Friday, 18 January 2008

Siku chache zilizopita nilizungumzia kuhusu "afya" ya muziki wa Bongofleva.Dhamira ya makala hiyo ilikuwa ni kuwaamsha wahusika na kuwakumbusha kwamba japo ni vizuri kula matunda ya jasho lao,wanapaswa kuwa makini wasije kujikuta wanakata kabisa na mimea inayotoa matunda hayo.

Leo napenda kuzungumzia nafasi ya muziki huo katika kuleta mabadiliko kwenye jamii.Nilisoma mahala flani kuhusu lawama dhidi ya rapa maarufu huko Marekani,Jay-Z,baada ya kutoa albam yake mpya ya American Gangster.Katika makala hiyo,mwandishi alimlaumu Jay-Z kwamba sehemu kubwa ya albam hiyo ilikuwa imetawaliwa na "meseji za kawaida za marapa"...kujisifia kwingi,blings,warembo,nk.Mwandishi huyo alidai kwamba alitegemea,katika nafasi yake kama mmoja ya majina makubwa ya Weusi nchini Marekani, Jay-Z angeelekeza jitihada katika "kuzisaidia 'hoods katika mapambano ya ukombozi wa kweli wa mtu Mweusi".Anyway,sijapata fursa ya kusikia nyimbo zote zilizo katika albam hiyo,kwahiyo siwezi ku-comment lolote katika hoja ya mwandishi huyo.Hata hivyo,alichokisema kina mantiki kuhusiana na muziki wetu huko nyumbani.

Wasanii wa bongofleva na wale wa aina nyingie za muziki (kama taarabu na muziki wa dansi) ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa ufisadi.Wengi wao hugeuzwa,ashakum si matusi,mithili ya "kondom za kisiasa".Hapo namaanisha kwamba baadhi ya wanasiasa huwatumia wasanii hawa wakati wa kampeni zao za kusaka uheshimiwa lakini wakishapata madaraka huwapuuza kabisa wasanii hao waliowapigia debe.Ni mithili ya kondom,ambayo kwa kawaida huonekana yenye umuhimu mkubwa (kwa wale wanaojali) kabla ya tendo la ndoa,lakini hugeuka takataka baada ya kutumika.

Wapo watakaodai kwamba wanasiasa wana haki ya "kukatisha" mahusiano na wasanii hao kwa vile huwaalika kwenye kampeni baada ya kuwalipa.Hoja hiyo inaweza kupingwa na ukweli kwamba fedha au malipo sio kila kitu (money isn't everything).Chukulia mfano wa mwalimu.Anapokufundisha anafanya hivyo kwa vile ni mwajiriwa wa taasisi ya elimu,na analipwa kila mwezi kukupatia elimu,achilia mbali uwezekano kwamba unalipia (ada) elimu hiyo.Lakini (pamoja na kupuuzwa kwao) walimu wanaendelea kushikilia nafasi muhimu katika jamii kwani ndio wafunguzi muhimu wa jitihada za binadamu katika kukabiliana na mazingira yake.Mfano mwingine ni wazazi.Wametuzaa,kutulea na kutusapoti katika makuzi yetu.Wapo wanaoweza kudai kuwa huo ni wajibu wao.Lakini tunafahamu kwamba wangetaka,wangeweza kabisa kzuia ujio wetu duniani (kwa baba na mama kuamua kutokuwa na watoto zaidi,kabla sie hatujazaliwa,au hata kutoa mimba zilizosababisha tuzaliwe).Tunaendelea kuwajali wazazi licha ya ukweli kwamba uzazi ulikuwa ni jukumu lao.Mifano hiyo miwili inaweza kulinganishwa na hoja yangu kwamba malipo yoyote yanayofanywa baada ya kutendewa kitu kikubwa hayawezi kulinganishwa na thamani ya matendo hayo.For that matter,fedha yoyote inayotolewa kama malipo kwa wapiga debe kwenye kampeni ya mwanasiasa haiwezi kulingana na mchango wa wapiga debe hao.

Nirejee kwenye kichwa cha habari cha post hii.Wengi wetu tunamfahamu Masudi Kipanya,mchora katuni maarufu huko nyumbani.Katuni zake nyingi huzungumzia matatizo yanayoikabili jamii ya Watanzania,na kwa hakika amekuwa mwiba mkali kwa wanasiasa wababaishaji na mafisadi.Anafanya kazi halisi ya sanaa kwani sanaa ni kioo cha jamii.Kwa bahati mbaya,wasanii wa muziki (hususan bongofleva) wamekuwa "wapole" sana katika mapambano dhidi ya maovu katika jamii yetu.Unakumbuka tungo kama Wauguzi ya Wagosi wa Kaya,au Ndio Mzee ya Profesa Jay?Hizi zilikuwa zina ujumbe mzito ambao kwa hakika ulikuwa unawakilisha kilio cha jamii.Tatizo kubwa la muziki wetu ni kwamba umetawaliwa sana na mada ya mapenzi.Hakuna ubaya kuzungumzia mapenzi,lakini yayumkinika kusema kwamba ili mapenzi yaende vema,shurti kuwe na kitu tumboni,barabara ya kufika kwa mpenzio iwe inafikika kirahisi,ukifika kwao usiku kuwe na mwanga (kwa maana ya upatikanaji wa umeme)....yaani hoja hapa ni kwamba mapenzi yanastawi vema pale huduma muhimu kwa maisha ya binadamu zinapopatikana kwa ufanisi.Ufisadi ni moja ya sababu kuu zinazokwamisha upatikanaji wa huduma hizo,na kwa sababu hiyo,wasanii wenye mahaba na dhima ya mapenzi kwenye tungo zao wana kila sababu ya kupambana nao (ufisadi) kwani vinginevyo wanachokiongelea kitaendelea kuwa ndoto za kujiliwaza tu.

Wapo wasanii ambao wana sababu za ziada za kupambana na mafisadi.Hawa ni pamoja na wale walioporwa wapenzi wao ambao walirubuniwa na nguvu ya fedha za mafisadi.Na kila msanii ana sababu nyingine ya kukabiliana na mafisadi (wadosi) wanaowalipa ujira mdogo ilhali wao (wadosi) wanatengeneza mamilioni ya bure.Ununuzi wa kazi za wasanii zinategemea hali ya kipato cha wateja wao (ikizingatiwa kwamba wengi wenye uwezo wa kiuchumi wako bize sana na masuala yao mengine kuliko kusikiliza tungo za nyumbani,na mafisadi wako bize zaidi na kuimarisha mikakati yao ya kulikamua taifa,kuangalia maendeleo ya miradi yao na kuboresha nyumba zao ndogo),kwa hiyo wasanii wana wajibu wa kushiriki mapambano ya kuboresha maisha ya wateja wao wakuu (wengi wao wakiwa waathirika wakuu wa ufisadi).

Tunahitaji akina (Masudi) Kipanya wengine kwenye bongofleva na miziki mingine kushirikiana na wale wote walio katika mapambano dhidi ya ufisadi huko nyumbani.Kelele za aina yoyote dhidi ya wahalifu (mafisadi) hao zitasaidia angalau kuwakumbusha kwamba tamaa na furaha zao ni kilio kwetu.

Hebu msikie Skinnyman anavyolalamika katika clip hii ya Council Estate of Minds kuhusu hali halisi ya maisha kwenye maghorofa (yaliyosahaulika,na makazi maarufu ya watu wa kipato duni) ya manispaa (Council estates)


1 comment:

  1. salaam,
    nimeipenda site yako, iko vizuri sana. nina wazo, mtu akisoma post anagundua kuwa hauko tanzania kwa sababu unatumia neno "huko" nyumbani tanzania.
    nafikiri usipoweka hilo neno la kutufanya tujue haupo sehem fulani inatupunguzia utamu na utandaa.

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget