Serikali sasa yatishia kulifuta Mwananchi
Wednesday, 20 October 2010 07:52
Mwandishi Wetu
SERIKALI imetishia kulifunga au kulifutia usajili gazeti la Mwananchi kwa madai kwamba linaandika habari za uchochezi dhidi ya serikali ya awamu ya nne.Barua ya serikali yenye kumbukumbu namba ISC/N.100/1/VOL.V/76 iliyoandikwa kwa mhariri mtendaji wa gazeti la Mwananchi, inaonya kwamba kama gazeti hili litaendelea kuandika habari ambazo imeziita za uchochezi dhidi yake, haitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi.
Hata hivyo, barua hiyo haijaweka bayana habari hizo ilizozielezea kuwa ni za mtazamo hasi dhidi ya serikali na ambazo imedai kuwa ni za uchochezi.
“Kwa barua hii unatakiwa kuacha mara moja tabia ya kuandika habari za uchochezi na kuidhalilisha nchi na serikali kwa kisingizio cha uhuru wa habari na uhuru wa kutoa mawazo ulioanishwa katika katiba ya nchi yetu," inaeleza barua hiyo ya Oktoba 11 iliyosainiwa na Raphael Hokororo kwa niaba ya Msajili wa Magazeti.
"Aidha ukiendeleza tabia hiyo, serikali haitasita kuchukua hatua stahiki za kulifungia gazeti lako au kulifutia usajili kwa mujibu wa sheria za nchi.”
Barua hiyo, ambayo imebeba kichwa cha habari kisemacho "Karipio kali kwa kuandika habari zenye mwelekeo wa uchochezi wa kudhalilisha", ni mwendelezo wa barua nyingine iliyoandikwa na mkurugenzi wa Idara ya Habari, Clement Mshana kwenda kwa mhariri wa gazeti hili Septemba 24, 2010.
Katika barua hiyo ya Mshana, serikali imedai kuwa gazeti la Mwananchi limekuwa na mtazamo hasi dhidi ya serikali na ikamtaka mhariri ajieleze.
Barua hiyo yenye kumbukumbu namba ISC/N.100/1/VOL.V/70, bila ya kutoa mifano, inadai kuwa Mwananchi imekuwa ikiandika habari hasi tu kana kwamba serikali haina zuri linalofanywa kwa wananchi wake na kutaka maelezo.
“Katika kipindi kirefu sasa, na zaidi wakati huu wa kampeni za uchaguzi, gazeti lako limekuwa likiandika habari zenye mtazamo hasi dhidi ya serikali. Habari hizo zimekuwa zikidhalilisha serikali iliyo madarakani ya awamu nne,” inasema sehemu ya barua hiyo.
Katika majibu ya barua hiyo ya kwanza, Mwananchi Communications Ltd (MCL), ilieleza kuwa baada ya kutafakari kwa kina ilishindwa kuelewa msingi wa tuhuma hizo ambazo hazina mifano yoyote ya habari inayodaiwa kuwa ni hasi kwa serikali.
“Baada ya kupitia barua yako na kuitafakari, imetuwia vigumu kuelewa msingi wa tuhuma zako kwa gazeti hili kuhusu mtazamo hasi dhidi ya serikali bila hata kutoa mifano ya habari ambazo zinabeba tuhuma zako kwa gazeti hili hasa unaposema kuwa kwa kipindi kirefu sasa, hasa wakati huu wa kampeni za uchaguzi,” inasema barua hiyo yenye kumbukumbu namba MCL/RN/09/VOL.1.27 iliyoandikwa na mhariri mtendaji wa MCL, Theophil Makunga.
Barua hiyo ya MCL inaeleza kuwa kimsingi habari za kampeni za uchaguzi katika kipindi hiki zinahusu vyama vya siasa na kuhoji sababu za serikali kujiona inaandikwa vibaya na Mwananchi wakati ni vyama ndivyo vinavyoshiriki kwenye kampeni.
Mhariri wa Mwananchi anaeleza katika barua hiyo kuwa kwa sasa gazeti lake linaandika habari za wagombea uongozi kutoka vyama mbalimbali na sera zao ili wananchi wafanye uamuzi siku ya kupiga kura na hakuna chama kilichoandika barua ya malalamiko.
“Kwa taarifa yako tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi Agosti 21, 2010, gazeti la Mwananchi halijawahi kupata malalamiko kutoka chama chochote cha siasa kinachoshiriki katika kampeni hizo juu ya kuandikwa vibaya. Kimsingi Mwananchi linachofanya ni kuripoti wanachosema wagombea wa vyama mbalimbali au kufanyiwa katika mikutano ya kampeni,” inasema barua hiyo ya MCL kwenda kwa Msajili wa Magazeti.
Katika barua hiyo, MCL inaiomba serikali kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu kuhusika kwa serikali katika kampeni za uchaguzi hadi gazeti hili lionekane lina mtazamo hasi.
“Kwa msingi huo, tunaomba ufafanuzi zaidi hapa; serikali inahusika vipi katika kampeni mpaka Mwananchi ionekane ina mtazamo hasi kwa serikali wakati vinavyoshiriki katika kampeni ni vyama vya siasa na wagombea wake,” inasema barua hiyo.
Baada ya barua hiyo, Msajili wa Magazeti alijibu kwamba majibu yaliyotolewa na MCL hayaridhishi na hivyo ofisi yake haikuridhika na utetezi huo.
“Kama tulivyoeleza kwenye barua yetu kwako kuwa katika kipindi kirefu sasa na zaidi wakati huu wa kampeni za uchaguzi, gazeti lako limekuwa likiandika habari zenye mtazamo hasi dhidi ya serikali. Gazeti lako sasa limeamua kufanya ‘house style’ yake ya kuandika habari zenye uchochezi na kudhalilisha nchi na serikali iliyopo madarakani,” inasema barua hiyo.
Katika onyo lake, serikali inasema kwamba picha, habari zinazopewa kipaumbele katika ukurasa wa kwanza wa gazeti zinatiwa chumvi kwa lengo la kuchochea wananchi waione serikali yao haijafanya chochote kwa maendeleo yao.
Akiongelea hatua hiyo ya serikali, Makunga alisema kwamba MCL imeshtushwa na karipio hilo ambalo halikuonyesha ni habari ipi ambayo gazeti la Mwananchi limekosea.
“Msajili hakunukuu hata sheria moja ya vyombo vya habari kuonyesha jinsi gani gazeti limekosea wala habari au kichwa cha habari chenye mtazamo hasi kwa serikali,” alisema Makunga.
Alisema Mwananchi imechukulia hatua hiyo ya msajili kuwa inatishia uhuru wa vyombo vya habari hasa katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi ambacho kinahitaji uvumulivu baina ya taasisi mbalimbali katika jamii.
Makunga alisema kwa kuwa Mwananchi na msajili inaonekana kutokubaliana katika suala hilo, wameamua kupeleka taarifa Baraza la Habari Tanzania (MCT) liweze kufanya uchunguzi kwa mujibu wa katiba yao.
Alisema msimamo wa sera ya uhariri ya MCL inasimamia kwenye ukweli na weledi pasipo kushurutishwa na vikundi vyovyote vya nje na ndani.Makunga alisema Mwananchi itaendelea kuandika habari za ukweli bila ya kumuonea mtu au taasisi yoyote kwa maslahi ya Tanzania.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment