Waislam wakiwa kwenye swala.Picha hii haihusiani moja kwa moja na habari ifuatayo |
Waislam wenye msimamo mkali wanashukiwa kuyachoma moto majengo mawili ya kanisa huko Zanzibar,tukio lililotokea Jumapili iliyopita huku waumini wa makanisa hayo wakipokea vitisho vya kuuawa.
Majengo hayo ya Kanisa la Assemblies of God (TAG) na Evangelical Assemblies of God Zanzibar (EAGZ) katika kijiji cha Masingini kilichopo kilomita 5 kutoka mjini-kati Zanzibar yalichomwa moto takriban saa 2 usiku,kwa mujibu wa Askofu Fabien Obeid wa EAGZ.Polisi wa Mwera walipata taarifa ya tukio hilo kesho yake asubuhi.
Matukio hayo ni mwendelezo wa vitendo vya kuwatisha Wakristo katika eneo hilo lenye Waislam wengi,na kuibua hofu kwamba Waislam wenye msimamo mkali wanaweza kudiriki kufanya lolote lile kuzuwia ustawi wa Ukristo.
“Muislam mmoja alisikika akisema, ‘Tumesafisha eneo letu kwa kuharibu makanisa mawili,na sasa tuna mpango wa kuwaua waumini wa makanisa haya mawili-hatutaruhusu kanisa kujengwa tena,’” alisema muumini mmoja wa kanisa ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Jengo hilo la matofali la TAG lilikuwa katika hatua za mwisho za ujenzi,na kwa mara ya kwanza Jumapili hiyo waumini walifanya ibada katika jingo hilo jipya.Jengo la EAGZ ambalo waumini takrban 30 walihudhuria ibada lilikuwa la udongo.
Pasta Michael Maganga wa EAGZ na Pasta Dickson Kaganga wa TAG walieleza hofu yao kuhusu hatma ya kanisa hapo Masingini.Mapasta wa Zanzibar walitarajiwa kukutana jana (Jumamosi) kujadili namna ya kukabiliana na uharibifu huo,alieleza Mwenyekiti wa Usharika wa Mapasta Zanzibar,Askofu Lonard Masasa wa Kanisa la EAGT.
Kwa muda mrefu Waislam wenye msimamo mkali visiwani Zanzibar,wanaoungwa mkono na baadhi ya viongozi wa serikali katika maeneo husika,wamekwaza uwezekano wa Wakristo kupata ardhi kwa minajili ya ujenzi wa majengo ya ibada.Kuna nyakati ambapo wamebomoa majengo yaliyopo na badala yake kuanzisha ujenzi wa misikiti.
Huku wakikanganywa na kutopata ushirikiano wa serikali katika kuwashughulikia wahusika wa matukio hayo,viongozi wa makanisa wameeleza kuwa uwezekano wa waliochoma moto majengo hayo kukamatwa ni mdogo.Mara nyingi,serikali huegemea upande wa wanaofanya matukio hayo,kuchelewesdha uchunguzi kwa hofu ya kuwaudhi Waislam walio wengi ambao wanapinga kuenea kwa Ukristo.
Mwaka jana,maafisa wa serikali katika eneo la Mwanyanya-Mtoni waliungana na Waislam wa eneo hilo kujenga msikiti katika eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kanisa la EAGZ,alieleza Pasta Paulo Kamole Masegi.
Pata Masegi alinunua ardhi mwezi Aprili mwaka 2007 kwa ajili ya ujenzi wa kanisa katika eneo hilo la Mwanyanya-Mtoni,na kufikia mwezi Novemba mwaka huohuo tayari kulikuwa na jengo lililotumika kama sehemu ya ibada kwa muda.Muda si mrefu Waislam wa eneo hilo walipinga hatua hiyo.
Mwezi Agosti mwaka jana,Waislam hao walianza ujenzi wa msikiti futi tatu tu kutoka kitalu cha kanisa.Mwezi Novemba mwaka huohuo,Pasta Masegi alianza ujenzi wa kanisa la kudumu.Waislam wenye hasira walivamnia eneo hilo na kubomoa msingi wa jengo hilo,alieleza Pasta huyo.
Viongozi wa kanisa waliripoti tukio hilo kwa polisi,ambao hawakuchukua hatua yoyote- na walikataa kutoa ripoti ya tukio,hivyo kukwamisha suala hilo kufikishwa mahakamani,alisema Pasta Masegi.
Wakati huohuo,ujenzi wa msikiti ulikamilika mwezi Desemba (mwaka jana).Hatma ya mpango wa ujenzi wa kanisa ilielekea kufikia ukomo mapema mwaka huu baada ya Mkuu wa Wilaya Ali Mohammed Ali kumfahamisha Pasta Masegi kuwa hana haki ya kufanya ibada katika jengo husika.
Kihistoria, wafanyabiashara wa Kiislam kutoka Ghuba ya Uajemi walifika visiwani Zanzibar mapema karne ya 10 baada ya kusukumwa na pepo za monsoon katika Ghuba ya Aden.Muungano wa visiwa hivyo na Tanganyika mwaka 1964 (na kuunda Tanzania) uliwaacha Waislam visiwani humo wakiwa na hofu kuhusu Ukristo,wakiuona kama njia inayoweza kutumiwa na Tanzania Bara kuwatawala,na tangu wakati huo kumekuwa na hali ya mashaka.
Imetafsiriwa kutoka Compass Direct News (Tarehe 25/11/2010)