Thursday, 15 August 2013


.
HUKO nyuma niliwahi kuandika makala kwa kuanza na maswali ambayo nitayarejea hapa kama ifuatavyo; Hivi tumerogwa? Je, inawezekana hatujarogwa lakini tumejiroga wenyewe? Au inawezekana tumerogwa, aliyeturoga naye karogwa kisha kafariki? (Wanadai aliyekuroga akifariki basi huponi)
Ni maswali ya ‘kipuuzi’ lakini yanaweza kuamsha hisia za msingi tukiangalia mwenendo wa taifa letu hivi sasa.
Sijui Mungu atupe nini. Ametubariki na nchi iliyoishi kwa amani na upendo kwa miaka kadhaa. Akatupatia Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ambaye licha ya kuhimiza umoja miongoni mwetu kama Watanzania, lakini pia alipigania umoja wa Bara la Afrika.
Nyerere alitambua mapema kuwa ni rahisi kwa nchi yenye makabila zaidi ya 120 kuwa vipande vipande kama isipounganishwa na itikadi ya kutufanya tuwe na umoja. Akahimiza siasa ya Ujamaa ambayo kimsingi ililenga kuondoa matabaka na tofauti za kinadharia na kihalisia, kutuacha sote tukiwa Watanzania.
Mungu pia ametujalia nchi yenye raslimali nyingi, utajiri ambao hata mataifa tajiri kabisa duniani yanatamani ungekuwa katika nchi zao.
Katika mazingira ya kuchafua kabisa, jitihada alizofanya Nyerere kutuunganisha zikaanza kuhujumiwa mara tu baada ya kung’atuka kwake. Chama alichokiasisi, CCM, kikamgeuka kupitia Azimio la Zanzibar, ‘uhuni’ uliotangaza kifo cha itikadi ya Ujamaa.
Tangu wakati huo, nchi imekuwa kama ‘imerogwa’ vile. Kwenye ubepari hatupo (maana kila Ilani ya Uchaguzi ya CCM inasema Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea) na Katiba yetu inabainisha hivyo pia. Kwenye Ujamaa nako hatupo, kwa sababu kila msingi uliobeba itikadi hiyo umetupwa.
Pamoja na rasilimali zetu lukuki tumeendelea kuwa nchi masikini kabisa duniani. Badala ya kuwa soko la bidhaa zinazotokana na utajiri wetu, tumekuwa ombaomba wakubwa huku viongozi wetu, bila haya, wanadiriki kutamka bayana eti tusipofanya ziara huko nje hatutopata maendeleo.
Sawa, safari za mfululizo huko nje zimefanikiwa kuleta viongozi wa mataifa makubwa zaidi duniani, Rais Xi Jinping wa China na baadaye ‘rais wa dunia’ Barack Obama wa Marekani. Kama kawaida, viongozi wetu wakatembea vifua mbele na kujigamba nchi sasa imepiga hatua ndio maana viongozi muhimu wa dunia wanatutembelea.
Ni kweli, ziara za marais Jinping na Obama zilifanikiwa kuiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia (kututangaza vizuri duniani).
Nakumbuka wakati wa ziara ya Rais Obama, taarifa moja ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ilibainisha kuwa Tanzania ni moja ya nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi duniani. Nani angebisha ilhali Wachina na Wamarekani wanapigana vikumbo kuitembelea nchi yetu?
Lakini kama vile tumerogwa, siku chache tu baada ya ziara ya Obama zikapatikana taarifa kuwa kulikuwa na ufisadi wa mabilioni ya shilingi katika maandalizi ya mkutano wa Smart Partnership, uliowakutanisha marais kadhaa wa Afrika.
Je, inaingia akilini maandalizi tu ya mkutano huo wa Smart Partnership yazue ufisadi wa mabilioni ya shilingi, kabla mpango husika haujaanza kutekelezwa? Niliwahi kuandika huko nyuma kuwa wakati Obama anahangaika na mawazo yake mazuri ya kutumwagia dola za Marekani, mafisadi nao wanahaha kuandaa mabakuli ya kudaka fedha hizo. Huo ufisadi wa fedha za maandalizi ya mkutano huo ni kama ‘utangulizi’ tu, filamu yenyewe inasubiri fedha zianze kumiminika.
Kama hiyo haitoshi, siku chache baada ya ziara ya Obama, jina la nchi yetu likianza kuvuma tena kwenye anga za kimataifa, safari hii tatizo likiwa ni kwenye biashara ya dawa za kulevya. Kwa hakika huwezi kumshangaa mtu anayedhani huenda tumerogwa, kwa sababu licha ya kupata bahati ya mtende ya jina letu kusikika kwa uzuri katika takriban kila kona ya dunia kutokana na ziara ya Obama, kwa makusudi tumechafua sifa hiyo.
Ni kama vile uamuzi fyongo wa Obama kufumbia macho ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu Tanzania ulikuwa ni ruhusa kwa vyombo vya dola na wahalifu (wakati mwingine ni vigumu kutofautisha kati ya chombo cha dola na wahalifu) kuendelea kuhatarisha usalama wa Watanzania. Tumeendelea kushuhudia matukio mbalimbali yanayozidi kuchafua taifa, ndani na nje.
Kutoka mahala kusikoeleweka, Jeshi la Polisi ambalo halioni aibu kuonekana linakitumikia chama tawala CCM kuwakandamiza wapinzani, likakurupuka na mkakati hatari wa ‘kuzusha’ kesi za ugaidi dhidi ya wanasiasa wa upinzani. Ni nchi iliyorogwa pekee inayoweza kufanya mzaha katika ugaidi. Ndio maana, majuzi tu, Jaji Simon Lukelelwa alitoa onyo kali kuhusu ‘kuchezea ugaidi’ wakati akitoa hukumu katika kesi iliyokuwa ikiwakabili viongozi kadhaa wa CHADEMA huko Tabora.
Wakati polisi na CCM wanacheza ‘mchezo mbaya’ wa tuhuma za ugaidi bila kujali madhara yake kwa hadhi ya nchi yetu, bado tumeendelea kuwa gizani kuhusu hatima ya mauaji ya Padre Evarist Mushi aliyeuawa kikatili huko Zanzibar, shambulio la bomu kanisani Arusha, na shambulio la bomu katika mkutano wa CHADEMA huko huko Arusha.
Na ghafla Jiji la Arusha limegeuka ‘uwanja wa vifo vya matajiri’, tukio la hivi karibuni ni la mauaji ya kinyama dhidi ya mfanyabiashara tajiri jijini humo, Erasto Msuya. Mauaji ya mfanyabiashara huyo yameibua hisia kuwa hata vifo vya hivi karibuni vya matajiri wengine wa maeneo hayo si vifo vya asili bali mauaji.
Lakini kama kuna tukio baya kabisa ni hili la majuzi la mabinti wawili kutoka Uingereza kumwagiwa tindikali Visiwani Zanzibar. Tangu nifike hapa Uingereza, zaidi ya miaka 10 iliyopita, sijawahi kusikia au kuona Tanzania ikitawala katika vyombo vya habari vya hapa kama ilivyo sasa kuhusiana na tukio hilo la tindikali.
Tukio hilo la tindikali limetuathiri hata akina sie, kwani majuzi tu kuna jamaa aliniuliza asili yangu ni wapi, na nilipomjibu "Tanzania" akakunja sura na kuniuliza “kule mlikowamwagia tindikali mabinti wetu waliokuja kujitolea kuwasaidia (volunteer)?” Aibu niliyopata inabaki nafsini mwangu.
Na sijui ni katika kutapatapa au kutaka kuwahadaa Waingereza, sakata la Sheikh Ponda Issa Ponda, ambaye inadaiwa amepigwa risasi na polisi, linafanya kile wanachoita Waingereza a bad case gets even worse (jambo baya linakuwa baya zaidi). Nisingependa kujadili kwa undani suala la Ponda, ambaye kwa hapa Uingereza anatajwa (kimakosa, kwa mtizamo wangu) kuwa ndiye mtuhumiwa wa uchochezi uliosababisha shambulio la tindikali kwa mabinti hao wa Kiingereza.
Ninaweza kuandika makala mfululizo zisizo na kikomo kuorodhesha masuala mbalimbali yanayoweza kumfanya mtu adhani tumerogwa (au tumejiroga) lakini cha muhimu sio lawama pasi kukaa chini na kujiuliza kulikoni?
Kuna udhaifu mahala fulani unaomwathiri kila Mtanzania. Tunaweza kumlaumu Rais Paul Kagame wa Rwanda kuwa ndiye tishio kubwa kwa Tanzania kwa sasa, lakini ukweli mchungu ni kwamba chanzo cha matatizo yetu ni ombwe la uongozi. Nchi imegeuka lawless (isiyo na sheria, ila sheria zipo tu linapokuja suala la kesi ‘feki’ za ugaidi wa CHADEMA).
Uhuni wa kuua siasa ya ujamaa umezaa ombwe la itikadi unganishi (integrative ideology) sambamba na kundi la maharamia ambao wapo tayari kwa lolote kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
Nimalizie kwa kuhadharisha tena kuwa nchi yetu sio tu inaelekea kubaya bali imeshafika mahala pabaya. Ni matumaini yangu Rais Jakaya Kikwete na wasaidizi wake wanasikia kelele zetu. Anaweza kuamua kupuuza kelele hizi na kuiacha nchi itumbukie katika korongo la kina kirefu, au achukue hatua za haraka kuinusuru nchi yetu.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/viongozi-nadhifu-kwa-suti-wahuni-kifikra#sthash.T1aviKJ2.dpuf

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget