Raymond Kaminyoge
TANGU Machi mwaka jana alipostaafishwa kazi na Rais Jakaya Kikwete, akiwa Mkuu wa Wilaya ya Mbalali, Mbeya, Hawa Ngulume amekuwa haonekani hadharani wala kusikika kwenye vyombo vya habari kama tulivyomzoea.
Tunakumbuka jinsi alivyoendesha operesheni ya kuwaondoa wafugaji katika Bonde la Ihefu wilayani humo na kusababisha habari zake kutawala kwenye vyombo vya habari na kusababisha malumbano makali kati ya wafugaji na wanamazingira.
Tunakumbuka pia alivyoendesha operesheni hiyo kwa yeye mwenyewe kutembea kwa miguu akisindikiza ng’ombe kuondoka kwenye bonde hilo hali iliyomfanya achukiwe na wafugaji hao lakini akapendwa na wanamazingira.
Tunashuhudia hivi sasa baada ya kuondoka kwa wafugaji kwenye bonde hilo, hali mazingira ni shwali kwani ukijani na uoto wa asili umeanza kurejea katika bonde hilo.
Hayo aliyafanya akiwa mkuu wa wilaya ya Mbalali kabla hajastaafishwa na kumpisha mwenzake Luteni Cosmas Kayombo.
Hayo yote yanakumbukwa na Ngulume, ambaye hivi sasa yuko katika hali mbaya kiafya nyumbani kwake Goba Kinzudi, jijini Dar es Salaam akisumbuliwa na maradhi ya vichomi na mapafu.
Hata hivyo, bado madaktari hawajathibitisha ni nini hasa kinachomsumbua kutokana na kukosekana kwa kipimo mbadala cha kupima kansa ya mapafu.
Mwananchi lilifika nyumbani kwake na aliamua kueleza yaliyokuwa moyoni mwake: “Nimeona bora nitumie chombo cha habari kufikisha ujumbe wa ugonjwa kabla sijafa.”
Anaongeza: “Kwa miezi mitatu sasa niko hoi kitandani, siwezi kutembea bila kusaidiwa, naiomba serikali inisaidie niweze kwenda India ambako kuna vipimo na tiba ya maradhi yanayonisumbua.”
Anasema ameamua kutumia gazeti hili ili kufikisha ujumbe kwa serikali na CCM kuhusu maradhi yanayomsumbua baada ya njia nyingine kushindikana.
“Nilipeleka taarifa kwenye chama changu kwamba naumwa nahitaji msaada, lakini sikujibiwa, pia nimefanya juhudi za kutaka kumwona Waziri Mkuu ili anisaidie lakini juhudi zangu hazikuzaa matunda, nimeamua nitumie chombo cha habari kabla sijafikwa na mauti,” anasema.
Ngulume ambaye ni kada maarufu wa CCM aliyetumikia nafasi ya ukuu wa wilaya kwa miaka 18, anasema maradhi yanayomsumbua yalianza baada ya kumalizika kwa mchakato wa kura za maoni za chama hicho.
Anasema aliomba ridhaa ya chama hicho kimsimamishe kuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Singida Mjini lakini hakufanikiwa.
“Katika mchakato ule, Mohammed Dewji alishinda na mimi nikawa mshindi wa pili, niliporudi Dar es Salaam nikaanza kujiandaa kwenda kumpigia debe Dewji, kama ulivyo utaratibu wa chama chetu, ndipo nikaanza kuumwa ghafla,” anasema na kuongeza:
“Nilipenda kushiriki kwenye kampeni ili kuwasaidia wagombea mbalimbali wa chama changu lakini anadhani Mungu hakupenda nifanye hivyo.”
Ngulume ambaye amewahi kuwa mkuu wa wilaya mbalimbali zikiwemo za Kinondoni, Bagamoyo na Kibaha anasema baada ya kuumwa amekuwa akipata tiba za aina tofauti lakini hazijamsaidia.
“Nasikia maumivu makali tumboni, utadhani kuna msumeno unakata viungo vyangu, usiku kucha sipati usingizi ni maumivu tu ndiyo yanayotawala mwili wangu,” anasema.
Anasema amekwishatibiwa kwenye Hospitali za Lugalo, Ocean Road na Imtu zote za Dar es Salaam lakini mbali ya kutopata nafuu, hali yake inazidi kuwa mbaya siku hadi siku.
“Katika hospitali ya Ocean Road nilitakiwa kupima kama mapafu yana maji ili kuthibitisha kama ni kansa ya mapafu lakini kipimo kilichopo kinatakiwa kukaa katika kinywa nami sina pumzi, hivyo ikashindikana kupima,” anasema.
Anaongeza kuwa hadi sasa hawezi kuweka wazi kuhusu maradhi yanayomsumbua kwa vile vipimo mbadala ya vile vya kuwekwa katika kinywa vinapatikana nje ya nchi.
“Ndiyo maana naomba msaada wa kwenda kutibiwa nje kwani nikipimwa ndipo naweza kupata tiba ya uhakika,” anasema kwa taabu.
Anasema katika kuhangaika kutafuta tiba aliwahi kwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili lakini cha kushangaza alikaa kuanzia saa 8.00 mchana hadi saa 11.00 jioni bila kuhudumiwa.
“Ndipo mtu mmoja anayenifahamu alipopita nilipoketi akanisalimia kwa kuniita mheshimiwa. Muuguzi mmoja jina ninalihifadhi akaja kutaka kunihudumia, nikamwambia ina maana siwezi kuhudumiwa hadi niwe mheshimiwa? Nikaondoka kwa hasira nikakataa kuhudumiwa,” anasema.
Siku moja baada ya kuzungumza na gazeti hilo, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi) aliyokuwa akifanya kazi chini yake ilitoa tamko la kusimamia matibabu yake nje ya nchi.
Ujumbe wa maofisa wa Tamisemi ulifika nyumbani kwa mkuu huyo wa zamani wa wilaya kumjulia hali. Hatua hiyo imekuwa faraja kwa Ngulume ambaye anasema ingawa bado ana maumivu makali, amefurahi kwani kuna maofisa kutoka Tamisemi waliomtembelea na kumpa matumaini kwamba huenda akaenda nje kutibiwa.
“Baada ya gazeti lenu kuandika habari zangu, ujumbe wa Tamisemi umefika nyumbani kwangu kuniangalia na kuniahidi kwamba utafanya mipango kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ili niweze kwenda nje kutibiwa,” alisema.
Alisema mbali na ujumbe huo, watu wengi ambao hawakuwa na taarifa zake, wameanza kumtembelea na wengine kumpigia simu wakimuombea kwa Mungu ili aweze kupona maradhi yanayomsumbua.
“Nawashukuru waandishi wa mwananchi, kwani nyie ndiyo mlioujulisha umma kuhusu hali ya afya yangu, ninaomba kwa Mungu usiku kucha ili niweze kufanikiwa kutibiwa kwani maumivu ninayoyapata ni makali.
CHANZO: Mwananchi
Tunachohitaji ni total reform kwa kila asasi na taasisi kwa mazingira ya sasa haviwezi kufanyika kwa sababu mfumo dume wa ubabaishaji na ufisadi unaoanzia toka ngazi ya juu kabisa ya Rais wa nchi hadi mjumbe wa kitongoji ni mbovu. Ndio sababu tulisema JK hawezi kuleta mabadiliko yeye anaweza porojo tuu....Tunahitaji kila kifanyiwe mabadiliko...Leo hii mawaziri wa serikali ya JK watatokana na wale walioshiriki kura maoni na kushinda kwa njia ya rushwa na hongo na uchachuaji katika uchaguzi mkuu hapo unategemea nini zaidi ya ubinafsi, uvunjaji wa sheria, uzembe kama wa Dr. Hosea na Takukuru yake, Ufisadi wa kagoda, Richmond na wadogo zake....Na pia tegemea wachumia tumbo wengine watachaguliwa kuwa mawaziri wa kuja kuendesha serikali ya ili mardi liende...Na pia tusishangae hata lowasa kuwa tean waziri mkuu au waziri wa wizara...hayo yote ndiyo yansababisha kushindwa kutoa huduma sahihi kwa wananchi wake kama huyu mama anavyotahabika sasa kwa sababu ya uababaishaji wa serikali CCM na viongozi wake.
ReplyDeleteWatanzania wanatakiwa kuelemishwa umuhimu wa siasa na wanasiasa imara, na wajibikaji kujenga uchumi imara...Siyo kama JK anavyosema mara nyingi hizo ni siasa tuu...anajaribu kutenganisha siasa na maendeleo ya uchumi kwa nadhari zake yeye zisizokuwa na tafiti yakinifu
CCM hawajamtelekeza huyu mama wala kukosea. Wanajuana. Huenda thamani yake ilikwisha pale alipostaafu. Na isitoshe, huenda walidhani kuwa wale wawekezaji walioharibu bonde la Ihefu aliowafadhili basi wangemlipa fadhili bila kujua kuwa madaraka yakikutoka kila kitu kinaporomoka. Nani, kwa mfano, leo anachangia NGO ya Anna Mkapa ilhali kuna ya Salma Kikwete? Huu ndiyo utawala wa kifisi na kimbwamwitu ambapo, kama tumbusi, kila mtu hurarua chake na kuishia. Kweli cheo ni dhamana. Hili ndilo somo toka kwa mama Hawa Ngulume. Hata polisi waliosimamia uchakachuaji uliopita kuna siku watakutana na adha na adhabu ya kazi ya mikono yao watakapostaafu. Weekend Njema
ReplyDelete