Tuesday, 15 June 2010

Japo mie si mchambuzi mzuri wa soka lakini naamini utaafikiana nami kuwa Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini zimeendelea "kuboa" wapenzi wa soka.Majuzi tumeshuhudia Waingereza walivyopelekeshwa na vijana wa Obama,huku kipa wao akiingia kwenye vitabu vya historia kama kituko cha mwaka.Kati ya wawakilishi wetu sita wa Bara la Afrika,ni Ghana tu waliotupa raha japo kwa ushindi kiduchu.Wenyeji South Afrika walilazimishwa sare (huku wakionyesha bayana kuwa ni wasindikizaji tu),Nigeria wakatutia machungu zaidi kwa kuonyesha kiwango duni dhidi ya Argentina (ambao nao hawakuonyesha kiwango kilichotarajiwa),Cameroon ndio wakatukata maini kwa kiwango cha chini kabisa cha soka huku Algeria wakifanya kilichotarajiwa (wasindikizaji).Matumaini ya Afrika sasa yamebaki kwa Ivory Coast wanaoingia dimbani mchana huu (kwa mida ya hapa Uingereza).


JapoUjerumani na Uholanzi, vigogo wengine wanaotarajiwa kufanya vizuri kwenye michuano hiyo,wameshaonyesha makali yao huku tukisubiria kuwaona Brazil,Uhispania na Ureno,sare ya Italia kwa Paraguay imeacha maswali kama Wataliano ni tishio kweli kama ilivyotarajiwa,japo wanafahamika kwa tabia yao ya kubadilika kadri michuano inavysonga mbele.

Kwahiyo,kwa kifupi hadi sasa Fainali hizo zinaweza kuelezwa kama "zinaboa" kwa kiasi flani japo ni mapema mno kufikia hitimisho hilo.By the way,hii ni wiki ya kwanza tu na kuna timu kadhaa ambazo hazijaingia dimbani.Yote katika yote,mshindi bayana katika kinyang'anyiro hicho ni VUVUZELA,matarumbeta yanayoendelea kutawala vichwa vya habari kuhusiana na michuano hiyo.

Wakati kuna "kelele" (mithili ya hizo za Vuvuzela) kwamba matarumbeta hayo yanakera huku wengine wakitaka yazuiliwe,Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na waandaaji wa michuano hiyo wameweka bayana msimamo wao kuwa Vuvuzela ni sehemu muhimu katika michuano hiyo.Ni utamaduni wa wenyeji,na kama tunavyofahamu "ukienda kwa Warumi inabidi uishi kama Warumi".Hata hivyo,tayari hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa dhidi ya kelele za Vuvuzela.Kituo cha runinga cha BBC kinachoonyesha michuano hiyo kwa hapa Uingereza (wakipokezana na ITV ya hapa) kina mpango wa kuwezesha watazamaji kubonyeza kitufe chekundu kwenye runinga zao ili "kuondokana na kelele za Vuvuzela" baada ya kupokea malalamiko 545 kutoka kwa watazamaji wanaodai kuwa matarumbeta hayo "yanawazingua".

Kadhalika,kampuni inayotengeneza Vuvuzela imetangaza aina mpya ya matarumbeta hayo ambayo itakuwa na "kelele pungufu",hatua inayotarajiwa kupunguza malalamiko zaidi.Jana,mchezaji Robin van Persie wa Uholanzi alionekana akilalamika kwa refarii kuwa hakusikia firimbi kuwa ameotea kutokana na kelele za Vuvuzela.Kadhalika,kipa wa timu ya Denmark Thomas Sorensen alieleza kuwa angetumia lugha za alama (sign language) kuwasiliana na wachezaji wenzie kwa vile Vuvuzela "zilikuwa zikimeza sauti yake".Mwanasoka wa Ureno,Christiano ametamka bayana kuwa angependa kuona Vuvuzela zikipigwa stop katika michuano hiyo.


Na kama wasemavyo Waswahili kuwa "kufa kufaana",tayari kuna "wajanja" wameibuka kutengeneza faida kutoka kwa wanaokerwa na kelele za Vuvuzela.Kampuni moja ya Ujerumani inaripoti kuwa imevumbua "teknolojia ya kuchuja kelele za Vuvuzela"ambapo mtazamaji akichomeka kidude kiitwachoSurfpoeten kwenye runinga yake,basi makelele ya Vuvuzela yanakuwa kwishne (angalia picha ifuatayo).
Lakini wakati hayo yakitokea,umaarufu wa Vuvuzela unazidi kupaa kiasi cha baadhi ya watu kuhisi kuwa bila kujali yeyote atakayetwaa ubingwa katika Fainali hizo,mshindi halisi atabaki kuwa Vuvuzela.Inaripotiwa kuwa supamaketi maarufu hapa Uingereza,Sainsbury,imeshauza Vuvuzela 22,000 katika masaa 12 ya mwanzo wa mashindano hayo na mchezaji wa Timu ya Taifa ya Uingereza Jamie Carragher ameshanunua Vuvuzela mbili kwa ajili ya wanawe.Kadhalika,inatarajiwa kuwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya hapa utashuhudia Vuvuzela kadhaa kwenye mechi mbalimbali.Wachezesha kamari wa Paddy Power wanaendesha kamari ya kubashiri timu gani itakuwa ya kwanza kuuza matarumbeta hayo kwa mashabiki wake huku Manchester United wakiongoza kwa turufu ya 4/1.

Na katika kuthibitisha kuwa Vuvuzela imejichukulia umaarufu mkubwa,tayari kuna app ya Vuvuzela kwenye simu ya kisasa ya iPhone.Well,kama kuwepo kwa app hiyo hakujakuonyesha umaarufu wa Vuvuzela,idadi ya dowloads yaweza kukushawishi kwani tayari apps 750,000 (yaani robo tatu ya milioni) za Vuvuzela zimeshakuwa downloaded tangu ilipozinduliwa.Inatarajiwa kuwa Vuvuzela app (angalia picha yake hapo chini) itaweza kutumika kwenye iPad na iPod.


Mwisho,kama kuna watu wananufaika vya kutosha na vuguvugu la Kombe la Dunia basi ni Rais wa TFF Leodgar Tenga na wababaishaji wenzake waliojiingiza mkenge kuialika Brazil kisha kuambulia kipigo cha magoli matano na hasara ya bilioni kadhaa.Hata hivyo,licha ya usahaulifu wa kawaida wa Watanzania,michuano hiyo inawasaidia sana akina Tenga kwa vile macho ya mashabiki wengi wa soka wa Tanzania yameelekezwa huko Afrika Kusini na hivyo kusahau kuhusu deni walilobebeshwa na akina Tenga.Ni dhahiri kuwa michano hiyo itapomalizika mwezi ujao,habari ya hasara na deni hilo itakuwa imezikwa na kusahaulika kabisa.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget