Saturday, 13 March 2010


Moja ya maeneo yeynye kuhitaji mtazamo mpya katika Tanzania ni haki za raia.Ni ukweli usipingika kwamba nchi yetu ina haki za aina mbili: kwa wenye nacho/vigogo na kwa walalahoi.Kuna mifano mingi ya kuthibitisha hilo lakini hapa nitaonyesha mifano michache kuokoa muda.Mzee wa Vijisenti Andrew Chenge alipopata ajali iliyopelekea vifo vya watu wawili,jeshi la polisi lilikurupuka kuunda tume ya kuchunguza ajali hiyo.Baada ya ajali hiyo,zimetokea ajali nyingine kadhaa zilizopelekea vifo vya watu kadhaa lakini hatujasikia jeshi la polisi likiunda tume kuchunguza ajali hizo.Jibu jepesi ni kwamba waliopoteza maisha kwenye ajali hizo si vigogo hivyo 'hakukuwa na umuhimu kwa kuundwa tume za uchunguzi'.Mfano mwingine ni kauli ya Rais Mstaafu Ben Mkapa kwamba wanaoajiri mahauziboi na mahazigeli wanapaswa kuwa na mafaili ya waajiriwa wao ili pindi likitokea tatizo wapatikane kirahisi.Mkapa aliyasema hayo alipoenda kumpa pole Balozi Andrew Daraja kufuatia mauaji ya mkewe ambayou yanadaiwa kufanywa na hauziboi wa balozi huyo. Kwanza,tukio zima la kifo cha mke wa Balozi linatengeneza mazingira ya ukiukwaji haki za hauziboi husika.Ieleweke kuwa nami nimeguswa na mauaji hayo ya kinyama lakini hiyo haiwezi kuhalalisha jamii kujichukulia sheria mkononi na kumhukumu hauziboi huyo.Jeshi la polisi ndilo lenye mamlaka ya kuchunguza mauaji hayo na kisha kuiachia mahakama itoe hukumu.

Twende kwenye ushauri wa Mkapa.Kwa mawazo ya Rais huyo mstaafu,kuwa na mafaili yenye taarifa za mahauziboi na mahauzigeli kutasaidia kuwapata kirahisi pindi wakihusishwa na vitendo visivyofaa.Mkapa anaelekea kuthamini zaidi haki za vigogo wenzie wanaoajiri mahauziboi na mahazigeli huku wakilipwa mishahara kiduchu na kutumikishwa kama watumwa,ilhali anapuuza haki za waajiriwa hao ambao ni adimu kwao kuwa na mikataba ya ajira huku ajira zenyewe zikiwa mithili ya maandishi ya chaki ubaoni (blackboard).Ukijisugua tu na ubao,yanafutika.

Japo wazo la Mkapa sio baya kihivyo,lakini kwanini lije wakati huu ambapo hauziboi anahusishwa na mauaji ya mke wa mwanadiplomasia Daraja?Ni hadithi zilezile za barabara kukarabatiwa kukiwa na ziara za viongozi wakati zimesahauliwa miaka nenda miaka rudi kwa vile tu watumiaji wa barabara hizo si vigogo.Kama kulikuwa na umuhimu wa kuwepo mafaili yenye taarifa za watumishi wa ndani basi isingehitaji kusubiri hadi hauziboi atuhumiwe kumuua mke wa balozi.

Na ni kwa vile walalahoi hawana uwezo wa kumudu kuajiri wanasheria wazuri lakini kwa namna 'jamii ilivyokwishatoa hukumu dhidi ya hauziboi wa Balozi Daraja' ni dhahiri kesi yake mahakamani ingestahili kufutwa kwani 'ameshahukumiwa uraiani'.Mkapa alipaswa kutambua kuwa kauli yake kama Rais Mstaafu inaweza kabisa kutafsiriwa kuwa nae amefuata mkumbo wa kuamini kuwa 'ukiwa mlalahoi na ukatuhumiwa,basi unabaki mkosaji hadi itakapothibitika vinginevyo' (guilty until proven innocent).

Mlalahoi Jerry Muro alipotuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa mtuhumiwa wa rushwa (funny,isn't it?),kamanda Kova na vijana wake wakakurupuka chap chap kutujulisha kuwa jeshi lake lina teknolojia za kisasa za kufuatilia wala rushwa (sijui kwanini hawajashea ujuzi huo na TAKUKURU).Lakini wakati Kova akituaminisha mazingaombwe hayo,tunabaki na maswali kwamba kama vyombo vyetu vya dola viko makini kiasi hicho ilikuwaje basi wale majambazi wa EPA walimudu kutuibia mabilioni yetu pale Benki Kuu,mahala paliposheheni mitambo ya kisasa ya ulinzi?Au kwani teknolojia iliyotumika kumnasa Muro haikutumika kuwabaini majambazi wa Richmond?Na kwanini isitumike kumfahamu Kagoda ni mdudu wa aina gani?

Jibu rahisi ni kwamba Muro aligusa maslahi ya wakubwa (na vijana wao in the name of Jeshi la Polisi) na wakaamua kumpa 'jambajamba' (excuse my language) ili 'atulie'.Chenge ameendelea 'kutanua' licha ya tuhuma za vijisenti vyake vyenye thamani ya bilioni huko visiwani Jersey.Na bado teknolojia ya jeshi la polisi iliyomnasa Muro haijafanikiwa kuona kama Chenge anastahili kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.Jawabu la utata huo ni jepesi: Chenge ni kigogo,na Muro ni mlalahoi.

Magereza yetu yamesheheni wezi wa kuku na vibaka wengineo huku majambazi halisi wa uchumi wetu wanaendelea kutudhihaki mitaani wakiwa kwenye ma-vogue yao ya bei mbaya.Tanzania yetu imefika mahala ukijaribu kukemea uovu unaohusisha vigogo unaonekana kama mhaini,na utaandamwa zaidi ya Wamarekani wanavyomtafuta Osama bin Laden.Na kwa huko mtaani,ukiwa na bahati mbaya ya kuwa na mke/mpenzi mzuri anayetamaniwa na kigogo,andika umeumia.Nakumbuka hadithi ya jamaa mmoja aliyepewa kitengo nje ya nchi ili kigogo aliyekuwa anatoka na mkewe apate wasaa mzuri wa kufaidi 'haki za vigogo zilizoangukia kwa bahati mbaya kwa mlalahoi'.

Ni katika mazingira hayo ndio maana baadhi ya watu wanadiriki kuamini kwamba laiti Babu Seya na wanae 'wasingegusa haki za vigogo' angeendelea kuwa uraiani akitumbuiza na bakulutu zake.Siungi mkono ulawiti lakini wajuzi wa kona za Dar es Salaam wataafikiana nami nikisema kuwa kuna vigogo wengi tu wanaofanya michezo michafu kwa vibinti vidogodogo mitaani lakini wadhifa wao unawalinda,na wanaishia kuitwa 'viwembe' badala ya kuwa jela kama Babu Seya.Again,mwanamuziki huyo na mwanae Papii Kocha wako 'mbele ya sheria' kwa vile ni walalahoi na si uzito wa makosa yao.Nithibitishie kuwa siko sahihi (prove me wrong).

Wito wangu kwa walalahoi wenzangu ni huu: kaa ukitambua kuwa sheria na haki nchini mwetu zina sura mbili: upofu kwa makosa ya vigogo na macho makali (hata kwenye giza) kwa walalahoi.Fanya manjonjo yako ukitambua ukweli huo mchngu,ukigusa 'haki' za vigogo,andika umeumia.Tambua kwamba wanywa gongo huko Uwanja wa fisi wanapokamatwa na vyombo vya dola (mara nyingi hawanywi pombe hiyo hatari kwa vile hawajali afya zao bali uchumi mbovu) tunaambiwa kosa lao ni kutumia kinywaji hicho haramu lakini ikitokea vigogo na watoto wao wakajihusisha na kuuza na kutumia madawa ya kulevya,hawagusiw kwa vile 'ni haki yao kujistarehesha' (ndio maana ile orodha ya wauza unga ambayo ex-minister Mwapachu aliikabidhi kwa JK haijafanyiwa kazi hadi kesho).

Ni ukweli mchungu na unaoumiza lakini ubaki ukweli na hali halisi.By the way,Waingereza wanasema TRUTH HURTS!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget