Saturday, 10 August 2013
Moja ya magazeti makubwa nchini Israel, Jerusalem Post, limeandika kuwa mabinti wawili wa Kiingereza walioshambuliwa kwa tindikali huko ZANZIBAR walikuwa wanaharakati na wanachama wa Shirikisho la Vijana wa Kiyunani (Federation of Zionist Youth).
Kwa namna flani, ukaribu wao na harakati hizo za Kizayuni unaweza kuwa miongoni mwa sababu zilizopelekea mabinti hao, Kirstie Trup na Katie Gee, kushambuliwa. Hisia iliyopo ni waliofanya shambulio hilo walisukumwa zaidi na 'kuwaadhibu Wayunani na marafiki zao,' kama ambavyo imekuwa ikitokea sehemu mbalimbali duniani. Inafahamika kuwa vikundi vyenye msimamo mkali wa Kiislam kama vile Al-Qaeda vimekuwa na uhasama mkubwa na Wayahudi.
Wakati huohuo, Shirika la Utangazaji wa Uingereza (BBC) linaripoti kuwa serikali ya Zanzibar imetangaza zawadi ya shilingi milioni 10 kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazopelekea kukamatwa kwa wahusika wa shambulio hilo.
Tukio hilo la kikatili bado linatawala vichwa vya habari kwenye magazeti, TV na radio, hapa Uingereza.
Gazeti la kila siku la Daily Mirror linaelezea jinsi mtalii mmoja kutoka Uingereza,Sam Jones, alivyojitoa mhanga kumwokoa Katie baada ya kumsikia akilia kwa uchungu kutokana na maumivu ya kumwagiwa tindikali.
Sam aliyekuwa visiwani Zanzibar na girlfriend wake, Nadine, alieleza kuwa Katie alikuwa akilia kwa kelele na kuomba amwagiwe maji huku tindikali ikiunguza ngozi yake. Mtalii huyo alifanikiwa kupata maji na kummwagia Katie.
Mhanga mwingine wa tukio hilo, Kirstie, alikutwa na wasamaria wema mtaani akilia kwa uchungu baada ya kumwagiwa tindikali, na walimbeba hadi baharini na kumtumbukiza majini kwa ajili ya kudhibiti madhara zaidi ya tindikali.
Hadi sasa polisi wa Zanzibar wameshawahoji watu saba. Pia wametoa amri ya kukamatwa Sheikh Ponda Issa Ponda, ambaye wanadai alihamasisha shambulio hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment