Askari trafiki feki akamatwa. Askari polisi feki akamatwa. Ofisa Usalama wa Taifa feki akamatwa. Hizo ni habari zilizotawala vyombo vya habari huko nyumbani hivi karibuni, ambazo kimsingi zinaashiria tatizo kubwa la uwepo wa watendaji feki wa taasisi za usalama.
Wakati lawama kubwa zinapaswa kuelekezwa kwa matapeli hao waliojipachika majukumu yasiyo yao, kwa hakika hatuwezi kutozinyooshea kidole taasisi husika kwa ‘kuruhusu’ wahalifu wafanikiwe kujivisha utumishi wa taasisi hizo pasi kujulikana kwa muda mrefu tu.
Binafsi sikushangazwa sana na taarifa za polisi na trafiki feki kwa sababu utendaji kazi wa baadhi ya polisi hauna tofauti na wahalifu. Sasa kama polisi halisi wanaweza kujihusisha na uhalifu, kwa nini matapeli wasiige mfano kwa kujidai polisi, japo ni feki?
Mara kadhaa tumesikia taarifa kuhusu polisi wanaojihusisha na uhalifu, na ni majuzi tu kulikuwa na taarifa za kuchefua, baadhi ya polisi wakikamatwa na fuvu la binadamuAidha fuvu hilo ni la raia aliyeuawa na polisi hao au lilifukuliwa kutoka kaburini kwa minajili ya ushirikina au kutisha raia wasio na hatia watoe rushwa, si rahisi kufahamu.
Takriban kila mwananchi ‘wa kawaida’ ambaye amewahi kufika kituo cha polisi atakuwa anafahamu kuwa njia pekee ya kupata huduma inayostahili ni kwa ‘kumpatia chochote (rushwa) afande’ ili ashughulikie kilichompeleka mwananchi huyo kituoni hapo. Kwa kifupi, Jeshi la Polisi linanuka rushwa.
Kilichonishitua zaidi ni hiyo habari ya Ofisa Usalama wa Taifa feki. Kama nilivyotanabaisha awali, yayumkinika kuamini kuwa matapeli waliojifanya polisi walifanikiwa katika ‘upolisi’ wao feki kwa vile si jambo la ajabu kwa polisi kudai rushwa. Kwa lugha nyingine, sidhani kama kuna Mtanzania anayeweza kushtuka akiombwa rushwa na polisi kiasi cha kudhani kuwa polisi huyo ni feki.
Lakini kwa hili la matapeli kumudu kujifanya maofisa usalama wa taifa sio tu ni jambo la kuogopesha bali pia linalohitaji kuangaliwa kwa undani zaidi.
Itakumbukwa kuwa majuzi, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe alizungumzia tatizo la kushamiri biashara ya dawa za kulevya. Pamoja na mengi aliyoozungumzia, Mwakyembe alinukuliwa akishauri Idara ya Usalama wa Taifa ijiangalie upya.
Nadhani, kimsingi, Dk Mwakyembe alitumia lugha ya kistaarabu badala ya kutamka bayana kuwa miongoni mwa wanaofanikisha dawa za kulevya kuingia au kupita katika mipaka ya nchi ni baadhi ya maofisa wa usalama wa taifa.
Na hata kama Mwakyembe asingesema hayo (na hakutamka waziwazi), mtu yeyote anayeelewa utendaji kazi wa Idara hiyo hatoshindwa kuelewa kwamba taasisi hiyo ni sehemu ya tatizo hilo la kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya.
Ninaandika haya kwa sababu nina uhakika idara hiyo inawafahamu kwa majina, sura na makazi wahusika wa biashara hiyo hatari. Na ufahamu huo sio jambo la jana au juzi. Wahusika wanaofahamika kwa muda mrefu, lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.
Lakini licha ya kuwafahamu wahusika, kwa mujibu wa taratibu za kazi za taasisi hiyo, kila mpaka wa nchi yetu una Ofisa wa Idara hiyo ambaye ana jukumu la kuchunguza na kuzuia uwezekano wa watu wasiotakiwa au vitu visivyotakiwa kuingia nchini.
Sasa kama maofisa hao wanatimiza wajibu wao ipasavyo, iliwezekanaje, kwa mfano, shehena kubwa ya dawa za kulevya ya ‘akina Masogange’ ikaingia nchini na kusafarishwa hadi Afrika Kusini ilikokamatwa?
Jibu ni aidha maofisa husika walikuwa ‘busy’ na masuala yao binafsi, au wao pia walikuwa miongoni mwa waliofanikisha kuingizwa kwa shehena hiyo.
Katika mazingira ya kawaida, suala hili linaweza kuonekana dogo tu, na lisilopaswa kuumiza vichwa vyetu. Lakini kimsingi, kama tuna maofisa usalama wanaoweza ‘kuruhusu’ dawa za kulevya zipite chini ya uangalizi wao, kipi kitawazuia kuruhusu magaidi wasipite alimradi wana fedha za kuwafanya maofisa hao wapuuzie wajibu wao?
Pengine baadhi ya wasomaji wanaweza kuhisi kuwa nimekuwa nikiiandama sana taasisi hiyo muhimu. Ukweli ni kwamba kanuni za msingi kabisa za Idara ya Usalama wa Taifa wa nchi yoyote ile ni “Idara legelege husababisha taifa legelege.” Na moja ya viashiria vya udhaifu wa taasisi kama hiyo ni kushamiri kwa vitendo vinavyofanya umuhimu wa kuwa na taasisi kama hiyo.
Hapa ninamaanisha kuwa ukiona taifa fulani linaandamwa na matukio ya ufisadi, basi Idara yake ya Usalama wa Taifa ni legelege, sambamba na matukio mengine yanayohatarisha ustawi wa nchi kama vile ufisadi.
Kwa lugha nyepesi, kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya-kama ilivyo kushamiri kwa ufisadi - ni uthibitisho bayana kuwa taasisi hiyo muhimu imelegalega.
Ni katika mazingira hayo ya kulegalega kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa ndipo tunashuhudia matapeli wakipata ujasiri wa kujifanya maofisa wa Idara hiyo.
Kuna msemo kuwa ‘ili uongo ufanikiwe sharti uwe na ukweli ndani yake.’ Naam, matapeli wanaojifanya maofisa wa Idara hiyo wanafahamu fika kuwa kuna maofisa halisi wanaofanya yale yale yanayofanywa na baadhi ya polisi, yaani kutumia nyadhifa zao kwa minajili ya uhalifu.
Ningetamani sana kuhitimisha makala hii kwa kushauri nini kifanyike. Lakini nadhani nisipoteze muda wangu na wako msomaji kutoa ushauri utakaopuuzwa. Kutarajia uongozi wa taasisi hiyo ‘ujiangalie’ kama alivyoshauri Mwakyembe ni mzaha. Kwa nini watendaji wanaonufaika kwa kukiuka taratibu za kazi wajichunguze ilhali wanajua bayana hakuna ‘mwenye jeuri’ ya kuwachukulia hatua?
Kutarajia kwamba watawala wetu wanaweza ‘kuweka kando uoga’ na kuwavaa mashushushu wetu kuwaeleza kuwa ‘ndugu zetu, tunawatengea fedha nyingi kwa ajili ya usalama wa taifa letu, lakini hali inazidi kwenda kombo’ ni ndoto za mchana.
Labda, Rais Jakaya Kikwete, katika miezi takriban 20 iliyobaki kabla ya kumaliza awamu ya pili ya urais wake, atafakari upya kuhusu azma yake njema ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania, aamue ‘liwalo na liwe’ na kupambana kwa dhati na vyanzo halisi vya ufisadi na kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya. Akitaka anaweza, kwani uwezo anao, na sababu anayo, kinachohitajika ni nia tu.
0 comments:
Post a Comment