• RIPOTI MPYA YA UNDP YAANIKA KILA KITU
na Tutindaga Mwakalonge
SHIRIKA la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), limetoa ripoti yake ya hali ya maendeleo duniani inayoichambua Tanzania kuwa moja ya nchi zilizo nyuma sana kimaendeleo kwa kuwa na watu wengi wanaokabiliwa na umaskini.
Ripoti hiyo inayopima maendeleo ya nchi husika kwa kutazama maendeleo ya watu wake ilizinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam jana na kuitaja Tanzania kuwa nchi ya 148 kati ya nchi 169.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika kila Watanzania mia moja, 36 wanaishi katika hali mbaya sana ya umaskini, sawa na asilimia 36 ya watu wote, milioni 41.3.
Pia ripoti hiyo ya kimataifa imeonyesha kuwa katika kila Watanzania mia moja, 97 wanaishi kwenye umaskini wa kipato wa chini ya dola 2 za Marekani kwa siku, sawa na chini ya takriban sh 2,000 za Kitanzania kwa siku.
Aidha, ripoti hiyo iliyobeba kauli ya ‘Utajiri halisi wa mataifa’, imeonyesha kuwa katika kila Watanzania mia moja, 89 wametajwa kuishi chini ya dola moja ya Marekani kwa siku.
“Kwa takwimu hizo, Watanzania wengi wako katika umaskini wa kutisha kwa sababu ya kuwa na uwezo duni wa kifedha wa kumudu maisha yao ya kila siku”, alifafanua mtaalamu mmoja aliyehudhuria uzinduzi huo.
Hata hivyo, pamoja na takwimu hizo, Wizara ya Fedha na Uchumi, kupitia kwa Katibu wake, Ramadhani Khijjah, iliendelea kusifia mwenendo wa ukuaji wa uchumi nchini huku ikidai kuwa sekta za elimu na afya zimekuwa zikichochea ukuaji wa uchumi.
CHANZO: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment