchi iliyouza mali hiyo kuja kwetu! Kwa vile hawa watu wamesajili kampuni China na Dubai na nyaraka (invoices) wamezitoa wao, hivyo Tiscan inapata majibu kutoka kwa watu walewale. Mapato ya Serikali yanahujimiwa kuanzia hapa,” anasema ofisa mwingine wa serikali ambaye amewahi kukwama kudhibiti uhalifu huo.
Habari za ndani ya sekta ya forodha zinaeleza kwamba kutokana na mafanikio yao katika kukwepa kodi, wamefikia hatua ya kuhodhi utoaji bandarini wa aina fulani ya bidhaa.
“Sasa ni vigumu sana, na kwa kweli hakuna wakala mwigine anayethubutu kutoa bandarini bidhaa za nguo kwa kuwa nyaraka za kampuni nyingine zifikapo Tiscan au Longroom huwekewa bei za juu ambazo hazilipiki ili kuwakatisha tamaa waagizaji ambao kwa sasa wamechoshwa na huduma za vijana hawa zilizojaa kiburi na dharau.
“Hali hiyo imewafanya waagizaji kukosa pa kwenda bali kwa vijana hao na wakabaki wakisikitika jinsi vyombo vya dola vinavyowekwa mfukoni kwa hasara ya jumla ya Taifa. Waagizaji wanalalamika kwamba hawana tena uhuru kwa kuwa wanalazimika kutumia kampuni moja tu ambayo bei zake hazina majadiliano. Ukienda kubembeleza unaambiwa katafute wakala mwingine ambaye hata hivyo huwezi kumpata kwa kuwa hawa wamehodhi kila kitu,” anaeleza mtoa habari wetu ndani ya sekta ya kodi.
Mfanyabiashara mmoja mzalendo ameliambia Raia Mwema kwamba vijana hao wamewakatisha tamaa wafanyabiashara wengi huku wao wakiwa na uwezo wa kutoa bandarini mizigo siku na wakati wanaotaka wao.
“Wanatoa inapofika fleet ya magari kama 20 kwa wakati mmoja. Wanafanya hivyo baada ya kusafisha njia au kusubiri siku ambayo hakuna ‘wanoko’ kwenye shift fulani huko Forodha. Inawasaidia pia katika mambo ya rushwa kwani fungu moja linatolewa kwa ajili ya makontena mengi zaidi. Hii ina athari kwa sisi waagizaji ambao kontena zetu nne au tano zinaweza kuwa zimefika mapema, lakini ikabidi zisubiri nyingine kwa wiki nne au tano ili nyaraka ziende pamoja na gharama (rushwa) iwe ndogo,” anaeleza mfanyabiashara huyo mwenye ofisi zake maeneo ya Kariakoo.
Mfanyabiashara huyo anaeleza kwamba kwa hali halisi iliyopo kwenye mfumo wa ukusanyaji kodi, ni vugumu kukwepa ushuru kwa kudanganya kiasi (idadi) cha mali kilichomo kwenye kontena (false declaration) au kuweka bei ndogo au ya chini ya ile bei halisi (under invoicing), lakini kwa kampuni hiyo hilo linawezekana kwa kuwa mfumo mzima tangu serikalini, Tiscan na TRA umekuwa nyuma yao kutokana na nguvu kubwa waliyonayo vijana hao.
Imeelezwa kwmaba kwenye kampeni za mwaka 2005 kampuni hiyo ilichangia chama tawala Sh. Milioni 200 na kwamba katika mwaka huu wameahidi kuchangia milioni 500 huku ofisini kwao zikiwa zimejaa picha walizopata kupiga na viongozi wa juu wa chama tawala na Serikali katika hafla za uchangiaji kampeni.
Ili kufahamu kiasi cha mapato ya Serikali yanayopotea angalia hesabu hizi:
Kontena la nguo za kawaida lenye urefu wa futi 20 laweza kuwa na thamani ya Dola za Marekani 60,000.00 hadi Dola za Marekani 80,000.00 kutegemeana na aina, ubora na idadi ya nguo zenyewe. Ushuru wa jumla ni 48% ya thamani halisi (cif value). Kwa hiyo kama thamani ni Dola za Marekani 60,000.00 x 48% = Dola za Marekani 28,000. Kwa thamani ya Dola 1 ya Marekani = Sh.1400, ushuru kwa kontena hili katika shilingi ni 40,320,000.
Kama kontena ni la thamani ya USD 80,000, ushuru ni 80,000.00 x 48% ambazo ni sawa na Dola za Marekani 38,000.00 na kwa Sh ni 53,760,000.
Kwa mujibu wa habari za ndani ya TRA, vijana hao wanakadiria gharama zote kwa meta za ujazo kutoka China hadi Dar es Salaam, na hivyo kontena la futi 20 ambalo lina meta za ujazo 36, ina maana gharama zote ni Dola za Marekani 450 x 36 = Dola za Marekani Dola za Marekani 16,200 ambazo ni sawa na Sh. milioni 22.68.
Ikiwa utaondoa gharama halisi za kusafirisha kontena hadi Dar es Salaam ambazo ni Dola za Marekani 2,500, basi kinachobaki ni Dola za Marekani 16,200 – 2500 = Dola za Marekani 13,700.00 au Sh. 19,180,000.
Uchunguzi wa Raia Mwema umeonyesha kwamba sehemu kubwa ya fedha hutumika katika kulipia ushuru kidogo, rushwa kwa maofisa sehemu mbalimbali husika, gharama za bandari na usafiri wa bandarini kwenda kwenye maghala yao.
“Kwa uzoefu wangu hawa jamaa kontena la nguo la futi 20 hawalipi zaidi ya Sh. milioni 10. Hii ina maana ya kuwa badala ya kulipia gharama halisi ya zaidi ya Sh. milioni 40 wao wanalipa milioni 10 tu. Kwa hiyo, kwa mfano mmoja tu, Serikali hupoteza Sh. milioni 30 kwa kila kontena la nguo la futi 20 linalotoka bandarini. Ikiwa makontena 100 yanaweza kutoka bandarini kwa wiki moja, ina maana serikali hupoteza milioni 30 x 100 = bilioni 3 kwa wiki. Kwa mwaka mmoja hii ni sawa na shilingi bilioni 156,” anaeleza mtaalamu wa kodi ambaye kwa sasa ni mstaafu.
.
CHANZO: Raia Mwema
0 comments:
Post a Comment